Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buhigwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ALBERT O. NTABALIBA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UWEKEZAJI WA MITAJI YA UMMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuhitimisha Hoja ya Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, kama tulivyoiwasilisha leo asubuhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikupongeze wewe Mwenyekiti kwa kuongoza vizuri, lakini naomba niwapongeze Waheshimiwa Wabunge na Mawaziri waliochangia hoja hii, pia nimpongeze Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuchangia tena hoja hii. Tumepata wachangiaji 16 kwenye hoja hii na wengine 14 wamechangia kwa maandishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata hoja za wachangiaji tofauti na mchangiaji wa kwanza alikuwa Mheshimiwa Joseph Haule ameongelea mikataba ya Chuo Kikuu na Mlimani City, ameongelea mikataba ya TANESCO, ameongelea mikopo inayodaiwa na TANESCO na PSPF. Kamati inakubaliana na yeye kwamba hii mikataba kama tulivyosema kwenye ripoti yetu iweze kuangaliwa upya kwa sababu tunaamini kwamba hii asilimia kumi wanayoipokea katika miaka 50 ni ndogo sana, huenda thamani halisi baadae ikawa siyo nzuri. Kwa hiyo, tunaamini kwamba mapendekezo ya Kamati yaweze kuzingatiwa na yaweze kufanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikataba ya TANESCO kama Mheshimiwa Waziri alivyoongea na Kamati yetu imeongea vizuri, ni mategemeo yangu kwanza kipengele cha mikataba kama AG alivyosema nayo Kamati inashauri iweze kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu madai ambayo Serikali inadaiwa na PSPF tunakushukuru Mheshimiwa Waziri wa Fedha umeongea, ni concern ya Kamati kwamba speed inayotumiwa kuhakiki na kulipa madeni ni ndogo sana. Kwa hiyo, Kamati inaona kwamba Serikali bado hapa haijafanya juhudi kubwa, tunaomba kwamba Serikali iweze kuendelea na juhudi kubwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi wameongelea vile vile Ofisi ya TR kwamba kwa nini Ofisi ya TR iwe ni msimamizi wa mifuko. Waheshimiwa Wabunge ndiyo tuliotunga sheria hii mwaka 2010, Cap. 370 tulitunga ambayo mifuko inawekeza fedha nyingi na TR ndiye msimamizi wa Serikali. Kwa hiyo, ni wajibu wa TR kuhakikisha kwamba shughuli zote za Serikali na mashirika yake inaziangalia, na ni hakika kwamba Msajili ni kazi yake kuziangalia hizi sheria. Ukiangalia sheria inayounda Mifuko ya Hifadhi inaangaliwa vile vile na Benki Kuu na SSRA, lakini ni kazi ya TR tena kufanya uhakiki wa mambo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wajumbe wengi wameongelea kuhusu bodi na wengine wameenda mbele zaidi kuongelea mambo ya TANAPA. Kamati tumesema bayana, hatujaficha, Serikali ni wavivu katika kuteua bodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Mamlaka ya Uteuzi nafikiri haipelekewi mapendekezo mapema kiasi kwamba, mfano kwenye mashirika 41 tuliyokutana nayo; mashirika 13 yalikuwa hayana bodi na yapo mashirika mengine tuliamua kuyarudisha kwa sababu Mwenyekiti wa Bodi hakuwepo. Kwa hiyo, ni vizuri mamlaka zinazohusika ziweze kuteua bodi. Hata hivyo, tunaipongeza Serikali mmeanza kuchukua hatua, tunaomba hiyo hatua iendelee ili muweze kukamilisha mashirika yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, limeongelewa suala la National Housing, Mheshimiwa Omary Mgumba amesema haiwezekani National Housing ijenge, isimamie yenyewe, ikague ubora na kila kitu. Kwa hiyo, Wajumbe wana wasiwasi kwamba lazima kuwe na chombo kingine cha kuihakiki National Housing ili kuangalia accountability kwa sababu ni shirika hilo hilo linaloshughulikia mambo yote. Kamati imependekeza na iko kwenye mapendekezo ili Serikali iweze kuyaangalia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata mchango