Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Devotha Methew Minja

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nami nichangie katika Mpango wa Serikali wa Maendeleo 2017/2018 kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nimemsikiliza sana Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake, lakini ni lazima tuseme ukweli, hali ya maisha ya wananchi vijijini ni ngumu zaidi na wanaishi kwa kula mlo mmoja na wengine wanashindwa hata kupata mlo kutokana na mazingira magumu. Zipo taarifa kutoka vyombo mbalimbali yakiwemo magazeti, mitandao kwamba Septemba, 2015 mabenki yalikuwa na faida ya shilingi trilioni 64, lakini Septemba, 2016 faida za mabenki ni shilingi trilioni nne.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii Waziri anasema uchumi umekua! Hivi kweli uchumi umekua, difference ya shilingi trilioni 60 ni gap kubwa. Serikali lazima ijitathmini, imekosea wapi? Hivi sasa mabenki yanajiendesha kwa hasara, hayatengenezi faida. Kama hayatengenezi faida, Serikali inakosa kodi na pia, hata wananchi nao wanakosa mikopo katika benki. Benki za Serikali ndiyo zipo hoi zaidi, TWB, Twiga Bancorp, TIB, ndiyo zimesinzia kabisa kwa kuwa na mtaji wa negative. Tumeshuhudia Serikali kuichukua Twiga na kuipa jukumu BOT kusimamia.
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mengi ya kujiuliza katika Serikali hii wakati kuna hali ngumu za maisha kwa wananchi, lakini Serikali imeshindwa kuzuia matumizi ya hovyo hovyo yanayogharimu fedha na kusababisha hasara kwa Taifa. Mfano halisi ni Benki ya TIB ambayo malengo yake ilikuwa ni kuendeleza kilimo, kutoa mikopo, kusaidia katika miradi ya umwagiliaji, kujenga na kuwekeza katika miradi ya kilimo, lakini zilizokuwa idara zake sasa hivi nazo zimekuwa ni benki kamili; TIB Cooperate, TIB Commercial, TABB Bank ya Kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, benki zote hizi ma-CEO wao wote wanalipwa zaidi ya shilingi milioni 20 na kama imeshuka ni baada ya Mheshimiwa Rais kutoa tamko la kupunguza mishahara. Pia, katika hili, benki zote hizi zina Wakurugenzi wanaolipwa zaidi ya shilingi milioni 10, lakini hakuna wanachofanya; kuanzia asubuhi hadi jioni wanahudumia watu wawili au watatu tu kwa siku kwa sababu, benki hizi Makao Makuu yake yapo Dar es Salaam badala ya benki hizi kuwa vijijini kuwasaidia wakulima ambao kwa zaidi ya 80% kilimo hicho kinatengeneza uchumi wa nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ugumu wa maisha unaonekana waziwazi katika uwekezaji wa viwanda; Bakhresa ameripotiwa na vyombo vya habari kuwa, zaidi ya 70% ya biashara zake zime-freeze na anatarajia kuhamishia hub zake katika nchi nyingine za Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha TTPL hivi sasa kilikuwa kinasindika zaidi ya tani 46,000, sasa hivi kiwanda hiki kinasindika tani 16,000 lakini cha kushangaza Serikali haitazami viwanda vya ndani vilivyo ndani, lakini inaangalia kujenga viwanda vipya badala ya kuangalia kwa jicho lingine viwanda hivi. Badala ya Serikali kutegemea kuanzisha viwanda vipya visivyo na tija na kuacha vya zamani vikiendelea kuteketea, lazima Serikali ikubali kuelezwa ukweli, ikae chini na kujipanga na kuweka vipaumbele vya kuendelea kutafuta mbinu za kufufua uchumi na kuwaondolea wananchi mateso ya ugumu wa maisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, priorities za Serikali kwa wananchi wake hazieleweki. Tatizo la mikopo kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu; kama uchumi umekua, kwa nini wasikopeshwe kama tunakusanya shilingi trilioni saba? Kwa nini Mfalme wa Comoro asingesaidia kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya Vyuo Vikuu? Priority ni uwanja wa mpira wa kisasa Dodoma au kujengewa Msikiti na siyo kusaidia wahanga wa Kagera ambao hawajui hatima ya maisha yao?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kama takriban zaidi ya mwaka watumishi hawajui hatma ya maisha yao. Hawajui lini zoezi hili litamalizika; hawakopesheki na mabenki, kisa uhakiki. Hii siyo sawa. Serikali ina watumishi wa umma siyo zaidi ya 5,000, uhakiki gani usioisha? Uhakiki gani unazuia watumishi kupanda madaraja na kushindwa kupata haki yao ya msingi ya kupata mikopo?