Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nichukue fursa hii kukushukuru sana kwa nafasi hii niliyopata ya kuchangia Mpango huu wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao unaenda kuleta matumaini makubwa ya Tanzania yetu mpya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba pia nichukue fursa hii kwa haraka haraka kumshukuru na kumpongeza sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kasi kubwa na nzuri anayokwenda nayo na hasa hii ya kutumbua majipu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi tunasema kwamba Mheshimiwa Rais aendelee kusonga mbele na sisi tupo pamoja naye maana katika nchi hii kama kuna watu ambao wametuangusha kwa kiasi kikubwa na kwa muda mrefu ni watumishi. Wametuangusha kwa muda mrefu na watu walikuwa wanahisi kwamba labda wao ni watu wasioguswa. Napenda kusema Mheshimiwa Rais anaendelea kuwapa hata Waheshimiwa Mawaziri wetu ujasiri wa kufanya kazi na sisi Wabunge na Watanzania kwa ujumla wake tunawaunga mkono. Lazima twende mbele zaidi ikiwezekana tuiangalie Sheria yetu ya Utumishi maana huko watu ndipo walipokuwa wanajifichia wakihisi kwamba hawana namna ya kuweza kuguswa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya, naomba sasa nielekee katika kuzungumzia Mpango wetu wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao unakwenda sambamba na uchumi wa viwanda ili kuelekea katika uchumi wa kati.
Mheshimiwa Spika, jana nimesikitika sana katika Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani rafiki yangu mwasilishaji kaka yangu Mheshimiwa David Silinde alikuwa anakatisha tamaa suala la viwanda na akafika mahali akazungumzia mpango ule wa Serikali wa kuanzisha industrial business hub pale Kurasini kwa kusema kwamba kwa kufanya vile ni kama tunakaribisha Wachina sisi tunajigeuza kwenda kuwa wachuuzi, nadhani hajaelewa vizuri jambo hili.
Mheshimiwa Spika, namwambia Waziri wa Fedha aharakishe sana ile Kurasini business hub ipatikane kwa haraka. Wachina kule kwao wanafunga vile viwanda wanakuja kufungua hapa Tanzania. Namkaribisha aanze kuona namna Wachina wanavyokimbilia hapa Tanzania kufungua viwanda pale Mkuranga, tuna viwanda vingi na vinajengwa kila siku ya Mwenyezi Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivi sasa kiwanda kikubwa cha tiles kinajengwa pale Mkuranga katika Kijiji cha Mkiu. Kile kiwanda cha marumaru kitalisha East Africa nzima. Tutakapopata business hub pale Kurasini maana yake ni kwamba watu watakuwa wanajua one business stop center ipo pale Kurasini na watakwenda kupata bidhaa zinazozalishwa pale. Sisi leo pale tuna viwanda vya cement wenzangu wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa wanaomba viwanda vya cement. Tuna kiwanda cha cement cha RHINO, tuna kiwanda cha cement cha Diamond pale, tunatengeneza mpaka yeboyebo pale Mkuranga.
