Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, nami naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwanza kwa kunipa afya na kunijalia kufika siku ya leo niweze kuchangia kwenye huu Mpango.
Mheshimiwa Spika, naanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwanza kwa kasi kubwa ambayo ameanza nayo. Kasi hii inawatisha watu wote. Ukiona maadui zako wanaendelea kukusifia, basi lazima ujue kuna tatizo. Kwa hiyo, wale ambao wanaona hawafanyi kazi, nadhani wanaogopa kivuli chake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nampongeza Rais kwa kurudisha nidhamu ya Watumishi wa Serikali. Nchi yetu ilikuwa inarudishwa nyuma na mambo mengi sana, likiwemo suala la Watumishi wa Serikali kutokuwa na nidhamu; nidhamu ya muda, lakini hata nidhamu ya utendaji. Hili kama litasimamiwa vizuri, tunaanza kujenga spirit ambayo mtu akiingia ofisini, anafahamu kwamba yuko pale kwa ajili ya kufanya kazi ya wananchi. Hili ni lazima lisimamiwe vizuri pamoja na viongozi wengine walioko ngazi ya chini.
Mheshimiwa Spika, pia nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kurudisha nidhamu ya matumizi. Naamini tulikuwa ni nchi ambayo tunaweza angalau kujitegemea kwa kiwango fulani lakini matumizi yetu yalikuwa yanakiuka baadhi ya mambo na kuonekana ni nchi maskini sana. Nampongeza pia kwa zoezi lake la kuhakikisha kwamba Watanzania wanalipa kodi.
Mheshimiwa Spika, suala la kodi ni suala ambalo Tanzania ilikuwa inaonekana anayelipa kodi ni mshamba. Watu wengi walikuwa wanajisifu kwa kutokulipa kodi. Sasa hivi utasikia malalamiko ya watu wengi kwamba wamebanwa. Watumishi wa Serikali tulikuwa tunalipa kodi kubwa zaidi kuliko wafanyabiashara.
Mheshimiwa Spika, ombi langu tu hapa ni kwamba, zipo lugha ambazo zinatuchonganisha; zinamchonganisha Mheshimiwa Rais. Wapo Watumishi wa Serikali wanakwenda kulazimisha watu walipe kodi kuliko ambayo inatakiwa kulipwa anasema na ni kwa sababu ya Serikali yenu. Naamini watu hawa wakifuatiliwa, kodi ni kwa manufaa ya umma.
Mheshimiwa Spika, nampongeza Waziri wa Fedha kwa kuja na Mpango wake huu. Naamini kwamba hivi vipaumbele ambavyo vimewekwa kwenye Mpango huu kama vitasimamiwa, tunaweza tukaifikisha Tanzania sehemu nyingine.
Mheshimiwa Spika, tunalo ongezeko la mapato ya TRA, mapato yetu ya kodi. Nawapongeza sana! Wasiwasi wangu ni mmoja tu hapa, yapo malalamiko sana kwa wafanyabiashara; hakuna uniformity pale bandarini. Leo atakuja mtu ana container, declaration inaonesha vifaa vilevile ataambiwa Shilingi milioni 20, lakini mtu yuleyule akirudi next time ataambiwa Shilingi milioni 50, lakini jana yake utaambiwa mtu mwingine amelipa Shilingi milioni tisa.
Mheshimiwa Spika, nadhani iko haja ya kuweka utaratibu, badala ya kuacha hii freelance ambayo mhusika anaweza aka-gamble nayo na kuhamasisha rushwa, uwekwe utaratibu ili kila mtu kabla ya kufanya importation, ajue kwamba mzigo huu nikiufikisha Tanzania anakwenda kulipa kodi ya shilingi ngapi.
Mheshimiwa Spika, bila kufanya hivyo, tutaendelea kuruhusu watu kukaa mezani na kujadili na matokeo yake yatakuwa kama aliyosema Mheshimiwa Keissy jana kwamba gari ile ile unanunua Dola 10,000, ukija pale, mtu wa TRA analazimisha iwe Dola 50,000, anakadiria kodi anayoitaka. Matokeo yake, watu wanakimbia gari pale bandarini, halafu Serikali inauza gari zile kwa bei rahisi zaidi kuliko ambayo alikuwa ameisema mhusika. Mimi nasema Serikali inafanya kazi nzuri, tunaipongeza, lakini ni lazima itoe macho zaidi katika suala hili.
