Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa sababu ni dakika tano nitakwenda kuongea kwa kifupi sana. Kwanza kabisa naunga mkono ripoti za Kamati zote mbili, lakini zaidi naomba Serikali ifanyie kazi ripoti ya Kamati ya Uwekezaji kwa yale yote ambayo tumeshauri pale na ambayo tumeyaona field. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa haraka haraka nisisitize kwa yale ambayo tumeandika kwenye Kamati yetu. Ni kweli kabisa tumeona athari ambazo zinajitokeza kwa kutokuwa na bodi kwenye taasisi na mashirika ya umma. Taratibu zinataka kwamba mchakato wa kuweza kuwa na bodi baada ya ile nyingine kukaribia kuisha walau uanze miezi sita kabla, lakini tumeshuhudia Serikali hii taasisi zinakaa bila bodi zaidi ya miaka miwili hadi miaka mitatu. Na mfano tumetolea Bodi ya TANAPA, imekaa zaidi ya miaka mitatu tunaona kabisa ile kesi ya concession fee ilihukumiwa tarehe 12 Septemba, 2014, lakini Serikali ikaona ni bora Taifa liendelee kupoteza kila mwaka zaidi ya shilingi bilioni 10 kuliko kuunda Bodi ya TANAPA ambayo ingeweza kufanya maamuzi na kuweza kupata fedha ambazo ni takribani zaidi ya shilingi bilioni 20 zimepotea, ambazo zingeweza kwenda kujenga zahanati na vitu vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine kumekuwepo na watumishi kukaimu kwenye nafasi za watendaji wakuu kwenye mashirika yetu na taasisi kinyume kabisa na sheria inavyosema. Unakuta mtu amekaimu zaidi ya miaka miwili hadi mitatu, wakati inatakiwa ndani ya miezi sita mtu aweze kupatikana kwa nafasi husika. Hii inasababisha mashirika yetu, taasisi zetu zisiwe na ufanisi katika utendaji na tutaendelea kuona mashirika yakiwa yanajiendesha kihasara kwa sababu hatujaweza kutengeneza management ambayo kwanza kabisa imebobea na inajua ni nini inafanya. Ukimkaimisha mtu hawezi akafanya decision kwa sababu hajua kwanza ultimatum ya nafasi yake ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni kuhusu madeni ambayo Serikali inadaiwa na hazi taasisi. Unakuta imepata huduma lakini inashindwa kulipa madeni haya. Kwenye Kamati tumeainisha; mfano ni madeni makubwa kutokana na mifuko ya hifadhi ya jamii, tumeona madeni takribani kwenye PSPF ukiyachukua yote kwenye categories zile tatu ni takribani shilingi trilioni 3.47 za wanachama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, alikuja Naibu Waziri wa Fedha akatuahidi kwamba watatoa hati fungani ya takribani shilingi bilioni 290 ambayo ilikuwa ni deni linalotokana na miradi, lakini mpaka leo hawajaweza kutoa hiyo hati fungani, hawajaweza kulipa malimbikizo ya madeni ya mwajiri kwenda PSPF, hawajaweza kulipa takribani shilingi trilioni 1.7 ya yale madeni ambayo waliyachukua kwa wastaafu wale wa kabla ya mwaka 1999. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuishii hapo tu, Shirika kama DAWASCO ni shirika dogo sana, lakini unakuta linadai shilingi bilioni 16 kutoka kwenye Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Hizi shilingi bilioni 16 zingeenda DAWASCO zingeweza kusaidia na kuboresha huduma ya maji Dar es Salaam na Pwani, lakini unakuta hawalipi wakiambiwa hawalipi kwa sababu ni Jeshi basi linaendelea tu wanapata huduma. Ifike wakati hizi taasisi kama hazilipi na zenyewe zikatiwe maji, haiwezekani Mtanzania anashindwa kulipa 20,000 mnamkatia maji, lakini taasisi ya Umma inadaiwa mpaka shilingi bilioni 16 hamuwakatii maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni uonevu na Mtanzania wa kawaida akisikia anashangaa sana, yaani akishindwa kulipa bili ya maji ya shilingi 10,000, 20,000 anakatiwa maji lakini unakuta mnadai zaidi ya shilingi bilioni 16 na bado huduma ya maji inaenda. TANESCO wanawadai, TSN wanadai, LAPF wanadai, Serikali mnadaiwa madeni mengi sana. Tuweze kulipa haya mashirika ili yaweze kujiendesha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine kwa haraka haraka kabisa, wakati tumepitia kwenye hizi taasisi tumegundua kwamba hizi taasisi zinajiendesha kihasara. Tatizo lingine ni kwamba fedha wanazozipata wanazitumia kwenye matumizi ya kawaida badala ya uwekezaji. Kwa mfano, kama ilivyoainishwa kwenye baadhi ya mashirika; tumeona NSSF walitumia zaidi ya asilimia 17 kinyume kabisa na vile ambavyo matakwa yanataka asilimia 10 kwa mwaka wa fedha 2015/2016; lakini pia kamati imeainisha AICC na mashirika mengine. STAMICO inajiendesha kwa hasara, wanaweza wakawa wanakopa benki wanakuja wanajitumia kwenye matumizi ya kawaida ambayo ni kinyume kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni kuhusu mikataba ambayo mashirika yetu yanaingia, taasisi zetu zinaingia hasa zikiwa kwenye ubia na wawekezaji wengine. Hii imekuwa inalipeleka taifa letu kwenye shimo siku zote. Na ninashindwa kuelewa wataalam wetu ni kwamba tunakuwa hatujui ni nini tunafanya au hatuna uzalendo wa kutosha. Kwenye taarifa yetu umetolewa mfano wa mkataba wa Mlimani City; kwamba sisi tunakubali kuingia mkataba wa kupata gawio la asilimia 10 ya faida na tunasema kwamba tunaingia mkataba mpaka baada ya miaka 50 ndipo tunaweza tukapata ile mali, na ukiangalia ubora wa yale majengo ya Mlimani City ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, ni dhahiri kabisa ndani ya miaka 50 tutakuwa tunapata mabua. Yaani wale wawekezaji watafaidika wataondoka sisi wakitupa asilimia 10 tu, Taifa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante,