Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika hizi hoja zote mbili za Kamati. Nijikite zaidi katika taarifa hii ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa. Na mimi nakubaliana kabisa na Kamati ya LAAC kwa changamoto ilizoziona mojawapo ikiwa ni pamoja na baadhi ya Halmashauri kutochangia kabisa ule mfuko wa vijana na akina mama. Pia Halmashauri kutopeleka fedha kwenye kata na vijiji na uzembe wa ukusanyaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, hebu tutambue tu jambo moja kwamba mwaka jana ndiyo tulikuwa na uchaguzi na zaidi ya asilimia 70 ya Madiwani ni wapya lakini na hawa Wakurugenzi ni kweli kwamba zaidi ya asilimia 50 ni wapya, kwa hiyo, hata ile namna ya usimamizi wa fedha ni tatizo.
Kwa hiyo, nadhani cha kwanza kinachopaswa kufanyika hawa Madiwani pamoja na Wakurugenzi wanahitaji kupata mafunzo ambayo yatawasaidia au litawawezesha kuwa na udhibiti na usimamizi mzuri wa hizi fedha zao. Pia hii itasaidia kuondoa ile migongano iliyopo kati ya Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa kwa sababu hawa Madiwani wanajua majukumu yao lakini na Mkurugenzi naye atakuwa anajua majukumu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka hata sisi Wabunge tulipokuja humu Bungeni bado tulipata orientation. Sasa leo inakuwaje hawa Wakurugenzi wapya wanachaguliwa wengine kutoka maeneo ambayo hawajawahi kuhusika kabisa na masuala ya uongozi halafu wanafika wanapewa majukumu na tunategemea kwamba wanaweza ku-perform. Kwa hiyo, nadhani hiyo ni dosari ya kwanza pamoja na kwamba Serikali inabana matumizi lakini ione uwezekano wa kuendelea kutoa mafunzo kwa ajili ya Madiwani na hawa Wakurugenzi ambao ni wapya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la makusanyo kuchukuliwa na Serikali, ukiangalia kwenye ile Sheria Na. 7 na Na. 8 zilizounda Halmashauri za Miji pamoja na Halmashauri za Wilaya ilikuwa inasema wazi kwamba lengo la Serikali ni kuzijengea Halmashauri uwezo ili ziweze kujiendesha.
Sasa mimi najiuliza kama tunafika mahali tunachukua vyanzo vya Halmashauri tunavirudisha Serikali Kuu huko ndiko kuijengea ile Halmashauri uwezo? Kwa hiyo, tunadhani kwamba huu utaratibu wa Serikali Kuu kuona kwamba kuna chanzo hapa ambacho inaweza ikakusanya zaidi ikachukua halafu tukaiacha Halmashauri, halafu tunarudi kuilaumu kwamba haikusanyi wakati huo hata zile fedha ambazo tumeahidi tunapeleka hatuwapelekei mimi sidhani kama tunatenda haki hata kidogo. Kwa hiyo, nadhani tuna kila aina ya sababu ya kuendelea kuzijengea uwezo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia mapato yote au kodi zote ambazo zinadaiwa na Serikali Kuu ni za lazima yaani ukiletewa barua na Serikali Kuu kwamba kodi hii unapaswa ulipe, unapewa siku tofauti na hapo ni kwamba hatua kali zitachukuliwa. Ndiyo maana ukiangalia TRA wanapoenda kukusanya mapato yao wanaandamana na polisi, lakini ukiangalia hawa Halmashauri ambao tunategemea wakusanye siku zote mapato yao ni ya ku-negotiate yaani ni majadiliano na sana akiwa na askari atumie askari mgambo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kutokana na hali hiyo ni dhahiri kwamba haya mapato tunayotegemea kutoka kwenye Halmashauri haziwezi ku-perform kwa asilimia tunayotegemea kwa sababu mapato ya Halmashauri inaonekana ni hiari lakini mapato ya Serikali Kuu hayo ni lazima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hilo nalo lazima tuliangalie na tuone kwamba ni kwa kiasi gani tunaweza kuzijengea uwezo hizi Halmashauri au Serikali za Mitaa ili ziweze kujiendesha zenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala lingine ni maslahi ya Wenyeviti wa Mitaa pamoja na Madiwani. Nadhani hilo tunatakiwa kuliangalia zaidi ili nao waweze kujisikia kama viongozi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naunga mkono hoja.