Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii adhimu na mimi niweze kuchangia taarifa hizi mbili za oversight committee ya PAC na LAAC.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaingia ndani kwenye kuona madudu makubwa ambayo yameainishwa na Mdhibiti pamoja na viongozi wa hizi Kamati, niungane na wenzangu na mimi kuzungumzia juu ya weledi mdogo walionao Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli ambao uko dhahiri kwamba kama kuna jambo ambalo Halmashauri zetu zitakwama ni kuwa na watendaji dhaifu, ni kuwa na Wakurugenzi ambao hawajui walifanyalo. Na jana hapa wakati Mheshimiwa Waziri wa Habari anajibu baadhi ya hoja nilistaajabu sana aliposema kwamba walioteuliwa ndio watakaokuwa watekelezaji wazuri wa Ilani ya CCM. Kama CCM imekaa ikiwategemea Wakurugenzi wa aina ile ninawathibitishia mnakwenda kushindwa. Kama aina ya Wakurugenzi tulionao ndio mnaowategemea kufanikisha Ilani ya Chama cha Mapinduzi wanakwenda kushindwa muda mfupi ujao.
Mheshimiwa Naibu Spika, aina ya Wakurugenzi tulionao hawajui walitendalo na Mheshimiwa Waziri mimi nakuambia tuna Wakurugenzi ambao wanafanya mambo ya ajabu kweli kweli kwenye Halmashauri. Baraza la Madiwani linakaa likapitisha maamuzi yake, Mkurugenzi anabeba document anampelekea Mkuu wa Wilaya anakwenda kumwambia hebu pitia haya sahihi kweli haya? Yaani Mkuu wa Wilaya sasa ndiye anayefanya maamuzi kwa niaba ya Halmashauri. Kwa hiyo, tumekuwa na Wakurugenzi ambao hawajui walifanyalo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nawaomba katika namna ya kuwasaidia na kuzisaidia Halmashauri zetu, Serikali ihakikishe inatoa mafunzo kwa Wakurugenzi hawa mliowateua from nowhere. Mfumo wa utendaji wa kazi Serikalini unajulikana na unatambulika, huwezi kumtoa mtu kutoka huko kwenye NGO ukampeleka kwenye taasisi kubwa kama Halmashauri, ni shida. Mmetengeneza matatizo makubwa kwenye Halmashauri zetu.
T A A R I F A...
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Naibu Spika, hajanipa taarifa alikuwa anachangia, kwa hiyo obvious siwezi kuikubali na mimi ninachokichangia ninachangia kwa mujibu wa taarifa hii iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya LAAC, kwamba asilimia 60 ya Wakurugenzi waliokutana nao wameonyesha udhaifu kwamba hawajui walitendalo, ndiyo taarifa inavyosema. Hatuchangii kwa mujibu wa mtu, hapa ninachozungumza tunachangia Taarifa za Kamati. Kwa hiyo, ukisema ukitoa taarifa maana yake unampa taarifa Mwenyekiti wa Kamati aliyewasilisha hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika kwa hiyo niendelee kusisitiza kuna haja ya kuwapa mafunzo, kuna haja ya kuwapa semina ili watende vile mtakavyo, ili watende kwa mujibu wa sheria na ili tupate manufaa na mafanikio kwenye Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la TIB (Tanzania Investment Bank), ukisoma Taarifa ya Mkaguzi ukasoma na Taarifa ya Kamati ya PAC inaonesha kwamba Tanzania Investment Bank imetoa mikopo zaidi ya shilingi bilioni 64 kwa watu ambao hata kuwataja hawataki. Taarifa ya Kamati inaeleza kwamba hata Mwenyekiti wa Bodi alivyoitwa kwenye Kamati aje aeleze kwamba hizi shilingi bilioni 64 imewakopesha akina nani ameshindwa kuwataja na katika masikitiko yangu makubwa Mwenyekiti wa Bodi juzi alikuja hapa kutueleza mambo ya EPA, namheshimu sana Mheshimiwa Profesa Palamagamba Kabudi, akaonesha kwamba ni mzalendo sana. Kama ana kiwango hicho cha uzalendo kinachomshinda kutaja hawa waliokopeshwa bilioni 64 ni nini? Na taarifa inaonesha kwamba wao wamefungua kesi 21 kuwashtaki watu, akina nani? Wanapata ukakasi gani kuwataja hawa waliowakopesha shilingi bilioni 64? