Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia Taarifa zilizoko mbele yetu. Awali niwashukuru sana watoa hoja wote, Kamati zote mbili kwa taarifa zao nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda nitakwenda straight kwenye hoja. Naomba nianze kwa kusema kwamba, tunayo hifadhi moja tu Tanzania yenye urithi wa kipekee, hifadhi ambayo ina vivutio ambavyo haviko sehemu nyingine Tanzania, Afrika na hata Dunia nzima na ni Hifadhi yetu ya Ngorongoro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hifadhi ambayo imekuwa inatuingizia kipato kikubwa sana kwa Taifa hili, lakini kwa karibu miaka 10 sasa, hifadhi hii isipoangaliwa kwa makini inakwenda kupotea ndani ya Tanzania. Hifadhi hii imewekwa ndani ya Urithi wa Dunia, imeingia kwenye Maajabu saba ya Dunia na imewekwa chini ya UNESCO, Shirika la Uhifadhi la Dunia, lakini Watanzania ambao tumepewa hadhi ya kuwa na hifadhi hii tumeshindwa kuitunza na sasa hivi hali ya hifadhi hii inakwenda kupotea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Ngorongoro inakabiliwa na tatizo kubwa la watu kulima ndani ya hifadhi, Ngorongoro inakabiliwa na watumishi kutafuna fedha za hifadhi, inakabiliwa pia na kuongezeka kwa mifugo. Jana nilikuwa nasoma vyombo vya habari, tayari Ngorongoro hata watumishi wanahamishwa wanakataa wanakwenda Mahakamani kushtaki. Najaribu kuelewa kwamba, miaka mitano ijayo tunayo Ngorongoro?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, hadhi ya Hifadhi ya Ngorongoro iendelee kubaki kama Urithi wa Dunia kwa vizazi vya leo na vizazi vijavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeunda Tume hapa Tanzania kwa ajili ya kupitia migogoro ya wakulima na wafugaji na kuweza kuondoa mauaji yanayotokea ndani ya nchi yetu. Hata hivyo napenda kujua, Tume hii imeshaanza kazi, itamaliza lini? Tume hii ambayo inahusu Wizara nne na wataalam kutoka Wizara nne wakati bado inaendelea na kazi bado kuna wataalam na watendaji wanaopita kwenye maeneo ya hifadhi na kuweka alama katikati ya nyumba za watu bila kushirikisha Ofisi za Wilaya, Wakurugenzi hata Wabunge kwenye maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba tujue, Serikali imeamua kuunda Tume, itekeleze kwanza jukumu la Tume. Tume ije na mpango kamili utakaoweza kutoa suluhu ya kutosha kuondoa migogoro ya wafugaji, kuondoa migogoro ya wakulima na migogoro ambayo watu wanapoteza maisha yao hapa ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwamba, Wizara ya Ardhi wamefanya kazi nzuri; wamefungua kanda nne ndani ya Tanzania kuweza kurahisisha huduma za ardhi. Pamoja na kufungua Kanda nne ndani ya nchi yetu bado kuna tatizo kubwa katika Halmashauri zetu, manispaa zetu pamoja na majiji la kutokuwa na fedha za kutosha kuweza kupima maeneo. Tunayo shida kubwa sana Waheshimiwa Wabunge, nchi yetu haijapimwa, maeneo mengi hayajapimwa, migogoro inaongezeka kwa sababu pamoja na kwamba Wizara inajitahidi; na namshukuru Mheshimiwa Lukuvi anafanya kazi nzuri, lakini bado.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iangalie namna ya kuweza kutoa fedha kama revolving fund kwenye manispaa zetu, kwenye halmashauri zetu pamoja na kwenye majiji, wapewe fedha wapime maeneo, wakishayapima wayauze wapate fedha, warejeshe fedha. Hiyo kazi ilianza kama miaka mitano iliyopita kwenye Manispaa za Dar-es-Salaam; Temeke, Ilala na Kinondoni, sikujua ule mpango uliishia wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaomba, ule ulikuwa ni mpango mzuri, tuliusapoti lakini umeishia katikati. Ni mpango mzuri, Serikali iwezeshe, ipeleke watalaam wa kutosha kwenye halmashauri, ipeleke vifaa kwenye manispaa, kwenye majiji na halmashauri, lakini pia, itoe fedha waweze kupima kuhakikisha kwamba, nchi yetu inapimwa. Kutegemea Wizara peke yake tutachukua miaka mingi sana kuweza kupima maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo tatizo kubwa sana la makazi holela. Mimi kila nikiongea juu ya ardhi nazungumzia makazi holela. Tumekuwa kama Serikali hatujipangi. Leo kila ukienda watu wanaanzisha miji miwili, mitatu, baada ya miezi mitano, baada ya mwaka ni mji tayari. Tayari wanahitaji huduma za maji, barabara, na umeme. Serikali kwa nini isiwe na mpango? Watu waambiwe kajengeni pale? Kwa nini inasubiri wananchi wajiamulie wenyewe wakakae wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukianza kutembea kuanzia Dodoma, elekea Morogoro unaenda Dar-es-Salaam, vijiji vinaanzishwa kidogo, kama utani. Serikali ipo, viongozi wapo, wataalam, lakini wanaona