Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Salome Wycliffe Makamba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia Mpango huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa namsikiliza kwa makini sana Mheshimiwa Waziri wakati anawasilisha Mpango wake na nikazidi kupata maswali mengi ya utekelezaji wa Mpango wake kwa sababu mambo mengi ambayo ameyaandika yanaonekana kwenye nadharia na huenda yasitekelezwe au yasitokee kabisa kama Mpango uliopita. Mheshimiwa Waziri anasema kwamba anataka kuweka mazingira mazuri ya kibiashara kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunafanya maendeleo ya viwanda Tanzania
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mazingira hayo mazuri ya kibiashara Mheshimiwa Waziri hakuyaeleza kinaga ubaga na hilo linanitia mashaka, kwa sababu nikifikiria moja kati ya vitu ambavyo ni vya kipaumbele ili tuweze kukuza viwanda Tanzania tunaongelea habari ya umeme, miundombinu lakini mpaka leo na hata ukiangalia katika bajeti tuliyonayo hakuna nguvu ya ziada ambayo Serikali imeiweka kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunapata maendeleo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoa mfano wa mazingira ambayo tunaishi Watanzania leo, bei ya umeme bado iko juu na wanasema kwamba wamepunguza kwa asilimia mbili lakini effect yake katika punguzo hilo haionekani katika uhalisia wa maisha ya Mtanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia katika mazingira ya sheria ambazo Mheshimiwa Waziri alitakiwa azieleze kwamba ndiyo zimerahisisha utekelezaji wa sera hii ya viwanda, sioni kama ameonesha kwa njia yeyote ila ameweka sheria kwa ajili ya kuvutia wawekezaji wadogo wadogo, labda kama yeye alipokuwa anaongelea maendeleo ya viwanda alikuwa anaongelea wawekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii wawekezaji wadogowadogo hasa wale wanaohusika na mazao ya kilimo wanawekewa vikwazo, wanawekewa sheria ngumu na wanawekewa tozo mbalimbali ambazo mwisho wa siku zinawafanya wazidi kukwama katika harakati hii ya kujiendeleza katika kutengeneza malighafi kwa ajili ya maendeleo ya viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano moja katika Jimbo la Kahama Mjini, Jimbo lile kuna watu wanashughulika na biashara ya upakiaji na uchakataji wa zao la mpunga, lakini leo hii ukiangalia tozo ambazo wanatozwa watu wale mpaka wanafikia hatua ya kukata tamaa kujihusisha na zao hili la kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wamewekeza fedha zao kwa ajili ya kutengeneza na kupaki zao hili la mpunga, lakini kuanzia asubuhi mpaka jioni umeme hauwaki, ukiwaka jioni Polisi wanapita wanasema hairusiwi mtu kufungua kiwanda usiku. Kwa hiyo, wanajikuta ndani ya mwezi mzima watu wale wanashindwa kufanya uzalishaji, kwa hivyo hata zile fedha ambazo wamewekeza mle wanashindwa kuzirejesha kama walizikopa kwenye mabenki, lakini pia wanashindwa kuzizalisha ili ziweze kuwaletea faida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu hawa ukiangalia ambao ni wazalishaji, Mheshimiwa Waziri anasema kwamba, anataka kuendeleza viwanda, lakini nimesikitishwa na taarifa ya Waziri anasema kwamba bei za mazao zinapaswa zizidi kushuka. Swali hasa lilikuwa limeelekezwa kwenye zao la maziwa ambapo Mkoa wa Shinyanga tunafuga sana ng‟ombe, kwa sasa hivi lita ya maziwa ni shilingi mia nne mpaka shilingi mia tano na watu wale hawanufaiki, kumfuga yule ng‟ombe ni gharama, sindano moja inakugharimu kuanzia laki nne mpaka tano kwa ngombe mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ile shilingi mia nne, shilingi mia tano kwa lita ya maziwa unaambiwa izidi kushuka sasa sijui yauzwe lita moja shilingi mia mbili, hapo sijamuelewa vizuri! Kwa maana hiyo, ni kwamba, tunawakatisha tamaa wakulima, tushushe bei ya zao la maziwa, tushushe bei ya zao la pamba, tushushe bei ya zao la tumbaku, halafu unasema watu tuko katika harakati za kuzalisha malighafi ya kutosha ili tuweze kuendeleza viwanda Tanzania!
