Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kukushukuru sana kwa kupata nafasi ya kuchangia katika mjadala huu unaohusu Kamati yetu ya Viwanda na Biashara na Mazingira lakini nikienda sambamba na ile ya Mitaji na Uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nichukue fursa hii kupongeza sana Kamati yetu, imefanya kazi nzuri yenye kupendeza ambayo imeeleza mambo mbalimbali hasa hii ya Viwanda na Biashara ambayo ningependa nijielekeze kwake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi naomba niwe shuhuda mzuri sana wa Tanzania ya viwanda. Katika Jimbo langu la Mkuranga mpaka sasa nina viwanda 56 vyenye kufanya kazi na nina viwanda 11 ambavyo wakati wowote vitakamilika. Katika hivyo 11, kimoja ni kile kipya na kikubwa kushinda vyote katika Afrika Mashariki na Kati, kiwanda cha tiles ambapo tutakuwa na uhakika sasa wa kutokuagiza tiles kutoka nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakuwa na uwezo sisi wenyewe katika nchi yetu kupata huduma hii bila kuagiza kutoka mahali kokote. Kwa fursa hii kwa kweli kabisa napenda niipongeze sana Serikali yetu kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya ya kuwavutia wawekezaji wale na wakaja katika Jimbo letu la Mkuranga na kuwekeza pesa zao nyingi kabisa juu ya kujenga kiwanda hiki kikubwa cha tiles.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema ukweli uwepo wa viwanda umetuinulia sana uchumi wetu sisi watu wa Mkuranga na nchi kwa ujumla wake. Mwaka jana 2016/2017 mwaka huu ambao tunamalizana nao tuliweka kadirio la kupata service levy isiyopungua milioni 500 na sasa tutakuwa na uhakika wa kupata service levy isiyopungua bilioni moja katika huu mwaka wa 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima niseme ukweli na hapa ndipo nilipokuwa nataka nisisitize sana, kwamba bado tunayo fursa kubwa zaidi ya kuwa na viwanda vingi zaidi, hasa hususani katika Jimbo la Mkuranga na sehemu zingine katika nchi. Kazi kubwa ambayo ningependa niiseme hapa ni kwa wenzetu wa Wizara ya Nishati na Madini, wajitahidi sana katika kuhakikisha nishati hii ya gesi, ya umeme, iweze kuwa ya uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nimekikosa kiwanda pale Mkuranga cha kutengeneza nguo katika eneo la Dundani. Mwekezaji amekuwa yuko tayari kabisa ataajiri vijana wasiopungua 14,000 lakini sharti la kwanza anataka umeme wa uhakika. Sasa pamoja na jitihada kubwa sana za kuwavuta wawekezaji zinazofanyika na wao wanaitikia, lakini bado tunayo changamoto kubwa ya nishati. Kwa hivyo wenzetu wa nishati wajitahidi wahakikishe mipango yao ya kusambaza gesi katika viwanda vyetu iende sambamba na mahitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mathalani katika viwanda hivi vyote 56 hakuna kiwanda hata kimoja leo kinachotumia gesi na hilo bomba la gesi limepita hapo hapo Mkuranga. Kwa hivyo wenzetu ni lazima watuambie; nimemsikia Naibu Waziri asubuhi anasema kuna zaidi ya bilioni tano ambazo zitaelekezwa katika kwenda kusambaza gesi majumbani katika maeneo ya Tabata na Sinza na kwingine kule Dar es Salaam, lakini hakueleza ni kiasi gani cha fedha ambacho kitatumika kwenda kutengeneza mtandao wa mabomba ya kusambaza gesi katika viwanda hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kupata huduma hii ya nishati kwa bei nzuri na hatimaye uzalishaji wa bidhaa katika viwanda vile uwe ni wa gharama nafuu na hatimaye kumsaidia Mtanzania mlaji wa zile bidhaa zinazozalishwa katika viwanda vile ili aweze kupata zile bidhaa kwa bei nzuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wetu alipokuja katika kiwanda cha Bakhresa aliagiza jambo hili, aliagiza kwa sababu watu Bakhresa food industry wameomba wapate gesi kwa muda mrefu na bado hawajafanikiwa mpaka hivi sasa. Jambo ambalo linapelekea uzalishaji wa bidhaa katika viwanda mbalimbali katika maeneo yetu unakuwa ni wa gharama kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo tuwaombe wenzetu watuambie ni namna gani, viwanda viko vingi sana, vinaingia kila siku ya Mwenyezi Mungu lakini je, tumetengeneza mazingira ya namna gani ya kuweza kuvisaidia kupata huduma hii ya gesi na nishati kwa urahisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwezekana nawashauri na kuwaomba wenzetu hawa wa nishati na madini waone umuhimu wa kuiweka Mkuranga kuwa hata na substation yake ya umeme, uwezekano huo upo na wala hakuna tatizo lolote la eneo wala hakuna tatizo lolote la upatikanaji wa gesi. Gesi tap ziko pale valve namba 12 na 13 katika maeneo ya Mbezi na Mkiu zinapatikana kwa wingi kwa hivyo tunawaombeni sana mtuweke substation pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati huu wa viwanda ni lazima kama ilivyopendekezwa na Kamati katika ukurasa wake wa 50 juu ya elimu ya ufundi. Vijana wetu wengi sana wanakwenda kuwa vibarua katika viwanda hivi, lakini tunaomba sasa ikiwezekana na wenzetu wa elimu muone umuhimu wa maeneo kama haya ya viwanda kuyapa uwezekano wa kuwa na vyuo vya elimu, ili vijana wetu waweze kupata elimu na hatimaye waweze kwenda kuwa na uwezo wa kwenda kuajiriwa katika viwanda vile. Hivi sasa unaweza ukakuta ni asilimia ndogo sana ya vijana wa Mkuranga ambao wanafanya kazi katika viwanda hivyo. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri anayehusika pia alitazame hili jambo kama ilivyopendekezwa na Kamati yetu ya Viwanda na Biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia ningeomba sana masuala haya ya ukuaji wa viwanda na sisi tumejiandaa vizuri na tayari maeneo yapo ya kutosha. Mathalani tunalo eneo pale katika Kijiji cha Dundani, zaidi ya ekari 700 na Waziri wetu wa Viwanda na Biashara amekuwa akilitaja kila mara. Sasa afanye kazi ya kuhakikisha wananchi wale zaidi ya miaka minne sasa, asiwe anakuja tu kaka yangu Mwijage kulitangaza lile eneo, awalipe fedha za fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale watu wamezuiwa kufanya chochote katika eneo lao, sasa ni miaka minne hawawezi kuendeleza chochote, hawazalishi chochote, hawasafishi maeneo yao ni kwa sababu wamejitolea eneo lao lile liwe ni eneo la viwanda. Sasa wale wananchi wamekata tamaa, ni lazima tuone ni namna gani either hawa wa Mkuranga au ni kwingineko kokote katika nchi watu walikojitolea katika kuhakikisha kwamba Tanzania ya viwanda inapatikana, basi mambo haya yakamilike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana nisisitize tena kwa mara nyingine juu ya kupatikana kwa nishati ya gesi katika viwanda vyetu ili uzalishaji uwe wa gharama nafuu. Ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja.