Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Eng. Gerson Hosea Lwenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi uliyonipa. Nianze kwanza kwa kuishukuru Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji, kwa uongozi wake mzuri ambao umesaidia sana Wizara yangu katika kutekeleza majukumu ya kuwapatia Watanzania maji safi pamoja na kilimo cha umwagiliaji. Pia niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, wamezungumzia kwa uchungu kabisa matatizo ya wananchi wetu wanaokosa huduma ya maji hasa katika maeneo ya vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba hatujafikia malengo, ukiangalia Azimio Namba Sita la Umoja wa Mataifa linasema kwamba nchi wanachama wote wahahakikishe wananchi wao wanapata maji kwa asilimia 100 ikifika mwaka 2030. Sasa Tanzania ni mwanachama lakini sisi kwa nchi za Afrika tuliamua kwamba jambo hili la kuhakikisha kwamba tunawapatia wananchi maji safi na salama kwa haraka zaidi kuunda Umoja wa Mawaziri wa Maji katika Afrika ambao unajulikana kwa jina la AMCOW na Tanzania imepewa heshima ya kuwa Mwenyekiti kwa miaka miwili kuanzia mwaka 2016 mpaka 2018. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba Rais wetu ndiyo atakayekuwa anazungumzia suala la maji kwenye vikao vya Umoja wa Nchi za Afrika kwamba mmefanya nini. Mnajua jambo hili la kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji ni lazima tuwe na nguvu ya pamoja. Kama tulivyobuni katika Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kwamba haitawezekana Serikali peke yake kuweza kufikisha huduma ya maji kwa wananchi wote ni lazima tuwe na nguvu ya pamoja ya Serikali, wananchi pamoja na washirika wa maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana mwaka 2007/2008 mpaka Juni 2016 tulianzisha Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ya awamu ya kwanza. Washirika wa maendeleo pamoja na Serikali waliweza kuweka fedha kwenye mfuko kiasi cha bilioni 1.6 ni karibu trilioni 3.2, hizi ni fedha nyingi na tumeweza kujenga miradi mingi zaidi ya miradi 1,800 ili kuondoa hali ilivyokuwa huko mwanzo na sasa tumefikia mahali ambapo angalau wastani wa maji vijijini, wananchi wanapata kwa asilimia 72. Hii haina maana kwamba kila kijiji kina asilimia 72, viko vijiji vingine vina asilimia 30 na vingine vina asilimia 80. Sasa ukichukua wastani kwa kuangalia idadi ya watu wanaopata maji kwenye vituo ambavyo vimejengwa imefikia asilimia 72.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine ambalo tunalipata ni kwamba Serikali imejenga miradi mingi lakini miradi mingi haifanyi kazi kama Waheshimiwa Wabunge mnavyosema. Serikali pia imeanza kubuni mradi mwingine wa kuhakikisha hii miradi iliyojengwa kwa fedha nyingi za Serikali iinakuwa endelevu na inafanya kazi. Tumefanya tathmini wastani wa asilimia 30 ya miradi mingi iliyojengwa haifanyi kazi. Serikali ya Uingereza kupitia Shirika la DFID tumeanzisha mpango mwingine wa kuhakikisha miradi hii inakuwa endelevu, imetoa kama Euro milioni 80, bilioni 214 kwa kila kituo cha maji kitakachotengenezwa na Halmashauri wanapewa fedha zaidi ya paundi 1500. Mpango huu tumeshaupeleka nchi nzima kwa Halmashauri 185.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge tuzihamasishe Halmashauri zetu ziiingie kwenye mfumo huu ili miradi yote ambayo tayari tulishaijenga na tumetumia fedha nyingi iweze kufanya kazi na wananchi wetu waweze kupata maji. Ni Halmashauri 57 ndiyo zimeitikia wito huu, naomba Halmashauri zilizobaki pia ziingie kwenye mpango wa kujenga vituo vya maji. Ukishajenga kituo kimoja unaongezewa fedha na DFID ili kusudi uweze kujenga vituo vingi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika programu ambayo tumeanza Julai, 2016 awamu ya pili ya programu tayari washirika wa maendeleo wameweza ku-pledge kiasi cha dola bilioni 1.6 ambazo zitaingia kwenye utekelezaji wa miradi, katika vile vijiji ambavyo vilikuwa havijapata miradi tutaviingiza kwenye hii program. Tayari nimetayarisha mwongozo toka mwezi wa Julai, nitawapa nakala Waheshimiwa Wabunge kabla hamjaondoka muondoke na huu mwongozo wa kuhakikisha kwamba Halmashauri zetu kwanza zinakamilisha miradi iliyokuwa inaendelea na pia zinaanzisha miradi mipya ili kusudi tufikie hii mipango ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepita kwenye Halmashauri unakuta wanasema kwamba tunasubiri fedha, fedha haziwezi kuja kwa sababu hata zikija huna kitu cha kufanya. Unatakiwa uanze maandalizi, uweze kufanya manunuzi baada