Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza niseme tu kwamba mimi ni Mjumbe wa Kamati hii ya Utawala na Serikali za Mitaa, kwa hiyo naunga mkono maoni yote ambayo yamewasilishwa na Kamati yangu hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipata fursa ya kushiriki Kamati kwenye ziara na kuangalia miradi na kwenye mawasilisho mbalimbali ambayo yalifanyika kwenye Kamati yetu, yapo maeneo muhimu ambayo nataka kuchangia hapa. Jambo la kwanza; tulizungumza hii Kamati inahusika na mambo ya utawala na tukaangalia eneo la kero kwa wananchi, rushwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, rushwa imekuwa ni kubwa ingawa upande wa Serikali ukizungumza nao watakwambia rushwa imepungua kwelikweli, si kweli. Jambo hili limechagizwa sana na kauli ya Mheshimiwa Rais kwamba maaskari wanaruhusiwa kuchukua rushwa ndogondogo, 5,000 hela ya sabuni na kubrashia viatu. Bahati mbaya sana kwa sababu ya hofu na woga uliopo hakuna mtu ambaye alienda front kumshauri ama kubadilisha ile kauli na imekuwa ni kero kwa wananchi na hasa vijana wa bodaboda ambao wanajitafutia maisha katika jua kali, wanaombwa sana hizi fedha mnaita ndogondogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni maoni yangu kwamba ni muhimu upande wa Serikali wakaliangalia jambo hili upya na ni muhimu kuangalia pia kauli za viongozi wetu na hasa Mheshimiwa Rais. Haiwezekani kiongozi ambaye ameapa kuitii Katiba ya nchi na sheria na kanuni anasimama hadharani bila hofu wala woga anasema askari wakipewa sh. 5,000 ya kiwi ya viatu ni sawasawa kabisa na anasema ni hela ya kiwi, lakini hili jambo limekuwa ni kero kwa wananchi wetu ambao kimsingi maisha ni magumu na kipato ni kidogo na unapokosa sh. 5,000 inaweza kupelekea hata kung‟oa matairi na mambo mengine chungu nzima ambayo yanafanyika, hilo ni eneo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo tuliliona ni eneo la TASAF. Mimi ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, kwa hiyo nafahamu vizuri namna ambavyo watu wetu wamepata msaada mkubwa kupitia fedha hizi na ni mpango mzuri pamoja na kwamba zipo changamoto mbalimbali ambazo inabidi zifanyiwe kazi kwa maana ya kuboresha ili hii fedha iendelee kupatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia wapo wananchi wengi sana ambao hawana uwezo na michakato haikuwapitia, wakazikosa. Kwa hiyo, niishauri Serikali, ni muhimu yale maeneo ambayo watu walikuwa wanakidhi vigezo, wana uwezo mdogo na hawakupata zile fedha, basi maeneo hayo yaangaliwe upya ili watu hao waweze kupata msaada wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni yangu ni kwamba ni muhimu hizi fedha pamoja na kuwapa watu wetu ili kuwasaidia wapo wachache, kama tulipokwenda Zanzibar, Pemba na Unguja ikaonekana baadhi ya maeneo ya Tanzania Bara yamefanya hivyo, wale wazazi wanapewa zile fedha wanatumia wanabakisha kidogo wanaweka miradi midogomidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri tuwekeze kwenye miradi midogo midogo kwa sababu mpango huu sio mpango wa miaka yote, maisha yao yote, kama wakijifunza ku-save kidogo wanatumia na wakaanzisha miradi midogomidogo hata akili zao zinachangamka katika kujipangia mapato na matumizi yao. Kwa hiyo tungependekeza jambo hili muhimu likachukuliwa kwa uzito. Wawezeshwe fedha lakini pia waelekezwe namna ya kuwekeza kwenye miradi midogo midogo ili iwasaidie huko baadaye. Hata kama fungu hili likiondolewa watakuwa wamejipanga vizuri juu ya namna ya kupata huduma kwa sababu lengo ni kuwasaidia hapa walipo na waweze kujiinua kimaisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli wamepata msaada, wengine