Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Richard Phillip Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru kwa hii nafasi. Nami kwanza nianze kuunga mkono hoja ya Kamati hii ambayo report yake ni nzuri kweli kweli na imesheheni mambo mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti naomba nianze kwa kuchangia upande wa Mfuko wa kusaidia Kaya masikini (TASAF). Mfuko huu tunamaoni kwamba uendelee kuwepo. Uendelee kuwepo kwa misingi kwamba sisi ni Wabunge, tumezunguka, tumefanya ziara maeneo mbalimbali, wazee bado wanalilia uwepo wa pension. Sasa kama wazee tu wanalilia walipwe pension kwa ajili ya kuwasidia sasa je, hizi kaya masikini kwanini tuziondoe? Kwa hiyo tunaomba sana Serikali huu mfuko uendelee kuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la msingi ni kuboresha, katika kupitia majina kila baada ya miaka mitatu ikibidi iwe miaka miwili, kwa sababu kumekuwa na changamoto za maeneo mbalimbali, Watendaji wetu kule chini wanakuwa wanachakachua majina wanaweka watu ambao hawana sifa za kufaidika na huu mfuko. Katika kuboresha, badala tu ya kuangalia kutoa fedha, tuone jinsi gani tutoe fedha kiasi na tutoe hata shughuli ndogondogo kama za ufugaji wa aina mbalimbali wa ndege au wanyama ili ziweze kuwaongezea kipato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili lililozungumzwa kwenye ripoti ya Kamati ni kuhusu fomu za maadili, Watumishi wengi wa Serikali kwa mujibu wa sheria tunatakiwa tujaze fomu za maadili, lakini kwenye ripoti ya Kamati humu wamehimiza kuhusu TEHAMA. Serikali iangalie jinsi gani TEHAMA iweze kutumika ili tuweze kupunguza gharama na kuwa na ufanisi pia kwenda na wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, uwasilishaji wa fomu za maadili Wabunge wengi waliweza kusafiri tena kurudi kuzileta fomu kwenye Kanda, Watumishi wa Serikali wamesafiri kwenda kwenye Kanda kuwasilisha fomu, ilikuwa ni gharama magari ya Serikali yametumika na fedha za Serikali. Kwa hiyo, tuombe sasa tupate mfumo wa kuwasilisha hizi ripoti kimtandao – web based reporting. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nichangie kuhusu utawala bora. Kweli Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wameteuliwa na Mheshimiwa Rais katika kutekeleza na kumsaidia, lakini tuombe wajaribu kuangalia ile sheria inayowaruhusu kutoa amri mbalimbali kama vile amri za kukamata. Ni makosa gani ambayo yanapaswa kuingia kwenye hiyo amri ya masaa 48 ya kuweza kukamatwa. Kwa hiyo, yaangaliwe ni makosa ya aina gani, kwa sababu sheria ilitungwa na wana mamlaka hiyo ya kuitumia basi waende kwenye Kanuni na kuangalia ni makosa ya aina gani, hatubezi utendaji wao bali tunaunga mkono wanavyofanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili litakuwa sambamba pia na masuala ya kiutawala kwa upande wa utumishi. Tumesikia kauli mbalimbali, Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa anamshusha mtu cheo au anamfukuza kazi badala ya kufuata taratibu za kiutumishi katika kuchukua hatua hizo. Kwa hiyo, tuombe sana Serikali wayaangalie makosa ambayo yamekwishafanyika kwa kipindi hiki na Waziri husika afanye utaratibu wa kutoa barua au mwongozo ambao utaweza kusaidia utendaji wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo tunapenda sana katika utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ni mfuko ule wa kuwakopesha vijana na akinamama kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri zetu. Ufuatiliaji umekuwa ni hafifu sana, OC ziende kwa wakati ili mapato yetu ya ndani yaweze kutengwa. Inatakiwa asilimia 60 iende kwenye miradi ya mendeleo. Ndani ya asilimia 60, asilimia 10 ni kwa ajili ya vijana na akinamama. Sasa Halmashauri nyingi mpaka sasa hivi ukiwauliza miezi hii sita wametenga kiasi gani utakuta hakuna Halmashauri ambayo imeshatenga zaidi ya hata asilimia 20.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba OC ziende ili mapato ya ndani yote yasitumike kwenye shughuli za kila siku na vijana wetu na akinamama waweze kukopeshwa fedha na ndiyo utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu Tume ya Utumishi ya Walimu. Tume hii imeanzishwa na kwa mujibu wa Kamati kuna changamoto sana kwenye upande wa bajeti na baadhi ya sheria na kanuni zinazoongoza. Tujaribu kuangalia kwanza mfumo. Tume hii sasa hivi inavyofanya kazi kwenye Wilaya kuna zile Kamati za kinidhamu, kwa hiyo kama Wilaya ina Halmashauri mbili au tatu sasa ushughulikiaji wa ile Kamati unakuwa ni mgumu kidogo kwa sababu ya composition ya Wajumbe wa ile Kamati wanatoka sehemu mbalimbali na ruzuku fedha zinakuwa hazipatikani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeshauri mfumo huu uende kihalmashauri na Mkurugenzi azifadhili hizi Kamati za nidhamu za Walimu kwa ajili ya ufanyaji kazi. Kama zitakutana mara tatu kwa mwaka au mara mbili ili kuwa na mapitio kabla ya bajeti na baada ya bajeti na Walimu wanapata promotion mbalimbali. Pia coordination ndiyo itaenda vizuri kati ya TAMISEMI na Utumishi kuhusu upandaji wa madaraja ya Walimu, mambo ya kinidhamu ndiyo yataenda vizuri. Kwa hiyo, tunaomba Tume hii Sheria ibadilishwe ambayo itakuwa inaweza kuongoza katika kuhakikisha kwamba Walimu wetu, maslahi yao na kesi zao ambazo zimekuwa ni nyingi na ndiyo ajira kubwa ya Halmashauri au upande wa TAMISEMI idadi kubwa ni Walimu. Kwa hiyo, ni muhimu sana tuweze kubadilisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho tungeomba sasa upande wa Serikali kuhakikisha kwamba Halmashauri zetu zinalenga kwenye kufuatilia promotion au madaraja ya Walimu na mishahara yao ibadilishwe na iendane na bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja ya Kamati hii. Ahsante sana.