Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

Hon. Conchesta Leonce Rwamlaza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

MHE. CONCESTTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuongea machache kutoa maoni yangu juu ya taarifa za Kamati ambazo zimetolewa leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya LAAC kwa hiyo nianze kwa kuunga mkono maamuzi na mapendekezo ambayo yametolewa na Kamati yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, maneno mengi yameshasemwa lakini ni muhimu na sisi tuendelee kuyasema, tuyawekee uzito wake lakini na kuwekea msisitizo kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Bunge lako nilirudishe nyuma wakati Serikali imefuta Serikali za Mitaa mwaka 1972 na kuweka mfumo wa madaraka Mikoani. Serikali ilifanya hii decentralization lakini baadae Serikali iligundua kwamba ilishindwa kutoa huduma kwa wananchi. Kwasababu Serikali za Mitaa ni vyombo ambavyo viko pale kutoa huduma kwa watu wa ngazi ya chini, lakini pia vinatekeleza Sera ambazo zinaelekezwa na Serikali Kuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kama wenzangu walivyosema, kama Halmashauri zitakwenda katika mwenendo huu tunakwenda kuziua na kuzifuta kama ilivyokuwa mwaka 1972. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na mfumo wa ukaguzi katika Halmashauri. Wakaguzi wa Ndani hawana kasma, Wakaguzi wa Ndani wako chini ya Mkurugenzi. Katika ukaguzi wetu tumegundua Mkaguzi wa Ndani mmoja ambaye alijitokeza kujibu hoja za uhasibu wa Halmashauri. Sasa tukajiuliza, huyu ni auditor wa ndani lakini yeye amejitokeza kujibu hoja za mhasibu ambazo tumemuuliza, je, huyu anaweza kusimamia kweli ukaguzi katika Halmashauri yake?
Kwa hiyo tunachoishauri Serikali, ihakikishe inaimarisha Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani ili Halmashauri hizi na Wakurugenzi waweze kukaguliwa na hata wenyewe hawa ma-auditors wa ndani waweze kushauri Halmashauri zao katika mambo ya fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee Mfuko wa Wanawake na Vijana wa asilimia 10. Mfuko huu uko very sensitive, kila Mbunge anauhitaji, anahitaji kuona Halmashauri inatoa mchango wa asilimia tano kwa vijana na aslimia tano kwa wanawake ili waweze kuwa na shughuli za kufanya. Tuwaweke vijana wawe busy, wasiingie kwenye panya road, tuwaweke akina mama waweze kupata kazi za kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wasiwasi wangu katika ukaguzi wetu na kuhoji Halmashauri, kila Halmashauri ina deni kubwa la mifuko hii, lakini madeni hayo yamesababishwa na maagizo yanayotoka juu ambayo yanawapa deadline yaani yanawapa ultimatums ku-raise tengeneza madawati Halmashauri, katika miezi miwili tunaomba madawati yako tayari. Wananchi? Hawana pesa za kuchangia. Halmashauri ifanye nini? Kwa hiyo, wanachukua mafungu kutoka own sources, wanachukua mafungu kutoka katika development wanatengeneza madawati na kwa kweli kama walivyosema wenzangu imekuwa ni mwanya wa kuiba hela za Serikali. Ukiwauliza wote wanakuambia kwamba sisi tumechukua hizi pesa kwa sababu tuliambiwa tutengeneze madawati katika miezi miwili, tumetengeneza maabara katika miezi miwili, kwa hiyo, matokeo yake pesa zinapotea bure.
Mheshimwa Naibu Spika, sasa wasiwasi wangu, hii mifuko, Halmashauri zote zinadaiwa mamilioni ya pesa, je, wana uwezo wa kulipa madeni haya? Kwa sababu kama walivyochangia wenzangu Halmashauri hizi zimekatwa mikono, haziwezi kuwa na pesa, Serikali Kuu imechukua vyanzo vyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano Katika bajeti ya mwaka jana kama mnakumbuka katika kitabu cha Waziri wa Ardhi, alionesha kwamba walikusanya shilingi bilioni 54 lakini walipeleka bilioni nne tu katika Halmashauri karibu 138. Mkoa wangu wa Kagera tulipewa shilingi milioni 138, Halmashauri ya Ngara ilipewa milioni nne kitu kama hicho. Sasa unaweza kuona kama wameweza kukusanya pesa zikaenda kule juu hazirudi, hizi kwa mfano za kodi ya majengo zitarudi? Nina wasiwasi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana katika kitabu chetu tumependekeza kwamba iundwe sheria ya mfuko huu. Hakuna sheria ni agizo sawa, lakini hata sheria yenyewe itazame ni jinsi gani mfumo huu unaweza kuwekwa na unaweeza kutumika. Kwa mfano, tumegundua kwamba hata makundi mengine yanayopewa mikopo ni hewa na yanayopewa hayarejeshi, kwa hiyo hiyo, mifuko haiwezi kurotate, hairudishi pesa tena. Kwa hiyo, mimi nashauri kwamba Serikali iziangalie hizi Halmashauri upya ziweze kupata makusanyo na ziweze kukata 5% kwa ajili ya vijana na 5% kwa ajili ya wanawake vinginevyo, itabaki katika hoja za ukaguzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Na namwomba Waziri mwende nalo hili kwamba, tuangalie upya namna ya kuweka mfuko huu, ili tuweze ku-materialize yaani uweze kuona kama