Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipia nafasi hii kwa asubuhi ya leo na mimi niweze kuchangia katika Mpango huu wa Maendeleo wa Miaka Mitano.
Mheshimimwa Naibu Spika, nianze tu kwa kuipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri iliyofanya katika masuala mazima ya huduma za jamii lakini suala la miundombinu, kilimo na mengine mengi likiwemo kubwa la umeme vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango huu ambao umewasilishwa tulipokuwa Dar es Salaam na leo Mheshimiwa Waziri hapa, maeneo mengi yameguswa lakini barabara nyingi zilishatengenezwa na sasa ni wakati mzuri katika miaka mitano hii kuangalia maeneo yale machache ambayo bado Serikali haijayafikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kukumbusha kwamba kuna barabara ambazo zimekuwa zikisemewa sana na viongozi wetu wakuu, Rais wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin Mkapa, lakini Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na hadi sasa Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli wa hapa kazi na juhudi zake zimeonekana katika barabara ya kutoka Mkiwa, Rungwa hadi Makongorosi. Serikali katika Mpango wa mwaka huu imeonyesha kwamba inajenga barabara kutoka Chunya hadi Makongolosi lakini niombe sana katika mipango endelevu barabara hii katika kipindi hiki cha miaka mitano ionwe na ikiwezekana iishe. wananchi wa Majimbo yanayopitiwa na hii barabara likiwemo la Mheshimiwa Kakunda na Jimbo langu mimi lakini ni barabara kubwa inayounganisha Mkoa wa Singida na Mkoa wa Mbeya kupitia Mkoa wa Tabora. Kumekuwa na ahadi nyingi, sasa si vibaya safari hii basi na sisi tukaonwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna ahadi nyingine ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alikuwa afungue barabara ya kutoka Mkoa wa Singida inapita katika Wilaya ya Chemba inakwenda Kiteto na hadi Handeni. Barabara hii ina fursa nyingi za wajasiriamali, maeneo ya wakulima wakubwa wa nchi hii wanaolisha Mikoa ya Dar es Salaam na hata Tanga wapo maeneo yale lakini sisi wakulima wa Mkoa wa Singida barabara ile kama itafunguliwa itakuwa na tija sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kilimo, nimpongeze sana Waziri wa Kilimo, kijana wetu, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba alipiga kazi sana wakati wa uchaguzi, alitembea nchi nzima na sasa juhudi zake zinaonekana. Nataka nimkumbushe tu kitu kidogo kwamba wafugaji wa maeneo yetu hususan katika Jimbo la Manyoni Magharibi wana shida kidogo ya maeneo ya malisho. Jimbo langu sehemu kubwa ni Hifadhi ya Rungwa Muhesi Game Reserve ambayo ina eneo kubwa. Kuna wafugaji wanaopakana na maeneo yale na kwa sababu maeneo yale sasa hivi wafugaji wanaotoka Mkoa wa Shinyanga wamekuwa rafiki zetu na wamekuwa wengi pale na mifugo imekuwa mingi, si vibaya tukaliona hili katika mipango yetu ijayo tukawapa fursa nao malisho kidogo yakawa yamekaa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Nishati na timu yake, Mheshimiwa Kalemani yuko hapa, amekuwa msikivu sana. Amenipa maeneo mengi, anafanya jitihada za kunipatia za umeme lakini naomba utekelezaji uwe wa haraka. Wataalam wamefika ila sijaona vizuri kwenye randama ya bajeti ya Mpango huu kama wamelizingatia hilo lakini naamini ananisikia na atalifanyia kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto zilizopo katika Jimbo langu ni pamoja na shida kubwa ya maji. Sisi mikoa ya katikati hatuna mito lazima tuchimbe maji. Katika Mji Mdogo wa Itigi kuna visima vikubwa sana vya maji na vizuri vimechimbwa na Serikali katika bajeti hii inayoisha. Niombe katika Mpango ujao wa Miaka Mitano basi tuwekewe miuondombinu ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la afya, tunazo changamoto, kuna zahanati zilijengwa na TASAF ambazo zina shida ya Waganga Wasaidizi ambazo ni pamoja na Gurungu, Njirii, Ipande, Kitopeni, Ukimbu na Kintanula. Sasa wakiziangalia hizi kwa macho mawili naamini Serikali ya hapa kazi hawa wanaolaumu baadaye wataacha kulaumu kwa sababu Serikali imefika kila mahali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze juhudi za Mheshimiwa Waziri wa Viwanda aliposema kwamba nchi hii itakuwa ya viwanda. Moja ya eneo ambalo nitapenda kuona juhudi za Serikali zinachukuliwa ni pamoja na kuwa na kiwanda kwa Mkoa wa Singida na mikoa yote ya katikati. Jimbo langu lina malighafi nyingi ya gypsum itakuwa vizuri kutengeneza ajira kwa ajili ya vijana wetu kwa sisi kupatiwa kiwanda cha malighafi inayopatikana pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la maliasili, kumekuwa na changamoto nyingi, hatujafika mahali pazuri kuvuna maliasili zetu. Tumekuwa tunaweka vikwazo matokeo yake kunakuwa na wezi wa mbao misituni kwa sababu hatuko rafiki sana katika kuhakikisha zile mali ambazo zime-mature kwa ajili ya uvunaji. Tumekuwa tuna-ban sana lakini pia tumekuwa na tatizo kubwa la uwekezaji katika kuhakikisha kwamba kuni hazitumiki nyumbani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaiomba Serikali ije na mpango mzuri wa gesi. Nchi yetu imegundua gesi, sasa gesi imefika Dar es Salaam si vibaya kukawa na mpango wa gesi ile iende Mwanza ipite Mkoa wa Singida na sisi tunufaike kama wananchi ambao ni walipa kodi wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mitamba alizungumza Mheshimiwa Naibu Waziri lakini bado hata mimi nasema bei zile ni kubwa si vibaya zikaboreshwa ili baadaye na wafugaji wetu nao wakanufaika sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana.