Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA – MWENYEKITI KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nichukue nafasi hii kuwashukuru wachangiaji wote wa hoja hii tuliyoileta mbele yenu, Taarifa hii ya PAC, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote mliotoa maoni yenu mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, sijaambiwa napewa muda gani!
NAIBU SPIKA: Una nusu saa Mheshimiwa lakini ukitumia muda pungufu ya huo utakuwa umefanya vyema zaidi.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA – MWENYEKITI KAMATI YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Muda niliopewa nusu saa na wachangiaji walikuwa zaidi ya thelathini, nikienda kwa kila mmoja, nadhani hatutamaliza leo, kwa hiyo, nitayaweka kwa mafungu kutokana na jinsi wachangiaji walivyochanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza wachangiaji wote walitupongeza Kamati zetu zote mbili za PAC na LAAC, tunawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, wachangiaji wote niliowasikia wamekubali kwamba PAC bila kuwezeshwa hatutaweza kufanya kazi yetu kikamilifu. Kwanza kwa sababu tukifanya ripoti tu kama tunavyoletewa bila kuwa na muda wa kwenda kuhakiki tutakuwa hatuwatendei haki waliotutuma kazi hii.
Kwa hiyo, ni wazi kwamba PAC lazima tukiletewa taarifa tuweze pia kwenda kuhakiki. Kwa hiyo tunaomba kama Bunge lako likaridhia kama kweli PAC inahitaji kuongezewa pesa ili ziweze kufanya kazi yake kikamilifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, wachangiaji wengi walisema kwa msisitizo tena kwa masikitiko, kuhusu jicho letu Wabunge, CAG ambaye bajeti yake ni ndogo sana kiasi kwamba hawezi kwenda kutembelea ile miradi mbalimbali maana ukisema tu sisi tufanye kazi, PAC kazi zetu zinategemea CAG analeta nini. Kama CAG hawezi kwenda kufanya audit ina maana PAC hatuna kazi. Kwa hiyo tungeomba sana CAG bajeti yake iongezwe, vinginevyo tutajidanganya Wabunge hapa na kazi hazitakwenda. (Makofi)
Mifuko hii ya jamii imeongelewa sana kwa uchungu na wachangiaji, Waheshimiwa Wabunge mbalimbali na Waziri amejaribu kujibu. Hata hivyo, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri na kusema kwamba walikuwa wanahakiki wafanyakazi hewa na amesema PSPF wameshamaliza, swali langu ni kwamba kama wamemaliza kwa nini hawapeleki, hawarudishi yale madeni ya PSPF ili waendelee kulipa mafao ya wastaafu?
Wastaafu wengi wamelalamikia sana sehemu hii kwamba mafao yao hawalipwi. Wabunge wengi wanapigiwa simu, mimi mwenyewe napigiwa simu kutoka Jimboni kwangu. Kwa hiyo tungeomba, sana kama wamemaliza na wanaendelea na Mifuko mingine, basi angalau Mfuko huu wawape pesa zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, kuna sehemu nyingine ambazo zinahitaji msisitizo kidogo. Suala la Lugumi ni suala ambalo limetuletea matatizo sana kwenye Kamati, maswali yamekuwa mengi kabla hata haijaundwa Kamati Ndogo na bahati mbaya Kamati yetu hadidu ya rejea yetu ilikuwa inatufunga sana kwenda kuhakiki kama vile vyombo vilinunuliwa na kufungwa ndiyo tulitumwa hivyo.
