Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Ally Mohamed Keissy

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza kabisa, naipongeza Wizara ya Nishati na Madini hasa Mkurugenzi Mkuu wa REA na Mkurugenzi wa TANESCO kwa kusaidia mradi wa kupeleka umeme kwenye Bwawa la Mfii, tegemeo kubwa la
maji Namanyere kupunguza kutoka shilingi bilioni 59 mpaka shilingi bilioni 23.

Mheshimiwa Naibu Spika, dawa ya deni ni kulipa. TANESCO inadaiwa shilingi bilioni 820 na TANESCO yenyewe inadai pesa. Kuna Mashirika maalum yanadaiwa pesa. DAWASA, Idara ya Maji, inadaiwa; yenyewe inauza maji, kwa nini isilipe hela za TANESCO? Wakala wa Umeme Zanzibar (ZECO) wanadaiwa pesa shilingi bilioni 123. Wakala tofauti na kitu chochote, ni sawa na mimi na duka langu, wewe unaleta mali yako nakuuzia kwa bei unayonipa mimi nakurudishia zile hela. Cha ajabu ZECO hairudishi hela TANESCO, ni aibu! Serikali nzima ya Bara inadaiwa shilingi bilioni 40, ZECO inadaiwa shilingi bilioni 123, tutafika wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba TANESCO wawe na mtindo wa kukatia umeme popote wanapodai.
Haiwezekani kuleana namna hii! Kuna Wizara zote za Serikali ya Bara zinadaiwa. Hakuna Wizara hata moja isiyodaiwa na TANESCO, ni ajabu. Mtu binafsi, mwanakijiji ambaye hana mbele wala nyuma, ananunua umeme kwa LUKU. Mwisho wa mwezi hana hela, hapati umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Wizara za Serikali hapa pamoja na Mashirika ya Serikali makubwa, hayalipi deni la TANESCO. Haiji kwenye akili ya binadamu kabisa! Dawa ya deni ni kulipa. Mwanakijiji hana mbele, hana nyuma, hana chochote analipa deni la TANESCO, anawekewa LUKU. TANESCO lazima ifanye operation nchi nzima hasa miji mikubwa. Kuna wizi wa ajabu wa umeme katika nchi hii. Kuanzia Dar es Salaam, Arusha, Mbeya, Sumbawanga, popote pale kwenye mji mkubwa, kuna wizi mkubwa wa umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara ya Nishati na Madini, kama haina wafanyakazi wa kutosha wakaazime JKT. Wachukue kwenda nyumba kwa nyumba, kijiji kwa kijiji; haiwezekani Shirika kupata hasara namna hii! Kuna wizi mkubwa wa umeme! (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile naiomba Serikali, msongo wa umeme kutoka Mbeya kwenda Kigoma kupitia Sumbawanga na Mpanda, hii mikoa mitatu au minne hii, inaleta hasara kubwa sana kwa Shirika hili la Umeme. Tunatumia majenereta, mafuta yanalika kwa kiasi kikubwa, hakuna faida TANESCO inapata kwenye Mikoa hii ya Kigoma, Katavi na Rukwa, Shirika hili linapata hasara, ndiyo maana Shirika hili linaingiza hasara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, haiwezekani tusipate umeme wa gridi ya Taifa kutoka Mbeya kwenda Kigoma mpaka Nyakanazi ili kuondoa mzigo kwa TANESCO. Haiwezekani mchakato kila siku; tupate umeme wa uhakika. Kwingine wanapata umeme wa uhakika, lakini mikoa hii mitatu, ni majenereta tu yananguruma. Kwanza yanaharibu mazingira kwa kusababisha moshi mijini. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu REA. Tatizo la REA ndugu zangu ni kutokupata hela za Serikali. Tuliamua hapa mafuta shilingi 150 iende REA, lakini hela haziendi. Asilimia 40 ndiyo hela zinakwenda, zikiingia Hazina hela zile, hazitoki kwa wakati. Wakandarasi hawafanyi kazi kwa sababu hawapati pesa. Mradi wa shilingi milioni 200 utafika milioni 300 kwa riba kwa sababu pesa hazipelekwi kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali, hela tunazoamua hapa Bungeni za 150 kila lita ziende moja kwa moja REA. Haiwezekani zikifika Hazina zinakwama zinatoka kwa masharti au zinabadilishwa njiani, haiwezekani. Kwa hiyo, naiomba Hazina ipeleke hela za REA ili wananchi wafaidike na umeme. Hatuwezi kumaliza vijiji hivyo 7,000 kama pesa haziendi, tunadanganyana hapa. REA wanapata kiwango cha chini cha pesa, hawawezi kuendelea kuweka umeme vijijini kama hawapati pesa. Tumeamua hapa na mafuta ni hot cake, mafuta
yanauzika. Tunauza mafuta, hela zinaingia, lakini hazijulikani zinakokwenda. Haiwezekani, lazima
wapewe pesa zinazohitajika ili Wakandarasi waanze kazi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naishauri TANESCO, sehemu za mapori makubwa, REA wapeleke nguzo za zege kuondoa hujuma ya kuchoma mapori na nguzo kuungua. Kuna mapori mazito na watu wetu hata ukiwapigia mbiu, useme mpaka uchoke, lakini kila msimu
