Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia hii nafasi. Kwanza kabisa nianze kwa kuwapa hongera Kamati zote mbili kwa kazi kubwa waliyoifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kwa kuchangia juu ya asilimia 10 ya fedha za akinamama pamoja na vijana. Ni kweli Halmashauri nyingi hawapeleki fedha hizi kwa kina mama. Ningeshauri kuwa hizi asilimia ziwe zinapelekwa kwa akinamama kusudi waweze kufanyia biashara zao na vijana pia waweze kufanyia kazi zao kwa sababu hizi fedha zinasaidia katika ajira. Watanzania wote tunafahamu kuwa ajira ni matatizo sasa hivi, kwa hiyo, hizi fedha zingesaidia kwenye ajira ya akinamama pamoja na vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kwa Serikali kuwa walisimamie kusudi hizi fedha ziweze kupelekwa kwa walengwa ambao ni akinamama pamoja na vijana. Pia na mimi naongelea kuhusu hii asilimia 20 ya ruzuku ya Serikali Kuu kutopelekwa kwenye vijiji pamoja na mitaa. Naungana pamoja na Kamati kama inawezekana zipelekwe moja kwa moja kwenye vijiji pamoja na mitaa yetu, kwa sababu hazipelekwi kwenye Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, naongelea kuhusu fedha za maendeleo ambazo kusema ukweli zinachelewa kupelekwa na wakati mwingine hazipelekwi kabisa. Tunawalaumu kweli Wakurugenzi, lakini unakuta kuwa hizi fedha wakati mwingine hazipelekwi kiasi kuwa miradi inasimama.
Mheshimiwa Naibu Spika, akinamama bado wanateka maji kwa sababu miradi ya maji bado haijaendelezwa. Barabara zimesimama huko kwenye Halmashauri zetu kwa sababu fedha hazipo, vituo vya afya pia vimesimama; kiasi vingeweza kuboresha na kupunguza vifo vya akinamama pamoja na watoto; lakini kwa sababu fedha za maendeleo hazipelekwi na wakati mwingine hazipelekwi kwa wakati na wakati mwingine hazipelekwi kabisa. Nashauri Serikali iliangalie jambo hili la kupeleka fedha za maendeleo kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kuhusu Mfumo wa EPICOR. Ni kweli Halmashauri nyingine bado hawajajua vizuri kutumia mfumo huu wa EPICOR kiasi kwamba inaleta hoja kwenye mahesabu. Kwa hiyo, Halmashauri hizi ambazo bado hawajajua kutumia mfumo huu wa EPICOR, naomba sana waweze kupata elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Ukusanyaji wa Mapato ya Ndani. Mapato ya ndani naomba Halmashauri waweze kusimamia. Imegundulika kwenye Halmashauri nyingi kuwa mapato ya ndani hayakusanywi kama inavyokusudiwa. Kwa hiyo, vyanzo vilivyopo pamoja na vyanzo vipya, Halmashauri waweze kusimamia kusudi iweze kukusanya kama inavyokusudiwa; kusudi miradi ya maendeleo iweze kutimilika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni mafunzo kwa Wakurugenzi. Ni kweli Wakurugenzi wengi wapya kweli hawajajua vizuri kazi zao. Nami naungana na Kamati kuwa waweze kupewa semina ya jinsi ya kufanya kazi zao ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kukaimu; nimekaa huko kwenye mikoa na kweli kukaimu kwa muda hakuna tija. Naomba Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI aliangalie hili, kama mtu ameshakaimu kwa muda mrefu aweze kupitishwa kusudi aweze kushika Idara moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mengi yameshaongelewa, kwa hiyo, naomba nimalizie kwa kusema kuhusu Walimu wa sayansi. Imeonekana kuwa Walimu wa sayansi ni tatizo kubwa, hivyo naomba sana liangaliwe, Mheshimiwa Waziri wa Elimu naomba aliangalie suala la Walimu wa sayansi liweze kushughulikiwa kusudi tuweze kupata Walimu hao, no science, no development.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja.