Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwela
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kuweza kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuungana na wenzangu katika kuchangia taarifa za Kamati mbalimbali, Kamati ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Kamati ya Maliasili. Kwanza naunga mkono taarifa za Kamati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza nizungumzie mgogoro kati ya wakulima, wafugaji na hifadhi za akiba za ardhi. Tulishazungumza mara kadhaa hapa kwamba zipo baadhi ya akiba za hifadhi ambazo hazina faida zaidi ya miaka 50 na ukimuuliza Waziri hii akiba ya hifadhi hii imeleta faida gani kwa Taifa hili au kwa wananchi hawa zaidi ya askari wa wanyamapori au askari wa misitu kuitumia kwa manufaa yao, kukamata wananchi na kuwatoza rushwa halafu kuwaruhusu wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie hifadhi ya akiba ya Uwanda Game Reserve. Hifadhi hii ni zaidi ya miaka 50 na wakati hifadhi hii imetengwa idadi ya wananchi ilikuwa kidogo lakini sasa hivi hifadhi hii inazungukwa na vijiji zaidi ya 15, zaidi ya wananchi 26,000. Kwa hiyo, wananchi wanashindwa walime wapi, lakini hifadhi hii ukiiangalia faida yake haipo matokeo yake askari wanatumia hifadhi hii kwa manufaa yao binafsi. Mwananchi akisogelea hii hifadhi hata kwa kupita tu anakamatwa, anadaiwa pesa, asipokuwa na pesa anakamatwa anarundikwa ndani na wengine wamekuwa vilema, wengine wamepoteza maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano, tarehe 2 Januari, 2017, mwananchi mmoja anaitwa Luanda Salanganda Malele amepigwa risasi kwenye goti na askari anayeitwa Limomo baada ya kumkuta nje ya hifadhi. Akaambiwa kuna mtoto wako tumemkamata, akawaambia mimi sina mtoto aliyekamatwa, wakamdadisi kumdai pesa akakataa wakamwambia wewe una mazoea ya kujidai mjuaji tukikuomba pesa hutupati, wakaanza kumtishia kwa risasi. Katika kumtishia akakimbia akaenda kwenye nyumba ya jirani wakamtandika risasi kwenye goti, goti limechanikachanika sasa hivi yuko Muhimbili anasubiri kukatwa mguu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sisi kama binadamu Mwenyezi Mungu kweli anaweza akapenda maonevu ya namna hii? Hizi hifadhi zimewekwa kwa ajili ya binadamu tena tunaita hifadhi ya akiba, tulishasema kwa nini Serikali isipite kufanya utafiti wa kina kuona hifadhi ambazo hazina faida, hata kama zina faida wanaangalia maslahi makubwa ya wananchi waweze aidha kurekebisha mipaka au kuziondoa kabisa. Kwa mfano, Uwanda Game Reserve haina manufaa kabisa kwa Taifa zaidi ya kusumbua wananchi kwa kuwakamata kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna Kamati inapita au Waziri aende kwenye hifadhi hii, akakutane na wananchi aweze kuzungumza nao wamueleze matatizo yao, vinginevyo yatatokea mapigano makubwa sana kwa hali iliyopo sasa hivi. Sisi tumebeba mzigo wa kila siku kutuliza hali hii ya hewa, kwa hiyo, tunaomba Serikali au Waziri afanye utaratibu wa kwenda kukutana na wananchi ili aweze kuwasikiliza na kutafuta muarobaini wa mgogoro huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kuzungumzia ni uhaba wa ardhi. Lazima tukubali ipo baadhi ya Mikoa au Wilaya zina uhaba wa ardhi na zina uhaba wa ardhi kwa sababu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)