Bahati mbaya hatukuwa na mkataba kwa hiyo hata kama tumekuta upungufu mengine hatuwezi kuyaingilia, lakini kibaya zaidi tulikuta vifaa vingi kweli vimelundikwa, havikufungwa sasa je, ni vya mradi huu au ni vya mradi mwingine ili tukipita vinaondolewa vinapelekwa kunakohusika? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama vilinunuliwa kwa nini havikufungwa? Kwa nini kazi haikuanza? Miaka yote hiyo tangu 2011 mpaka leo miezi mitatu vifungwe? ndiyo kazi kubwa tuliyokuwa nayo. Kamati yetu wameshindwa kujibu maswali mengine tunayokutana nayo, ni sawa na mtu amefungwa miguu na mikono halafu anaambiwa kimbia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme tu kwamba, maswali ambayo bado Kamati ilijiuliza baada ya kupata ile Taarifa ya Afisa Masuhuli 28/10; ni je, vifaa vilivyoharibika kabla havijatumika ilikuwa ni wajibu wa nani avitengeneze ndipo vifungwe? Iweje Serikali inasema inasubiri ipate hela za bajeti za mwaka 2016/2017 ndipo ivitengeneze. Hilo ni jibu ambalo hatujalipata bado. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine tulikuta vyumba ni vichafu sana, sehemu nyingi vilipowekwa hivi vyombo, je, lilikuwa ni jukumu la nani kutengeneza? Hatujui. Kwa hiyo Kamati yetu ilifanya kazi katika mazingira hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, samahani ninywe maji maana hili ni tatizo kubwa sana. Hili tatizo limeninyima usingizi, tunapigiwa simu kwamba ooh tumekatiwa chochote au tumetiwa mifukoni. Ninachotaka kusema Waheshimiwa Wabunge, kama kazi kubwa ya vifaa vile ilikuwa kuchukua picha za wahalifu pale kituoni, kuhifadhi taarifa, kwa nini hizo kazi kubwa mbili hazikufanyika miaka yote hiyo? Je, hivi vifaa vilikuwa vinafanya kazi kweli? Maana hii kazi ya kusema Mkongo wa Taifa ulikuwa haujafungwa ili kuwa na mawasiliano, hii ilikuwa stage ya mwisho, lakini ulitakiwa ukifika kituoni ukute picha, taarifa…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ili utusaidie sisi ambao si Wajumbe wa hiyo Kamati, haya maswali unayoyauliza saa hizi anayepaswa kujibu ni nani, kwa sababu maswali ya Wabunge wote hawa ni wewe Mwenyekiti ndiye unatoa ufafanuzi ndio waliyekuuliza. Sasa na wewe ukiuliza mimi sina majibu, mimi siyo mjumbe wa Kamati, kwa hiyo nataka kujua. Kwa sababu Serikali haitapewa tena nafasi tutaelekea kwenye mapendekezo mliyoleta kwenye hii ripoti yenu.
Kwa hiyo utusaidie vizuri ili baadaye Bunge hili litakapokuwa linafanya maamuzi kwenye yale mliyopendekeza humu liwe na taarifa za kutosha. Utusaidie tu hicho Mwenyekiti kwa sababu Bunge hili linawategemea ninyi. Sasa ukiuliza maswali na sisi hatuwezi tena kujijibu; inabidi utujibu wewe mwenyewe.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA – MWENYEKITI KAMATI YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na nilikuwa nihitimishe hivyo, kwamba ndiyo maana tumesema! Umeniwahi tu. Ndiyo maana tumesema hatuwezi kutoa majibu yoyote hapa kwa taarifa tuliyoletewa tarehe 28 mwezi Oktoba; wakati tunafunga taarifa yetu mpaka tutakapoweza kuhakiki kama kiti chako kilivyotuambia kwamba, tuhakiki hivi vifaa kama vimefungwa.
Kwa hiyo, ndiyo maana nilitaka kwamba hii ajenda haijafungwa, huu mjadala haujafungwa, tutakwenda kipindi kinachofuata kuhakiki, kwa hiyo tutaweza kuleta taarifa kamili; hivyo ndivyo ilikuwa nihitimishe.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nataka kulizungumzia ni suala la TIB. Labda niseme tu kwa ujumla kwamba majibu ya Mawaziri nimeyapata mengine yameniridhisha kiasi, maana kasema hizi hoja tutakutana nazo wakati CAG atakapopitia yatakuja. Hata hivyo, mahali ambapo bado pamenipa utata ni ukiangalia jibu ambalo alilitoa Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, kwamba kuna sheria ambayo inakataza mabenki kutoa taarifa za wateja wao.
