Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Doto Mashaka Biteko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. DOTO M. BITEKO – MWENYEKITI WA KAMATI YA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa
Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii nikushukuru sana wewe kwa kunipa fursa hii, lakini
vilevile niwashukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini pamoja na Waziri wa
Nishati na Madini na Wabunge wote waliochangia hoja hii. Kwa kweli michango yao imekuwa
mizuri na imeboresha sana taarifa yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wachangiaji kwenye hoja yetu walikuwa 32, hawa wote 32
wamechangia kwa kusema, lakini Waheshimiwa Wabunge tisa wamechangia kwa kuandika.
Katika kujumuisha hoja yetu nitaelezea tu mambo machache ambayo yamejitokeza kwenye
michango ya Waheshimiwa Wabunge na wachangiaji wengine kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo kubwa ambalo Waheshimiwa Wabunge wengi
wamelichangia ni suala la umeme, na suala la umeme hili wamelijadili katika maeneo yote
mawili – upande wa TANESCO na upande wa REA, hoja hii imechangiwa na Wabunge 27. Kwa
upande wa TANESCO, Waheshimiwa Wabunge wengi wameeleza masikitiko yao, wameeleza
msisitizo wao, wametoa maoni yao juu ya madeni ya TANESCO na kuomba kuwepo kwa
namna ambayo TANESCO itaweza kutoka kwenye mkinzano huu wa madeni makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye upande wa REA, Waheshimiwa Wabunge wengi
wamezungumzia juu ya usimamizi wa miradi ya REA, wamezungumzia vilevile upelekaji wa
fedha za miradi ya REA na na wakandarasi kuwashirikisha viongozi wakati wakandarasi hao
wanapokwenda site na kuongeza ule wigo (scope) kwenye maeneo ambako miradi hii
inakwenda. Mambo haya yote kwenye taarifa yetu tuliyaeleza na Waheshimiwa Wabunge
nawashukuru sana kwa michango yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa madini jumla ya Wabunge 19 wamechangia
hoja hii, na mambo yaliyojitokeza kwenye michango yao ni pamoja na suala la wachimbaji
wadogo wadogo. Kwanza wachimbaji wadogo wadogo kupatiwa maeneo ya kuchimba, lakini
vilevile wachimbaji hawa wadogo wadogo kupatiwa ruzuku ili iweze kuwasaidia kuchimba
kisasa. Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia vilevile hili jambo la wachimbaji
wadogo wadogo kuvamia leseni za wachimbaji, jambo hili kwenye Kamati pia na Serikali ilitupa
ufafanuzi wa kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia wamezungumzia suala la Tanzanite. Tanzanite
kupatikana Tanzania na Tanzania isiwe ya kwanza kwenye muuzaji wa Tanzanite linawakera
Waheshimiwa Wabunge wengi kama ambavyo linawakera Watanzania wengi. Lakini naomba
tu nitoe taarifa, Serikali jambo hili imelichukua kwa uzito wake na kwenye kamati tulipewa
taarifa kwamba Serikali imepeleka ukaguzi maalum (special audit) na nilidhani tusizungumze
sana hili kwa sababu baada ya taarifa ile kuja tutakuwa na mahali pa kuanzia kuishauri Serikali
vizuri. Kwa hiyo, nadhani hili tuiachie Serikali kwa sababu imeshalichukua kwa uzito wa aina
yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia STAMICO,
Wabunge sita wamechangia juu ya STAMICO na wameelezea juu ya kuhodhi maeneo mengi
ya STAMICO. Hili ni kweli, lakini hata kwenye kamati wajumbe walilizungumza kwa uchungu sana
kwa sababu STAMICO ana maeneo mengi ambayo ameyashikilia lakini hachimbi, ameingia
ubia na wawekezaji, wale wawekezaji kwa miaka karibu 12 hakuna wanachofanya. Tunaitaka
