Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Bukoba Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote nitumie fursa hii pamoja na majanga na madhara yote ambayo tumeyapa Mkoa wa Kagera lakini niupongeze Mkoa wa Kagera na hususani Walimu wetu wa Mkoa wa Kagera wa shule za sekondari kwa Mkoa wa Kagera kujitokeza kuwa Mkoa wa tatu kwa matokeo mazuri Kitaifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo, niipongeze Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba ikiongozwa na kijana wa mvuto na mnato Chief Kalumuna kama Mstahiki Meya kwa kuongoza Baraza, Halmashauri, Walimu na shule za sekondari kwamba Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba ninapotoka mimi ku-appear kama namba moja Kitaifa katika matokeo ya form four. Naomba ushirikiano ambao tunao pale Bukoba Mjini bila kujali itikadi zetu za kisiasa, sisi tukipiga mzigo tunapiga mzigo kweli kweli na matokeo yake tumeyaona kwa matokeo ya mwaka huu, nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, katika Mpango wa Maendeleo ulioletwa mwaka jana hapa, nilizungumza kwa kina kabisa matatizo ya Mkoa wetu wa Kagera na majanga ambayo tumeyapata na ya kihistoria ambayo yanasababisha mkoa ule kuwekwa katika orodha ya mikoa maskini. Japo matukio hayo ambayo yanatuathiri wananchi wa Mkoa wa Kagera yamegeuzwa sasa kama utani na majina mengine kutumika kama kututania japo ni majina ya kihistoria tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba Serikali kama Serikali na kupitia katika bajeti na mipango ambayo inaletwa na imesomwa hapa na Kamati, ni kazi ya Serikali kusimamia…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Lwakatare majina gani umesema?
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Majina?
MWENYEKITI: Ndiyo.
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Haya. Mwenyekiti ametaka kujua majina ambayo ni ya kihistoria na nafikiri watu wamekuwa wanayatumia vibaya majina kama Mto Ngono, Katerero, hayo ni majina tu ambayo yana historia yake. Kwa hiyo, naomba watu wanayoyatumia wanione niwaeleze umaana wake wasiyatumie vinginevyo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kazi ya Serikali kuangalia ustawi wa watu wake. Sisi wananchi wa Kagera na hususani Bukoba Manispaa ninapotoka Mwenyezi Mungu alipotuweka kule kijiografia na tukaumbwa kukaa katika nchi ya Tanzania badala ya Uganda hatukukaa kule kwa bahati mbaya. Serikali inapaswa itambue umbali wa kutoka kwenye centre ya maamuzi na sehemu kubwa ya kiuchumi kama Dar es Salaam na tukawa Bukoba, Serikali inapopanga mipango yake lazima izingatie suala la cost and price standardization katika baadhi ya mambo ambayo yanaweza yakatusaidia sisi kama Watanzania na kama Watanzania wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia kwamba baada ya tetemeko kumejitokeza tatizo la watu kupata malazi na kujenga upya nyumba, ni suala ambalo Serikali inapaswa ilizingatie katika mipango yake. Mama Ghasia na Kamati nzima kwa ujumla nawaomba tunapokwenda kwenye bajeti ya mwaka huu bila kuli-address suala la Kagera na matatizo ambayo tumeyapata na nimesikitika pamoja na kwamba tumekuwa tunalizungumza na Mheshimiwa Conchesta na jana amezungumza, inapokuja wakati wa majumuisho sijasikia mtu anayelizungumza hili lakini sisi kama wawakilishi wa wananchi wa Kagera hatutaacha kulizungumza kwa sababu tetemeko limeacha limetusambaratisha, uchumi umeparaganyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu fikiria mtu ambaye wamechangishana wakajenga nyumba kwa miaka saba anaishi na familia yake, leo tetemeko la sekunde tatu linasambaratisha kila kitu maana yake ni kusambaratisha uchumi wa familia na ukoo