Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Dr. Jasson Samson Rweikiza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. JASSON S. RWEIKIZA – MWENYEKITI WA KAMATI YA UTAWALA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii uliyonipa ya kuweza kujumuisha hoja ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, waliochangia kwa kusema katika hoja hii ni Waheshimiwa Wabunge 22 na wale waliochangia kwa maandishi ni 14. Nitumie fursa hii kumshukuru sana Waziri, Mheshimiwa Angellah Kairuki na Waziri, Mheshimiwa George Simbachawene kwa maelezo yao ambayo wameyatoa hapa ambayo kwa kiasi kikubwa yamejibu hoja mbalimbali ambazo zimeboresha uelewa wa hoja ambazo ningezisema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya mwaka ya shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa imepata wachangiaji 22 waliochangia kwa kuzungumza na 14 waliochangia kwa njia ya maandishi. Eneo la kwanza wamezungumzia Tume ya Utumishi ya Walimu (TSC) na wamegusia kero zinazowakabili walimu ambazo ni kama ifuatavyo:-
(i) Kutolipwa madai yao ya likizo;
(ii) Uhamisho;
(iii) Mishahara na kadhalika;
(iv) Walimu kunyimwa uhamisho;
(v) Mazingira magumu ya kazi;
(vi) Mrundikano wa wanafunzi darasani, ukosefu wa nyumba za kuishi na kadhalika.
(vii) Kushushwa vyeo kwa walimu na matamko ya watawala – Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya;
(viii) Bajeti ya Tume iongezwe ili iweze kujitanua katika wilaya nchi nzima;
(ix) Kasoro zilizobainika katika Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu zirekebishwe ili kuiwezesha Tume kutekeleza majukumu yake kikamilifu ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili walimu; na
(x) TAMISEMI ihakikishe inatenga fedha za kutosha katika bajeti ijayo ili kuondoa kero za walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni la utawala bora na rushwa. Katika eneo hili wachangiaji wamebainisha mambo yafuatayo:-
(i) Wasimamizi wa Serikali hawafuati sheria, kanuni na taratibu za utawala;
(ii) Watendaji wasijielekeze katika kuwajibisha watumishi tu bali wawajengee uwezo na mazingira bora ya kazi kabla ya kuwawajibisha;
(iii) Vita ya rushwa asiachiwe Mheshimiwa Rais peke yake, viongozi wote na jamii nzima wahusike katika mapambano haya;
(iv) Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wazingatie dhana ya utawala bora pamoja na sheria zinazoongoza utendaji wao;
(v) Watendaji wa Serikali waheshimu dhana ya mgawanyo wa madaraka (separation of powers) kwa mihimili mitatu yaani Serikali, Mahakama na Bunge ili kuepusha mgongano wa kiutendaji;
(vi) Haki za binadamu zizingatiwe wakati wa kuwawajibisha watumishi wanaopatikana na makosa ya kiutumishi;
(vii) Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wapewe semina elekezi kuhusiana na utekelezaji wa majukumu yao;
(viii) Watendaji wa Vijiji na Mitaa na Madiwani wapatiwe mafunzo ya kiutendaji na mishahara; na
(ix) Viongozi wawe makini kabla ya kutoa matamko na waache woga katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu, ni Halmashauri kutenga asilimia 10 ili kusaidia wanawake na vijana. Katika eneo hili wachangiaji wamegusia mambo yafuatayo:-
(i) Halmashauri nyingi nchini zimeshindwa kutekeleza agizo hili la Serikali kwa kukosa uwezo wa kifedha;
(ii) Hatua ya Serikali kuondoa ukusanyaji wa kodi ya majengo (property tax) katika Halmashauri imeathiri kwa kiasi kikubwa uwezo wa mapato ya Halmashauri;
(iii) Serikali haipeleki kikamilifu ruzuku katika Halmashauri; na
(iv) Serikali iangalie mpango wa kuelekeza shilingi milioni 50 za kila kijiji kusaidia vikundi vya vijana, akinamama na SACCOS. Katika eneo hili ni Halmashauri 13 tu ambazo zimepelekewa fedha katika kundi hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la nne ni TASAF. TASAF Awamu ya III imejielekeza katika kunusuru kaya maskini. Katika eneo hili wachangiaji wamegusia mambo yafuatayo:-
(i) Mpango huu umekuwa na mafanikio makubwa kwa kusaidia kaya maskini kuweza kumudu mahitaji ya msingi kama vile chakula, elimu na afya;
(ii) Umepunguza utegemezi wa kaya maskini kwa Waheshimiwa Wabunge;
(iii) Miradi ya maendeleo inayotekelezwa na TASAF ishirikishe wananchi wanaonufaika; na
(iv) Wananchi waelimishwe kuhusiana na mpango wa TASAF wa kusaidia kaya maskini.
