Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Abdallah Ally Mtolea

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Temeke

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza, nianze kulishukuru Bunge hili kwa maana ya Wabunge wote Mheshimiwa Spika na Mawaziri kwa namna ambavyo walinifariji mimi na familia yangu wakati nilipompoteza Mzee wangu mwezi Novemba mwaka jana. Mwenyezi Mungu awabariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nataka nijielekeze kwenye taarifa ya Kamati ya Sheria Ndogo. Imeonesha kuna umuhimu mkubwa sana wa Serikali kutunga Kanuni na Sheria Ndogo katika kuzisimamia rasilimali lakini wakati mwingine pia kuzipatia vipato Halmashauri. Mbali na changamoto ambazo Kamati imezionesha hapa za uandishi, uchapishaji, naliona tatizo lingine kubwa ambalo lipo katika utungaji wa hizi Kanuni na Sheria Ndogo kwenye Wizara lakini pia kwenye Halmashauri. Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo la kutokuwasiliana kwamba Kanuni au Sheria Ndogo inayotungwa na Wizara moja katika kulidhibiti jambo fulani haiangalii kitu gani kinafanywa na Wizara nyingine. Kwa mfano, watu wa NEMC wanaweka sheria za kudhibiti ukataji wa miti kwa maana ya matumizi ya mkaa na vitu vya namna hiyo. Watu wa Maliasili na wao pia wanatunga sheria za kuhakikisha kwamba wanalinda maliasili za nchi hii. Hata hivyo, unapotunga Sheria ya Kudhibiti Matumizi ya Mkaa lazima uangalie Wizara inayoshughulikia mbadala wa nishati inafanya kitu gani Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tumeona hapa kwa mfano Wizara ya Nishati inasema kwamba ina gesi ya kutosha lakini kwa sasa gesi hiyo haijaanza kutumika majumbani inasubiri TPDC wajenge miundombinu ya kuifikisha gesi hiyo majumbani. Jambo ambalo kwa maana ya kuipendezesha presentation linavutia sana, lakini ukija kwenye uhalisia unagundua hili jambo haliwezi kutekelezeka ndani ya miaka 50 au 100 ya hivi karibuni. Kwa sababu tukumbuke kujenga tu miundombinu ya kusambaza maji safi na maji taka mpaka leo hatujaweza kueneza nchi nzima, unawezaje kutegemea ndani ya muda mfupi kwamba TPDC watajenga miundombinu ya kuisambaza gesi nchi nzima? (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, unakuta yanayofanyika huku sasa yanasababisha matumizi ya mkaa yaendelee kuwa makubwa. Sasa kule tena mnatunga Sheria ya Kudhibiti Matumizi ya Mkaa maana yake bei ya mkaa itazidi kupanda na anayeteseka hapa ni mwananchi. Kwa hiyo, ugumu wa maisha tunausababisha na namna ambavyo tunasimamia hizi rasilimali zetu. Kwa hiyo, ni vizuri Wizara au Serikali ingekuwa yenyewe inaangalia hali halisi ikoje kabla haijatunga Sheria Ndogo kwa ajili ya kuzuia jambo fulani. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia inapotokea migogoro ni vizuri Serikali ikaenda haraka kutunga Sheria na Kanuni kwa ajili ya kumaliza migogoro hiyo. Vinginevyo inakwenda kuligawa Taifa katika hali ya kubaguana. Tazama migogoro iliyopo katika masuala ya ardhi. Ukienda sehemu ukikuta viongozi ni wakulima wanasema wafugaji wametuingilia na ukienda maeneo mengine wanasema kwamba wakulima wametuingilia. Matokeo yake tunaanza kuchukiana kwa kubaguana, huyu ni mkulima, huyu ni mfugaji. Mfugaji anamwingilia mkulima, mkulima analalamika. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, jana hapa mlisikia Mheshimiwa Mbunge mmoja amesema migogoro hii haishughulikiwi kwa sababu Waziri wa Kilimo ni mfugaji kwa hiyo anawaacha wafugaji waendelee kulisha kwenye mashamba ya wakulima. Sasa haya mambo ya kutosimamia vizuri rasilimali ndiyo inakuwa chanzo cha kuzibadilisha rasilimali ambazo zilikuwa neema zianze kuwa laana kwenye Taifa hili na hivi viashiria tayari vimeanza kuonekana. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, tazama rasilimali zetu, tuna rasilimali ardhi, gesi, madini na tuna rasilimali watu. Kwenye ardhi tayari wakulima na wafugaji wanagombana. Kwenye gesi tumeona yaliyotokea Mtwara, kwenye madini unaona wachimbaji wadogo na wachimbaji wakubwa wana migogoro. Kwenye rasilimali watu ndiyo hivyo, mtu mmoja anaweza kunyanyuka anawaambia nyie mnauza madawa ya kulevya. Hivi ni viashiria vya kuona kwamba sasa rasilimali zetu zinageuka kutoka neema kwenda kuwa laana.