Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nianze kwa kuunga mkono hotuba hii ambayo Mwenyekiti ameitoa ya Kamati yetu hii. Nami niseme ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti na kimsingi nimetaka tu kusema machache ambayo wenzangu mengi wameyasema, nataka kukazia machache ambayo kimsingi nayaona katika Kamati yetu yamekuwa ni changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka hasa kuzungumzia kwenye sekta ya kilimo ambayo wengi wetu wamesema habari ya uchangiaji kwenye pato la Taifa. Ukiangalia sekta ya kilimo inategemewa na wananchi wetu wengi sana kwa kipato. Ni kweli Serikali imewekeza fedha katika eneo hili lakini kwa uchache sana. Ukiangalia sasa hivi, ukuaji wa sekta ya kilimo, mwaka wa fedha wa 2014 inaonekana ulikua kwa asilimia 3.4 lakini mwaka huu kwa robo hii ya kwanza ambayo tumeiona ina ukuaji mdogo sana wa asilimia tatu. Nashauri Serikali iwekeze zaidi katika kilimo na mifugo kwa sababu wananchi wetu wengi wanaitegemea sana sekta hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo machache ambayo Serikali imejitahidi hasa katika kupeleka pembejeo za kilimo katika maeneo yetu lakini ukiangalia pembejeo zile zina utata, zinachelewa sana kuwafikia wakulima mara nyingi zinafika wakati ambapo mvua zenyewe zimekwisha kunyesha. Nishauri kidogo Wizara hii ya Kilimo kuangalia maeneo ambayo wanapeleka pembejeo hizi kuzipeleka kabla ya mvua ili wananchi waweze kupata pembejeo hizi mapema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mwaka huu Serikali imepeleka asilimia kidogo sana kwa wananchi wetu hasa pembejeo hizi ambazo kimsingi kwa sasa zimekuwa zikipiganiwa sana, Mikoa mingi imepata pembejeo baada ya mvua kunyesha. Pamoja na haya yote mazao yanayopelekwa kule, kwa mfano mahindi, yanapelekwa ya muda mrefu wakati wananchi wanahitaji mahindi au mbegu za muda mfupi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe Wizara iangalie wakati wanapeleka pembejeo hizi wapeleke pembejeo ambazo zinafaa kwa maeneo husika. Wataalam watusaidie kufanya research ili wajue katika ukanda fulani kama ni Nyanda za Juu Kusini, Mashariki au Magharibi, ni mbegu gani hasa inapaswa kupelekwa katika kusaidia jamii yetu. Vinginevyo wakiwa wanapeleka kama sasa kwa mfano wanapeleka hybrid maeneo ambayo yanahitaji samsung, itakuwa haina tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niizungumzie moja kwa moja kwa undani kwa sababu kilimo tunakifahamu. Mara nyingi pembejeo zinazopelekwa mahali pale wakulima wanakuwa hawazipendi tena kwa sababu ni za muda mrefu na hazifai katika eneo hilo zinapopelekwa. Kwa hiyo, naomba kabisa Serikali iangalie upya suala hili la pembejeo tunazozipeleka katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa pembejeo zinapelekwa wakati ambapo wananchi hawazihitaji tena, Serikali iangalie kama inawezekana ilete Bungeni tuone namna nzuri ya kusaidia twende kwenye mfumo wa moja kwa moja ili pesa hizi zinazotumika katika kupeleka pembejeo zitumike katika kushusha mbegu za mazao haya kuliko kupeleka msaada ambao mara nyingi unakuwa hauna tija tena katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niende kwenye eneo hili la mikopo. Serikali au Chama cha Mapinduzi ukiangalia Ilani yetu tumeweza kuonesha kwamba tunaweza kuwapa mikopo hii ya shilingi milioni 50 kila kijiji. Katika maeneo haya Kamati imejadili kwa kina na niipongeze sana Kamati yetu kwa sababu tumeona na niipongeze Serikali wamejiandaa kwa pilot area. Sasa niombe zile institutions ambazo zinahusika na suala la fedha ziwe aware katika kuelekeza na kutoa elimu ambayo itasaidia katika vijiji vyetu wakati pesa hizi zikifika kule chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri haya kwa sababu unajifunza kutokana na makosa yanayotokea mara nyingi sana katika jamii yetu. Ukiangalia miaka iliyotangulia katika Awamu ya Nne kulikuwa na mabilioni ya pesa maarufu Mabilioni ya Jakaya. Pesa hizi hazikufanya vizuri kwa sababu hazikuwa na monitoring nzuri. Sasa niombe, ili kuwa na matokeo chanya fedha hizi zikifika katika maeneo yetu ya vijijini pawe na mpangilio mzuri na elimu itolewe kabla ya kupelekwa fedha hizi katika maeneo haya ili wananchi wajue kabisa fedha hizi ni za mikopo, wasione fedha hizi ni bakshihi wakazitumia bila kujua namna ya kuzirudisha. Kwa maana najua wazi pilot area hela zitapelekwa maeneo machache ili waweze kurudisha na maeneo mengine yaweze kupatiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tena kuzungumzia suala la afya au Wizara yetu ya Afya. Ni wazi tumeona jinsi bajeti ya afya ilivyokuwa na changamoto hasa kwenye masuala ya dawa. Nataka niende katika maeneo mengine ambayo kimsingi wengi tumekuwa tukihitaji kujengewa zahanati na vituo vya afya. Tulikuwa na mpango wa kujengewa vituo vya afya na zahanati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mpango uliopo ni kujengewa zahanati, lakini kwenye maeneo yetu ya Halmashauri kuna maboma mengi sana ambayo hayajafikia kumalizika. Wananchi wengi wamejenga hospitali na zahanati na vituo vya afya ambazo zingine zipo kwenye lenta, madirisha na nyingine imebakia tu finishing.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Wizara ya Afya katika bajeti ijayo ione namna gani ya kuleta bajeti ili angalau tuweze kujenga au kumalizia vituo vyetu. Kwa mfano, Wizara ya Afya ikiamua ikaleta bajeti ambayo angalau kila Halmashauri ikajengewa kituo kimoja cha afya kwa mwaka wa fedha hii itasaidia sana. Hakuna Halmashauri ambayo imo haina viporo hivi. Kwa maana hii basi tukiwa na Halmashauri 183 zikajengewa kituo kimoja cha afya kwa mwaka mmoja, kwa miaka mitano ukizidisha mara nne tutakuwa na vituo zaidi ya 800 ambavyo vimejengwa kwa mwaka mmoja. Kwa hiyo, kwa kufanya hivi katika miaka mitano kufikia 2020 tutakuwa tumejenga vituo vingi na vilivyomalizika. Kwa hiyo, huo ulikuwa ni ushauri wangu wa jumla katika Wizara hii ya Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende katika suala la umeme vijijini. Itakuwa ndoto sana kwa Tanzania ya viwanda kuweza kupatikana bila kuwa na umeme wa uhakika. Inaonekana kabisa kwamba fedha ambazo zimepelekwa katika umeme (REA Vijijini) ni asilimia chache na sasa hivi tunasema REA III na REA II ambayo kimsingi inategemea kumalizika, bado maeneo mengi REA II haijafikia ukamilifu wake. Niombe Wizara iweke msukumo ili ile REA III iweze kuanza mapema, najua kwamba inakwenda kuanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Wizara iwaangalie wakandarasi hawa wanapopewa tenda wawe na uwezo wa kumaliza kazi mapema. Tangu Awamu ya Nne yapo maeneo ya REA II ambayo mpaka sasa hayajakamilika kabisa. Hali hii inaweza kutudumaza zaidi sisi Watanzania na kauli ya Mheshimiwa Rais ya kutegemea kupandisha Tanzania iwe katika uchumi wa kati itakuwa ndoto kama tusipoangalia maana kiwanda hakiwezi kuendelea bila umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huohuo niipongeze Wizara ya Maji inajitahidi sana katika maeneo haya ya kumalizia viporo vya maji. Kuna mpango ambao tunaendelea nao huu wa maji vijijini, niombe kabisa Wizara ya Maji na Waziri wa Fedha aone pia ipo miradi mingi ya maji ambayo kwa sasa ni viporo. Naomba sana Wizara ya Maji iangalie maeneo yale ili iweze kutoa fedha, hasa fedha ambazo naziona zinakuwa kizungumkutiā€¦
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.