wananyamaza kimya. Leo tumekuwa na nchi ambayo haijapimwa maeneo mengi, miji yake ni ya kiholela na bado inazidi kuanzishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Ardhi ifike mwisho kuwa na mji usiopimwa, usiopangwa, miji ambayo ni ya kiholela. Nchi nzima tunakuwa na vichuguu, hatutaki kuwa na nchi yenye vichuguu. Kwa hiyo tunaomba, Wizara inafanya kazi nzuri lakini haijaweza kudhibiti ujenzi holela kwenye maeneo mbalimbali ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala pia, la National Housing. Nishukuru kwamba, wanafanya kazi nzuri, tatizo kubwa ni jukumu la Serikali kuhakikisha wananchi wake wanapata makazi bora. National Housing inafanya kazi kwa niaba ya Serikali, ni kwa nini Serikali haiwezi ku-subsidize nyumba za National Housing ili wananchi wa hali ya chini waweze kukaa na kuishi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini National Housing inunue simenti bei ileile, mchanga bei ileile, vifaa vya ujenzi bei ileile utegemee wakauze nyumba rahisi? Haiwezekani! Pia, wanapeleka huduma za maji wenyewe, umeme wenyewe, miundombinu wenyewe. Serikali inatakiwa iweze kutoa baadhi ya vitu kupunguza gharama, nyumba za National Housing zinufaishe wananchi wote wenye hali ya kawaida na wenye hali ya chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasahivi nyumba za National Housing zinakaliwa na kununuliwa na watu wa hali ya juu, watu wa chini hawanufaiki kabisa. Kwa hiyo, hata ile maana ya kuwepo kwa National Housing yenyewe inakuwa haina tija kwa wananchi wa hali ya chini. Ni jukumu la Serikali kuhakikisha kwamba National Housing inakuwa na nyumba nzuri, lakini za standard ambazo mwananchi yeyote yule anayetaka kumudu anaweza kumiliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo tatizo, TANAPA inajitahidi inafanya kazi nzuri. Naomba Serikali ihakikishe inafungua, inaweka miundombinu kwenye maeneo ya hifadhi za Kusini, tuweze kufungua hifadhi za Kusini. Leo ukiangalia Tanzania National Park inajitahidi lakini ni upande mmoja wa Kaskazini. Huku maeneo ya Iringa kuna vivutio vizuri, Kitulo, Mbeya, maeneo mengi. Serikali ni wajibu wake iweke miundombinu kwenye National Parks nyingine zilizoko nje na Kaskazini ili tuweze kuwa na utalii nchi nzima. Vivutio vipo, tatizo ni kwamba, maeneo hayo hayawezi kufikika kwa sababu hakuna miundombinu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lipo tatizo lingine. Tumekuwa tunazungumzia suala la concesion fees kwenye National Park. National Park wame-introduce concesion fees kwa maana ya tozo ya vitanda kwa hoteli ambazo ziko ndani ya hifadhi kwa miaka zaidi ya 10 sasa. Wanatumia zilezile za miaka 20 iliyopita, Dola tano mpaka Dola saba, wakati huo imewekwa hii tozo Dola tano mpaka Dola saba tulikuwa tunalipa kitanda Dola 150 mpaka Dola 200, leo kitanda kimoja National Parks ni Dola 500 mpaka Dola 1,000 lakini tozo iko palepale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kwamba, Bodi haikuwepo, sasa Bodi imeshateuliwa tayari, naiomba Serikali mapema iwezekanavyo tozo mpya za National Parks ziweze kuwa introduced ili National Park ipate fedha za kutosha kuboresha miundombinu, lakini pia kuweza kusimamia utalii ndani ya hifadhi zetu za TANAPA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la Loliondo. Tumeona migogoro mingi ndani ya Loliondo. Naiomba Serikali; kwa taarifa ambazo tumezipata ni kwamba, sehemu ambayo inagombaniwa mpaka Mkuu wa Mkoa Mheshimiwa Mrisho Gambo wametofautiana yeye na Mheshimiwa Waziri ni eneo la chanzo cha maji. Katika eneo lile wanaokuja kufuga kule ni watu wa kutoka nje ya nchi, wameleta mifugo kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaomba kwenye masuala ya uhifadhi na hasa kulinda vyanzo vya maji tusiweke siasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumzia juu ya vyanzo vya maji. Nimesema eneo linalogombaniwa ni eneo ambalo linaonekana lina chanzo cha maji. Suala la kuwepo kwa chanzo cha maji haliangalii hifadhi au si hifadhi, ni chanzo cha maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka mingi tumeshuhudia mifugo Loliondo inakufa wakati wa ukame kwa sababu maji yanakosekana. Leo hata wale wa Loliondo wenyewe wakishindwa kutunza vyanzo vyao vya maji wakati wa ukame mifugo itakufa tu. Kwa hiyo, nasema kwamba, tuangalie interest ya Taifa lakini pia, interest ya wafugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ni chanzo cha maji kilindwe iwe nje ya hifadhi iwe ndani ya hifadhi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.