Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwanza naipongeza sana Serikali kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya na hasa hii dhana ya kuwajibika Serikalini, ni dhana muhimu sana. Haya majitu yasiyowajibika wala msirudi nyuma, yaendelee kutumbuliwa ili yapotee kabisa! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaendelea, napenda nimrudishe Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa hotuba yake nzuri aliyoitoa ukurasa wa 28. Ukurasa wa 28 kuna mambo ya nyongeza ambayo Mheshimiwa Waziri ameyasoma, kwenye kitabu hayapo. Yapo kumi nimeyasikia; moja mpaka kumi. Ulikwenda moja, tisa, kumi. Naomba yale kumi ya namna ya utekelezaji wa mkakati, ayaandike tuyapate. Ni ya msingi sana, nilimsikia vizuri sana kwa sababu nilikuwa hapa. Hilo ni ombi katika hotuba hii nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo mawili ya haraka haraka, la kwanza naomba nijielekeze ukurasa wa 15 ambapo Tanzania imekuwa ikipoteza uwezo wake wa kushindana kibiashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia zile takwimu, zinatisha kidogo, kwamba kuanzia mwaka 2012 tumekuwa tunashindwa kuvutia mitaji ya ndani na ya nje na mbaya zaidi mwaka 2016 inatarajiwa tutakuwa nchi ya 139 katika nchi 186 katika kuvutia mitaji ya ndani na nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri, katika mkakati mzima wa kutekeleza Mpango wetu mzuri wa miaka mitano inayokuja, ni muhimu sasa Serikali na Wizara tukajua ni kwa nini hasa tumeshindwa kuvutia wawekezaji? Ni kwa nini hasa tumeshindwa kuvutia mitaji ya ndani? Tatizo ni nini? Ni urasimu kwenye vyombo vyetu huko TIC au tatizo ni nini hasa?
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima iwepo sababu ambayo inafanya nchi yetu ishindwe. Katika nchi 186 kwa mujibu wa vigezo vya World Bank, tunapokuwa nchi ya 140, ni sawa na kuwa nyuma kabisa. Kwa hiyo, nawiwa kusema kwamba ni vyema Serikali yote ikae kuelewa kwa nini tumeshindwa kuvutia mitaji ya ndani na nje na ukizingatia mpango mzima kwa kiwango kikubwa, umetamka kwamba utashirikisha sekta binafsi?
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo ningependa kusema ni kilimo ambalo wenzangu wamelisemea, lakini niseme eneo dogo tu, kwenye Benki ya Kilimo. Mheshimiwa Waziri wa Fedha atakubaliana nami kwamba kama kweli tunataka kuwa nchi ya viwanda kwa dhati kabisa, ni lazima tuweke nguvu kubwa sana kwenye Sekta ya Kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya nyenzo za kukuza Sekta ya Kilimo ni pamoja na Benki hii ya Kilimo. Kwa mujibu wa hotuba hii, Benki ya Kilimo haina mtaji na kama inao ni kidogo sana. Ina Shilingi bilioni 60 tu, ukiachilia mbali kwamba Benki hiyo iko Dar es Salaam na wamekuja kwenye Kamati yetu tumewashauri kwamba wajitofautishe ili ikibidi sasa wahamie katika maeneo ya uzalishaji ili iwe Benki ambayo kweli ni kioo, ni Benki ya Wakulima na hakika isiwe Benki iliyoko Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina ushauri mmoja kwa Serikali na hasa Wizara ya Fedha, hatuwezi kuendelea kama ilivyokuwa mwaka wa 2015 kwamba Benki ya Kilimo haina mtaji, lakini wenzao wa TIB, Alhamdullah wana angalau Shilingi bilioni 212. Benki ya Kilimo ambayo tunaitarajia isaidie wakulima ili wazalishe, hatimaye nchi iingie kwenye nchi ya viwanda na viwanda vingi viwe vya kuchakata mazao ya kilimo, bado Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kuna haja kubwa kama Serikali mwangalie namna nzuri ya kuwezesha Benki hii ya Kilimo iweze kufanya kazi zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo njia nyingi. Kwa mfano, kama wenzetu wa DANIDA waliweza ku-support CRDB na mnaona ilipofika, kama wenzetu wa DANIDA waliweza ku-support PASS kule Morogoro na mnaona PASS ilipofika, kwa nini Mashirika rafiki na nchi rafiki pengine zenye masharti rafiki msizihusishe katika mkakati mzima wa kuiwezesha Benki ya Kilimo kupata mtaji unaoeleweka? Nina hakika mkifanya hivyo Benki hii itasambaa katika maeneo mbalimbali katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, niweke angalizo; hatuwezi kuzungumza nchi ya viwanda kama hatuwezi kuwezesha Sekta ya Kilimo. Hilo ni lazima tukubaliane kabisa na bado kuna matatizo makubwa hata kwenye bajeti ya Sekta ya Kilimo. Mheshimiwa Waziri unajua kwamba bajeti ya pembejeo iko chini sana. Sasa kama bajeti ya pembejeo ipo chini sana kwa maana ya mbolea, mbegu, viatilifu, tafsiri yake ni kwamba hiki kilimo tunachotaka baadaye iwe ndiyo nguvu ya kujenga viwanda vya ndani, hiyo azma inaweza ikashindwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ushauri wangu sincerely kabisa ni kwamba lazima tuangalie namna nzuri ya kutoa fedha za kutosha kwenye eneo la pembejeo na hasa mbolea. Kwa takwimu za wenzetu wa Wizara ya Kilimo ni kwamba hata uzalishaji wa chakula mwaka 2015 ulishuka kwa takribani tani 500,000. Ni dhahiri tukienda katika mfumo huu ambapo hata fedha za pembejeo za kilimo zimeshuka, tafsiri yake ni kwamba uzalishaji wa mazao ya kilimo utakuwa chini and consequently itakuwa ni ngumu sana kupata mazao ya kutosha kumudu viwanda vyetu vya ndani na hatimaye tuweze kuboresha maisha ya watu wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo limenivutia sana ni hii miradi ya kipaumbele hasa reli ya kati. Naomba Serikali ifahamu kabisa tukisema reli ya kati, maana yake ni reli inayoanzia Kigoma inaishia Dar es Salaam, ndiyo reli ya kati na ndiyo jina lake. Mwanzo wa reli ni Kigoma na mwisho wa reli ni Dar es Salaam. Msingi wake ni mmoja tu, kwamba hii reli kule Kigoma itakuwa ni mkakati wa ku-tape kutoka nchi ya Kongo Mashariki ambako kuna shaba nyingi sana, zinc nyingi sana na mbao nyingi sana!
Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu zinaonesha kwamba mzigo ulioko Mashariki ya DRC ni takribani tani milioni nne na hizo zinaweza kufika kwenye bandari na kwenda kwenye masoko nje ya nchi kupitia reli ya kati. Reli ya kati maana yake ni Kigoma - Dar es Salaam. Matawi yake ndiyo Tabora - Mwanza, Tabora – Kaliua – Mpanda na sasa hii mpya ya Uvinza – Msongati.
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo tafsiri ni muhimu sana ili tuelewane vizuri. Kwa sababu bila kuwa na tafsiri hiyo, tafsiri yake ni kwamba ule mkakati wa tani milioni nne za Kongo ya Mashariki, hautaweza kupita Bandari ya Dar es Salaam. Sincerely nashauri hata ujenzi wa reli ya kati kwa standard gauge uanzie Kigoma kwa ku-tape mali iliyoko DRC halafu reli hiyo itoke Kigoma ndiyo ijengwe kuelekea Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la mwisho ni utafiti. Nimesoma kwenye kitabu cha hotuba, Mheshimiwa Waziri wa Fedha umeanisha vizuri sana umuhimu wa utafiti, lakini liko jambo moja linahitaji uelewa tu wa jumla. Kwa nini Taasisi zetu za Utafiti, ili zipate fedha za Utafiti lazima eti zikashindanie COSTECH? Ni mambo ya ajabu kabisa haya! Nina hakika haya mambo ndiyo Mheshimiwa Magufuli hataki hata kuyasikia!
Mheshimiwa Naibu Spika, watafiti wako Ilonga, Uyole, Mlingano, lakini eti fedha za utafiti zinapelekwa COSTECH wakazishindanie ndiyo ziende kwenye Taasisi za Utafiti, kwa nini? Hivi unahitaji kwenda shule kulijua hili? Kwa nini pesa hizi zisiende kwenye utafiti moja kwa moja? Kwanza itapunguza urasimu na itapunguza muda wa fedha kutoka Hazina na kufikia Vyuo vya Utafiti.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, nakualika Mheshimiwa Waziri wa Fedha, utembelee Kituo cha Utafiti cha Cholima kilichoko Dakawa. Hicho ndiyo kituo ambacho ni known kwa utafiti wa mpunga. Waheshimiwa Wabunge, kama tukiendelea hivi bila utafiti kwenye Kituo hicho nchi hii tutakosa mchele kwa miaka michache ijayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati yetu tumekwenda pale, tumekuta mambo ya ajabu sana! Hawa watu wana miaka mitatu hawajapata fedha kwa ajili ya utafiti. Fedha kidogo waliyoipata, eti wanashindanishwa na COSTECH! Mimi sielewi! Wala haikuingia kwenye kichwa changu hata kidogo, kwamba watafiti, wasomi wazuri, Watanzania hawa wanaanza tenda, ku-lobby kule COSTECH ili wapate fedha kuendesha utafiti kwenye Vyuo vyao.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali mjue wazi kabisa kwamba Vyuo vya Utafiti hasa kwa mazao ya kilimo vinajulikana; vipo Uyole, Naliendele, Ilonga, Ukiriguru, Mlingano, Seriani na kadhalika. Wapelekeeni fedha hao moja kwa moja, ni wataalam na wasomi wazuri katika jambo hili. Kupitisha hizi fedha COSTECH ni kupoteza wakati tu na kuweka urasimu ambao hauna sababu. (Makofi)
Mwisho kabisa naomba nami kwa namna ya pekee niwashukuru wapigakura wangu wa Kasulu Mjini kwa kuniwezesha kurudi Bungeni, maana haya mambo ni mazito!
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuwashukuru, naomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na naunga mkono hoja. Mkakati ni mzuri na msonge mbele. Ahsanteni sana.