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukisikia kauli mbalimbali za Serikali zikibeza misaada, lakini ukiangalia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri inasema wazi kwamba gharama kwa ajili Mpango huu wa Maendeleo itakuwa ni trilioni 107 na Serikali itatoa trilioni 59 tu, hiyo baki inayobaki tunategemea kuitoa wapi? Bila shaka fedha hizo huenda zingetoka kwa wahisani au wafadhili na labda kukopa kwenye mabenki ambapo mwisho wa siku inaonekana kwamba fedha hizo tunashindwa kuzirejesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshindwa kutoa kauli badala yake inazidi kuwabeza hawa watu. Sasa hivi tuko katika ulimwengu wa teknolojia, wanazipata hizi taarifa na hakuna mtu yeyote anayeshtuka na kuona kwamba yule mtu anayetusaidia angalau kidogo tunatakiwa tumheshimu, badala yake tunatoa kauli za kukejeli na kauli za dharau, wakati leo hii waziri anathibitisha wazi kwamba ana zaidi ya nusu ya gharama ya bajeti ambayo hajui atakapoitoa. Matokeo yake anategemea kwenda kuzidi kuwabana watu kwa kuchukua property tax za Halmashauri, anategemea kwenda kuwabana watu kwa kuchukua kodi mbalimbali ambazo Halmashauri inakusanya kwa ajili ya kujiendesha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia katika mazao mbalimbali ambayo leo hii yalitegemewa yatunufaishe Watanzania. Wakati tunachambua sheria ndogo za Halmashauri, tulionamkulima amebebeshwa mzigo mkubwa sana. Kwa mfano, moja kati ya sheria ndogo mkulima anaambiwa achangie mpaka fedha kwa ajili ya Mwenge, hivi kweli Mwenge, kwa nini Serikali Kuu isitoe hiyo pesa kama kweli inaona hilo jambo ni la muhimu sana hata inambebesha mkulima mdogo kutoa hiyo pesa ikiwa ni moja kati ya tozo ambayo imelimbikizwa katika zao lake lile ambalo anategemea kuzalisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sioni sehemu ambayo Mheshimiwa Waziri ananieleza juu ya kuboresha ufundi stadi ili kuweza kupata watu ambao wataweza kufanya kazi katika hivi viwanda ambavyo vinategemewa kuanzishwa. Katika mikoa tumeona kuna VETA moja tu katika kila Mkoa na mtu anavyotaka kufungua Chuo cha Ufundi Wilayani kuna ukiritimba mwingi na process ndefu ambayo inamkwamisha mtu binafsi kuweza kufungua Chuo cha Ufundi au Chuo cha VETA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri afahamu kabisa kwamba tunayo sera ya kwamba mwekezaji anatakiwa kuajiri watu wanaozunguka eneo alilowekeza. Walio wengi na miradi mingi inawekezwa maeneo ya vijijini na maeneo yale hayana watu ambao wana elimu ya juu na wanategemea kupata watu ambao angalau wanaweza kuwa na elimu ya ufundi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano wa mgodi wa Buzwagi na Bulyanhulu ambayo ipo katika Vijiji vya Kakola na Wilaya ya Kahama, maeneo yale watu wengi siyo kwamba wana elimu ya juu, lakini hakuna Chuo cha Ufundi kwa ajili ya kuendeleza wale watu, unamkuta mtu anafanya kazi ya kibarua zaidi ya miaka minne, mitano, kwa sababu hana jinsi ya kusoma angalau masomo ya jioni ili aweze kupanda kutoka ile rank aliyopo kwenda juu, inambidi aendelee kufanya kazi ile itakayomtesa kwa miaka nenda miaka rudi halafu leo Waziri anasema anataka kuendeleza ufundi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado sijaelewa