Mheshimiwa Spika, kwa bahati njema sana bomba la gesi lipo pale na namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Viwanda Mheshimiwa Mwijage kwa namna ambavyo ananipa support kubwa ya kuwaleta wawekezaji waje kuwekeza katika lile bomba la gesi ambalo lina toleo lake katika vijiji vyangu vya pale Mkuranga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba niendelee kuunga mkono…
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nasema Serikali iendelee na mpango huu wa viwanda na sisi tumejipanga vizuri sana. Katika eneo moja ambalo tumejipanga vizuri pale Mkuranga ni hilo la viwanda, tuna hekari zaidi ya elfu kumi ambazo zipo tayari kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nipongeze sana Mpango wa Serikali wa Miaka Mitano ule wa kuboresha miundombinu yetu. Katika hili naomba nimwambie rafiki yangu Mheshimiwa Silinde na Kambi Rasmi ya Upinzani namna alivyopotoka tena amemtaja mpaka kipenzi chetu Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika ukurasa wa tisa eneo la barabara, eti Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kuwakumbusha Watanzania kwamba aliyekuwa Waziri wa Ujenzi wakati wa utekelezaji wa mpango uliopita ndiye Rais wa sasa, kwa hiyo hakuna matumaini. Nataka nimwambie matumaini ni makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza katika takwimu zake nataka nimwambie amekosea jambo moja kubwa. Waziri wa Fedha alipokuwa anasoma Mpango ule ametuelekeza kwamba mpango wa Serikali ulikuwa ni kujenga kilometa za lami 5,775 lakini mpaka tunafika Desemba 2014 zilikuwa zimeshajengwa zaidi ya kilometa 2,775. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hapa Waziri wa Fedha hakuweka mwaka wa 2015, kuanzia Desemba, 2014 mpaka 2015 na kufika hapa leo, Wizara ya Ujenzi katika muda huo ambao haukutajwa imejenga zaidi ya kilometa 500 za barabara za lami. Naomba nizitaje, Ndundu - Somanga kilometa 60, Tunduma - Sumbawanga kilometa zaidi ya 200, Lwanjilo - Chunya kilometa zaidi ya 36 na Iringa - Dodoma zaidi ya kilometa 259. Kwa namna ya kipekee kabisa naipongeza Serikali yangu namna tulivyojenga barabara za lami za kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako naomba niitaje barabara ya Ubungo Bus Terminal…
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mpaka Mabibo na Kigogo zaidi ya Kilometa 6.4, barabara ya kutoka Uwanja wa Ndege pale Jeti kwenda Vituka mpaka Devis Corner kilometa zaidi ya 10, barabara ya kutoka Ubungo Maziwa - External zaidi ya kilometa 2.25, barabara ya kutoka Kibamba - Mloganzila zaidi ya kilometa 4. Halafu watu hawa namna wasivyokuwa na shukrani tazama ukipita leo katika Jimbo la Ubungo unatoka Goba mpaka unakwenda kutokea Chuo Kikuu ni lami tupu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namwomba Waziri wa Fedha katika Mpango huu aoanishe na Waziri wetu wa Ujenzi sasa twende katika kuijenga barabara ya kutoka Mkuranga - Kisiju ambapo eneo hilo linakwenda kuwa la viwanda. Hii ni katika kukamilisha ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipokuja kuwaomba kura Watanzania wale wa Mkuranga aliwaambia barabara ile itajengwa. Nina hakika kwa mwendo ambao tunakwenda nao barabara ile itajengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sasa nielekee katika maji…
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Spika, nasikitika sana kusema kwamba muda wote huo ….
SPIKA: Mheshimiwa Ulega kuna taarifa ngoja uipokee.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Haya ahsante.
SPIKA: Mheshimiwa Silinde kifupi sana....
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Spika, sijaipokea kwa sababu rafiki yangu Mheshimiwa Silinde nimemkumbusha kwamba ujenzi wa barabara uliendelea katika mwaka wa 2015, asisahau na madaraja ambalo na yeye atakwenda kupigia picha pale Kigamboni. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, nasikitika kusema kwamba wenzetu hawa hata masuala ya maji hawakuyazungumzia. Tazama Serikali yetu ina mpango mzuri sana wa maji.
Mheshimiwa Spika, katika hili la maji, napenda niipongeze sana Serikali. Napenda niseme kwamba nina hakika katika miaka mitano hii ile ajenda yetu ya kumshusha mama ndoo kichwani itafanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mpango wa Maendeleo unaelekeza kwamba katika miaka mitano iliyopita takribani asilimia zaidi ya 60 ya Watanzania walipata maji safi na salama. Katika Jiji la Dar es Salaam, watu wanabeza tazama Jiji la Dar es Salaam lilivyopata bahati kubwa sana tena kwa pesa zetu wenyewe za ndani. Maji ya kutoka Ruvu Chini yamepita Bagamoyo yamekwenda mpaka Chuo Kikuu kule cha Dar es Salaam, bomba lile limelazwa kwa pesa ya Serikali yetu. Kwa kweli napenda sana niipongeze Serikali. Pia kuna mpango wa maji wa Dar es Salaam wa Ruvu Juu ambao sasa hivi unaendelea vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pale Mkuranga upo mradi mkubwa wa maji ambao utahudumia Dar es Salaam kwa maana ya maeneo ya Kigamboni, Mbagala na Kisarawe, mradi ule wa Kimbiji na Mpera. Naiomba Serikali sasa ihakikishe kwamba mradi ule unawanufaisha na watu wa Mkuranga katika vijiji vya Mkuranga, Dundani, Mwanambaya, Mwandege, Kipala Mpakani vyote viweze kupata maji yale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niishauri Serikali katika Mpango huu wa Miaka Mitano ihakikishe kwamba inatoa maji kutoka katika Mto Rufiji kwani zaidi ya asilimia 50 ya maji ya Mto Rufiji hayana matumizi yoyote. Kilometa hata 200 hazifiki kutoka Mto Rufiji kuja Dar es Salaam. Tuyatoe maji yale tuyalete Dar es Salaam, maji haya ya visima hayana hakika hata Naibu Waziri wa Maji jana alieleza hapa, Engineer Kamwelwe yeye mwenyewe amesema kwamba maji haya ya visima hayana hakika.
Mheshimiwa Spika, tutakapotoa maji kutoka Mto Rufiji yatanufaisha Wilaya za Rufiji, Kibiti, Mkuranga na yatanufaisha Dar es Salaam yote ya Kusini bila kuisahau Kisarawe. Naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha aweke mpango huu madhubuti wa kuhakikisha tunatatua kabisa kero ya maji katika Wilaya zetu na nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho, naomba nizungumzie suala la kilimo. Katika Mpango wa Maendeleo imeelezwa kwamba kutoka 2010 kurudi nyuma ilikuwa ni karibu asilimia mbili na point lakini kutoka 2010 kuja 2015 zilizidi kidogo asilimia ikaja mpaka asilimia 3.4 bado ukuaji huu ni mdogo. Pamoja na ukuaji huu kuwa mdogo bado nchi yetu imekuwa na chakula cha kutosha na mpaka tukawa na chakula cha ziada.
Mheshimiwa Spika, hivi sasa tuna tatizo kubwa la mabadiliko ya hali ya hewa, naiomba sana Serikali katika mpango wake wa bajeti hii tunayokwenda nao sasa ihakikishe kwamba mambo makubwa mawili, matatu yafanyike.
Mheshimiwa Spika, la kwanza, ni kuipa nguvu zaidi Wizara yetu ya Kilimo ili tuweze kujielekeza zaidi katika kilimo cha umwagiliaji. Hata pale kwangu Mkuranga ipo miradi ya umwagiliaji ya Changanyikeni, Yavayava na Kisere. Miradi ile yote haiendi vyema ni kutokana na ukosefu wa fedha. Ninayo matumaini makubwa kwamba katika mwaka huu tunaokwenda nao tutapata pesa ya kutosha na hatimaye miradi ile inaenda kutekelezwa na kukamilika na kuwanufaisha wananchi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili, ili kuhakikisha kilimo chetu kinaenda vizuri ni pembejeo. Ni lazima tuipe pesa ya kutosha pembejeo ili kilimo chetu kiwe na tija. Kwangu naomba sana pembejeo ya sulfur. Pembejeo hii ya sulfur nashauri iuzwe kama inavyouzwa cocacola dukani. Sisi wakulima wa korosho tukikuta sulfur inauzwa kwa wingi madukani tutaridhika sana. Nataka nikuhakikishie wakulima wote wa korosho baada ya hapo tutakipa chama chetu Chama cha Mapinduzi kura zote za ndiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuna matumaini mkubwa sana, tazama mfumo wetu wa stakabadhi ghalani, Waziri Mkuu juzi amekwenda kule Mtwara na Lindi ameboresha mfumo huu. Tunayo matumaini kwa kasi tunayokwenda nayo kero zote zinazotusumbua katika mfumo wa stakabadhi ghalani zitatatuliwa. Mwaka huu korosho imeuzwa zaidi ya Sh.2,500 kwa kilo katika Wilaya yangu ya Mkuranga. Watu wamepata pesa nyingi na mambo yanakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niunge mkono hoja ya Mpango huu wa Maendeleo. Ahsante sana.