unaweza kuleta impact kwa wanawake vinginevyo Halmashauri zitashindwa, mtazituhumu hapa na zitashindwa kabisa kukusanya hizi fedha na hawatakuwa na uwezo wa kuwasaidia wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye hoja ya Serikali kutokupeleka fedha. Serikali haipeleki fedha, lakini ziko Halmashauri nyingine zinapelekewa fedha nyingi nje ya bajeti. Kwa mfano katika kukagua tuligundua katika Halmashauri ya Mpanda katika mwaka wa fedha 2014/2015 walikuwa wametenga bajeti ya shilingi milioni 432 lakini wakapewa fedha shilingi milioni 303.8 ya ziada. Kwa hiyo, wakawa na fedha karibu milioni mia saba na kitu. Ukiuliza Hazina kwa nini mmewapa fedha ya ziada ambayo haipo kwenye bajeti? Hawana majibu, ukiuliza Mkurugenzi, hana majibu, tuonyeshe mmetumiaje hawana majibu. Sasa wasiwasi wangu ni kwamba, inawezekana kuna chain ya wizi kuanzia Hazina, TAMISEMI mpaka kwa Mkurugenzi. Kwa hiyo, tunaomba Serikali ilijue hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kama fedha zinaweza kutolewa za ziada basi CAG apewe maelezo na hata Kamati ipewe maelezo. Kwa hiyo, kuna mambo kama hayo ambayo yanafanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uteuzi wa wakurugenzi, watu wamesema sana. Si wote ni baadhi, lakini naomba niseme hapa kuna Chuo cha Hombolo. Serikali za Mitaa zina chuo cha kuweza kufundisha watu wake, sasa imekuwaje chuo hiki hakiwezi kutumika kufundisha watu? Kiko pale purposely kwa ajili ya kufundisha namna ya kuendesha Serikali za Mitaa, ni kwa nini watu hawapewi mafunzo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mafunzo pia yatolewe kwa Madiwani. Madiwani wetu wanakuja hata sisi hapa Wabunge, kuna wapya, kuna wa zamani, mnatuweka kwenye semina tunajifunza. Hata Madiwani wafundishwe ili waweze kukabiliana na executive. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakukaribisha siku moja uje kwenye kamati yetu huko ya LAAC, yako ma-book pale, yanakuja wale wataalamu wanakuandikia, book linalingana hivi, yaani unalinganisha biblia tatu, nne, tano unalitazama mpaka unaanza kujiuliza nianzie wapi? Na watu hawa wanafanya purposely ili ukienda pale utazametazame macho tu uwe kama buibui usielewe hata cha kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mtindo huo ndio ulio ndani ya Halmashauri mimi nimekuwa diwani tangu mwaka 2000, najua, wanaleta ma-book yaani madiwani wanaanza kuyatazama up side-down, na wale wanakuwa ile executive ina hawasomi. Unakuta Mkurugenzi ana degree, Bwana Mipango ana ma-degree, wengine wana CPA, wengine wana nini; halafu Madiwani wanaweka pale wanachanganya changanya. Madiwani wapewe mafunzo. Halafu wanakuta wameandika kwa kimombo bwana. Sasa wewe unaleta taarifa hii kwa madiwani unaandika kimombo wakati hata sheria ya uchaguzi inasema mtu ujue kusoma na kuandika. How? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninachoshauri Serikali isitazame haya mambo ya kubana matumizi haya, mnabanabana kitu gani? Na mnabana nini, hamjapata chochote, kwa sababu sisi LAAC tunafanya paper work. Huwezi kufanya paper work kwa hizi Kamati, wakati una watu huku wanajua kuchodoa, yaani ninyi hamuwajui watu wa Halmashauri. Huwezi kufanya paper work, wanakuja wameandika vitabu vizuri kabisa, wanapewa hata zile ripoti za CAG zile za ukaguzi, hati safi. Hati safi unakuta mtu amelamba shilingi milioni 300, shilingi milioni 500, utawauliza hata CAG, mnawapaje hati safi hawa watu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unaweza kuona kinachotokea. Kwa hiyo, tunaomba na wale madiwani wapewe mafunzo. Serikali isiseme kubana matumizi. Watanzania wana tabia moja, wana tabia ya kufanya mambo kimya kimya. Wanaweza kukubali kutii, bila kuwa na utii. Kwa hiyo Serikali hii itaendelea kuibiwa, haki ya Mungu mpaka mtakoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu gani? Kwa sababu huku chini sisi tunafaya pepar work. Tunashinda mle ndani ya kamati, kuanzia saa moja mpaka saa tatu usiku hatuna hata chakula, Naibu Spika, tupe na chai basi, maji moja, tunakagua vitabu vile mpaka tunachanganyikiwa lakini uko wizi mkubwa, na sisi tunawaambia haya kwa heri mwende, hatuendi kukagua, what do you expect? Mnachotegemea ni nini? Mtaibiwa yaani hata huku kutumbuana hakutakuwa na faida yoyote. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi Halmashauri naomba msiziue. Kama mkiendelea na mtindo huu wa kuwanyima fedha, mtindo huu wa kuhakikisha kwamba makusanyo yote mmewanyanganya, halafu ninyi mnawaambia kwamba jamani hamkusanyi mapato, wanakusanya wapi? Hakuna mapato ndani ya Halmashauri. Hakuna 5% za wananwake, hakuna 5% za vijana. Sana sana mtakuwa mnafukuza wakurugenzi mnatumbua na anayekuja mnatumbua wote mtawatumbua kwa sababu hawatakuwa na uwezo wa kuchangia hii 5%.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.