Mheshimiwa Spika, niende kwenye Mpango ambao Mheshimiwa Waziri ameuleta. Kwanza nianze na suala hili la elimu. Nimekuwa napata tabu kidogo kuona Tanzania ina output ya wasomi wengi sana, lakini kila kona wasomi wanalalamika ajira. Tatizo ni kwamba hata anayemaliza Chuo Kikuu akimaliza hawezi kujitegemea, akimaliza hawezi kujiajiri, hata yule aliyesomea ufundi, ukimwingiza ukampa kiwanda leo, akifika mle ndani hawezi kufanya kazi aliyosomea. Nasema kwamba, katika kipindi hiki cha miaka mitano, ni lazima mfumo wetu wa output katika vyuo vyetu usimamiwe vizuri ili watu wanaotoka waweze kuwa ni material ambayo inakwenda kupata kazi kwenye soko.
Mheshimiwa Spika, niende mbali, tuna output kubwa sana ya darasa la saba na output kubwa sana ya form four na form six ambao hawapati bahati ya kwenda kwenda kwenye Vyuo. Nataka kushauri, katika nchi zote ambazo zimefanikiwa kupambana na tatizo la ajira hasa kwa vijana, wameimarisha sana kwenye Polytechnic Colleges ambazo ndiyo zinaweza zikasaidia kupunguza tatizo la ajira. Kama tunaweza tukaweka katika Mpango wetu huu wa miaka mitano, tuweke mpango kuhakikisha kila mtoto aliyemaliza kidato cha nne, anakwenda Chuo cha Ufundi na iwe ni lazima. Hawa watu wataweza kujiajiri.
Mheshimiwa Spika, hivi sasa tumepeleka umeme katika kila kijiji, lakini mafundi wa umeme wanatoka Makao Makuu ya Wilaya. Hii sasa ilikuwa ni wajibu wa Serikali kuona kwamba tunaweka vyuo vya kutosha. Tunavyo Vyuo vya VETA, bado vyuo hivi ni gharama kubwa sana kwa wananchi wa kawaida. Chuo ambacho ulidhani angeenda mtu kusoma akapata ufundi, bado vyuo hivi vinachukua watu kwa kuchagua, wanakwenda watu 100 kati ya watu 10,000. Matokeo yake, bado kundi kubwa la vijana limezagaa mitaani, halina ujuzi wowote na Serikali nina uhakika hata tukizungumza kuwapa ajira, hawa sio sehemu ya kundi tunalofikiria.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka kushauri, pamoja na kuzagaa kwa vyuo, pamoja na mpango mzuri wa Serikali, tuweke mpango kabambe wa kuwa na vyuo vya ufundi ambavyo vitamlazimisha kila mtoto anayemaliza kidato cha nne, aende Chuo cha Ufundi ili apate kazi mbadala.
Mheshimiwa Spika, huwa nawaambia rafiki zangu tunaokwenda China; kule China ziko simu watu wanatumia hapa, zinatengenezwa mitaani tu, kwenye nyumba ya mtu. Ziko nguo zinashonwa mitaani, viko vitu vinatengenezwa hata ukitafuta kiwanda, huwezi kukipata kwa sababu kuna msambao wa viwanda vidogo vidogo katika kila kona na ndiyo namna tunavyoweza kupambana na tatizo la ajira kwa vijana, lakini na tatizo la viwanda.
Mheshimiwa Spika, kwenye Mpango kuna suala la viwanda. Tatizo langu ni kubwa. Hivi tunazungumzia viwanda vya namna gani? Viwanda hivi vitapata raw material wapi? Sehemu kubwa ya viwanda tunavyozungumza ni viwanda vya kilimo. Wilayani kwangu tuna Kiwanda cha Pamba cha Ginnery, kipo pale Kasamwa. Kile kiwanda hakijafanya kazi karibu miaka 15 sasa. Ukitazama uzalishaji wa zao la pamba umeshuka kwa kiwango ambacho kinatisha. Tatizo, kwa nini uzalishaji unashuka? Productivity ya uzalishaji inapungua wakati gharama za kilimo zinaongezeka! Viwanda tunavyozungumzia vinakwenda kupata raw material wapi?
Mheshimiwa Spika, nataka kushauri kwenye suala la kilimo, kwanza tu- invest kiasi cha kutosha kuhakikisha kwamba uzalishaji unaongezeka maradufu ili watu watakaoanzisha viwanda wapate raw material. Leo watu wanalima pamba wanapelekewa mbegu feki, halafu mwisho wa siku kwenye uzalishaji mdogo waliopata, wanakwenda kudaiwa na kulazimisha walipe. Matokeo yake ni watu wote wameacha kulima pamba, wanahamia kwenye mazao mengine.
Mheshimiwa Spika, nataka kushauri katika Mpango huu tuwekeze kiasi cha kutosha kuhakikisha kwamba uzalishaji kwenye mashamba, uzalishaji wa mazao katika viwanda ambavyo tunafikiria tunakwenda kuvipeleka, lazima tufikirie namna ya kuongeza mazao yawe makubwa zaidi. Uzalishaji uwe mkubwa zaidi; na njia hapa ni rahisi tu!
Mheshimiwa Spika, cha kwanza ni kuwa na wataalam wetu katika kila kijiji na kuhakikisha wanafanya kazi; lakini kuhakikisha pembejeo zinapatikana kwa wakati. Tulikuwa na tatizo la pembejeo Mheshimiwa Waziri wa Kilimo anajua. Pembejeo zinafika kwa wakulima mwezi wa kwanza. Wakulima wamekwishalima, wameshapalilia ndiyo pembejeo zinafika. Hawa watu wanalipwa!
Mheshimiwa Spika, tumeiambia Serikali kwamba kuna watu wanadanganya kwenye pembejeo, Serikali inatumia pesa nyingi sana, lakini haziwafikii wakulima; zinachelewa kufika. Ndiyo maana mtu analima heka tano za pamba anapata kilo 300. Ni kwa sababu pembejeo zinachelewa kufika. Kwa hiyo, nasema suala la viwanda liangaliwe vizuri kwenye suala la kilimo. Vile vile twende pia kwenye namna ambavyo tunaweza tukawaimarisha wananchi wa kawaida
Mheshimiwa Spika, sina tatizo sana na masharti ambayo yanayowekwa na watu wa Mazingira na kadhalika, lakini nadhani tume-copy sana mambo kutoka Ulaya kiasi kwamba tunashindwa kufikiria katika mtazamo wa Kitanzania, ni viwanda gani vinaweza vikasaidia wananchi wetu? Unaona kila siku tunapambana na watu wanaotaka kujikwamua.
Mheshimiwa Spika, kule Ulaya ukienda, mtu mwenye ng‟ombe wanne anaweza kuanzisha Kiwanda cha Siagi nyumbani kwake na akapeleka mazao yake kwenye Supermarket. Sisi kila siku tukienda kwenye mtu aliyeanzisha kiwanda, tunamfungia, huyu tunamfungia. Badala ya kuwasaidia hawa watu waimarike na wakue, tunawapunguzia uwezo. Utaona Serikali inapambana na watu wapunguze ng‟ombe, lakini haiwambii hao ng‟ombe wanaowapunguza itawasidiaje wabadilike kuwa na maisha tofauti.
Mheshimiwa Spika, mfugaji wa ng‟ombe anafanana sana na mtu mwenye mabasi kumi. Siku zote mtu mwenye mabasi kumi anataka afikishe mabasi 20. Hivi tuliwahi kumfuata mtu mwenye mabasi 20 tukamwambia apunguze idadi ya mabasi? Kwa nini tunafikiria kumwambia mwenye ng‟ombe apunguze, lakini hatumwambii apeleke wapi hizo fedha zake?
Mheshimiwa Spika, naomba sana kwenye hili suala la viwanda, tutafute namna ya kuwasaidia wananchi wa kawaida kuimarisha viwanda vidogo vidogo. Haijulikani SIDO ilifia wapi? Haijulikani kama ipo, inafanya kazi gani?
Nilitarajia tuone Tanzania ina Viwanda vya Sabuni kila Mtaa, Viwanda vya Nguo kila Mtaa na Viwanda vya kila kitu kila Mtaa. Sasa haya mambo hayafanyiki kwa sababu ya masharti mengi yanayowabana Watanzania na kuwafanya waendelee kutegemea bidhaa za kutoka nje.
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumze suala linguine. Kwenye Mpango naona kuna mpango wa kuongeza nishati. Nilisema wakati nachangia Hotuba ya Mheshimiwa Rais, nikasema naipongeza sana Serikali na mkakati wake wa kuimarisha njia ya umeme inayokwenda Kanda ya Ziwa.
