Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Korogwe Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza mimi nianze kwa kurudia tena kuwashukuru Wabunge wenzangu wote ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vilevile nirudi tena kuwashukuru kwa msaada mkubwa ambao Wabunge walinipatia nikiwa hospitalini nikiwa nimelazwa. Sitaacha kulisema hili kwa sababu wala sikutarajia, wala sikutegemea kama Wabunge wangejitokeza na kunipa misaada mbalimbali, Mungu awabairiki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimshukuru sana Waziri wa Afya pamoja na Naibu wake, Katibu Mkuu pamoja na Daktari wa Muhimbili, wamefanya kazi kubwa sana ya ziada. Sitaacha kulisema hili kwa sababu unapopata nafasi lazima uliseme. Bila Waziri wa Afya kulisimamia kidete kunipeleka mpaka ofisini kwake na kunihakikishia barua yangu inapita, nisingefika na leo hii nikaja kusimama na Wabunge wenzangu ili nitoe neno la shukurani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisimamie suala moja tu la insurance, Bima ya Afya. Katika muda ambao nimekaa hospitalini nikiangalia bima ya afya inatakiwa iboreshwe kwa hali ya juu sana; kwa sababu kama sisi tunapewa vile vitambulisho vya V.I.P halafu kuna wengine wakulima ambao hawana vitambulisho vya V.I.P; lakini sisi tuliopewa vitambulisho vya V.I.P tunaambiwa tukanunue dawa nje za kutibiwa maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba unapokatwa hela yako ni kwamba utibiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jubilee walikuwa wanatukata hela hapa, tulikuwa tunasafiri mpaka India. Tunakwenda tunatibiwa wala hatupati shida ya aina yoyote. Leo tumesema haya mambo yote yarudi katika upande wa Serikali, lakini cha kushangaza leo hii mtu ameugua Mombasa, ameumia, anakwenda na insurance yake anaambiwa hii haitambuliki hapa, basi matokeo yake inafika mahali anafika mwingine anawekwa dhamana kwa sababu ya mtu. Kitendo hiki kimetudhalilisha sana sisi Wabunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekaa hospitalini, nimetibiwa kwa muda wa karibuni siku 27 katika Hospitali ya Mikocheni, nimehudumiwa kila kitu lakini vipimo vya gharama kubwa nimelipiwa na insurance. Kipimo kidogo cha gharama ya 30,000 naambiwa nikanunue nje, sasa nini maana ya Bima ya Afya? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Bima ya Afya sisi Wabunge ambao tunazipitisha hapa yanafanyika haya, je huyo Mtanzania wa chini ambaye hana uwezo kabisa atakuwa amefika wapi? Naomba Wenyeviti, mmetuletea hili jukumu, kwa kweli Serikali tunataka waiboreshe sana Wizara ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiini cha matatizo ni Wizara ya Afya kutengewa hela ndogo ndogo ambazo hazina msingi; kwa sababu Wizara ya Afya peke yake; nimetoka India juzi, kule Wizara inadaiwa zaidi ya bilioni 37 na bado wanatakiwa Wizara ya Afya itusaidie sisi Watanzania tulioko ndani ya nchi. Sasa hivi kule watu wanaanza kukata tamaa kutuhudumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo; hatukatai kwamba Serikali imejitolea sana kwa hali na mali na mimi naishukuru sana Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli inafanya kazi ya ziada sana; tunapofanya mambo haya tuangalie na utaratibu kwamba hii Wizara tunaisaidia kiasi gani. Hakuna kitu kibaya kama mtu; afadhali ukose chochote, lakini upate elimu na upate afya bora. Bila Wizara ya Afya kunisimamia kidete, bila Bunge kunisimamia kidete, bila ya Rais kunisimamia kidete, leo hii nilikuwa nakatwa mguu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba sana; Wenyeviti wa Kamati wametuletea mapendekezo lakini hii Wizara ya Afya inapata hela lakini hela zake hazitoshelezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii katika vijiji, wananchi wameamua kujenga zahanati lakini wameamua kujitolea wenyewe, kwangu wamejitolea kujenga zahanati lakini zahanati hizo hazisaidii chochote kwa sababu ukienda Wizara ya Afya unakuta watu wanakaa pale kusaidia lakini inafika mahali watachukua wapi hela ili ziende kule vijijini zipeleke dawa? Dawa zipo kweli, lakini namna zile dawa zitakavyotumika vijijini lazima na sisi tuwaunge mkono hawa, lazima na sisi Wabunge safari hii tuhakikishe hii Wizara inapatiwa hela ya kutosha ambayo itatusaidia ili kuboresha mambo yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitasema kweli daima fitina kwangu mwiko. Kwa kweli Wizara ya Afya ni kiungo muhimu sana kwa mwili wa binadamu. Leo hii angekuwa ameugua mtu mwingine ningesema labda wanatutania, nimekaa siku 27 Mikocheni, nimekwenda Muhimbili kwa Mkurugenzi wa mifupa nimeona shida wanayoipata. Nimeenda Wizarani nimeona wanavyohangaika, wanahangaika kweli kweli kutusaidia lakini hela hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wenyeviti mfanye mambo yenu yote lakini hebu jaribuni kumsaidia Dada Ummy. Yeye kama Ummy ni Waziri, yeye kama yeye hawezi kupitisha chochote lazima ninyi Wenyeviti na nyie mtilie mkazo. Sasa mnapotilia mkazo baadhi ya mambo wakati mnafikiria kwamba yeye atakwenda kutafuta hela sehemu nyingine tunakuwa tunamuumiza na Serikali hii tusitarajie kila kitu watufanyie Serikali na sisi wenyewe tujitume ili tufanye mambo mazuri ili tufanikiwe vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana hii insurance; na Mwenyekiti akija aje na jibu Jubilee ilifanya makosa gani na kwa nini iliondolewa? Kwa nini ilikatwa? Kama ilikatwa tukaamua kuliweka Shirika la Bima la Serikali ni tatizo gani lisiwe linafanya kazi katika nchi hizi tatu za Afrika Mashariki ili itusaidie hata wengine badala ya kwenda mbali zaidi; hata Afrika ya Mashariki unaweza kupata huduma ya kutosha tukashughulikiwa na insurance.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya nirudie kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wenzangu, walinipa matumaini makubwa sana, hawakujali vyama vyao, hawakujali mimi ni nani, walinifanya nikawa najisikia kwamba si mnyonge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nisiache kumshukuru Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, nisiache kumshukuru Naibu Spika, nisiache kumshukuru Katibu wa Bunge Dkt. Kashilillah, walikuwa wananipa moyo wa dhati. Hatua ya mwisho nilikuwa nakaa ofisini kwa Naibu Spika akiniambia subiri subiri na leo subiri hii nimeweza kuja hapa, Mungu awabariki sana Waheshimiwa Wabunge, Mungu awabariki sana Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sitakuwa na mengi ya kuongea ila nilikuwa tu nataka nikazie hii insurance kwa sababu ikifika mahali hospitali nyingine ukienda hutibiwi bado hatujasaidia Watanzania. Kama umepewa insurance basi kila hospitali unayokwenda unatakiwa utibiwe kwa kutegemea ile kadi uliyopewa. Leo hii unachaguliwa baadhi ya hospitali, hospitali nyingine wakikuona wanakuona vile kama kituko, sasa kituko maana yake ni nini? Tunakatwa hela, wanazichukua halafu kwenye huduma unaambiwa dawa nyingine ukanunue wewe mwenyewe wakati umekaa hospitalini….
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya Mungu atubariki, naunga mkono hoja ya viongozi hawa.