Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. HASNA S.K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba na mimi nichangie kwenye Kamati hizi mbili ambazo zimewasilishwa leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wangu, nitazungumzia sana suala la watumishi. Kwenye Halmashauri yetu ya Uvinza tuna tatizo kubwa sana la watumishi. Hivi karibuni tulipokea barua kutoka Wizara ya TAMISEMI ikimtaka Mkurugenzi kuwasimamisha kazi watumishi wote ambao walikuwa wanafanya kazi kama vibarua ili wakae pembeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mbunge mwenzangu hapa kutoka Lushoto alikuwa anatolea mfano kwamba wao Halmashauri yao wanatumia shilingi milioni 28 kwenye own source kwa ajili ya kuwalipa watumishi ambao hawana vibali. Sasa nikawa najiuliza maswali, kwa nini Halmashauri zingine ziruhusiwe kuendelea kufanya kazi na wale watumishi ambao hawana vibali na Halmashauri zingine tuletewe barua ya kuwasimamisha watumishi ambao wameshafanya kazi zaidi ya miaka minne. Zaidi ya miaka minne mtu anafanya kazi, anaitumikia Serikali halafu ghafla tunawaweka pembeni tunasema kwamba ninyi ni vibarua hamna ajira rasmi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona hili nilizungumzie kwa sababu Halmashauri hizi mpya zilizoanzishwa 2012 zina uhaba mkubwa sana wa watumishi. Kwa hiyo, tutaomba Mheshimiwa Waziri husika, wa Utumishi na Waziri wa TAMISEMI waone namna ya kuliangalia hili. Tunaweza tukaendelea kutumia own source yetu kama ambavyo wenzetu wa Lushoto wanavyotumia ili tuwalipe hawa watumishi waendelee kutekeleza majukumu ya Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo pia kubwa la watendaji wa vijiji na leo kupitia wenzangu waliochangia nimejifunza kitu. Kwenye Halmashauri ya Uvinza Watendaji wa Vijiji 75% ni Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari na Walimu Wakuu wa Shule za Msingi. Leo tunasema watoto wanafeli kwenye shule za msingi, leo tunasema watoto wamefeli, matokeo sio mazuri kidato cha nne. Itakosaje kuwa matokeo mabaya wakati Walimu Wakuu hao hao kwenye baadhi ya Halmashauri ndiyo tunawatumia kama Makaimu Watendaji wa Kata na Makaimu Watendaji wa Vijiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe tu Wizara husika, Wizara ya TAMISEMI iliangalie hili ili ikitoa waraka, natambua kwamba kuna waraka mbalimbali huwa zinatolewa Serikalini, ili wakae chini wachunguze ni Halmashauri zipi zinazotumia Walimu Wakuu wa shule kama Watendaji wa Vijiji na Halmashauri zipi zinazotumia Watendaji wa Vijiji kupitia jamii zetu. Kwa nini tusitumie tu jamii? Kwa sababu kama kwenye kijiji mimi ninavyofahamu unaitishwa Mkutano Mkuu wa Kijiji wanaulizana nani miongoni mwetu anastahili kukaimu nafasi ya Mtendaji wa Kijiji? Then wanapiga kura yule aliyechaguliwa anakaimu kuliko kama sisi wengine Walimu hao hao ni wachache, hatuna watumishi lakini na hao hao wanafanya na majukumu ya kijiji. Kwa hiyo, niliona hili nilizungumzie kwa namna hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ni uhaba wa watumishi kwenye sekta ya elimu na afya. Halmashauri yetu tumejitahidi sana kuhamasisha, tuna vijiji 61, tunazo zahanati 33, lakini tumehamasisha hadi sasa tuna takriban zahanati 15 zimejengwa lakini hakuna watumishi. Kwa hiyo, unakuta tuna zahanati ambazo tayari tungeweza kuzianzisha lakini kwa uhaba wa watumishi wa afya tunashindwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu waliochangia kusema kwamba zoezi la uhakiki wa watumishi limeshachukua takriban mwaka mzima, limekwenda vizuri na sisi tunampongeza sana Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya Utumishi, lakini sasa waone ni namna gani wanaweza wakatoa ajira mpya ili sasa vijana wetu waliomaliza vyuo mbalimbali waajiriwe, huu uhaba wa watumishi kwenye sekta za afya, elimu na kilimo uweze kuondoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ambalo nataka kulizungumzia ni ugumu wa miundombinu na mazingira katika Halmashauri mpya. Na-declare interest kwamba nimekuwa DC siku za nyuma, tulikuwa tunaona kutoka Wizara ya TAMISEMI, wale wanaoshughulika na masuala ya Local Government wanatembelea zile Halmashauri mpya kuangalia changamoto ambazo wanazo na kuona ni jinsi gani wazisaidie ili ziweze kusonga mbele. Sasa Halmashauri ya Uvinza, tunatumia majengo yaliyoachwa na kambi zile za wakimbizi. Takriban four years tuko pale! Tunaishukuru Serikali juzi kupitia hii bajeti tunayomaliza 2016/2017 tumepata shilingi bilioni 1.1 kwa ajili ya kujenga jengo la Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tangu Halmashauri ile ianzishwe hatuna magari ya kuwasababisha Wakuu wa Idara na Mkurugenzi waweze ku-move kwenye vijiji wasimamie miradi ya maendeleo. Sasa naomba Serikali iweze kuangalia Halmashauri hizi maana unasikia Halmashauri kongwe zina miaka 20 bado zinapelekewa magari mapya lakini zile Halmashauri ambazo ni changa wala hazifikiriwi kupelekewa magari ili waweze kufanya kazi zao za kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana Waziri wa TAMISEMI aangalie Halmashauri hii ya Uvinza kwa jicho la huruma. Nashukuru sana tumepata Mkurugenzi, ni mpya lakini anajua majukumu yake ya utendaji wa Halmashauri. Kwa hiyo, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri tuangalie namna ya kuwezesha Halmashauri ya Uvinza ili tuweze kusonga mbele katika kutekeleza majukumu yetu ya maendeleo….
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru