Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MASUALA YA UKIMWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI, napenda kuwashukuru sana wachangiaji wote ambao wamechangia hoja hii, walikuwa wengi sana waliochangia kwa maandishi, lakini vilevile ambao walichangia kwa kuongea. Lakini kwa nafasi ya kipekee nimshukuru sana Waziri wa Sera na Bunge, Mheshimiwa Jenista Mhagama ambaye alishiriki vikao vyetu vyote na kwa ukamilifu kuanzia asubuhi mpaka muda ambao tulikuwa tunamaliza, namshukuru sana na kumpongeza sana.
Vilevile niwapongeze Wajumbe wa Kamati mpya ya UKIMWI kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wameifanya kuhakikisha kwamba taarifa hii inakamilika ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu kwa kusema kwamba vita dhidi ya masuala ya UKIMWI na vita dhidi ya dawa za kulevya inahitaji dhamira ya dhati. Bila dhamira ya dhati tutakuwa tunapiga porojo na tutakuwa tunaongea lakini vita hii hatutaiweza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisisitize katika maeneo machache na la kwanza nisisitize katika suala la sera. Katika Bunge la Kumi tulifanya mapitio ya Sera ya UKIMWI na Sheria ya UKIMWI lakini vilevile Sheria ya Tume ya Dawa za Kulevya ambazo zilielezea kuhusiana na muundo na mamlaka ambazo sheria hizi zimepewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nianze kwa kusema, kwa kweli Sera ya UKIMWI nayo ni ya muda mrefu, ni ya mwaka 2001 sasa hivi ni mwaka wa 16, tunahitaji tuipitie upya sera ile ili iweze kuendana na mazingira ya sasa. Vivyo hivyo, kuhusiana na Sera ya Dawa za Kulevya ni ya mwaka 2004, mbinu zimebadilika, mahitaji yamebadilika na aina ya dawa za kulevya yamebadilika, tunahitaji sera mpya ambayo itaendana na mazingira ambayo tunayo sasa. Sheria tulizozipitisha zimeelekeza kuhusu muundo mpya, tuiombe Serikali, ili kama tuna dhamira ya dhati katika vita hii, basi miundo hii ya hizi taasisi ambazo zimeundwa upya kisheria basi ziweze kufanya kazi ikiwa ni pamoja na kupewa watumishi ambao wanahitajika kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo nataka nigusie ni suala la fedha, taasisi zote mbili. Tumeanzisha Mfuko wa Masuala ya UKIMWI, ni jambo jema, Serikali iliahidi shilingi bilioni tano imetoa shilingi bilioni 1.5, mahitaji ya masuala ya UKIMWI kwa mwaka ni takribani shilingi trilioni 1.3, hivi sasa fedha ambazo zinapatikana katika masuala ya UKIMWI ni shilingi bilioni 800, tuna gap ya takribani shilingi bilioni 500, tunahitaji tuongeze nguvu zaidi. Fedha za wafadhili zinapungua, ni lazima sasa tujielekeze katika vyanzo vya ndani. Niiombe Serikali na Waheshimiwa Wabunge wote kwa pamoja, ni muda muafaka sasa kuungana, tuhakikishe katika bajeti inayokuja Serikali ije, au sisi kama Wabunge tupendekeze vyanzo mahsusi, kama ilivyokuwa katika Mfuko wa Barabara, kama Mfuko wa Mawasiliano na Mfuko wa Elimu, sasa tuwe na source maalum kwa ajili ya kuwezesha shughuli za UKIMWI. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono kauli ya Mheshimiwa Rais leo asubuhi. Katika Kamati yetu na kama mtasoma katika mapendekezo yetu, tulikuwa tunataka kauli za viongozi wa Kitaifa kukiri kwamba suala la dawa za kulevya ni janga, na leo asubuhi Mheshimiwa Rais ameitamka hiyo kauli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, na mimi niwaombe viongozi wengine, tuendelee kuibeba kauli ya Mheshimiwa Rais na sisi twende tukayasemee. Ndugu zangu, UKIMWI ulipoanza mwaka 1979 tulisema UKIMWI ni tatizo la sehemu fulani katika Tanzania yetu, hivi tuvyoongea hakuna familia ambayo haijaguswa. Na ninyi mtakuwa mashahidi, katika vijiji vyetu, vitongoji vyetu katika Wilaya zetu na Majimbo yetu, tuna wagonjwa ama tuna watu ambao wanatumia dawa za kulevya na waathirika wa dawa za kulevya. Tunapokwenda ni kubaya zaidi, tunahitaji tuweke nguvu sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yetu na sisi tungependa kusisitiza; tuna Kamati zetu katika halmashauri ambazo zinasimamia masuala ya UKIMWI na sisi kama Wabunge ni wajumbe wa zile Kamati za UKIMWI. Tunapendekeza na tungewaomba Serikali na hili mliwekee msisitizo, zile Kamati zipewe majukumu ya ziada ya kuwa ni Kamati za Halmashauri kusimamia masuala ya UKIMWI na dawa za kulevya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Kamati tunaunga mkono suala