kwa ujumla. Sasa tunapokuja kutaniana na naomba Mheshimiwa Msigwa ambaye ni Mwandishi Mkuu wa Mheshimiwa Rais pale Ikulu awe anatusaidia kutoa matamko kwamba safari hii Rais alikuwa anatania au safari hii Rais yuko serious. Hata leo nilisikia Rais wa Chama cha Wanasheria akihojiwa akasema aah, aah Rais alipowaeleza Majaji na Mawakili kwamba kuna Majaji ambao wanatetea wahalifu alikuwa anatania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba labda kuwe kunatolewa matamko kwamba Rais hapa anatania, hapa yuko serious kwa sababu mahali pengine utani mwingine unakuwa wa ukweli. Mfano pale alipotamka kwamba magari na pikipiki zikipita kwenye barabara ya mwendokasi zing‟olewe matairi na Mapolisi wakaamka wameng‟oa matairi ya pikipiki zote. Hata tulipoelezwa akina Lwakatare twende tukajenge Kiwanda cha Mabati ili tukauze mabati kwa Sh.1000, sijui Rais alikuwa anatania au alikuwa serious? Kwa hiyo, kama Rais alikuwa hatanii katika mipango ya bajeti tuanze na suala hili la cost and price standardization kwa vifaa vya ujenzi vinavyokwenda Kagera kama imeshindikana katika kuangalia policy na taxation kupunguza bei ya vifaa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sukari inalimwa Kagera lakini inauzwa Sh. 2,000, Sh. 2,200 hata pale pale Bukoba pamoja na kuwa kiwanda kipo kilometa 20 kutoka Bukoba Mjini lakini bei ni ile ile inayouzwa sukari Singida au Kahama ni kwa sababu ya standardization ya price. Vilevile TBL wanauza bia Sh. 2,500, Sh. 2,000 au Sh.1,500 hapa Dodoma na bei hiyo hiyo unaikuta Bukoba, kwa nini suala la cement, nondo, mabati ishindikane? Kwa nini Serikali kupitia kwenye bajeti na mipango thabiti isiliangalie suala hili ili wananchi wa Kagera kama ambavyo ni Watanzania wenzenu tukaweza kurudisha uchumi wa Wanakagera na makazi, tukajenga nyumba zetu kwani sasa hivi hali ni mbaya, nalieleza hili lieleweke. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mtakapokuwa mnajumuisha na hasa Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, naomba asipotezee kama ambavyo mmekuwa mnapotezea hamtujibu watu wa Kagera, mnatusadiaje suala hili katika mipango ya bajeti kwa sababu hali ni mbaya. Nalieleza hili na nitaendelea kulieleza kusudi lieleweke na hiyo ni sehemu ya kazi ya Serikali kuangalia wananchi wake wanapata malazi, chakula na mavazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tetemeko kutokana na uchumi kuparaganyika, Mkoa wa Kagera unategemea kupata njaa ndani ya mwezi Machi, hili tunalizungumza kwa uwazi, kutakuwepo na njaa. Natoa ilani hiyo acheni kutuletea takwimu ambazo ni za imaginations. Waheshimiwa njaa haina bouncer, tunaomba kabisa kabla janga hili halijaukumba Mkoa wa Kagera na hususani wananchi wa Bukoba Mjini ambao tunanunua ndizi kutoka Karagwe kwa Mheshimiwa Innocent, ndizi Mheshimiwa Innocent atawaambia, hakuna ndizi Muleba, hakuna ndizi Karagwe, wananchi wa Bukoba Mjini ambao sisi huwa tunatembeza mchuzi kununua ndizi, tuko katika hatari ya njaa na sasa hivi bei za vyakula zinapanda kama vile hazina akili nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba mtakapokuwa mnajumuisha hapa hebu toeni tamko mmejipangaje kutusaidia wananchi wa Kagera katika suala hili na hasa katika kuhuisha mfumo utakaowawezesha watu wapate vifaa kwa bei ya chini kwa sababu hali ni mbaya, ni mbaya, ni mbaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kagera nafikiri watanisikia Lwakatare hapa jembe lao nazungumza tena kwamba hali ni mbaya. Serikali itusikilize, iache kuja kututania mambo ya Katerero, mambo ya ngono hayatusaidii, sisi tuna shida. Wanaotaka Katerero waje tutawafundisha kijiji kipo, huo utaalam tutawafundisha. Ahsante.