Hapa ni kweli kwamba Serikali haichangii mchango wake katika TASAF. Tunayo takwimu hapa, katika miaka mitano iliyopita Serikali imetoa mchango kidogo sana katika fungu hili. Mwaka 2012/2013 bajeti ya Serikali iliyopitishwa ilikuwa shilingi bilioni nne, kiasi kilichotolewa ni shilingi bilioni 2.5, kiasi kilichobaki ni shilingi bilioni 1.5.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka uliofuata kiasi kilichoidhinishwa ni shilingi bilioni 18.5, kiasi kilichotolewa ni shilingi bilioni tatu, kilichobaki ni shilingi bilioni 15.5. Mwaka uliofuata kiasi kilichoidhinishwa ni shilingi bilioni 14, kilichotolewa ni sifuri, kilichobaki ni shilingi bilioni 14. Mwaka uliofuata iliidhinishwa shilingi bilioni 14, ilitolewa shilingi milioni 600 ikabaki shilingi bilioni 13.4. Mwaka uliofuata (mwaka jana) iliidhinishwa shilingi bilioni 14, ilitolewa sifuri, ikabaki shilingi bilioni 14.
Kwa hiyo, katika miaka mitano hii Bunge liliidhinisha shilingi bilioni 64.5 na iliyotolewa ni shilingi bilioni 6.1, ikabaki shilingi bilioni 58.4. Kwa hiyo, kwa kweli Serikali haijatoa mchango wake mkubwa katika eneo la TASAF. Kamati inasisitiza kwamba Serikali iongeze mchango wake ili wananchi waweze kunufaika na mpango huu wa TASAF III.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tano ni utumishi wa umma. Katika eneo hili wachangiaji wamegusia mambo yafuatayo:-
(i) Hatua ya Serikali kusitisha ajira na upandishaji vyeo kwa watumishi imeathiri watumishi ambao wanakaribia kustaafu. Serikali iruhusu ajira kwani kuna wahitimu wengi ambao wako mitaani wakisubiri ajira za Serikali;
(ii) Watumishi wanaofanya kazi wapewe motisha;
(iii) Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa, Wakurugenzi wa Halmashauri na Watendaji wengine ambao hawakuwa katika utumishi wa umma kabla ya uteuzi wao wapewe semina elekezi kuhusiana na namna ya kutekeleza majukumu yao; na
(iv) Maamuzi ya Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya dhidi ya watumishi yanavunja moyo watumishi hao na kusababisha baadhi yao waone kwamba haina thamani kuwa mtumishi wa umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la sita ni utoaji wa elimu ya msingi bila malipo. Katika eneo hili, wachangiaji wamepongeza hatua ya Serikali kwani imekuwa na mafanikio ambayo hata hivyo yana changamoto mbalimbali, nazo ni kama ifuatavyo:-
(i) Uhaba wa vyumba vya madarasa;
(ii) Uhaba wa nyumba za Walimu;
(iii) Matundu ya vyoo na kadhalika;
(iv) Uhaba wa Walimu;
(v) TAMISEMI inashindwa kugharamia uendeshaji wa shule za Serikali kutokana na kuwa na mambo mengi; na
(vi) Bado wazazi wanawajibika kuchangia mahitaji ya wanafunzi kwani Serikali ilichoondoa ni ada na michango ya uendeshaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo yalikuwa mambo ya jumla lakini Waheshimiwa Wabunge katika michango yao vilevile wamegusia mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waitara katika mchango wake amesema mambo kadhaa na akalaumu kwamba kuna viongozi ambao wanatoa matamshi ambayo yanakatisha tamaa, akamsema Rais kwamba ametoa matamshi ambayo sio mazuri. Mimi nasema hii siyo sahihi. Mheshimiwa Rais amejipambanua kwamba yeye hapendi rushwa, amesema wazi kwamba rushwa kwake ni mwiko. Hata ndani ya Chama cha Mapinduzi ambacho ndiyo chama chake, amesema uchaguzi mwaka huu atakayetoa rushwa hatateuliwa kugombea nafasi yoyote. Pia amefanya kazi kubwa sana ameanzisha Mahakama ya Mafisadi ambayo inapinga rushwa na mambo mengine ambayo tumeyaona. Amezungumzia mambo mengi lakini sitayasema yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kiteto amesema kwamba Mabaraza ya Madiwani, RCC na kadhalika visifanyike wakati wa vikao vya Bunge. Kamati inaunga mkono hoja hii nzuri kwani Waheshimiwa Wabunge wana mchango mkubwa kwenye Mabaraza ya Madiwani, vikao vya RCC na vikao vingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Japhary Michael amezungumzia mambo mengi, mojawapo ni kuhusu elimu bure. Hakuna elimu bure, elimu inalipiwa na anayelipia ni Serikali na Serikali inalipia kutokana na kodi za wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwalongo amesema kwamba Watendaji wa Vijiji, wa Mitaa na wengine waajiriwe wasikaimu muda mrefu. Kamati inaunga mkono, ni hoja nzuri, wakikaimu muda mrefu wanakuwa hawana maamuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, amezungumzia pia suala la kuwa na shule za awali katika shule za msingi na maeneo mengine na akasema kwamba ni vizuri shule za awali ziwe pale ambapo wanafunzi hao wapo kwa sababu ni wadogo kutembea umbali mrefu ni vigumu sana. Kamati inaunga mkono hoja hii ili kufanikisha ili azma ya kuwa na „K‟ tatu zile, Kusoma, Kuandika na Kuhesabu. Mtoto akianzia shule ya awali anapata msingi mzuri anapokwenda shule ya msingi na sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini amezungumzia Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa kupewa posho. Ni jambo jema, tunashauri Serikali ijitahidi kuongeza mapato ili iweze kuwalipa posho Wenyeviti wa Mitaa, Vitongoji na Vijiji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini amezungumzia TASAF II kwamba ni jambo zuri limewasaidia sana wananchi hasa kaya maskini. Takwimu zilizopo zinaonesha kwamba katika miaka mitatu iliyopita TASAF III imetumia zaidi ya shilingi bilioni 400 na zaidi ya kaya milioni moja zimenufaika na mpango huu. Watu wengine wanatumia vizuri mpango huu na wanajinufaisha wanakuwa na miradi ya kujikwamua na umaskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ameshauri kwamba mpango huu uboreshwe ili fedha hizi zitumike vizuri zaidi. Kamati inaunga mkono hoja hii kwa sababu kuna baadhi ya watu ambao wakipata hela hizi za TASAF wanalewea pombe na kuna wengine ambao sio watu maskini kama ilivyosemwa na wachangiaji wengi lakini wamo kwenye mpango huu. Kwa hiyo, Kamati inashauri kwamba ni vizuri mpango huu ukaboreshwa. Mpango mzuri zaidi ni kama alivyosema Mheshimiwa Rais kwamba hizi pesa badala ya kutolewa bure watu waajiriwe kwa kazi ndogondogo hizi za usafi kwenye mitaa, kuzibua mitaro, kupanda miti, kujenga madarasa, kujenga kliniki na kadhalika ili waendelee kupata pesa lakini vilevile tupate maendeleo kadha wa kadha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Balozi Adadi Rajab amezungumzia Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi Dar es Salaam. Amepongeza na kwa kweli Kamati inashukuru kwa mchango huo, mradi huu ni mzuri sana. Tangu uanze mwezi Mei, 2016, barabara ile ya Morogoro sasa haina msongamano wa magari, imekuwa ni barabara nzuri. Tunashauri kwamba mradi huu usimamiwe vizuri zaidi ili barabara nyingine Phase II, Phase III mpaka Phase VI zikamilike. Barabara ya Kilwa, Barabara ya Bagamoyo, Barabara ya Pugu na nyingine zijengwe kwa utaratibu huo wa mabasi yaendayo kasi ili Jiji la Dar es Salaam liondokane na kero za msongamano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia pale kwenye mradi ambao umekamilika wa Kimara Ferry (Kivukoni), pale Ubungo interchange pajengwe flyover haraka sana basi linakaa pale dakika 10, 15 