Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia machache juu ya hoja hizi za taarifa za Kamati, Kamati ya Katiba pamoja na TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na taarifa ya Kamati ya Katiba. Napenda tu kuongelea kuhusu utawala bora na nitajielekeza katika chaguzi zinazoendelea katika nchi yetu. Kuchagua viongozi na uchaguzi ukiwa huru na haki ni sehemu mojawapo ya kupanga viongozi na njia mojawapo ya kulea demokrasia katika nchi yoyote iliyopo duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, magomvi mengi ambayo yanatokea katika nchi tunazozisikia duniani zilizo nyingi inatokana na uchaguzi usio huru na haki na dhuluma zinazotokea katika uchaguzi, manyanyaso yanayotokana na uchaguzi, wakati mwingine kulazimika kutangaza matokeo ambayo siyo halali na hufanya wananchi wachukie na baadaye wanaamua kuchukua hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema haya kwa sababu nimeshiriki chaguzi hizi za juzi ambazo zimemalizika za Madiwani. Tulikuwa na Kata moja tu katika mkoa wetu, Kata ya Kimwani na nilishiriki kikamilifu mpaka mwisho. Mambo niliyoyaona napenda niyaseme hapa, kwamba sasa hivi uchaguzi katika nchi yetu umegeuka, Jeshi la Polisi limekuwa Chama cha Siasa na wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matendo niliyoyaona, bunduki, mabomu na vitisho ni dhahiri kwamba Watanzania hawawezi kuingia katika uchaguzi wakijiamini na matokeo ninayoyaona watu watakuja kuchoka na haya mambo ambayo yanafanywa na Jeshi la Polisi. Ukiisoma vizuri, mimi hakuna mahali ambapo nimeona katika Sheria ya Uchaguzi ambapo Askari wanahusika kwenda na mabomu, ninachojua wanakwenda kulinda vituo, wako Mgambo, wako Polisi, wanakwenda kulinda vituo. Kipindi hiki nimeshuhudia Polisi wanakuja na mabomu wanazuia wananchi kutoka vijijini kwenda kupiga kura.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wako hapa vijana wa bodaboda ambao unakuta wakati mwingine wale wapigakura wanatoka mbali mno na vituo, kutokana na jiografia mbalimbali jinsi nchi yetu ilivyo. Mtu analipa bodaboda kwenda kupiga kura Polisi wanamzuia njiani yule bodaboda kumpeleka huyo mtu kwenda kupiga kura.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo machafu ambayo nimeyaona na kwa kweli sisi Waheshimiwa Wabunge tunapaswa kukemea mambo haya. Uchaguzi ni jambo huru, uchaguzi ni watu wanakwenda kuchagua viongozi wao, tunajua katika nchi yetu kwamba tunakwenda kwa mfumo wa Vyama Vingi, ni lazima vyama vifanye ushindani na hata kiongozi atakayepatikana ajue kwamba hicho cheo amekifanyia kazi. Hakuna sababu ya kufikishana tunakofikishana, nina wasiwasi kwamba sasa kadri tunavyokwenda tunalea vijana wetu katika kuleta chuki na baadaye huko mbele yanaweza kutokea mambo ambayo tunayaona katika nchi hizi za jirani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimeshuhudia Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, ma-OCD, yaani kwenye Kata moja tu yenye wapigakura 8,000, lakini Serikali nzima ipo pale na watu wakishasikia kwamba Mkuu wa Mkoa yuko pale, Mkuu wa Wilaya yuko pale, kuna watu wengine hawakuzoea hayo na Watanzania walio wengi wako tofauti huwezi ukalinganisha na Wakenya, hawapendi mambo ya ugomvi. Kwa hiyo, unapokwenda kuwanyanyasa watu mwishowe wanaona hawana haja ya kwenda kupiga kura, matokeo yake watu wanashindwa kupata haki yao. Naomba Serikali iyatazame na hata Tume ya Uchaguzi iyatazame ili tuweze kupata viongozi wetu wazuri na tuendelee kulea demokrasia katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuliongelea ni kauli ambazo zinatolewa na viongozi wa juu ambazo mimi naziita kama kauli za mzaha, zinaweza kutolewa na Wakuu wa Mikoa na Wilaya, lakini zinapotolewa na viongozi wetu wa juu kwa kweli zinashangaza, siwezi kusema zinatisha au