Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

Hon. Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kwa upande wangu kwanza, nipende kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha leo hii tunajadili hoja muhimu sana za Kamati, lakini kubwa zaidi nipende kuzipongeza Kamati zote mbili.
Kamati hizi mbili zote zilizowasilisha hotuba zake hapa zimetuonesha kwamba, ni jukumu gani tunatakiwa tulifanye katika kipindi hiki cha sasa baada ya kupata ripoti hizi zilizofanyika mwaka 2014 na 2015. Tukiwa mwaka 2016 sasa, kama Wabunge na kwa ujumla kama Serikali tujue tutafanyaje ili wananchi waweze kupata huduma bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze katika Kamati ya LAAC. Naomba nimpongeze Mwenyekiti na timu yao yote ambayo katika njia moja au nyingine, wao wanatusimamia zaidi kwa karibu katika ofisi yetu. Naomba nikiri wazi kwamba, maelekezo waliyoyatoa kwetu sisi na kaka yangu Boniface Simbachawene tumepata viongozi ambao wanatushauri ili kazi yetu iweze kufanyika vizuri katika kipindi cha sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja mbalimbali lakini zote zina mashiko. Hoja ya kwanza ilikuwa ni suala zima la Sheria ya Manunuzi na kweli ukifuatilia ripoti ya Mkaguzi na hali kadhalika Kamati ilivyofanya uchambuzi mbalimbali ilibainika kwamba kuna changamoto kubwa sana na kutoa maelekezo nini tukifanye. Katika hili, ofisi yetu imeshaanza kuyafanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza tumetoa maelekezo katika Halmashauri zote; kwa vile tuna watendaji katika ngazi mbalimbali wengine wakiwa wapya, wahakikishe katika utiifu wa utendaji wa kazi zao, jambo la kwanza wanazingatia Sheria ya Manunuzi ili kuleta tija katika Halmashauri zetu. Hata hivyo, ukifuatilia ile ripoti imeonesha maeneo mbalimbali ambayo watu walifanya mambo ya hovyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikwambie na nilijulishe Bunge lako kwamba, katika eneo hili tumechukua hatua mbalimbali. Katika Halmashauri mbalimbali baadhi ya Wakurugenzi wamepoteza nafasi zao, lakini baadhi ya Wakuu wa Idara waliobainika, wameweza kuchukuliwa hatua mbalimbali na hivi sasa wengine wamepelekwa mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hili katika ofisi yetu hatutavumilia kabisa, wale wote ambao wameonekana ni kikwazo ambao kwa njia moja au nyingine wamehujumu fedha za Serikali na sisi tukiwa tumepewa dhamana katika eneo hilo; naomba tulihakikishie Bunge lako kwamba, ofisi yetu imejipanga hivi sasa tutafanya marekebisho makubwa sana na ndiyo maana nimesema kwamba, Kamati imeibua jambo hili ambalo ni jema, ni maelekezo na sisi tunakwenda kulifanyia kazi.
Suala lingine ni Udhaifu Katika Usimamizi na Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo. Ni kweli, Kamati ilibaini kulikuwa na udhaifu mkubwa sana katika maeneo mbalimbali, lakini katika eneo hili kulikuwa na marekebisho ya kimuundo kidogo baada ya kupitia hizi hoja mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ofisi yetu hivi sasa kuna Kitengo Maalum cha Ufuatiliaji ambacho kinafuatilia maeneo mbalimbali katika jitihada za kuhakikisha kwamba miradi hii iweze kutekelezeka vizuri, hasa kwa fedha zilizotolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, jukumu lake kubwa vilevile ni kuhakikisha kwamba inatoa ushirikiano wa karibu zaidi na Ofisi ya CAG na Kamati ya LAAC. Ndiyo maana katika kipindi chote cha mijadala baadhi ya wawakilishi wa kitengo hiki walikuwepo katika mijadala hii kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa jinsi ya kufanya katika maeneo mbalimbali ili yaweze kuleta tija katika eneo letu la kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana katika suala zima la ufuatiliaji, Waziri wangu hapa alitoa maelekezo mbalimbali hata kule Kigoma na Kasulu na baadhi ya watu katika maeneo mbalimbali walichukuliwa hatua za kinidhamu mara baada ya kubainika kwamba baadhi yao walishindwa kutimiza wajibu wao wa kikazi waliopewa. Katika taarifa mbalimbali hivi sasa, ukisoma racket news, ukiangalia kule Kinondoni, Kondoa, Kahama, Kigoma-Ujiji na maeneo mengine mbalimbali baadhi ya watu wamechukuliwa hatua. Hii ni kwa sababu tunatekeleza lile ambalo limeonekana kwamba lilikuwa ni changamoto kubwa sana katika ofisi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna kila sababu kulinda rasilimali hizi za wananchi ili ziweze kuleta tija katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja inayohusu uzembe katika kusimamia Mifumo ya Makusanyo ya Mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika hilo na ndiyo maana tumefanya kazi kubwa sana. Wakati tunaingia pale na kaka yangu Boniface Simbachawene Halmashauri zilizokuwa zinakusanya kwa kutumia mifumo ya kielekitroniki zilikuwa chini ya asilimia 30; leo hii tumefikisha karibuni asilimia 92. Hata hivyo, tumetoa maelekezo mbalimbali katika zile Halmashauri mpya ambazo hazina network hasa za umeme na tutafanya kila liwezekanalo kuhakikisha tunafikia lengo la asilimia 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini, maelekezo haya ya Kamati tuna kazi kubwa tunayoifanya katika ofisi yetu hapa na tutafika mahali pazuri na ndiyo maana leo hii Halmashauri mbalimbali zimeweza kukusanya karibuni mara mbili ya ukusanyaji wa mwanzo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nikushukuru sana, na kwa vile nina ufinyu wa muda, nipende kushukuru. Kubwa zaidi ni Kamati iliyotusaidia na naomba tukiri katika Kamati hii kwamba, ofisi yetu itajitahidi kutekeleza maelekezo yote kwa mustakabali wa nchi yetu ambao tunajua ndiyo tija wanayoitarajia wananchi wetu wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja.