Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Ajali Rashid Akibar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Newala Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nichukue nafasi hii kukushukuru wewe mwenyewe kwa kunipa nafasi hii, lakini pili nichukue nafasi hii pia kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuweka hai sisi Waheshimiwa Wabunge. La tatu nikipongeze chama changu Chama cha Mapinduzi jana kwa kutimiza miaka 40, ni umri wa mtu mzima kwa kweli. Maana sijasikia kama Chama cha Mapinduzi kimepongezwa, kwa hiyo nitoe taarifa kwamba jana ndio kilikuwa kinatimizia miaka 40 kakweli nakipongeza sana, nampongeza Katibu Mkuu na Mwenyekiti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine nipongeze kamati zote mbili kwa maana ya Kamati ya UKIMWI pamoja na Kamati ya Huduma za Jamii. Ukiangalia mustakabali wa hizi kamati zote mbili kwenye taarifa zao yaani utaona kabisa hizi Kamati zote zimefanya kazi kubwa sana tena kwa muda mfupi na kila kitu kimeelezwa humu, hakuna jambo ambalo ni geni ambalo sisi Waheshimiwa Wabunge tunaweza tukalizungumza nje ya yale ambayo Kamati imeyazungumza; kwakweli Kamati nazipongeza sana kwa ufanisi wenu wa kazi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yale mapungufu ambayo yanazungumzwa na mimi ningechukua nafasi hii kuchangia mapungufu ambayo nimeyaona hasa yale ambayo nimeona kuhusu dawa za kulevya. Upungufu inaonesha kabisa kwamba kulikuwa na mamlaka ambayo imeanzishwa kisheria ambayo ilikuwa imepitishwa kutoka mwaka jana lakini ukamilishwaji wa hii Kamati ndipo yote haya yanatokea leo kamata kamata inakuwa nani hajulikani akamatwe na yule ambaye asikamatwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inaonesha kwamba ile mamlaka ambayo ilikuwa imeanzishwa ule mchakato mpaka leo haujakamilika; haina commissioner, ina upungufu wa vitendea kazi na rasilimali watu. Japo kuwa kuna watu tumewasomesha lakini watu hao hawafanyi kazi, tuna polisi wa kutosha, lakini hawawezeshwi hawa watu ili wafanye kazi leo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sisi ambao tumewahi kuwa Waheshimiwa Madiwani Jijini Dar es Salaam hili suala la kamata kamata la unga ni suala la muda mrefu sana. Vinginevyo watu watakuwa wanatuhumiwa, Wabunge wengine watakuwa wanakamatwa au watakuwa wanatajwa lakini wataambiwa wamehusika. Huu mchezo tusipokuwa makini sana itakuwa sawasawa na mchezo wa chura maana watoto walikuwa wanarusha mawe kwenye maji halafu ule mchezo watoto wanacheka, lakini chura wanalia; wakawaambia nyie watoto huo mchezo mnaoufanya ni mauti yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hatujui kwamba ni nani ambaye anawajibika moja kwa moja, kwa hiyo Kamati sababu ile watu wenye mamlaka hawajapewa mamlaka wala hawajawezeshwa kufanya kazi. Kwa hiyo, wale Mawaziri wanaohusika na tasnia hii waje waileze Kamati kwamba je, ni lini sasa hizi taasisi na hizi zinaanza kufanya kazi kwa ufanisi ili tujue nani anaewajibika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusifanye masihara ni gharama kubwa sana kutengeneza majina lakini kuyaua unaweza kuyaua kwa muda mfupi sana, tusifanye masihara kutengeneza jina. Lakini vile vile tulikuwepo pale tuliona watu ambao wametengeneza majina wameharibiwa hayo majina, lakini je, ni nani ambaye atakuja kuwajibika kwa kuharibiwa jina? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kamati imezungumza vilevile kuhusu udhaifu ambao umejitokeza wa ukosefu wa fedha. Inaonesha kabisa kwenye tasnia ya afya, kwa sababu afya ndio lango kuu la nchi hii, tunategemea afya na elimu. Lakini utaona kabisa kwamba afya pamoja na elimu zote hizi zimepelekwa TAMISEMI. Kwa hiyo, maana yake ni kwamba Wizara ya Elimu yenyewe inakuwepo pale ceremonial kama policy makers, lakini hawasimamii moja kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati sisi tunasoma tulikuwa tunajua kwamba kila kitu ambacho kilikuwa kinahusu elimu tulikuwa tunaenda Wizara ya Elimu lakini leo ukitaka kujua nini kuhusu elimu ukienda Mkoani au ukienda Wilayani Wizara ya Elimu kule, kule wewe utakuta tu TAMISEMI pamoja na Local Government kwa kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ina maana huwezi kujua kwamba kwenye ubovu wa elimu ni nani anaewajibika? Anaewajibika ni TAMISEMI au Wizara ya Elimu moja kwa moja? Kwahiyo, ningeomba hawa Mawaziri wawili wanapokuja hapa waje watueleze kwamba ni nani ambaye anawajibika moja kwa moja ili tujue kwamba ile idara ya ukaguzi iliyopo pale TAMISEMI nani ambaye anasimamia kuiwezesha fedha ili ikafanye ukaguzi ili ubora wa elimu uwe juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo hivyo upande wa afya; utadhani kana kwamba Wizara ya Afya nao ni policy makers wao wanatengeneza tu sera, lakini moja kwa moja vile vituo vya afya ambavyo vipo vijijini ambavyo havina dawa; huku tunaambiwa kwamba dawa zipo lakini ukienda vijijini dawa hazipo kabisa. Lakini vilevile tuna sera za wazee tunasema kabisa tunapokwenda kule tunaenda kujinadi kwamba aaah, sasa hivi matibabu kwa wazee zipo bure; Lakini tunaulizwa sasa hivi imeshachukua muda mrefu sisi wazee bado tunapata shida ya kupata tiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo, Mheshimiwa Waziri wa Afya aje atueleze kwamba ni lini hii sera itakuwa imeshakamilika na hawa wazee watapata tiba ambayo moja kwa moja itakuwa bure ili nasi tuweze kujikimu kama Waheshimiwa Wabunge wamewahi kuzungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Elimu na Wizara ya Afya isipokuwa makini; mimi nadhani kwamba Wizara ambayo ninaipongeza ni Wizara ya Maji. Ukienda hata huko kwenye Local Government unakuta kabisa Wizara ya Maji inakuwa na uwajibikaji, ukienda kwenye Idara ya Maji unaona kabisa kwamba hawa watu wa maji wanajishughulisha moja kwa moja. Kwahiyo, ningeomba kwamba hizi Wizara mbili, kwa maana ya Wizara ya Afya pamoja na Wizara ya Elimu na yenyewe ichukue mfumo huo huo, kwa maana kwamba wawe wanasimamiwa wanafika mpka huko chini ili kwenda kusimamia kuhakikisha kwamba haya mambo yetu yanakwenda badala ya kuwa yamesimama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi michango yangu ilikuwa ni hiyo miwili ya kuhakikisha kwamba hawa Mawaziri wanatupa taarifa ni nani ambaye ambaye anawaibika kati ya Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja kwa kuwa hoja yangu ilikuwa ni fupi, asante sana!