Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupembe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kushukuru kwa kupewa nafasi hii, lakini pia namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa kuwasilisha Mpango mzuri ambao unaonesha mwanga wa maendeleo katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kwamba, ili tuweze kuendelea na kufikia uchumi wa kati, tunahitaji mipango mizuri kama ilivyooneshwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2016/2017 na 2016 - 2020. Katika Mpango huu kuna sehemu moja ambayo nitaiongelea sana hasa miundombinu ya barabara. Ili tuweze kuendelea kama nilivyosema, ni lazima tuwe na barabara nzuri ambazo wakulima wengi wanazitegemea, lakini pia hata viwanda vinategemea barabara au miundombinu. Barabara nyingi zinazokwenda vijijini ambako ndiko tunakoweza kupata malighafi za kuendeshea viwanda vyetu ambavyo tunasema kwamba tunataka tuingie kwenye uchumi wa viwanda, ni mbaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokuwa na barabara nzuri, tunapokuwa na barabara za lami inakuwa rahisi kwa wakulima hawa kuweza kusafirisha mazao yao ambayo ndiyo malighafi za viwanda na hatimaye wakaweza kuuza mazao yao kwa haraka zaidi na yakapata bei nzuri zaidi; lakini siyo bei tu, hata ubora wa mazao yao na ubora wa bidhaa ambazo zitatokana na haya mazao zitakuwa bora zaidi na hatimaye kuweza kupata faida kubwa au kupata products ambazo zinaweza kuuzwa hata nchi za nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilivyo sasa hivi, products zetu nyingi zinakataliwa, haziwezi kupata soko la nje kwa sababu tu hazina ubora na inaonekana kwamba ubora huu unakosekana kwa maana ya kwamba bidhaa nyingi zinafika kiwandani zikiwa zimechelewa au zimeharibika. Kwa mfano, kama bidhaa za matunda, zinafika kiwandani zikiwa zimeharibika. Kwa hiyo, hata zao lake au lile zao linalokuja kutoka kiwandani linakuwa halina ubora na hatimaye zinakataliwa kwenye masoko mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba pia Mpango uweze kuboresha miundombinu ya barabara. Kwa mfano, katika maeneo ya uzalishaji, mimi natoka Jimbo la Lupembe ambapo sehemu kubwa tunazalisha chai, lakini tunazalisha matunda, mananasi, tunazalisha matunda mengine kama parachichi na mengineyo. Barabara za kule hazipitiki kwa hiyo, wakulima wanashindwa kuuza mazao yao.
Mheshimiwa Waziri hasa Waziri wa Ujenzi, ukienda kuangalia jinsi gani wananchi wanavyomwaga haya mazao, jinsi gani chai inavyomwagwa kila siku, utawaonea huruma na utatamani kulia. Kwa hiyo, tuombe miundombinu hasa ya maeneo haya ambayo yana uzalishaji mkubwa, barabara zitengenezwe vizuri ili hatimaye wananchi waweze kuuza mazao yao na hatimaye kupata faida na kama Taifa kuweza kuongeza uchumi wa nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara zetu kwa mfano nikisema hii ya Lupembe, ilishaingia kwenye ilani ya mwaka 2010 kwamba itatengenezwa kwa kiwango cha lami na mara moja kwenye Bunge la Bajeti fedha zilishakadiriwa kwamba tutapewa, lakini fedha hazikutoka. Nashangaa mwaka huu pia sijaiona kwenye Mpango kama itaaanza kutekelezwa hasa huu Mpango wa mwaka 2016/2017 wakati tayari ilishaahidiwa kwamba hii barabara itatengenezwa kwa kiwango cha lami.
Kwa hiyo, nakuomba Waziri wa Ujenzi nafikiri unanisikia vizuri sana na ni msikivu, hebu tujaribu kuingiza au tuingize kwenye Mpango ili sasa mazao haya ya chai na chai ya Lupembe mnaifahamu ni chai bora na ilikuwa ni moja ya chai bora duniani, ilikuwa na soko kubwa sana na zuri sana. Waliokuwa wanafuatilia mambo ya soko la chai wanajua jinsi gani ile chai ilivyokuwa na soko zuri duniani, lakini leo imepotea kwa sababu pengine ya ubovu wa njia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika Mpango wetu naomba tuangalie sana maeneo yale ambayo wakulima wanazalisha mazao mbalimbali hasa mazao ambayo yanaweza kuuzwa nchi za nje na yakatuingizia fedha za kigeni. Kwa hiyo, tukifanya hivyo, tutawawezesha wananchi hawa kwanza kuuza mazao yao, lakini pia hata bidhaa zetu ziwe na ubora na kwa kupitia hivyo tutaweza kupata fedha za kigeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia barabara zinapokuwa nzuri, tunawavutia wawekezaji. Tunasema tunaenda kwenye uchumi wa viwanda, wawekezaji hawawezi kwenda kuwekeza kwenye maeneo kama ya Lupembe ambapo barabara haipitiki wakati wa kifuku; maana yake ni kwamba, watapoteza kwa maana ya kwamba watazalisha lakini hizo bidhaa zao au mazao yao ambayo wamezalisha, hawataweza kuyauza yakiwa na ubora wake kwa sababu ya ubovu wa barabara. Kwa hiyo, maeneo haya ya uwekezaji ni lazima tuhakikishe kwamba barabara zinapitika muda wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, viwanda tunavyovifikiria, ni lazima