Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Peter Joseph Serukamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. PETER J. SERUKAMBA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuchangia hoja yetu ya Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Wabunge waliochangia kwa kusema humu Bungeni Wabunge 32 na Wabunge waliochangia kwa maandishi ni Wabunge 20. Kwa kweli wote waliochangia, waliochangia humu ndani wamekubali mapendekezo yetu na wote ukiangalia wameeleza, walikuwa wanachangia kule ambako sisi tumeweka haya mapendekezo kama Kamati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ambayo ningependa kulitambulisha Bunge lako, ni muhimu sana tulifahamu mwanzo kabisa. La kwanza, Waheshimiwa Wabunge, Tanzania sensa ya mwaka 2012 ilisema kama Taifa tunakuwa kwa 2.7 percent, sasa maana yake tunaongeza Watanzania wenzetu karibia milioni mbili kwenye population yetu. Unaposema hivyo maana yake gharama za afya lazima ziongezeke, lazima gharama za education ziongezeke, sasa hii ndiyo changamoto tuliyonayo na changamoto yetu hii kubwa ni ya kifedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ambalo Wabunge wengi sana wamesema na wote waliochangia humu walikuwa wanaongelea matatizo yaliyopo kwenye zahanati, kwenye vituo vya afya, kwenye hospitali za wilaya, matatizo yalipo kwenye shule za msingi, yaliyopo kwenye shule za sekondari. Moja ya mapendekezo yetu tuliyotoa kama Kamati na ninaomba Waheshimiwa Wabunge tuitafakari upya, tuangalie mfumo wetu wa D by D. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wote waliosema, zaidi ya asilimia 80 tulikuwa tunaongea mambo ya TAMISEMI, hatukuongelea sana mambo ya Waziri wa Afya, mambo mengi ya Waziri wa Elimu. Lakini kwenye Kamati yetu wanaokuja mbele ya Kamati yetu ni Waziri wa Afya; Waziri wa Elimu na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, lakini wanaoshughulika na utendaji wa kila siku wako TAMISEMI. Wanafunzi wakifeli sana tunasema Waziri wa Elimu hatoshi, lakini Waziri wa Elimu anaishia kwenye sera; walimu wanafundishaje, wanaajiriwaje, whether kuna madarasa, whether kuna chaki, hazipo, yeye Waziri wa Elimu hajui. Vituo vya afya vinasimamiwa na Halmashauri zetu, kukitokea leo ugonjwa mkubwa watu wakafa au madaktari, tutahangaika na Waziri wa Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge, kwa nini nasema hili, nataka kama Bunge tutafakari upya mfumo wetu wa kutoa elimu na afya nchini. Ni nia ya Serikali kuhakikisha kila kituo cha afya kina daktari, kina theatre ili tuweze kupunguza vifo vya akina mama na watoto. Lakini anayewaajiri hao ni nani, yuko TAMISEMI. Pendekezo letu linasema na ninaomba Waheshimiwa Wabunge mtuunge mkono kwamba umefika wakati sasa watakapokuja mbele ya Kamati, Wizara ya Afya aje na mtu wa TAMISEMI, kama ni Wizara ya Elimu aje na mtu wa TAMISEMI ili matatizo yale tuwe tuna watu wawili ambao mmoja anashughulika nayo kisera na mwingine anashughulika nayo kwenye utekelezaji. Mimi hili naliona ni tatizo ambalo lazima tulipatie majawabu na wanaoweza kutoa majawabu hayo ni sisi Waheshimiwa Wabunge, naombeni tutekeleze wajibu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hilo ambalo mimi niliona ni la kijumla zaidi, na mimi kwangu hili ndiyo tatizo ninaloliona zaidi, nilikuwa namsikiliza dada yangu Mheshimiwa Jacqueline, anaongea mambo ya Tunduru, lakini yote anaongelea kituo chake cha zahanati, anaongelea kituo chake cha afya, anaongelea hospitali yake ya Wilaya, lakini kwa kweli aliyekuwa anamwambia sio kwenye Kamati yetu, alikuwa anamwambia mtu wa TAMISEMI, na watu wengi ambao wameongea humu ndani wameongea mambo yanayotokea kwenye Wilaya zao. Kwa hiyo ni muhimu sasa tuuangalie mfumo wetu upya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ya mfumo, nilitaka niongee suala la ufaulu kwenye shule za sekondari kwa sababu sisi huko tumelisema ili tuone tunaendaje kwenye suala la ufaulu. Nikisema suala la ufaulu nitaomba niunganishe na shule za binafsi na za umma, na katika mapendekezo yetu tumesema kuhusu shule za binafsi na za umma.
