Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Maulid Said Abdallah Mtulia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa namshukuru kaka yangu Mheshimiwa Kuchauka kwa kukubali kunipa nafasi hii badala yake. Pili, nakushukuru wewe Mheshimiwa Mtemi Chenge, kwa kunipa fursa hii adhimu kabisa na namna bora unavyotuendesha katika mjadala wetu huu. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, kwanza, napenda nianze na kuelezea hali halisi ya uchumi na hasa nikichukua Jimbo langu la Kinondoni kama case study. Mimi kama mwakilishi nilijitahidi kupita kwa watu wangu; hali ni mbaya sana kwa wananchi wetu. Imefika mahali katika Manispaa yetu ya Kinondoni, mahoteli yanafungwa, nyumba za wageni zinafungwa, saluni watu hawaendi; hata sasa hivi tumerudi mtu ananunua nyembe anamtafuta mwenzie anampa kitana, anamnyoa nywele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale waliokwenda saluni sasa hivi hawafanyi tena scrub. Akiambiwa afanyiwe scrub, anasema hana muda, ana jambo anawahi. Hali imekuwa mbaya zaidi mpaka kwa akinamama lishe. Dar es Salaam imefikia sasa vijana hawali mchana. Mimi mwenyewe nimeshawahi kukaa na vijana nikawakuta wamechanga, wamesonga ugali wenyewe na samaki wa kukaanga wanakula. Wanakwepa mpaka kwenda kula kwa mama lishe. Hawa akinamama lishe wamekopa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusisitiza hapa, mzunguko wetu wa pesa kwa wananchi ni mdogo sana. Nimesikitika umetolewa mchango hapa na Mbunge mwenzangu kijana, nimekatishwa tamaa sana. Kwa sababu sisi vijana tunategemewa kuja kuwa viongozi wa baadaye na inapofikia kijana haamini, analeta porojo kwenye suala la kiuchumi, mimi imenikatisha tamaa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme suala la bajeti ya nchi yetu siyo suala la vyama, ni suala la Kitaifa. Tunapolichukua suala hili tukalifanya ni la vyama matokeo yake inakuwa mchezo wenu ni mauti yetu. Napenda tuangalie kwanza msingi wa bajeti yetu, kwa sababu inaonekana tulipotoka na tulipo ni tofauti. Hivi msingi wa bajeti yetu ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeambiwa msingi wa bajeti yetu ni Ilani ya Chama cha Mapinduzi; wakati mwingine ni hotuba ya Mheshimiwa Rais; Mpango wa Miaka 25 wa Maendeleo na mengine mengi yanaingizwa hapa. Turudi tuangalie misingi yetu tunayoitumia katika kutengeneza bajeti zetu. Kama utaratibu ndiyo huu, hatuwezi kufika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la bajeti ya nchi tukaikabidhi kuwa eti kigezo kikubwa ni ilani ya chama wakati hili jambo linahusu nchi nzima; nafikiri hapa ni mahali pa kuanza kubadilika. Lazima suala la uchumi wa nchi yetu liwe ni suala la kitaifa, tukubaliane tunataka kwenda wapi na kwa namna gani. Vyama vya siasa vipimwe kwa kutekeleza mpango kwa ufanisi, visiwe vyama vya siasa vinatuletea mipango hapa ya kila siku ya kuibuka. Leo ikipangwa ilani hii, nasi tunaitikia ilani hii, kesho akija Mheshimiwa Rais akatoa hotuba hii, nasi tunafuata hotuba hii. Haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima mpango wa uchumi wa nchi yetu usiwe wa kikundi cha watu wachache, tukubaliane; halafu vyama vya siasa vipimwe utekelezaji wa mpango wetu wa uchumi tuliokubaliana. Wananchi watamchagua mtu kwa kutekeleza mpango wetu tuliokubaliana. Isiwe mtu akipata nafasi ya kuongoza nchi hii, basi yeye ndio awapangie watu waende wapi. Hili nafikiri kuna mjadala hapa inabidi tufanye ili tupate muafaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kuna tatizo kubwa la nidhamu ya bajeti yetu. Ukiangalia bajeti yetu tulichokubaliana na watekelezaji wetu, watu wetu wa Serikali wanavyotekeleza, ni tofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye bajeti, tulikubaliana hapa tutanunua ndege nne; lakini leo unaweza ukasikia mtu anajigamba eti tumeshalipa hela ya ndege sita. Msingi wa bajeti uko wapi? Kwa nini bajeti inapitishwa kama sheria? Leo nchi ya Tanzania imekuwa kama genge; mtu anaamua kufanya matumizi kwenye genge lake na siyo suala la Tanzania kuendeshwa kwa msingi wa bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unaweza ukamsikia kiongozi wetu anakwenda mahali anasema nyie nitawapeni shilingi bilioni 10 hapa mjenge; nyie Magereza nawapa shilingi bilioni moja hapa mjenge; nyie Magomeni, nawapa shilingi bilioni 10 hapa mjenge; nyie sijui Katavi au wapi, nitawapeni hapa mjenge TRA ya shilingi bilioni ngapi! Hatuwezi kwenda kwa mtindo huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nidhamu yetu ya matumizi ni muhimu sana na lazima Bunge liheshimiwe kwa kuwa linapitisha bajeti na inakuwa sheria na ihakikishe inafanya kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti. Hili ni muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli wa mipango yetu; hivi tumeongeza mipango yetu ya maendeleo ya bajeti kutoka 26% au 27% tukaweka asilimia 40; ni kweli tulikuwa tunakusudia kutekeleza? Hivi kweli tunachokipanga tunakusudia kukitekeleza? Kwa nini hatuwi wakweli? Imefika mahali na sisi Wabunge tunapenda kuongopewa. Inafika mahali sisi Wabunge wenyewe tunataka Serikali ije kutuletea muujiza hapa. Nitafanya hivi asilimia 200, nitafanya hivi asilimia 300 mpaka mtu mmoja siku moja akasema kwanza asilimia mwisho 100. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini hatuwi wakweli katika mipango yetu? Hivi wachumi wetu hawa hawajui projection ya mapato yetu? Leo inafika bajeti yetu, tumepeleka mipango yetu, fungu la maendeleo asilimia 20, tena inapelekwa kwenye quarter ya tatu mwezi wa 12. Hivi kweli watendaji wetu, wapangaji wetu wa mipango hawajui uhalisia wa hali yetu? Kama tunataka tubadilike tutoke hapa tulipo, tuwe wakweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiunga mkono sana Kamati ya Bajeti, imeeleza mambo mengi mazuri sana na kwa kweli kama Serikali itayafanyia kazi tutatoka. Nawaomba Wabunge wenzangu, bajeti ijayo na mipango ijayo; mpango ambao siyo realistic tuukatae. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mapato tuliyotegemea kutoka kwa wafadhili imekuja asilimia 16 tu na mapato tuliyokuwa tunayategemea kutoka kwa wafadhili ni zaidi ya shilingi trilioni 10.08. Asilimia sita ni sawasawa na shilingi trilioni moja. Kamati inatuambia kwamba hawajui kwa nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Serikali na kuliomba Bunge lako Tukufu; tuna tatizo sisi na tatizo letu hatutaki kuambizana ukweli. Kuna jambo linasemwa kwamba sisi Zanzibar hatuko vizuri. Sisi ni Watanzania, ni wenyewe kwa wenyewe; hivi Wazanzibari wale wakikaa pamoja kuna tatizo gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili Mheshimiwa Rais aliyepita Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete alitumia nguvu kubwa sana na muda wake mwingi kuwaunganisha Wazanzibari, Wazanzibari wakafika wakawa na Serikali yao ya Umoja wa Kitaifa. Hivi jamani sisi kama Taifa tunakwenda mbele au tunarudi nyuma? Baada ya kufika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, leo tunakwenda tunarudi nyuma? Naomba hili jambo lizungumzwe wale wenzetu wakae pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naamini kabisa, hizi pesa za nje zinakawia; miongoni mwa sababu ni pamoja na huu utengamano wa Zanzibar, inaweza ikawa ni sababu. Hili jambo tusilichukulie kishabiki; ni jambo la Kitaifa, ni letu; sisi ni wenyewe kwa wenyewe, kwa nini tusikae kama Taifa tukatatua tatizo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, viongozi wetu wote wapo na wote walikuwa ma-senior katika uongozi wa nchi hii. Nani asiyemjua Mheshimiwa Maalim Seif, nani asiyemjua Mheshimiwa Mzee Shein? Wote hawa wanajua na wote wana malengo ya kuhakikisha Wazanzibari wanafika mahali pazuri. Tukizungumza kama Taifa, naamini tutatoka na pesa hizo tutazipata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni kwamba mipango yetu haizingatii hali yetu ya kimazingira. Hivi sisi tangu nchi hii imeumbwa, kuna samaki kule baharini wanapita, wanavuliwa huku juu Somalia, South Africa, wanapita wale samaki kila siku. Nimeongea na wataalam wa samaki wanasema, wale wanakua na wakishakua wanakufa. Sisi tangu tumepata uhuru nchi hii hatujawahi kutumia resource ile ya samaki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Magufuli kuna kipindi aliikamata ile meli, wakapatikana samaki wengi, yule mtaalam anawaambia Watanzania hawajui hata resources zilizopo kwenye bahari yao, wananchi waliambiwa waende wakachukue samaki watu wamekwenda na mabeseni, kumbe samaki mmoja beseni halitoshi.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani, kwa nini hatuangalii mazingira yetu, Tanzania kwa jiografia yetu tunapokuwa maskini wenzetu hawatuamini, hawatuelewi, hawaelewi kwa nini tumekuwa maskini sisi, lakini sisi tukipanga mipango hatuangalii jiografia yetu, hatuangalii vitu gani sisi tunavyo wengine hawana, tunataka kufanya vitu wanavyofanya watu wasiokuwa na vitu kama vya kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaimba tu hapa viwanda, hivi sisi kweli tunaweza kwenda kwenye viwanda, kwa nini tusiende kwa yale tunayoyaweza. Sisi tunaweza kulima na watu wetu wanakuwa kwenye kilimo na tuliambizana hapa kilimo ndiyo uti wa mgongo, hayo ni majina – Kilimo Kwanza, kilimo cha kusonga mbele, majina yalikuwa mengi, lakini kimsingi kilimo ni uti wa mgongo. Kwa nini hatu-invest kwenye kilimo? Leo tunategemea…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. MAULID S.A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.