Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami naomba nichangie kuhusu taarifa ya Kamati ya Bajeti. Nakushukuru kwa nafasi hii, lakini nisingependa kurudiarudia yale ambayo yamesemwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niipongeze sana Serikali kwa kweli kwa kazi nzuri lakini kwa nidhamu ya matumizi ya fedha inazokusanya. Nidhamu ya matumizi ya fedha kwa kweli imeongezeka sana. Kwa hiyo, naomba Serikali iendelee na utaratibu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita sana kama ulivyoshauri kwenye maoni na mapendekezo ya Kamati. Maoni ya Kamati hasa ukusanyaji wa ulipaji wa deni la TANESCO. Deni hili limekuwa likikua siku hadi siku. Mwaka 2014/2015 deni la TANESCO lilikuwa shilingi bilioni 186.4. Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati, inasema deni hili sasa hadi Agosti, 2016 limefikia shilingi bilioni 794.9. Kutoka shilingi bilioni 186 kwenda shilingi bilioni 794. Kwa hiyo, limeongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukijipa mwaka mmoja mbele, usishangae likafikia shilingi trilioni moja, sasa ni kwa nini deni hili linakuwa siku hadi siku? Nani halipi deni hili la TANESCO? Ni kwa nini halipi? Kama ni Taasisi za Serikali, nina uhakika zinapata kasma ya kulipa umeme. Taasisi hizi; watu binafsi na mashirika ya umma, kwa nini hawailipi TANESCO pesa zake ambapo yenyewe inatoa huduma ya umeme? Ni lazima ilipwe, kwa sababu ni azimio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kupitia Bunge lako, deni hili ni kubwa; ndiyo maana TANESCO kwa sababu ya madeni makubwa inatumia nguvu nyingi lakini hailipwi na ndio maana wanafika mahali TANESCO wanataka kupandisha bei ya umeme. Inawezekana sababu mojawapo ni hii. Kama hili deni la shilingi bilioni 794 lingelipwa hata robo tatu, nina uhakika TANESCO ingeweza kujiendesha. Vinginevyo, TANESCO itakufa, itashindwa kufanya kazi yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia viwanda, kama hatuna umeme wa uhakika na wenzangu wamesema kwamba umeme unakatikakatika, lakini kama TANESCO haipewi fedha zake, viwanda hivi vitakufa kwa sababu hakuna umeme wa kutosha. Naomba sana Serikali iangalie na tulishauri mwaka 2014 - 2016 kwenye taarifa ya nishati na madini, wakati deni lilikuwa shilingi bilioni 186, lakini nashangaa kwa nini Serikali haitaki kulipa deni hili, mpaka limefikia shilingi bilioni 794. Naomba sana Serikali deni hili lilipwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunahitimisha hapa, mhusika mwenye taarifa hii alisema, hasa kuhusu deni la TANESCO, shilingi bilioni 794 lazima lilipwe vinginevyo TANESCO itakufa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tulipitisha vizuri kabisa hapa, sheria nzuri kuhusu gesi na mafuta. Sheria ile tukakubaliana kwamba kwa sababu tumepitisha sheria hii, ambayo na kwenye mapendekezo ya Kamati imo, kwamba kukamilisha kwa kanuni ya sheria ya kusimamia, mapato ya mafuta na gesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa tulipitisha mwaka juzi, 2015 nami nilikuwa Mwenyekiti, tukapitisha hapa, tukategemea kwamba Serikali sasa, kwa mfano mwaka jana, 2016 kanuni hizo zingekuwa zimeshakamilika. Mpaka leo kanuni hizo hazijatekelezwa. Hivi tatizo hasa ni nini? Hizi shughuli za gesi na mafuta zinafanyikaje kama kanuni hazipo? Naishauri Serikali itekeleze agizo la Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekubaliana na Kamati imesisitiza, sijui Serikali inapata kigugumizi kwenye eneo gani? Kwa sababu tunategemea umeme wetu kupitia maji kwa maana ya hydro, gesi; lakini tukasema twende mbali zaidi, kwenye umeme wa joto ardhi (geothermal), tutoke hapo twende kwenye solar power.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ukitazama, tumekubaliana humu humu kwenye Bunge suala la umeme wa upepo pale Singida; sasa nauliza, hivi tatizo hasa ni nini? Tukitegemea chanzo kimoja au vyanzo viwili; hydro pamoja na gesi, lakini tunataka tusonge mbele zaidi umeme wetu huu tuuze nje, tupate pesa nyingi za kigeni, lakini tuweze kujitosheleza kwenye umeme wetu wa ndani hasa tunapotaka kwenda kwenye uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda hivi tunavyovisemea, bila kuwa na umeme wa uhakika wa bei nafuu usiokatikakatika, hatuwezi kufika. Itakuwa ni hadithi tu! Ni lazima tujitosheleze na umeme wa kwetu kwa sababu tuna vyanzo vingi, Mungu ametujalia, vyanzo vingi tunavyo isipokuwa ni kuvisimamia na kuvitekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kama tumekubaliana jambo fulani litekelezwe, kwenye eneo fulani, hivi tunashindwa nini kulitekeleza? Leo tuambiane, kwenye geothermal tumesikia asilimia ngapi? Tukubaliane kwenye umeme wa jua, asilimia ngapi? Tutoke hapo twende kwenye umeme wa upepo, asilimia ngapi? Ukitoka hapo, kule Liganga na Mchuchuma ni maneno tu, yanasemwa kila siku; Liganga, Mchuchuma; Liganga, Mchuchuma; hata tutakapokuja tena kesho kutwa, Liganga, Mchuchuma! Ni history tu! Tufike mahali tuseme hili linawezekana, tunaliacha. Nafikiri hata huku kwenye taarifa ya Kamati, limesemwa hili la Liganga na Mchuchuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe umekuwa muda mrefu huku ndani, inawezekana tangu umeanza U-AG Liganga Mchuchuma umeisikia, lakini imefikia wapi? Sijui kuna mgonjwa gani huku anayezuia kila siku! Liganga Mchuchuma kila siku, lakini kama kweli tungeamua tukawekeza pale Liganga Mchuchuma, tungepata umeme wa uhakika, tungepunguza matatizo. Ukiwa na vyanzo vizuri vya umeme nina uhakika hata bei ya umeme itashuka. Ukiwa na vyanzo vingi vya umeme, utauza nje ya umeme wako huu, utapata fedha za kigeni, lakini ni mizunguko tu, tunazunguka lakini hatufiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema mambo matatu haya, kukamilishwa kwa kanuni na sheria za kusimamia mapato ya mafuta na gesi, lakini kuilipa TANESCO deni lake, shilingi bilioni 790, pia kukamilisha kwa miradi mbalimbali ya vyanzo vya umeme, tufike mahali tumalize tuhamie kitu kingine. Mengine najua yamesemwa sana, sitaki kurudia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu kuhusu taarifa hii, ni hayo. Nashukuru sana.