wamesomesha watoto, wengine wamejenga hata vibanda hata kama ni vibovu lakini imesaidia kwa kweli. Kwa hiyo, ile kauli ambayo inaonekana kwamba kuna taarifa huu mpango haujasaidia; leo wale wazazi ambao hawana uwezo, watu wetu wale, badala ya kwenda kupanga foleni kwa Diwani au kwa Mbunge kuomba hela ndogondogo wanakwenda kupanga foleni kwa Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo cha muhimu hapa fedha ni muhimu, ni kuboresha mazingira ambayo yana changamoto mbalimbali na uwazi uwepo, wale wahusika wapewe, hilo ndilo jambo la msingi sana. Mtu ambaye anashauri kwamba hii fedha iondolewe, kwa kweli huyu mtu ni wa kulaani sana, hawatakii mema watu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la watumishi hewa. Ni kweli kwamba Serikali imechukua hatua ya kuangalia watumishi hewa, lakini jambo hili linachukua muda mrefu sana. Wapo watu ambao maslahi yao yamezuiliwa kwa sababu ya hoja ya watumishi hewa na hasa ajira mpya kwa vijana wetu. Sasa ni muhimu jambo hili kuwe na deadline, kwamba mnafanya kwa muda wa mwezi mmoja, miwili, mitatu au minne, jambo limalizike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu watumishi hewa; kwanza watu wanataka kujua nani ni mtumishi hewa ajulikane na hawa ndio wanaotakiwa wawajibishwe; wale waliopokea fedha na wale viongozi ambao ni wa Utumishi waliotengeneza miundombinu ya kupata watumishi hewa, wasiwawajibishe watumishi wasiokuwemo. Kwa sababu kama kuna fedha inalipwa kutoka kwenye akaunti, wale wakubwa wawajibishwe. Hata hivyo, jambo hili liishe ili watu wetu wapate ajira na waweze kutumikia Watanzania kwa ubora zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la utawala bora. Leo asubuhi nilisikitika sana Mheshimiwa Simbachawene. Kwanza anajua hapa karibuni umetengenezwa mgogoro mkubwa sana Serikali za Mitaa. Lilizuka jambo la mihuri hapa mpaka wenyeviti wenzangu wa mitaa wakafikia hatua ya kuandamana, kuunda Kamati mbalimbali na kuanza kufanya zile kazi. Sasa hapa ni muhimu tukajua, zipo kazi za Wenyeviti wa Mitaa, zielekezwe vizuri. Mtendaji anapoajiriwa anajua kazi zake na Wenyeviti wa Mitaa waelekezwe. Sasa kutujumlisha kwamba wote tunapiga maeneo ya umma si kweli, mimi ni Mwenyekiti wa Mtaa, sina kesi ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni muhimu maelekezo yaende kwamba kama kuna Mwenyekiti ambaye kwa kweli ametumia nafasi yake vibaya huyo awajibishwe. Wale ambao wamepewa, kwa mfano Mheshimiwa Waziri ukiulizwa tangu uchaguzi umefanyika mwaka 2014 ni mpango gani mmefanya kutoa semina kwa Wenyeviti wa Mitaa, Madiwani na hata watendaji? Mtu amekuja hapa Hombolo kapata mafunzo yake, kapata ajira akifanya makosa sio fault yake ni fault ya Wizara, kwa hiyo naomba Wizara itimize wajibu wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, nimesikitika sana leo asubuhi, sisi tunasema Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wanajiita Marais; wewe umeunga mkono hiyo hoja kama ni kweli eti kwa sababu madaraka yanashuka kutoka kwa Mheshimiwa Rais, kwa hiyo nchi hii kila mtu ni Mheshimiwa Rais! Sisi tulichouliza ni kwamba, Wakuu wa Wilaya wanahujumu mpaka Waheshimiwa Wabunge, hatuheshimiani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amefanya ziara Dar es Salaam pale Ukonga, kwa heshima nimetoka nyumbani kwangu nimekwenda kwenye eneo lile, nikakuta, Mkuu wa Mkoa anatukana watumishi kwamba ninyi ni mizigo, ninyi ni misumari. Mwanamke, yule mama wa Kinondoni, ninyi wanawake mnasema hapa wanawake wapewe fursa wafanye kazi! Afisa Utumishi wa Kinondoni Makonda anamwambia wewe ni mzigo, hivi nani amekuweka hapa! Toka hapa potea pale mbele!