mwingine unaohusiana na TBA kwamba sasa hivi kuna mwamko TBA iweze kujenga majengo, je, nani anaikagua hii kampuni na haitoi gawio kwa Serikali. Kwa hiyo, nalo hilo Wajumbe wamelichangia nalo tunahisi kwamba Serikali iweze kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo walioonesha masikitiko makubwa. Waheshimiwa Wabunge, Serikali hii ina mashirika na taasisi 264 na mtaji wa mashirika haya yote ya Tanzania ukiyajumlisha ni trilioni 23 lakini faida kwa mwaka kwa mashirika yote ya Tanzania yenye mtaji wa trilioni 23 yanaleta faida ya bilioni 422 ambayo ni asilimia 1.83 ambayo Kamati hairidhiki. Huwezi kuwa na mtaji wa trilioni 23 ukaleta faida kidogo namna hii. Hata kama ingeweza kuleta ten percent ingeweza kuiingiza Serikali trilioni 2.3 ikaweza ku-boost mapato ya Serikali. Kwa hiyo, TR anayo kazi kubwa kuhakikisha kwamba mchango wa mashirika haya lazima uongezeke. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wajumbe wameongelea tena mashirika mengine kama STAMICO ambayo kwa kweli na sisi ni kampuni ambayo tuliihoji inaenda kwa hasara, inatumia ruzuku ya Serikali na huku ni msimamizi wa madini. Kwa hiyo, ni matumaini yetu kama Wizara iweze kuipa nguvu hili Shirika la STAMICO na kuipa mitaji ili iweze kujiendesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Lulida ameongelea jambo moja pale la kusema pale kuna mwekezaji kwenye national housing pale Kawe ni kweli. Kamati tumetembelea pale ule uwekezaji wote uliopo Kawe wa National Housing yuko mwekezaji mmoja mmbia ambaye viwanja vile kweli alinunua kwa milioni sita mwaka 1995 nafikiri. Lakini yeye ameingia ubia na National Housing kwa fifty fifty, miradi ile ni mikubwa lakini yeye ametumia bilioni sita kuingia kwenye mikataba mikubwa. Haya ni mambo ambayo yanaendelea kwenye uwekezaji wa mitaji ya umma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawashukuru tena Wizara kwa kuteua Bodi ya TANAPA, kama Mheshimiwa Nsanzugwanko alivyosema kuna kesi iliamuliwa pale ambayo ilitakiwa shilingi bilioni 10 ziwe zimeletwa Serikalini kwa ajili ya kutoza, lakini nashukuru kwamba imechelewa kwa miaka mitatu hatujui Kamati tunajiuliza kesi inaamuliwa kwamba shilingi bilioni 10 ziingie Serikalini lakini bodi haiteuliwi ili iweze ku-effect hizo fedha zije, zinakaa miaka mitatu, Kamati inajiuliza kulikuwa na nini? Kwa hiyo, tunashukuru sana kwamba Mheshimiwa Waziri amesema sasa bodi imeteuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu madeni; Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameyaongelea vizuri lakini yapo madeni ya majeshi, maji kwenye taasisi za Serikali, hayo nayo ni muhimu sana muweze kuyafanyia malipo ili kunasua hizi taasisi za umma ziweze kujiendesha. Kwa kweli ukikutana nao wanasikitika, tungeomba muweze kuwasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upo mwongozo wa TR ambao unasema mashirika ya umma yaweze kutumia asilimia kumi tu ya mapato yote, lakini yapo mashirika katika uchambuzi wetu tumekuta yanatumia zaidi ya asilimia kumi. Kwa hiyo, ni mategemeo yetu kwenye mapendekezo kwamba Serikali itaweza kuyachukua.
Lipo pendekezo moja la Mheshimiwa Elibariki Kingu ambaye ameenda kinyume, anasema haafiki kabisa kwamba TR aweze kusimamia mifuko ya jamii kwa sababu TR anayo mashirika mengi. Tukumbuke Mheshimiwa Kingu ni kwamba tulishatunga sheria, mpaka sheria itakapobadilishwa. Ni haki ya TR kuhakikisha kwamba Mifuko ya Hifadhi ya Jamii nayo anaiangalia kwa sababu inaweka uwekezaji na Serikali ndiyo inadhamini hata kama watakuwa wameshindwa kulipa fedha za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuhitimisha sasa naomba Bunge lako likubali maazimio na mapendekezo ya Kamati kama yalivyopendekezwa kwenye kitabu chetu. Baada ya kusema hayo nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.