vizuri mkakati wa Waziri anaposema anataka kuuza viwanda, kwa sababu kwa upeo nilionao ni kuwa viwanda vikubwa vinatokana na viwanda vidogovidogo ambavyo vinaanzishwa na wananchi wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii pale Kahama tunalo soko la wakulima, wale watu wamejiunga kwenye ushirika na wamekusanya fedha zao wamejitahidi wameweza kutengeneza lile soko na leo linaonekana ni moja kati ya masoko makubwa katika Mji ule. Hata hivyo, leo ukiangalia soko lile Serikali imekubali ule ushirika kuupeleka ukauzwa kwa mtu binafsi, wakati Sheria ya Ushirika iko wazi kwamba soko lile lilitakiwa liuzwe kwa ushirika mwingine ulio hai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili linaungwa mkono na Serikali, kibali kimeshatoka, soko lile ambalo wananchi wamekusanya jasho lao linapelekwa kupewa mtu binafsi, wakati wale watu waliweka nguvu. Nilitegemea Serikali iwasaidie, iwawezeshe, iwape mtaji ili lile soko liweze kuwa kubwa, liweze kukidhi mahitaji ya ndani na ya nje ya Mji ule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutilia mkazo katika elimu. Kama kweli tunataka kwenda katika biashara ya viwanda ni lazima tuhakikishe tunatoa elimu ambayo ni ya ubunifu na wananchi wana uwezo wa kutoa ubunifu kwa ajili ya maendeleo ya viwanda. Elimu tuliyonayo leo hii ni ile ya kukariri, ndiyo maana unasikia mara leo Mama Mheshimiwa Ndalichako anasema kuna GPA, mara anarudi kwenye Division, ni kwa sababu hatuna system ambayo inaweza kutambua njia sahihi ya utoaji wa elimu Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tuko serious hatuwezi kusema tunaenda kuendesha elimu kwa njia ya mtu kutoa matamko tu kwenye magazeti. Elimu inatakiwa iboreshwe kwa kufanyiwa utafiti na ikidhi mahitaji ya Watanzania na siyo kwa kukidhi mahitaji ya Serikali ya CCM inasema hivi, kesho inakuja Serikali nyingine inasema mnawayumbisha watoto mnawa- frustrate, naomba Serikali iwe serious tunapoongelea masuala ya elimu kwa ajili ya mabadiliko ya viwanda hatuongelei tu suala la kufurahisha chama fulani au chama fulani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, ningependa kuongelea suala zima la miundombinu. Barabara za Mitaa na barabara za TANROAD, barabara hizi zimegeuzwa kama mitaji. Tunayo barabara ambayo inatoka Kahama inaelekea Kakola pale Jimbo la Shinyanga kuunganisha na Jimbo la Msalala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inafahamika wazi kwamba uwezo wa ile barabara haiwezi kubeba magari ya ukubwa wa namna ile ambayo yanapeleka mizigo mbalimbali kuelekea mgodini na kuelekea Geita, badala yake TANROAD imegeuza ile barabara kama mtaji, kila mwaka ile barabara inafanyiwa repair, inamwagiwa kifusi na ku-level, sasa hivi ni zaidi ya miaka kumi tangu mgodi ule umeanzishwa barabara ile inafanyiwa repair kila mwaka na mamilioni ya fedha yanapotea. Naomba Waziri husika alitazame hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoongelea maendeleo ya viwanda hatumaanishi kudunduliza pesa, bora kama fedha ni ndogo basi tuwekeze mahali ambapo tunaona kwamba italeta tija na italeta maendeleo ya nchi hii, lakini siyo tunaruhusu watu wanatumia hii kama ni njia ya kujinufaisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.