ya pale hela itakuja kwa certificate. Mfumo huu umetusaidia toka Januari mpaka Desemba tumepeleka shilingi bilioni 177 kwenye Halmashauri zetu kwa ajili yamaji vijijini na miradi mingi imekamilika sasa hivi wananchi wanapata maji. Tumeshafika zaidi ya asilimia 76 kwa sababu miradi inakamilika na wananchi wanaendelea kupata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana ndugu zangu tusibaki tunasema fedha haziji, fedha zinakuja kwa kazi maalum, haziwezi kuja zikakaa tu. Tumekuta baadhi ya Halmashauri wanazo fedha kwenye akaunti lakini hakuna wanachokifanya. Sasa nasema tuache ufanyaji kazi wa kimazoea, lazima kila wakati watu twende kwenye mfumo wa kutoa matokeo. Tukija kwenye mfumo wa kutoa matokeo nina hakika wananchi watapata maji kulingana na malengo ambayo Serikali imeweza kuweka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema maji ni uhai, maji ni uchumi na maji pia ni utu. Hautaweza kujenga viwanda kama maji hakuna. Hivi vitu vyote lazima tufanye kwa pamoja. Najua kabisa Serikali inaweka bajeti ya kutosha kwa ajili ya kuweza kuandaa miradi mikubwa. Kila mmoja alikuwa anasimama hapa anataka maji ya Ziwa Victoria, anataka maji ya mito mikubwa, tutakwenda kufanya vile jinsi tunavyojenga uwezo wa nchi. Hata hivyo, kwa kuanzia tulisema tuanze na miradi ambayo uendeshaji wake unaweza kufanywa na vijiji lakini jinsi tunavyoendelea…
Lazima Serikali tutaingia kwenye miradi mikubwa. Nitasema miradi michache ambayo kwa mwaka huu wa kwanza tumeweza kufanya.

TAARIFA.....

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, angenipa nafasi ili kusudi niweze kumuelewesha aweze kuelewa. Nimesema tulishatoa mwongozo toka Julai tulivyoanza mwaka wa fedha ambao unaelezea kila kitu kuhusu miradi inayoendelea pamoja na miradi mipya. Na mimi nitampa nakala ya mwongozo huo aangalie ili akasimamie Halmashauri yake nini cha kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge mnielewe na mnikubalie kwa sababu tukianza kubishana hapa ndiyo maana miradi haiendi, naomba sana. Wabunge wote nitawapa mwongozo, nitawapa na taarifa ya utekelezaji wa programu ya awamu ya kwanza. Kwa hiyo, tumepeleka kwa maandishi na pia tumewafanyia semina hawa Wakurugenzi na Wahandisi wa Maji kuhusu jambo hili, lakini unafika mahali mtu bado anashangaa shangaa, haelewi cha kufanya. Sasa hayo ni majipu itabidi tuanze kuyatumbua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu niseme baadhi ya mafanikio ambayo tumeweza kupata. Mradi mkubwa wa kutoa maji kutoka Mto Ruvu, Ruvu Chini na Ruvu Juu umekamilika. Hivi sasa tunaweza kuzalisha maji lita milioni 502 kati ya milioni 544 zinazohitajika kwa ajili ya Jiji la Dar es Salaam. Tatizo letu tulilonalo lilikuwa ni mtandao na sasa hivi Serikali tunaendelea na kujenga mtandao maeneo yote ambayo hayana mtandao ili kusudi waweze kupata maji. Kwa mwaka huu wa fedha Serikali itaweka fedha zaidi katika kujenga mtandao katika maeneo ambayo hayana maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nielezee mradi mkubwa wa kutoa maji kutoka Ziwa Viktoria kupeleka Tabora, Nzega na Igunga mpaka Sikonge. Tayari tumeshapata mkandarasi, tumepeleka Serikali ya India tupate no objection ili tusaini mkataba, mkadarasi yule aweze kuanza kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mradi pia wa kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka Miji ya Magu, Misungwi, Lamadi na kupanua maeneo ya Ilemela katika Jiji la Mwanza. Tarehe 16 tunasaini mkataba, Waheshimiwa Wabunge wa maeneo hayo nawakaribisha tuje tusaini mkataba na kazi ile inaanza mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mradi wa kutoa maji ya Ziwa Victoria kupeleka miji ya Kagongwa, Tinde na Isaka, tayari mkandarasi tumeshampata tuko kwenye maandalizi ya kuweza kusaini mkataba na kazi ile itaanza mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, umezungumziwa mradi wa milioni 500 wa Serikali ya India wa Mheshimiwa Deo Sanga, Mji wa Makambako, Muheza pamoja na ile Miji 17 ikiwa ni pamoja na Zanzibar. Hatua tuliyofikia mpaka sasa tuko kwenye hatua ya kumpata Mhandisi Mshauri atakayefanya usanifu wa kina na kutengeneza makabrasha ya zabuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matarajio yangu tunavyoanza mwaka wa fedha 2017/2018 tender zitatangazwa na kazi ile itakwenda kuanza kufanyika. Kwa hiyo, Mheshimiwa Deo Sanga pamoja na wale wote wa miji ile 17 tunakwenda kuikamilisha kazi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi hii uliyonipa.