Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makambako
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Kwanza nizungumzie suala linalohusiana na maji. Kwenye bajeti ya kipindi kilichopita kuna miradi mikubwa ambayo tuliipitisha hapa. Kwa mfano, kuna miradi mikubwa ya maji ya miji ya Makambako, Njombe na Wanging’ombe ambapo ilionyesha fedha zinatoka Serikali ya India. Kwa hiyo, ni vizuri Waziri atakapokuwa anasimama atuambie Serikali imejipangaje juu ya kutatua tatizo la maji kwa mradi mkubwa huu wa Makambako, Njombe na Wanging’ombe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni suala la pembejeo hizi za ruzuku ambapo Mkoani kwetu Njombe zinachelewa sana. Sisi tunaanza kupanda kuanzia mwezi wa 11 na kuendelea. Kwa hiyo, Serikali ijipange vizuri msimu huu tunaokwenda sasa kuona kwamba pembejeo hizi zinafika kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la tatu, kuna hawa wasambazaji ambao mpaka sasa wanaidai Serikali na mpaka sasa wako watu ambao wamefilisika, wako watu wanauziwa nyumba zao. Ni lini Serikali italipa deni hili ambalo wananchi hawa walisambaza pembejeo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la nne, ni suala la lumbesa kwa wakulima, nadhani Serikali ijipange vizuri suala hili lipigwe marufuku kwa nchi nzima ili kusudi isiwaumize wakulima.
Mheshmiwa Mwenyekiti, jambo la tano ni mifugo. Suala la mifugo limekuwa ni tatizo kubwa sana kwa wafugaji na wakulima na watu wanapoteza maisha. Aidha, Kamati au ninyi Serikali muone namna ambavyo nchi ya Sudan wana mifugo mingi kuliko sisi lakini hakuna tatizo la wakulima na wafugaji, waende kule wakajifunze wenzetu kule wanafanyeje mpaka hakuna migogoro ambayo ipo kama huku kwetu kila wakati mara watu wameuawa na kadhalika. Kwa hiyo, nadhani Serikali ijipange kuona namna ya kuondoa tatizo hili la mifugo na wakulima kwa sababu limekuwa ni kubwa sana, siyo kitu kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la sita, hapa kuna watu wamezungumzia Wizara hii ya Kilimo. Mimi niseme ndugu zangu, Waziri huyu Tizeba na Naibu wake wakati fulani tunawalaumu bure tu, sasa watachukua wapi fedha kama hawana fedha? Nadhani sisi tuungane kwa pamoja kuona namna ambavyo tunaiambia Serikali ili bajeti ya msimu huu tunaokwenda iwe nzuri kuliko bajeti iliyokwisha ambapo ilitengwa shilingi bilioni 20 tu ambazo hazijatosha kitu chochote.
Kwa hiyo, nilikuwa nadhani sasa badala ya kumlaumu Waziri na Naibu wake na Wizara kwa ujumla, tuone namna ambavyo sasa Serikali inajipanga kuona msimu huu tunakuwa na bajeti ya kutosha kwa sababu ndiyo uti wa mgongo kwa wakulima wetu. Nadhani tukifanya hivyo, Serikali ikiongeza bajeti tutakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mengi lakini kwa sababu na mimi nipo kwenye Kamati hii nirudie tena kuzungumzia hili suala la maji, Waziri utakaposimama uwaambie wananchi wa Makambako wataondokana lini na tatizo kubwa hili la maji na uwaambie fedha za kutoka nje wananchi wale wa Njombe, Wanging’ombe wanazipataje na mpango huu sasa unaendeleaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.