Nikajiuliza kama hivi ndivyo, hivi hii taarifa ya TIB tuliletewa kwenye Kamati ili iweje? Imeletwa kwa minajili gani? Kupewa taarifa watu wamepewa hela, watu hawalipi, leo nahoji tujue zile kampuni ambazo zimepewa hela hizi, miaka hawalipi tunaambiwa hapana, hamuwezi kufanya hivyo, hawawezi kutoa siri za wateja. Hizi pesa kwanza ni za nani? TIB inawajibika kwa nani?
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema Spika amefanya makosa kutojua hiki kifungu kwa vile ameshawaandikia TIB kwamba watuletee hizo taarifa za yale mashirika sugu yanayodaiwa ambao hawajataka kuleta hizo taarifa tukaziona ili Bunge lako likatoa maagizo kwamba wachukuliwe hatua gani. Je…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, umemtaja Spika, hapo kwamba pengine hakukijua hicho kifungu; kifungu anakijua, maagizo aliyotoa haimaanishi ninyi mtaletewa hiyo taarifa moja kwa moja ndio utaratibu ambao tunautumia siku zote. Kwa hiyo si kwamba kifungu hakikujulikana ama hakukiona, anakifahamu kifungu na ametumia sheria nyingine kuitisha ile taarifa. Itakapomfikia yeye ataangalia namna bora ya kuileta kwenu kama ni taarifa ambayo inapasa kutolewa basi atawaletea. Kama ni ile ambayo haipaswi kutolewa basi hatoileta; tuendelee.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA – MWENYEKITI KAMATI YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru lakini naomba uniache kwa vile Kamati… (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, inaniwia ngumu kwa sababu kwa maelezo yako wewe ndio unatusaidia tufanye maamuzi na maamuzi lazima tufanye leo. Sasa nikisema nitapata muda wa kujibu baadaye sina na wewe ndio unayetusaidia ili tufanye maamuzi baadaye, Bunge zima hili linakutegemea wewe tu ndiyo mwenye hoja hii.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA – MWENYEKITI KAMATI YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Sitaki kubishana na kiti, lakini nimeshapata taarifa, lakini pia nilikaa nikajiuliza ambalo labda litaingia huko. Hivi wateja sugu wanapotolewa kwenye magazeti kwamba hawalipi maana yake nini? Nafikiri Waheshimiwa Wabunge, hiyo hoja tuiache, tusubiri Spika atakapotuletea ile barua na majibu yake tutajua tufanye nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, tukija kuhusu suala la na SACCOS. Mheshimiwa Mhagama amelijibu, nafikiri alikuwa anawajibu wale Waheshimiwa Wabunge waliosema kwamba NSSF isitoe mikopo kwa SACCOS; amelijibu vizuri. Kamati yetu tatizo lake lilikuwa si hilo, Kamati yetu tumesema tatizo hapa ni kwamba NSSF imeweka utaratibu wake kwamba, mkopaji au atakayekopeshwa atumie vigezo hivi. Kwanza imeweka ceiling kwamba kukopa ni kuanzia minimum ni milioni 50, maximum ni bilioni moja. Pia wakasema collateral lazima ionekane kwamba iwe ni 50% ya ile amount unayotaka kukopa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tatizo letu lilikuwa je, wale waliopewa zaidi ya bilioni moja mpaka bilioni mbili na laki tano, ni sawa sawa hiyo? Si sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kwa wale ambao wamepewa mikopo ambao hesabu zao zilikuwa hazijakaguliwa, lakini wakapewa mikopo, tukasema si sawasawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, tukasema wale ambao hawajarejesha mikopo ile, maana pesa hizi ni za kulipa mafao ya wastaafu, hivyo si sahihi na ndiyo maana sisi tumesema, tunaomba CAG aende akahakiki akafanye ile kazi ili atuletee taarifa kamili. Nani wamelipa na nani hawajalipa, nani wamefanya kinyume ili iletwe katika Bunge lako au katika Kamati tuweze kuleta katika Bunge ili lichukuliwe hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, ya kuzungumza ni mengi nimerukia kwa Manaibu, ndiyo nilikuwa nakwenda nikiangalia hizi responses zilizotoka kwa wenzangu mbalimbali ambao wamechangia. Sasa naweza nikarudi nyuma kidogo kuzungumzia mengine ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyasema; ili kwamba hata muda ukiisha tutakuwa angalau zile important areas tumezipitia.