viwekezwe au twende tukaviwekeze kwenye maeneo ambayo yana uzalishaji. Inakuwa haipendezi wala haina tija kwa mkulima kama kiwanda kinakuwa mbali na maeneo ambayo hawa wakulima wanazalisha. Inapokuwa hivyo ni kwamba, wananchi, wale wakulima wanakosa bei nzuri ya mazao kwa sababu hapo katikati wanacheza wale middlemen, wananunua bidhaa kwa wakulima kwa bei ya chini na wanawauzia wamiliki wa viwanda kwa bei ya juu. Kwa hiyo, tayari wakulima wetu wanapoteza soko la bidhaa zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili tuweze kuwahamasisha wakulima, lakini pia wakulima wetu waweze kupata tija ya mazao wanayozalisha, ni lazima tuwavutie hawa wawekezaji wa viwanda mbalimbali kwenye maeneo ambako hawa wakulima wanazalisha, ndipo hapo utaweza kuwasaidia wakulima wakapata tija kwa kilimo chao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda peke yake na barabara peke yake haitoshi. Ni lazima huduma za msingi hasa huduma za afya kwa maana ya Hospitali, Zahanati na Vituo vya Afya vijengwe kwenye maeneo haya ambayo kuna uzalishaji mkubwa, lakini pia kuna viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika Halmashauri yangu ya Wilaya ya Njombe haina hospitali hata moja. Sasa hutegemei maeneo kama hayo wawekezaji watakuja kuwekeza kwa kuwa huduma ya afya haipo. Ni lazima tuangalie upande mwingine. Tunapotaka kuwekeza tuangalie na factors nyingine ambazo zinaweza zikasababisha wawekezaji waweze kuwekeza au inaweza ikasababisha viwanda vyetu viweze kukua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilivyo sasa hivi ukiangalia hata kwenye Mpango, viwanda vingi vimeelekezwa mijini. Sasa vinavyoelekezwa mjini tunawanyima asilimia zaidi ya 80 ya wakulima wanaoishi vijijini au watu wa vijijini. Kwa hiyo, tukitaka kufungua fursa za ajira, ni lazima tufikirie sasa kuanza kuwekeza kwenye maeneo ambako wakulima wapo na vijana wengi wanaishi ili tufungue ajira huko vijijini, watu wabaki vijijini kuliko sasa hivi wote wanavyokimbilia mjini. Sasa kama watakimbilia mjini, nani atakayezalisha huko vijijini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema kwamba tunafungua viwanda kule Ludewa, sasa bidhaa nyingine ambazo zinategemea hivi viwanda, watapata wapi kama hatutaweka mazingira rafiki ya kuwawezesha vijana wetu waweze kubaki vijijini? Kwa hiyo, tunaomba kwenye Mpango pia tuweke vizuri ili hatimaye tuweze kuhakikisha kwamba tunaweza kufanikiwa hasa kuingia kwenye uchumi huu wa kati ambao ni uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nishati, nalo ni suala ambalo linaendana pamoja. Tukitaka tuvutie wawekezaji wa viwanda hivi vya kati na vikubwa, ni lazima tuhakikishe kwamba maeneo yetu mengi yanakuwa na nishati ya kutosha; yanakuwa na umeme wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilivyo sasa hivi, kwa mfano, eneo langu ni la uwekezaji; kuna mazao mengi ambayo yana tija ambayo watu wengi wanaweza wakapata faida, lakini wawekezaji wanashidwa kuwekeza kwa sababu umeme siyo wa uhakika. Kwa hiyo, naomba Waziri wa Nishati pia katika Mpango huu tujaribu kulifikiria kuhakikisha kwamba tunasambaza umeme katika maeneo ya uzalishaji hasa maeneo ya Lupembe ambako kuna wawekezaji wengi wazuri, wanakuja lakini hawawezi kuwekeza kwa sababu hakuna nishati ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nijaribu kulisema kidogo juu ya Mpango huu, tujaribu kujadili juu ya kuhakikisha kwamba hawa vijana au wananchi ambao tumesema tutawezesha kwa kuwapa Shilingi milioni 50 kila Kijiji, ni lazima tutengeneze mpango mzuri hasa kwanza, kutoa elimu ya ujasiriamali; elimu ya matumizi ya hii mikopo ambayo tunaipanga iende kwa wananchi kule vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wengi walioko vijijini hawana elimu ya kutosha ya ujasiriamali, hawana uelewa wa kutosha wa ku-generate mkopo na mwisho wa siku wapate faida. Ni lazima tuweke mpango ni jinsi gani tutatoa elimu kwa wananchi wa vijijini ili mkopo huo wakiupata waweze kuutumia vizuri na mwisho wa siku waweze kupata faida na ile faida iweze kurudishwa na hatimaye tuweze kuongeza uchumi wa kila mmoja na hatimaye uchumi wa Taifa zima kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima tujipange kuhakikisha ni jinsi gani tutatoa elimu na siyo kutoa elimu tu; jinsi gani tutawasaidia katika kuwatafutia masoko ya bidhaa ambazo pengine watakuwa wanazalisha ili ule mkopo uweze kuleta tija? Tukiwaacha tu hivi hivi tukapeleka tu zile fedha, itakuwa kama ilivyokuwa yale mamilioni ya Kikwete. Zitaenda fedha nyingi na mwisho wa siku kitakachorudi, hakuna. Kwa hiyo, tutakuwa tumepoteza mamilioni mengi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo nafikiri inatosha. Nashukuru sana na naunga mkono hoja.