likisubiri kuruhusiwa kwenda. Sasa inakuwa tena siyo kasi ni kama mabasi mengine ya kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Richard Mbogo katika utawala bora amezungumzia kwamba baadhi ya Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na viongozi wengine wanatumia vibaya madaraka yao. Wanakamata watu hovyo, kuwaweka ndani hovyo, kuwapunguza madaraka na kadhalika. Kamati inaunga mkono hoja hii kwamba kwa kweli ni vizuri Serikali ikaangalia sheria inazingatiwa kwa sheria zipo. Kamati za nidhamu, za ajira zitumike na siyo mtu mmoja kutoa maamuzi ambayo wakati mwingine yanakinzana na sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Bashe amezungumzia mambo mengi lakini moja amesema kwamba hela ya TASAF hii inayotolewa kwa wananchi iwe accounted for. Kabla ya kupewa fedha nyingine aeleze ile ya kwanza ameitumiaje. Ni wazo zuri katika kuboresha utoaji wa fedha hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Tunza katika mchango wake wa maandishi amesema ni vizuri Serikali ikaangalia matumizi ya gesi na mafuta tuliyogundua. Watu wapate elimu kuhusu matumizi au fursa zilizopo katika utajiri huu. Inawezekana baadhi ya wananchi wakafikiri kwamba baada ya kugundua mafuta na gesi basi hakuna kufanya kazi, ni kula tu, hapana wafahamu kwamba kuna fursa na wazitumie vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ruth Mollel amechangia akasema kwamba Bunge siyo huru na akatoa mfano kwamba hakuna Bunge live. Sisi tunasema hii siyo kweli, Bunge kutokuwa live haina uhusiano wowote na kutokuwa huru. Tuliamua wenyewe hapa ndani kwamba Bunge lisiwe live kwa sababu ambazo zilielezwa humu ndani pamoja na gharama, TBC ilishindwa kuendesha mradi huo wa Bunge kuwa live. Kwa hiyo, hii haina uhusiano na Bunge kutokuwa huru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, akatoa mfano mwingine kwamba Mahakama zimenyamaza kuhusu mikutano ya hadhara ya vyama. Mahakama haiwezi kutoa maamuzi bila mtu kwenda mahakamani. Ni lazima mtu afungue kesi na ndipo asikilizwe Mahakama itoe uamuzi. Kwa hiyo, Mahakama zipo huru mwenye malalamiko yoyote aende Mahakamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Omary Tebweta amezungumia mambo mengi lakini mojawapo ni kuhusu asilimia 10 kwenda kwa vijana na wanawake, asilimia 50 maendeleo na asilimia 40 kwenye Other Charges (Matumizi Mengineyo). Ameeleza vizuri na sisi tunakubaliana naye kwamba baadhi ya Halmashauri zinatumia mwanya huu kujipatia hela ya matumizi mengineyo. Inatenga fungu la asilimia 40 kwa Matumizi Mengineyo, inatenga labda shilingi bilioni mbili ikifahamu fika kwamba haiwezi kupata shilingi bilioni mbili kwa mapato mengine ya ndani lakini inapanga makusudi shilingi bilioni mbili ili hela yote iingie kwenye Matumizi Mengineyo. Tunashauri utaratibu huu udhibitiwe na asilimia 40 iwe ni kweli asilimia 40 ya yale mapato ambayo wamepata sio Mapato Mengineyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Conchesta Rwamlaza amezungumzia uchaguzi kutokuwa huru. Kamati haikubaliani naye. Uchaguzi ni huru na ni wa haki. Hata juzi kwenye kata zile zilizorudia uchaguzi CCM imeshinda kwa haki. Mtu yeyote ambaye haridhiki na matokeo Mahakama zipo, aende mahakamani alalamike, apeleke ushahidi ahukumiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia niombe sasa Bunge lako Tukufu likubali Taarifa hii ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa na maoni na mapendekezo yaliyomo katika taarifa hii. Nashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.