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wengine wamezungumzia kuhusu tatizo la bandarini kuhusu zile meli, kweli wamesema kama sisi tulivyosema kwamba inakuwaje meli iingie mpaka itoke miezi 18 taarifa zake hazijajulikana, hawajalipa. Hilo limezungumzwa na sisi tuliliweka katika taarifa yetu. Kwa hiyo tumesema kwamba bandari yetu inatakiwa iangaliwe kwa ukaribu sana ili iweze kufanya kazi zake kama inavyotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la TRA na misamaha ile ya kodi, pia tumeleta katika Bunge lako ili ijulikane kwamba TRA wapewe maagizo ili wafanye kazi zao. Kuhusu ile misamaha hewa watuambie wale ambao wana misamaha hewa wamechukuliwa hatua gani? Ndiyo maana tumeleta hilo ili nalo kama Kamati yetu ilivyopendekeza tupewe majibu kwamba wamechukuliwa hatua gani kwenye misamaha ile ambayo hawakukidhi, wengine ni misamaha hewa, ifanyiwe kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mengine kwa kweli in general yamezungumzwa sana hayo ya kuhusu TR na kuelezea jinsi ambavyo Kamati yetu imependekeza kwamba TR awezeshwe ili na yeye aweze kufanya kazi yake vizuri. Tunampongeza sana kwa kweli ameisaidia sana Kamati yetu na hivyo tunaamini kwamba atakavyozidi kupewa nguvu ataweza kuendelea kufanya kazi nzuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu haya Mashirika yetu ya EWURA, SUMATRA kwa kweli tumesisitiza na Waheshimiwa Wabunge wameliongelea kwamba zile tozo wanazoleta kule Serikalini hazikubaliki, kwamba wapunguze administrative expenses zao ili waweze kutoa tozo linalokubalika Serikalini.
Mheshimiwa Naibu Spika, mengine samahani kidogo mnisamehe, maana yameingiliana na ya wenzetu, ya LAAC lakini at the end of the day tunakubali kwamba, pesa za maendeleo kwa kweli Mheshimiwa Waziri wa Fedha ni vizuri ziende kama zinavyopitishwa na Bunge, otherwise nchi yetu tutapiga kelele hapa, lakini hatutapiga hatua, zipelekwe kwa wakati. Ili zile bajeti zinazopitishwa hapa zihakikishwe kwamba zinafika kule zinakotakiwa ziende.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Kilimo amejitahidi sana kuelezea aliyoyaelezea na kuhusu ile ya wafanyakazi kwamba wanaangalia sababu nyingine na kwamba hawakusimamishwa tu kutokana na yale mahindi mabovu, kwa hiyo, tunajua kwamba tutapata taarifa kamili katika ukaguzi ujao ili tuweze kujua hatma yao imekuwa ni nini. Hayo maghala aliyoahidi naamini yatajengwa ili yafanye kazi vizuri na nguvu ya wakulima isipotee bure.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri nimejitahidi ku-cover maeneo mbalimbali na naamini kwamba eneo kubwa la hii taarifa yetu masuala yake yalikuwa yamewekwa katika mafungu hayo niliyoyataja ndiyo maana nimeya-sum up.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba kwamba Bunge lako Tukufu sasa lipokee na kukubali taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali pamoja na mapendekezo yaliyomo katika taarifa hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. Ahsante.