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii tuombe, kama Mwenyekiti wa Bodi anashindwa kutaja au kama Mtendaji Mkuu wa hii Benki anashindwa kuwataja, rungu lako la Bunge lifanye kazi ili hawa waliokopeshwa shilingi bilioni 64 ambao hawatajiki waje waelezwe ndani ya Bunge humu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichangie juu ya suala la misamaha ya kodi kwenye uingizaji wa mafuta. Mheshimiwa Waziri wa Fedha anatafuta sana pesa kwenye kodi. Taarifa ya Mkaguzi inaeleza kwamba mwaka 2012/2013 Geita Gold Mines na Resolute Tanzania Limited walipatiwa msamaha wa kodi ya mafuta, lakini wao ule msamaha wakautumia nje ya mizania, nje kabisa ya utaratibu wakahamisha yale mafuta kwenda kupeleka kwenye kampuni nyingine. Zaidi ya bilioni 22 zinaoneshwa hapa kwamba watu wa Geita Gold Mines walihamisha kodi ile ya mafuta kwenda kuipa kampuni nyingine yale mafuta, jambo ambalo ni kinyume kabisa na Tamko la Serikali Namba 480 la mwaka 2002.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji hizi bilioni 22 ambazo zilitolewa, ambazo zilikuwa ni kodi ya msamaha kwa Geita Gold Mines pamoja na Resolute Tanzania Limited, fedha hizi zipatikane, Waziri wa Fedha ulisikie hili, ulifanyie kazi ili kodi iweze kurudi kwa Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine naomba nichangie juu ya ucheleweshaji wa fedha kutoka Hazina kwenda Halmashauri na kwenda Wizarani. Kumekuwa na tabia iliyozoeleka kwamba Hazina inasubiri robo ya mwisho ya mwaka wa fedha ndipo hupeleka fedha nyingi kwenye Halmashauri, ama inasubiri robo ya mwisho wa mwaka kupeleka fedha nyingi Wizarani, matokeo yake nini kitatokea? Miradi ya maendeleo iliyokuwa inatekelezwa inaongezeka riba na Serikali inapata hasara kubwa kwa kuwa imechelewesha malipo ya wakandarasi. Lakini jambo la pili, fedha nyingi zinapelekwa katika Halmashauri katika kipindi ambacho muda wa utekelezaji unakuwa unakaribia kwisha kabla ya mwaka wa fedha kuisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma report inaonesha wazi kwamba katika mwaka wa fedha 2012/2013 zaidi ya shilingi trilioni 1.8, fedha ya maendeleo haikupelekwa, zaidi ya asilimia 38. Lakini pia ripoti inaonyesha kwamba zaidi ya Shilingi bilioni 19 zilipelekwa katika kipindi cha mwisho kabisa cha robo ya mwaka, fedha za OC na fedha zile hazikutumika. Katika mazingira kama haya tunatengeneza mwanya wa watendaji wetu wa Halmashauri wafanye vitendo ambavyo siwezi kusema kama ni wizi, isipokuwa si vizuri kwa mujibu wa sheria za fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine Serikali imepunguza sana uwekezaji wake kwenye baadhi ya taasisi. Ukisoma ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imeonesha kwamba uwekezaji wa Serikali katika Shirika la TAZARA hisa zake zimepungua sana. Serikali imepunguza hisa nyingi katika Benki ya NBC, lakini pia hata katika mashirika mengine ambayo hapo awali yalikuwa na hisa nyingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kupungua kwa hisa za Serikali katika TAZARA ina-reflect nini? Serikali imekuwa na uwekezaji mdogo katika hili shirika la reli ambalo tuna-share na watu wa Zambia. Kama Serikali ya Tanzania haipeleki fedha za kutosha TAZARA which means kama wenzetu wa Zambia kama wataendelea kuwekeza katika hili shirika mwisho wa siku hawa watu wa Zambia watakuwa wanamiliki hisa nyingi TAZARA kuliko vile ambavyo sisi Watanzania tunamiliki hisa maeneo hayo. Ni jambo la aibu sana shirika la reli ambalo