la viroba linaharibu vijana wetu, linaharibu kizazi chetu, linaharibu Taifa letu. Tanzania tunapoelekea sasa hivi tunakuwa ni Taifa la watu walevi, na bahati mbaya sana tumezi-package hizi pombe kwa kiwango cha chini sana. Leo nilikuwa naongea na Mheshimiwa Mbunge mmoja anasema kule Kanda ya Magharibi pombe hizi zinauzwa shilingi 300, mpaka watoto wadogo ambao wanapewa nauli ya kwenda shuleni wana uwezo kununua ile pombe. Sasa niiombe Serikali, kwa kweli kama ni mapato yote yanapatikana kwa njia hii haramu haiwezekani, tupige vita viroba na sisi kama Wabunge tutawaunga mkono ili tuondokane na hili janga tuweze kujenga kizazi imara kwa miaka ijayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi wamegusia suala la tohara; ni kweli katika suala la kitaalam ni intervention ambayo imeonekana inaweza ikasaidia katika kupunguza ugonjwa ya UKIMWI, ni kitu ambacho kimekuwa proven. Lakini hatuwezi tukalazimisha mtu akafanye tohara, muhimu tuwekeze katika elimu na watu waelewe umuhimu na faida ambazo wanaweza kuzipata kutokana na jambo hili, naamini hilo tukiweza itatusaidia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tuna changamoto kubwa sana; tumetoa elimu, na tuliwekeza sana katika elimu ya UKIMWI lakini inaonekana bado tuna changamoto kubwa. Maambukizi kwa vijana kati ya miaka 15 mpaka 19 ni makubwa sana, kwa mujibu wa takwimu ambazo zimetoka hivi karibuni za Tanzania Demographic Health Survey zinaonesha…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniruhusu kuendelea. Nilikuwa nasema kwamba, katika rika la vijana wa miaka 15 mpaka 16, hususan kwa wasichana, asilimia 27 wameshapata ujauzito. Sasa tunahitaji kwa kweli tuwekeze nguvu kubwa sana katika rika hili kupunguza mimba za utotoni, lakini vilevile katika kupunguza maambukizi. Na hili suala la elimu naomba sana, tunahitaji sisi wenyewe Waheshimiwa Wabunge tujielekeze huko, lakini vilevile katika jamii nzima kuhakikisha kwamba jamii na sisi kama wadau tunashiriki katika kuwajenga vizuri kimaadili watoto wetu, lakini vilevile kuwapa elimu jinsi ya kujikinga na maambukizi ya UKIMWI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kuligusia ni hususan katika upande wa dawa za kulevya, kuna intervention ama mkakati ambao unasaidia kupunguza athari kwa wagonjwa ambao wanatumia dawa za kulevya. Niseme jambo moja ambalo limeongelewa hapa, watumiaji wa dawa za kulevya sio vichaa, na watumiaji wa dawa za kulevya sio wahalifu na hawapaswi kuwekwa jela, ni watu ambao wanahitaji kupata msaada wa tiba na magereza sio sehemu yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuwatia moyo, tumeipiga vita na baadhi nimesikia ni maneno yapo ya kupiga vita sober houses, hatuhitaji kupiga vita sober houses, tunahitaji kuziboresha kuwasaidia na kuzisimamia na kuziratibu. Lakini vilevile Serikali iongeze nguvu kuhakikisha kwamba tuna rehabilitation center yetu ambayo tumekuwa tunaijenga pale Dodoma na tuliliongea hilo, Serikali iweke msukumo tuimalize ile pale. Watumiaji wa dawa za kulevya wasiwekwe Isanga ili sasa wawekwe kule wakapate tiba, wapate msaada wanaohitaji ili warudi katika jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwashauri Waheshimiwa Wabunge maana yake na mimi nasoma kwenye mitandano na magazeti, kutoka katika dawa za kulevya sio shughuli ndogo. Ni sawasawa na huyu ambaye anatumia sigara, kuna mwingine anaweza akaacha papo kwa papo, lakini kuna wengine wanaweza wakachukua hata miaka mitano; anaingia, anatoka, anaingia anatoka. Wanahitaji msaada mkubwa sana badala ya kuwanyanyapaa tuwasaidie waweze kurudi kwenye mstari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na niokoe muda wako, nishukuru, mapendekezo yetu tumeyatoa na tumeyatoa kwa kirefu sana. Niombe sana Serikali ijaribu kuzingatia ili tutakapokutana tena katika Kamati basi itupe mrejesho wametekeleza kwa kiasi gani na wapi wamekwama na kiasi gani wamekwama ili na sisi kama Kamati ya Bunge ambayo inasimamia suala hili tuweze kutoa na kushauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, nakushukuru sana kwa kunipa fursa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nitoe hoja kwamba yale mapendekezo ambayo tumetoa kupitia katika taarifa yetu yaweze kupokelewa na kufanyiwa kazi na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.