Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye hoja iliyopo mbele yetu. Kwanza, moja kwa moja nimpongeze shangazi yangu, Mheshimiwa Mama Lulida, alichokisema Mheshimiwa Mama Lulida ndiyo kitu ambacho kinatokea Mtwara, lakini pia ndivyo vitu vinavyotokea Lindi. Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi ambayo ndiyo iliingia mikataba ya kuuza maghala ambayo yalikuwa ni viwanda vya korosho Mtwara, Lindi, Newala, kwanza imepoteza ajira kwa watu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaomba basi tu-review upya ile mikataba kwa sababu tunaamini pamoja na ugumu uliopo kule ndani lakini Rais ana nia ya dhati kabisa ya kuwasaidia watu wa Mtwara ili waweze kupata ajira. Sisi Mtwara hatuna shida ya malighafi, tuna malighafi ya korosho ambayo inategemewa sana India. Malighafi pekee wanayoitegemea wale ni kutoka Mtwara ambayo ni korosho na tumeona mwaka huu korosho imeuzwa mpaka shilingi 3,800. Ili kuweza kuongezea wale wananchi kule kipato, tunataka sasa vile viwanda vifufuliwe korosho hii tubangue kule wenyewe. Kwanza ikibanguliwa kule moja kwa moja itauzwa kwa bei kubwa kwa sababu gharama za usafirishaji na tozo nyingine hazitakuwepo, hii pesa atakwenda kuipata mkulima moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tumeshuhudia maghala haya ndiyo yamekuwa sehemu ambazo zinakwenda kuwafilisi na kuwaibia wananchi, hawapati haki zao stahiki. Maghala haya kule ndani imeingia mikono ya wakubwa ukitaka kugusa biashara za maghala Mtwara basi unatafuta ugomvi na wakubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tukuombe, hakikisha unapitia vizuri hii mikataba ukishindwa wewe kuisema tupatie sisi tutasema, mpe pale Mheshimiwa Mama Lulida atasema, nipatie mimi nitasema, lakini kimsingi tunachotaka mwishoni wananchi wa Mtwara, wananchi wa Masasi wawe na viwanda vyao vile vya zamani. Viwanda hivi vilijengwa kwa kukopa pesa nchi za nje, ambapo ninaamini bado Serikali hii inaendelea kulipa pesa wakati viwanda vimeuzwa kwa bei rahisi, kwa hiyo nikuombe kabisa upitie hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema tena kidogo kuhusiana na suala la biashara ya mafuta. Watu wengi, na hapa ndani tumeona wakiwa wanachangia, sasa hivi tunaona bei ya mafuta imepanda sana, hata kama tunasema imepungua, asilimia 42 ya tozo mbalimbali zilizopo kwenye bei za mafuta zinakwenda Serikalini kuendesha vitu mbalimbali, lakini tunawatengenezea ugumu hawa wafanyabiashara wa mafuta. Kwa hiyo, tuone namna gani tunaweza tukawasaidia, tuangalie hizi tozo na kuzi-review. Haiwezekani asilimia 42 yote iwe kama sehemu tu za kodi, mfanyabiashara apate shilingi 120 au 150 sehemu ya kazi anayoifanya pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kimsingi tujaribu kuangalia, tunaposema kwamba watu wa Mtwara sisi tuna shida hatuna shida hasa ya viwanda kama mnavyovisema. Hivi karibuni tu Mheshimiwa Waziri niliongea nawe nikakueleza, tunaweza tukapata juisi kwenye mabibo, tunaweza tukapata nipa kwenye kochoko inayotokana na mabibo, lakini lengo hasa ni kwenda kumuongezea mkulima kipato. Hivi vitu vikiuzwa, hata tukiuza korosho shilingi 3,000, lakini tukauza mabibo yetu yanayokwenda kutengeneza juisi, tukauza zile kochoko zinazokwenda kutengeneza gin, tukaachana na hivi vitu vya ku-import itakwenda kuongezea pia kipato Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona hapa tunasema tunataka kupata mapato kwenye Serikali kwa kutumia vileo, ukiangalia asilimia kubwa ya wananchi vijijini ni wanywa gongo, wanywa gongo hawa, na hii gongo tunasema ni pombe haramu haijarasimishwa, lakini ndio wengi wanaokunywa gongo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiamua sasa kurasimisha ikazalishwa vizuri kwenye vyombo vinavyotakiwa kodi itakwenda kuongezeka kwenye vileo, sawasawa na ilivyo konyagi sawasawa na ilivyo gin sawasawa na ilivyo kwenye K-Vant watu wa Arusha. Kwa hiyo tutoe leseni za watu kuweza kupika gongo ambayo ipikwe kwenye viwanda vinavyotakiwa, ipimwe vizuri, irudi ikaingizie kipato Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakataa bure, asilimia 75 ya Watanzania wanaoishi vijijini wanakunywa gongo, na hii tutambue kama vyanzo vya mapato kwa sababu tutatoza kodi. Tunasikia sifa kutoza kodi kwenye grant’s, tunasikia sifa kutoza kodi kwenye konyagi wakati tunajua wazi wanywaji wa konyagi na grant’s si wengi kama walivyo wanywaji wa gongo. Kwa hiyo tunapoteza mapato, tuangalie namna bora ya kufanya ili tuweze kuzalisha hivi vitu lakini pia itaongeza kipato cha wakulima wetu kama ilivyo kwa wakulima wa miwa. K-Vant inatengenezwa kwa kutumiwa miwa, miwa ni mazao ya wakulima, konyagi inatengenezwa kwa kutumia chemicals nafikiri, lakini pia nipa inatengenezwa kwa kutumia mabibo ambayo inaongezea kipato wakulima kama tutarasimisha na kununua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri nikuombe utakapohitimisha utuambie sisi watu wa Mtwara mna mpango gani na viwanda vyetu vilivyouzwa kiholela holela vya korosho, vinaweza kutoa ajira kwa vijana wetu wote maeneo yale, tunaweza kuongeza tija kwenye korosho. Mheshimiwa Mama Riziki Lulida amesema hapa kwamba hizi ajira zinapelekwa India, tunajisifu tume-export tani laki mbili za korosho kupeleka India, lakini hatufikiri kama tumeondoa ajira za watu zaidi ya 10,000 au watu 20,000 kupeleka India, tunataka kuweka viwanda vya aina gani? Tuwaombe Mtwara tunataka tu viwanda vya kuanzia vya korosho, wala hatuhitaji kutengeneza nondo katika hali hii, korosho yetu isitoke na kwenda nje, iwe processed palepale ili kuweza kuiongeza thamani, muwashawishi wale wawekezaji waliopo kule waje Mtwara kujenga viwanda sio sisi tuwapelekee kwao malighafi, ninaomba ulichukue hili na tafadhali ulifanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.