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkuu wa Mkoa, kwenye public, kwenye mkutano wa hadhara, yule mama ameshindwa hata kutembea miguu imekuwa mizito, hayo ndiyo mambo tunayokataa hapa. Mkuu wa Mkoa yupo kwenye mkutano eneo la mgogoro, limeunda Kamati pale, Diwani amefanya kazi yake, Afisa Utumishi amekwenda, Afisa Mipango ya Maendeleo wa eneo lile, Mkuu wa Mkoa anakuja pale kwa sababu ana polisi anamwambia Diwani apate fursa ya kutoa taarifa, mimi hata kusalimia alinizuia, akasema hiki kikao ni cha Mkuu wa Mkoa, halafu tuheshimiane namna gani? Hayo ndiyo mambo ya msingi ya kuzungumza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani shule zinafelisha; mwaka jana Mkuu wa Mkoa wa Simiyu ameagiza mkoa mzima, eti wakuu wa shule amewatumbua, halafu mnataka matokeo yawe mazuri yataanzia wapi, hatuheshimiani kwenye kazi. Kwa nini Mkuu wa Mkoa asione kuna shida? Tumesoma ile sheria vizuri, kama kuna shida, kama kuna mkuu ninayempongeza sana ni Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, nilimwona kwenye TV, naomba mumpigie makofi basi hata huyu amefanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu amekwenda anajadili matokeo ya form four, ameita watumishi kwenye idara husika, anasema tulifanya kikao tukasema atakayezembea eneo lake atawajibishwa, anasema naomba idara husika ya elimu iwajibishe wahusika, simple. Kwa hiyo, ukishasema hivyo watafanya utafiti, watafanya enquiry fulani, itakuja taarifa anayehusika na mambo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, haya mambo ndiyo tunataka yafanyike. Hatutaki watu wazembe ila hatutaki watu waonewe tunataka mtu akiwajibishwa; na Waziri ni Mwanasheria wa eneo hili, wote wawili, Waziri wa Utumishi na Waziri wa TAMISEMI na nawaheshimu sana ndugu zangu, lakini tunataka utaratibu tu. Hivi Mkuu wa Mkoa kweli ni rais kwenye mkoa wake! Ni rais kwenye wilaya yake! Kwa hiyo kuna vitu ambavyo mnadanganya watu hapa, naomba tuheshimu hiki chombo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachosema sisi ni kwamba hatupingi kila kitu, yapo mambo yanafanyika mazuri tunaunga mkono. Tunapiga kelele sana kwa mambo mabaya, kukatisha watu tamaa na matumizi mabaya ya madaraka. Hivi inawezekana Mheshimiwa DC amekwenda kwenye mkutano, anamwambia Diwani kamata weka ndani halafu tupige makofi? Ni kiongozi mwenzake halafu anataka ampe ushirikiano, hizo taarifa anazipataje na hao ni watu ambao kwa kweli wameletwa kwenye maeneo yale na kuna mtu amepigiwa kura na watu wake, kwa hiyo mnajenga chuki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Nkamia amesema hapa leo asubuhi, kwamba inawezekanaje DC anatukana wananchi halafu huyu anasema eti ndiyo Rais wa eneo lile…
MWENYEKITI: Ahsante.