zinashangaza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano; Mkuu wa Nchi alipotembelea Mkoa wa Kagera na mnajua Mkoa wa Kagera ulikumbwa na tetemeko, katika mkutano huo alikuwepo Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Wilfred Lwakatare ambaye ni Mbunge wa Bukoba Mjini, alipewa nafasi ya kuongea na nafasi hiyo aliitumia kutoa mawazo kwa niaba ya wananchi, mawazo aliyoyatoa ndiyo mawazo tunayopaswa kutoa sisi Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapotoa mawazo lazima Serikali ione kwamba huyu mtu ni mwakilishi wa wananchi, aliiomba Serikali na alishasema hata ndani ya Bunge hili kwamba tungependa katika Mkoa wa Kagera, tunajua hamuwezi kujengea watu wote, lakini Serikali inaweza ikatoa ruzuku katika viwanda vya mabati, viwanda vya nondo na viwanda vya saruji ili wananchi wa kule waweze kupata vifaa kwa bei ndogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo siyo la ajabu, wakati Mamlaka ya Kuuendeleza Mji wa Dodoma (CDA) enzi zile za Awamu ya Kwanza, jambo hili limewahi kutokea, vifaa vilijengwa na ikapigwa chata kuonesha kwamba ni ofa ya kuja kutengeneza Mji wa hapa Dodoma. Kitu hicho kinaweza kufanyika hata Mkoa wa Kagera na hata mahali pengine ambapo watu wanaathirika namna hiyo. Majibu yaliyotolewa na viongozi wa juu – maana yake hatuwezi kutamka majina, ukitamka hapa utakutwa hapo mlangoni, niseme Serikali, nikitamka hapa Askari wanaweza kunisubiria hapo maana yake na wenyewe mmeshawafanya wamekuwa wanasiasa, alisema anamwambia Mheshimiwa Lwakatare akajenge kiwanda!
Waheshimiwa Wabunge ninyi mtajenga viwanda? Mimi nimekua, sasa hivi nina umri mkubwa wa kutosha tumejifunza kuhusu madini ya tin yaliyopo Kyerwa Karagwe tangu nikiwa mtoto wa miaka nane tu niko darasa la tatu, sijawahi kuona Mbunge ambaye anajenga kiwanda pale na wamekuwepo Wabunge mbalimbali pale. Kwa hiyo, kiongozi wa nchi anapotamka maneno ya namna hii, mimi nayaita ni maneno ya mzaha lakini pia inatonesha vidonda vya watu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kusema Mheshimiwa Mbunge akileta mawazo, hata kama anatoka opposition alichaguliwa! huwezi kumwambia basi nenda kajenge kiwanda hata mimi nitakusaidia, Mheshimiwa Lwakatare hela ya kujenga kiwanda ataitoa wapi, wengine wananiambaia eti yeye alijenga wapi, Chato hakuna kiwanda cha mabati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nayasema haya, hatuwezi kuacha kusema tutakuwa waoga mpaka lini? Maana yake Rais wa Nchi au Kiongozi Mkuu wa Nchi au hata kama ni Waziri ni dhamana anawakilisha watu wake na Mkoa wa Kagera hatupendi sana kuomba omba na mara nyingi hamleti msaada kule, miaka nenda rudi hamjatuletea misaada. Tuna uwezo wa kujitegemea, lakini hii imetokea na tetemeko tunajua siyo la Chama, ni maafa ya nchi lakini wananchi hawakupewa kauli za kuwastahi waweze kukaa vizuri, wakitulizwa wanajua kwamba Rais wao amewaambia maneno mazuri. Kwa hiyo, ningependa Viongozi kauli hizi sizifurahii na watu wengine katika Mkoa wa Kagera kusema ukweli hawakufurahishwa na kauli hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalize kwa kuongelea kuhusu suala la TAMISEMI kidogo, labda niongelee kuhusu elimu tu. Kwamba elimu ni bure sawa, inatolewa au labda ni ya malipo lakini niongelee Bukoba Vijijini tu ambako nafanyia kazi na Mheshimiwa Rweikiza nafikiri na yeye ataniunga mkono pale. Mnakumbuka huku nyuma kuna Mkuu wa Wilaya moja anaitwa Mnari, amewahi kuwapiga Walimu wa Bukoba Vijijini viboko. Pamoja na kuwapiga au asiwapige, mazingira ya kule siyo mazuri na pia hakuna Walimu. Katika kipindi cha bajeti hapa niliomba kwamba mtusaidie Walimu Bukoba Vijijini. Mwaka huu tumepewa zawadi ya Kinyago. Pale Mkoani wanatoa vikaragosi vile, tumepewa hicho, tunaomba Mheshimiwa Simbachawene atusaidie, atupe Walimu Bukoba Vijijini. Hilo ndilo ombi langu.