Mheshimiwa Spika, nimekuwa na wasiwasi sana ya kuwa na njia moja kuu ya umeme ya kupelekea robo tatu ya nchi. Napenda kushauri, katika Mpango huu, ile njia iliyotajwa katika Mpango; ya Nyakanazi, ni njia ya muhimu sana. Nchi nyingi zinapata majanga! Linaweza kutokea janga katikati hapa, nusu ya nchi ikawa giza na nchi hii inakwenda kuwa nchi ya viwanda. Ina maana tutasimama uchumi wetu siku hiyo hiyo. Ni lazima tutafute namna ya kuimarisha njia ya pili ya umeme.
Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wangu wa Geita, bado umeme unazimika na kuwaka muda wowote kwa sababu njia iliyopo ni ile iliyokuwa inapelekea umeme Sengerema. Umeme ni mdogo sana. Wananchi pale kukatika kwa umeme kwao ni suala la kawaida, lakini umeme mzuri upo jirani tu Katoro pale.
Mheshimiwa Spika, nimezungumza na Waziri mara kadhaa na nimeomba sana katika mwaka huu wa fedha, umeme wa uhakika upelekwe Geita. Ni Mkoa mpya, Mkoa ambao tunatarajia utakuwa na viwanda vingi. Sisi katika Kanda ya Ziwa ni wakulima wakubwa sana wa nanasi, ingawa nanasi zile Mheshimiwa Mbunge mwenzangu alisema zinafaa kutengeneza madawa ya kienyeji, lakini tunapozungumzia viwanda, basi lazima wakulima waambiwe ni mananasi yapi yanayofaa kwa ajili ya kuuza kwenye viwanda, kwa sababu ardhi inakubali kulima nanasi, kahawa na mazao mengine. Ni lazima tukubaliane kwamba tunahitaji umeme ili huu umeme uweze kuwasaidia wananchi wa Geita.
Mheshimiwa Spika, katika Mpango huu, naomba sana, sisi Kanda ya Ziwa kama walivyosema wenzangu, tunalo tatizo la bidhaa zote zinazotoka Dar es Salaam kufika Kanda ya Ziwa zikiwa zimepanda bei. Ukifika Geita leo, utakuta bandali moja ya bati inauzwa Sh. 280,000/= wakati bandali hiyo hiyo Dar es Salaam inauzwa Sh.160,000/=. Ni kwa sababu ya matumizi ya barabara. Tunaomba sana reli, reli ikiimarika, itasaidia kupungua gharama za vifaa vya viwandani ambavyo vinapanda bei kila siku Kanda ya Ziwa.
Mheshimiwa Spika, hata gharama ya mafuta iliyoko Geita ni kubwa kuliko iliyoko hapa, ni kwa sababu tatizo kubwa ni Usafirishaji. Hatuwezi kuendelea kujenga barabara zinazobomoka kila baada ya miaka miwili kwa sababu inabeba mizigo mikubwa. Tuwe wakweli! Kama barabara hizi zinatumia mamilioni ya shilingi, tunakopa, wenzetu wanakaa wanasema hawaoni faida ya mikopo na barabara hizo zinakufa, keshokutwa tutalazimika kuzijenga upya kabla ya kulipa madeni. Njia pekee ya kufanya suala hili ni kuimarisha sana mfumo wetu wa reli ili tuweze kuhakikisha kwamba tunakuwa na bidhaa zinazopungua bei.
Mheshimiwa Spika, nimeona kwenye Mpango, kuna mpango wa kujenga Uwanja wa Ndege Chato. Kutoka Geita kwenda Chato ni kilometa zaidi ya 150. Geita ni Makao Makuu ya Mkoa. Naomba sana Wizara hii itakapofika, tunataka kujua kama kutakuwa na mpango wowote kwa Geita kupata uwanja wake wa ndege. Watu hawawezi kutembea kilometa 160; tunakubali kwamba Mheshimiwa Rais anatoka Chato na sisi tunafurahi kuwa na Mheshimiwa Rais Chato, lakini Geita kama Makao Makuu ya Mkoa, tunataka uwanja wa ndege.
Mheshimiwa Spika, Geita tunayo machimbo mengi sana ya dhahabu. Kwa bahati mbaya Serikali imekuwa inapambana zaidi na maskini kuliko inavyopambana na umaskini.
SPIKA: Mheshimiwa Kanyasu, kama unaunga Mkono hoja, dakika zako zimekwisha.
MHE. COSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.