tunalimiki kwa pamoja, tumelianzisha kwa pamoja sisi Watanzai kuwa nyuma katika kupeleka fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ni la msingi sana lazima tulizungumzie ni suala la Halmashauri na fedha za vyanzo vilivyofutwa. Halmashauri zetu zinajulikana kwamba kuna vyanzo Serikali imevifuta katika kumpunguzia mzigo mlipa kodi kule ndani ya Halmashauri, hili jambo lilikuwa jema sana na sisi tulidhani kwamba ili Halmashauri ziweze kujiendesha kwa ufanisi Serikali mngekuwa mnapeleka pesa kwa wakati. Lakini leo hii tuhojiane humu ni Halmashauri gani imepata pesa kutoka Serikalini au kutoka Hazina katika vyanzo vilivyofutwa na Serikali? Inatoa justification kwamba Serikali mnahatarisha uhai wa Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya Halmashauri huko ni mbaya na ubaya huu umechochewa kwa kiwango kikubwa kabisa na kufuta baadhi ya vyanzo ambavyo vilikuwa vinatusaidia kwenye Halmashauri kuendesha Halmashauri zetu. Mmevifuta, kufanya compensation mpaka sasa hamfanyi, pesa hampeleki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwahiyo ni jambo ambalo Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Waziri wa TAMISEMI wanatakiwa kutazama, kwa sababu Halmashauri zinakufa na Halmashauri zikifa ita-justify kwamba performance yako siyo nzuri Mheshimiwa Waziri wa Fedha, haitakuwa jambo jema kwako Halmashauri kufa kwa kikwazo tu kwamba Waziri wa Fedha hapeleki fedha kwenye Halmashauri kutokana na vyanzo vilivyokufa.
Kwa hiyo mimi niombe sana, Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI wewe unajua, unazunguka kwenye Halmashauri unajua kwamba Halmashauri zote zina vilio vya juu ya fedha za vyanzo vilivyofutwa, kwa hiyo ni jambo la msingi wewe kumbana Waziri wa Fedha aweze kupeleka hizo fedha katika Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho la kumalizia, naona muda umekaribia sana, kwamba Mkaguzi na Taarifa za Kamati zinaonesha wazi, Mkaguzi fungu la pesa alilotengewa ni dogo kiasi kwamba halimuwezeshi kufanyakazi yake ipasavyo, na cha ajabu ni kwamba kwa mujibu wa bajeti inaonesha kwamba mtapeleka fedha shilingi milioni sijui 50 katika kila kijiji, ingawa kwenye bajeti hazionekani lakini wenyewe mnasema bado maana yake hayo maneno mnayarudia kwamba mtapeleka hizo fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama mnapeleka fedha vijijini maana yake kwamba mnapanua wigo wa kazi za Mkaguzi kutoka kwenye central government kwenda mpaka kwenye local government mpaka kwenye village level, kwa sababu popote zilipo fedha za Serikali Mkaguzi ana wajibu wa kwenda kuzikagua. Ikiwa hamjamtengea fungu la kutosha huyu Mkaguzi hizi kazi ataifanyaje?
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi napata wasiwasi kwamba tunakuwa na Serikali ya aina gani ambayo inaogopa kivuli chake yenyewe, Serikali inayoogopa kukaguliwa, Serikali inayopambana na rushwa kwamba mnajionesha, mnaji-brand kwamba nyie mnapambana na rushwa lakini kumuwezesha Mkaguzi kwenda kukagua hamtaki, tutajuaje weledi wenu wa kupambana na rushwa? Mimi napata wasiwasi kwamba inawezekana mnatumia kumminya huyu Mkaguzi asiende kuwakagua ili udhaifu wenu na aina ya ufisadi mwingine mnaotengeneza huko sisi tusije tukaujua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninaomba sana, ninaomba sana, ikiwa Serikali inampango wa kumfunga kama ni midomo au kama ni miguu huyu Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali asiende kukagua fedha za Serikali mnajikaanga kwa mafuta yenu ninyi wenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.