Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa
nafasi niweze kutoa mchango wangu.
Kwanza nianze kumpongeza sana Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu kwa kazi nzuri
waliyofanya katika kuandaa taarifa yao. Pia nimpongeze Waziri na Wizara yake, wamekuwa
wakifanya vizuri sana kwenye barabara zetu za Geita kwa ujumla, tunaona kazi za TANROADS
zinavyofanyika vizuri, hatuna mashaka. Lakini zipo changamoto ndogo ndogo ambazo
tunaiomba Wizara iweze kuzipa kipaumbele barabara ambazo tayari Mheshimiwa Rais wa
Awamu ya Tano akiwa Waziri alianzisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kutoka Geita kwenda Kahama, lakini na
barabara ya kutoka Bwanga kwenda Biharamulo na kwenda Runzewe, yakikamilishwa haya
ataongeza tija sana kwenye Mkoa wetu wa Geita. Pia nimuombe Waziri aendelee kuona
huruma zile kilometa 57 tulizoahidiwa kwenye Jimbo la Geita Vijijini, sisi wenzenu huko
tulikozaliwa vijijini hatujawahi kuona lami kabisa, tunaiona mjini tu kwa wale ambao wanapata
bahati ya kusafiri. Sasa angalau kwa mwaka huu ukianza hata kilometa moja/mbili na sisi
tukapata kuzungumza kwamba tunaanza kuingia kwenye dunia ya Awamu ya Tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini kwa
kazi nzuri ya kuandaa taarifa pamoja na changamoto mbalimbali mlizokumbana nazo. Niiombe
Wizara pamoja na kwamba wametuwekea umeme kwenye Jimbo la Geita Vijijini, tumepata
umeme mijini tu, kwenye vijiji vingi ambavyo vinazalisha hasa vya wakulima, umeme haukuingia,
lakini tumeahidiwa kwenye REA Awamu ya Tatu mtatukumbuka. Nimuombe Waziri kwa huruma
yako uwaangalie wananchi wa Jimbo la Geita Vijijini katika vijiji ambavyo tumeviomba
viingizwe kwenye REA Awamu ya Tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kushauri, nimekuwa nikizungumza hapa mara nyingi
kuhusiana na suala la wachimbaji wadogo kwenye Mkoa wangu wa Geita na kwenye Jimbo
langu la Geita. Wananchi wa Geita wamekuwa na kilio cha muda mrefu sana na awamu zote
tumekuwa tukiahidiwa, Awamu ya Tano ilipofika tulipomuomba Mheshimiwa Rais aliona huruma
na akaturuhusu tupewe magwangala. Sasa nimuombe ndugu yangu Mheshimiwa Profesa, ni
kweli ulivyotuahidi kwamba mnang‟ang‟ania kuomba magwangala mtakiona cha moto, sio
mchezo tuliona cha moto kweli kweli maana badala ya kupewa magwangala tulipewa mawe
ya kujengea nyumba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikawaambia ndicho ulichokiahidi kwenye mkutano kwamba
tutakiona cha moto, tulivumilia tu, tumekula hasara na wananchi wangu sasa hawana tena
shida na magwangala kama ulivyosema. Wamenituma nikuombe kwa kuwa eneo la GGM ni
kubwa na wewe ni mtaalam wa miamba ninaamini hutarudia tena kuwapa kwa sababu sisi na
wananchi wangu wote ni darasa la saba kule, hawana utaalam wa miamba kule sisi tuna
utaalam moko tu kuchimba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe kwa kuwa wewe ni Profesa, term hii basi usirudie
kuwapa na wewe ule mwamba wa mbali kama uliowapa mwaka 2012, uwaangalizie
Nyamatagata na Samina walipokuomba. Ni sheria, sasa imeshapita miaka mitano, wamege lile
eneo ambalo wachimbaji wangu wakienda na la saba lao wakichimba tu wakifika kwenye
magoti angalau wawezi kupata hata dhahabu kidogo kidogo kufidia yale machungu ya
SACCOS zile ulizoziunda wewe. Kwa kweli cha moto tumekiona, na tumeamini Profesa wewe ni
bingwa kwa sababu wa darasa la saba tumefeli kwenye hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe tu Mheshimiwa Waziri, kumekuwa na kilio cha
muda mrefu sana kwa wananchi wa Wilaya ya Geita kwenye eneo la STAMICO, na eneo
linalopiganiwa ni dogo sana na wewe ulivyokuja kule term hii ulituahidi leseni zile zinaisha mwezi
wa tisa, tunazisubiria, ama uwape wazungu au uturudishie, hapo hatutajali cha Profesa
tunaanguka la saba kwa nguvu mule.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nikuombe sana usi-renew hiyo leseni bila kumega
eneo ukatupa la saba na sisi tukapate riziki pale, tumelia mara nyingi Rais ametuahidi,
umetuambia kuna kesi ya Sinclair lakini Sinclair, wewe unazo message kwenye mtandao wake
anamtukana mpaka Mkuu wa nchi, kwamba anaendesha nchi kibabe na unaijua hiyo email,
lakini bado unasema tukimnyang‟anya ile atatupeleka mahakamani.
Sasa kama muda wake unaisha mwezi wa tisa wallah nakwambia la saba tutakaa pale,
yaani ikifika tarehe 27,28 tunaanguka porini. Na ulituahidi ukajisahau ukatamka na tarehe,
bahati nzuri la saba huwa hatusahau tarehe, tunasahau kila kitu tarehe 28 tuko kwenye lile
eneo, tutalichukua kwa nguvu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niliona mchakato wa EWURA wakati anatumbuliwa
Mkurugenzi wa EWURA nikawa najaribu kujiuliza, hivi kweli kwa nini Mkurugenzi wa TANESCO
anatumbuliwa peke yake na Wakurugenzi wale wengine, ni kwa sababu kweli walifanya vikao
mpaka wakakubaliana na EWURA bila Profesa kupita kuona documents zile? Nikawa
nashindwa kuelewa, nikasema ipo siku ntapata nafasi, ninayo document ya Mheshimiwa
Profesa Muhongo ambayo yeye mwenyewe anamwandikia Mheshimiwa Dkt. Mpango tarehe
30, Septemba akimpelekea mpango kazi wa TANESCO, na wameweka mapendekezo yao
humu ndani ukihitaji nitakupa kama unahitaji wanamuomba EWURA kufikia mwezi wa 12 awe
amepandisha umeme, na yeye ameisaini hii document, iko saini yako hapa usitikise kichwa
ntakukabidhi Mheshimiwa.
Baada ya mwezi wa 12 amevua koti tena akawasakizia wenzie, na saini yake iko humu.
Naomba sana hebu tuangalie tusiwe tunatumbua tu watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, lile la wachimbaji wadogo…
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, lile la wachimbaji wadogo kupelekwa kupewa ruzuku ya Katavi…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Musukuma muda wako umekwisha. Ahsante.