Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nomba nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia taarifa hii ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii na Kamati ya UKIMWI. Namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa uhai ili niweze kusimama hapa siku hii ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la elimu bure. Nichukue nafasi hii kuipongeza sana Serikali kwa kuthubutu kuweza kutekeleza elimu hii bure. Dhamira ni njema, lakini katika mpango huu bado kumekuwa na changamoto nyingi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la elimu napenda kuzungumzia kwamba elimu bure sawa inatolewa, lakini pia ukienda kwenye shule zetu za primary na za secondary kumekuwa na changamoto ya upungufu wa madarasa; lakini bado katika Mkoa wangu wa Ruvuma kuna changamoto katika Wilaya ya Namtumbo katika sekondari ya Nungu Kata ya Hanga.
Kwenye hiyo sekondari ambayo sasa imeanza kidato cha tano; na changamoto iliyoko hapo inafanana kabisa na changamoto iliyoko katika Wilaya hiyo hiyo katika sekondari ya Nasulu Wilayani Namtumbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu sekondari hizi zilipoanzishwa kwa kidato cha tano hawajapelekewa pesa kwa ajili ya chakula. Kwa hiyo niombe, tunapoamua kutoa elimu bure ni vizuri basi tukajikita kwenye mambo ya msingi. Kwa mfano; mtoto hawezi kuendelea kusoma na akajituma vizuri zaidi na kuweza kuwa msikivu katika masomo kama hatakuwa amepata chakula. Wazabuni ambao wamejitokeza kutoa huduma katika shule hizi wameshafanya kwa kiasi walichoweza, lakini imefika mahali wanakwama kwa sababu hawajawezeshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa Walimu pia unachangia kwa kiasi kikubwa. Hili ni eneo ambalo wajumbe wenzangu wengine Waheshimiwa Wabunge wamechangia; kwamba bado maboresho dhidi ya Walimu hawa yanatakiwa ili Walimu waweze kuwa na moyo wa kuendelea kutoa huduma hii ya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende pia kwenye suala la afya katika Wilaya hiyo hiyo ya Namtumbo. Hospitali hiyo inajengwa kwa takribani miaka mitano sasa na haijakwisha. Mpaka sasa hivi ninavyozungumza, hospitali hii ya Wilaya ya Namtumbo bado ina jengo la OPD tu, hakuna wodi wala hakuna theatre.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Wilaya ya Namtumbo ni wilaya kubwa sana na imejumuisha kata nyingi, zaidi ya kata 23, bado wilaya hii inahudumia pia mji mdogo wa Lusewa; Wizara ingefanya jitihada za makusudi kuhakikisha kwamba hospitali hii ya Wilaya inakwisha ili iweze kuendelea kutoa huduma kwa sababu akinamama wengi wajawazito wanapata shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hizi kata zilizopo pale katika Wilaya ya Namtumbo nyingi zimekuwa kwenye maeneo ya mbali. Unakuta kutoka kwenye kituo au Makao Makuu ya Wilaya kwenda kwenye maeneo ya pembezoni, maeneo mengine yanafikia kama kilometa 100, kilometa 70 na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri kwenye Wilaya hii ya Namtumbo, kwa maana ya Hospitali ya Wilaya, angalau ingekamilishwa wodi ya akinamama ili kuweza kuwafanya akinamama waweze kujifungua salama. Kwa mfano; kuna kituo hiki cha Lusewa; Kituo hiki cha afya cha Lusewa kimekuwa kikihudumia wanawake ambao wakati mwingine wakizidiwa wanajikuta wanalazimika kwenda katika hospitali ya Mbesa ambayo iko karibu kilometa 150 kutoka Wilayani Namtumbo na usafirishaji wa akinamama hawa wakishakuwa kwenye hali mbaya mara nyingi wamekuwa wakibebwa na pikipiki. Yanatengenezwa matenga huku nyuma, wanawekwa kwenye matenga ili waweze kusafirishwa ili kufikishwa kwenye hospitali ya Mbesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana, mama yangu Ummy, naomba asikie kilio hiki cha wanawake wa Mkoa wa Ruvuma ili waweze kusaidiwa kwenye eneo hili ambalo imekuwa ni eneo tete sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende pia kwenye Wilaya ya Tunduru katika zahanati ya Legezamwendo. Zahanati ya Legezamwendo ni zahanati ambayo imezungukwa na vijiji karibu sita; zahanati hii bado haijakamilika na sasa hivi tayari inakaribia miaka minne. Niombe basi zifanyike jitihada za makusudi kuhakikisha kwamba fedha zinakwenda ili zimalizie zahanati ile ili iweze kutoa huduma kwa wananchi ambao kimsingi baadhi yao tayari wameshapewa hata zile kadi za CHF ili waweze kuzifanyia kazi hizo kadi zao na waweze kupata huduma ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika katika Hospitali ya Wilaya ya Tunduru. Hospitali ya Wilaya ya Tunduru ni ya muda mrefu sana ambayo inahudumia karibu Halmashauri mbili zenye zaidi ya Kata karibu 54; na unapoambiwa Kata zaidi ya 54 kwa Wilaya ya Tunduru ni eneo la kilometa za mraba nyingi mno kiasi ambacho kutoka kituo kimoja mpaka kufika Hospitali ya Wilaya ni parefu mno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe miundombinu ya Hospitali ya Wilaya ya Tunduru iweze kuboreshwa ili wale wote wanaopata huduma katika hospitali ile waweze kupata huduma stahiki. Ingawaje sasa katika hospitali hiyo kumekuwa na mrundikano mkubwa sana wa wagonjwa kiasi ambacho hospitali inazidiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wakati tunaendelea kufanya miundombinu mingine, nadhani tuanze na hii Hospitali ya Wilaya tuiangalie ili tuweze kupata theatre; theatre ipo lakini ipanuliwe zaidi ili kuendelea kuboresha huduma hizi. Pia madawa na vifaa tiba viongezeke mara dufu ya vile vinavyotolewa sasa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.