na kuiomba Serikali kwamba sasa ifike mahali hawa wabia walioingia JV na STAMICO waanze
kufanya kazi, vinginevyo itakuwa ni kupoteza muda.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wanaovamia yale maeneo ambayo yako dormant
utakosa sababu ya kuwaondoa kwa sababu wewe hilo eneo umelishika. Kwa mfano
Mheshimiwa Bukwimba amezungumzia suala la Bacllif. Pale kuna leseni 12 ambazo STAMICO
wameingia mkataba pamoja na TANZAM 2000; lakini toka wameingia makubaliano hayo
hakuna kinachoendelea. Kwa hiyo, wananchi wale wanaweza kuvamia kwa sababu hawaoni
jambo lolote linaloendelea, na Serikali imechukua hatua juu ya jambo hili, inaielekeza STAMICO Mheshimiwa Naibu Spika, na niwaombe Waheshimiwa Wabunge waliopendekeza
kuifuta STAMICO, mimi nadhani tui-capacitate STAMICO. Itakuwa ni jambo la aibu sana sisi
wenyewe, Serikali, Watanzania tunaanzisha shirika letu wenyewe tunaliua halafu tunaanzisha
lingine, kwani Watanzania tutawatoa wapi? Si ni hawahawa tutakaowapata kuunda shirika
lingine? Mimi nilikuwa naomba tuipe nguvu, tuisimamie vizuri STAMICO iweze ku-deliver kwa
wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachopungua pale STAMICO ni mambo mawili; jambo la
kwanza ni upelekwaji wa fedha lakini jambo la pili ni usimamizi ulio madhubuti. Mimi naomba
nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Wizara, kila mara wanapitishapitisha mikono yao pale
STAMICO. Ninaamini baada ya muda fulani pengine tunaweza tukaona matokeo yanabadilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, upo mgodo wa Serikali ambao ni wa Stamigold. Mgodi huu
unasimamiwa vizuri sana na Watanzania, kuanzia mfagizi, mlinzi mpaka MD wa mgodi ule ni
Mtanzania, mswahili mwenzetu. Nao wana changamoto ambazo wamezieleza. Changamoto
ya kwanza wanayoizungumzia hawana MDA, ile Mining Development Agreement,
tumewaomba Serikali wahakikishe wanafanya kazi ya kuwapatia hiyo MDA.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile mitambo waliyonayo yote ni ya kukodi hawana
mtambo hata mmoja wa kwao, jambo ambalo linasababisha gharama ya uendeshaji wa
mgodi ule kuwa kubwa sana, zaidi ya asilimia 31.7 ya gharama za uendeshaji zote zinakwenda
kwenye ukodishaji wa mitambo. Tumeiomba Serikali na katika hili nitumie nafasi hii kuiomba
Wazara ya Fedha kama migodi mikubwa ya kigeni tunaipa exemption ya mafuta, kwa nini
mgodi wetu wenyewe wa Stamigold ambao kwa asilimia mia moja ni wa Serikali, na wenyewe
tusiupe exemption ili na wao wapunguze gharama za uendeshaji, tuapte faida haraka?
Tunatoa fursa hii kwa wageni, migodi ya ndani tunaibinya, nilikuwa naomba jambo hili
lichukuliwe kwa uzito wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wamezungumza juu ya mafuta, ujenzi wa farm tank na hili
tumelipata kutoka kwa wadau wote tuliokutana nao, wameeleza umuhimu wa kuwa na
Central Storage System ya mafuta baada ya kuwa yamepakuliwa kabla ya kusafirishwa
kwenda kwa watumiaji wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudie tena, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa
michango yao na kwa kweli niseme toka nimekaa kusikiliza mchangiaji wa kwanza mpaka wa
mwisho mimi binafsi nimejifunza vitu vingi. Wameona mambo haya kwa macho ya tofauti
pengine na kamati tulivyoona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninaomba sasa Bunge lako likubali
kuipokea taarifa hii na kuwa Maazimio ya Bunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.