lazima wachome mapori. Hawa watu ni hatari sana! Kwa hiyo, nawaomba, sehemu ambazo ni misitu minene, waangalie kutafuta nguzo za zege ili kuepuka kuitia hasara TANESCO. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimefurahi na REA III. Waziri ametuhakikishia kwamba transformer zote na waya zote watanunua katika viwanda vyetu. Hiyo itasaidia kabisa kwanza kuharibu hela zetu za Kigeni kwenda kununua transformer mbovu nje au China wakati Arusha
kuna transformer imara na zinatosha miradi yetu kuzalisha umeme. Tuna viwanda vingi pamoja na TANESCO ina-share katika East Africa Cable, wanunue waya pale. Haiwezekani kwenda kununua waya nje wakati tuna waya zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile wajiepushe kupitia Wakandarasi ambao ukienda, inapitia kwa watu wanazidisha bei ajabu! Miradi ya ajabu; unakuta mtu unayechukua tenda kuagiza waya nje, haijulikani ananunua bei gani kule anakuja kutubamiza bei wakati tuna viwanda vyetu wenyewe hapa nchini. Huu ni ubadhirifu na ufisadi wa hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu bandari. Ndugu zangu hii nchi ina bandari Mungu kaibariki. Nilikwenda Bandari ya Mtwara hata Afrika Kusini hakuna bandari kama ya Mtwara. Bandari ya Tanga ambayo ingesaidia Mkoa wa Kilimanjaro, Mkoa wa Arusha, Mkoa wa Manyara na Mkoa wa Mara na Tanga yenyewe, ni ajabu watu wa Tanga na Kilimanjaro wanatumia Bandari ya Mombasa. Ni aibu kubwa kwa Serikali, wakati tuna bandari yetu wenyewe. Mungu katupa bandari katika mwambao wa bahari, lakini ni ajabu tunatumia Bandari ya Mombasa kuliko kutumia Bandari ya Tanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta mpaka watu wa Dar es Salaam, wafanyabiashara wa Dar es Salaam wanatumia Bandari ya Mombasa, ni aibu kubwa kwa Serikali. Ni aibu, tumekuwa kama Burundi au Rwanda ambao hatuna bandari! Tujiulize mara mbili mbili, kuna nini hapa?
Kuna mdudu gani? Lazima tuimarishe bandari zetu ili wananchi wafaidike na bandari zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kwenda hovyo hovyo, tunafanya kazi hovyo hovyo. Serikali iwe kali kidogo kwa kiongozi yoyote anayeingia tenda, manunuzi ya ajabu ajabu yanayotuumiza sisi, mdudu wa manunuzi huyu; lazima achukuliwe hatua kali. Haiwezekani wewe kitu unajua, hata mimi ambaye sikusoma na wala sio Mkandarasi, unajua kabisa hiki kitu sh. 10/= unakwenda kuandika sh. 500/= na unatia saini cheque inatoka! Kusema ukweli hao ndio maadui wa nchi. Hawa nilikuwa nazungumza siku zote! Huyu mdudu manunuzi, tungewakamata hawa tukawapiga risasi siku ya Ijumaa au Jumapili watatu au wanne, wangeshika adabu. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani hii Serikali ni tajiri kuliko Ubelgiji, kuliko Ureno, leo unashangaa hapa wanasema Ureno inajenga reli ya kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro. Ni aibu, wakati sisi ni matajiri kuliko Ureno. Ureno maskini wa Mungu wale leo hata chakula
hawana. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali ifuatilie. Naishukuru sana REA lakini wapewe hela kwa wakati ili wafanye miradi yetu na vilevile wafikirie vijiji ambavyo viko nyuma sana, kuna mikoa iko nyuma sana, ndiyo waelekeze REA III. Kuna mikoa mingine kuna umeme
mpaka chooni. Sasa watufikirie na sisi kule Rukwa ambao tumekuwa nyuma kabisa, tumepata umeme miaka miwili iliyopita. Ni ajabu kabisa katika nchi hii! Ndiyo tufikirie zaidi kutupelekea huu mradi wa tatu na wananchi wetu wapate mwanga. Wananchi wa kule siyo wezi kama hawa
wa Dar es Salaam au Dodoma. Huku kuna wizi; tukipita leo hapa hapa Dodoma, tutakamata wezi siyo chini ya 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani Shirika lipate hasara, ni wizi mkubwa! Pamoja na mashule haya, viwanda hivi, wanasaga usiku, wote ni wezi. Kwa hiyo, nawaomba sana Wizara ya Nishati na Madini wanisikilize. Operation maalum ifanyike, pamoja na Waheshimiwa Wabunge humu tumo, haiwezekani. Ndiyo nimesikia juzi juzi wanalaumu sana Ma-DC. Leo kuna Wabunge walikuwa Ma-DC humu, walikuwa wanakemea mpaka bangi, Mheshimiwa Mwamoto ni shahidi kule Kibondo, lakini leo ni Mbunge, akiona bangi,…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Anaogopa kura zake zitapotea.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Keissy muda wako umekwisha, ahsante sana.