Waheshimiwa Wabunge, kwa wale ambao wamefuatilia matokeo ya form four haya yametoka juzi; Ukihesabu shule ya kwanza mpaka ya 200, shule za umma ni shule 17 tu. Ukichukua shule ya kwanza mpaka ya 100, shule za umma ni shule saba. Hili ni tatizo lazima tutafute ufumbuzi. Kwa hiyo, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge na hili linatokea na mimi ninasema ni muhimu sana sasa Wizara ya Elimu, shule hizi za binafsi pamoja na kwamba wanafanya biashara lakini wanatusaidia Watanzania.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo jukumu kama Bunge ya tuhakikishe zinatoa elimu bora. Waziri amesimama hapa anasema; shule ya Feza haina wanafunzi wengi, akailinganisha na shule ya Kibaha yenye wanafunzi wengi, ukilinganisha hivyo yes, lakini tumekuwa na seminari zina wanafunzi 40 zinaongoza miaka yote. Hoja yetu hapa, naombeni kama Bunge tuhakikishe tunatenga fedha nyingi ili shule za umma ziwe na fedha waweze kusimamia ili tuweze kupata ubora kwenye shule zetu za sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo niwaombe Watu wa Wizara ya Elimu kwenye moja ya pendekezo letu, tunaomba Wizara ya Elimu wajikite kwenye kuhakikisha tunapata ubora kwenye Shule zetu za umma. Na mimi hapa Waheshimiwa Wabunge mnikubalie na Kamati yangu, nimpongeze sana Rais Magufuli kwa kuamua kuleta elimu bure. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ameleta elimu bure maana yake nikusaidia watoto wa maskini, wale wasio na uwezo. Sasa niwaombe watu wa Wizara ya Elimu tuhakikishe tunaboresha hizo sekondari zetu. Ikitokea sasa mzazi ameamua kuacha shule ya bure ameenda shule ya kulipia hilo ni tatizo lake. Haiwezekani sisi tuanze sasa kusema, shule za kulipia tuwapangie school fees, hapana. Sisi ndiyo maana kama Serikali nadhani mliangalia busara ya hali ya maisha ya watu mmesema shule zetu ni za bure. Hapa kuna mzazi ameamua kuacha shule ya bure ameamua kupeleka mtoto kwenye shule ya kulipia tumuache alipe anavyoweza kwasababu ni maamuzi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka niongelee suala la afya. Wizara ya Afya Wabunge wengi sana wameongelea suala la dawa. Waheshimiwa Wabunge kwanza niipongeze Serikali na sisi Kamati tumeipongeza sana. Ukiangalia bajeti ya mwaka huu iliyowekwa kwa ajili ya dawa, ndugu zangu tukubaliane kama Bunge tuwapongeze Serikali bajeti ni kubwa sana. Challenge ambayo nawapa watu wa Wizara ya Afya na Wizara ya Fedha, Wizara ya Fedha, fedha mnajua mtawapa na tunapeleka shilingi bilioni 20 kila mwezi kwa sababu dawa lazima kuna process ya kuyanunua, naiomba Serikali hasa Waziri wa Fedha, tuna mifuko yetu ya jamii tunapoanza mwaka tuiombe iipe pesa kule MSD wanunue dawa, lakini kila mwezi wanapoleta disbursement yao iende kurudisha hela kwenye Mifuko ya Jamii maana yake ni nini? Tutakuwa tumetatua tatizo la uwepo wa dawa ili ziende kwa wakati na kwa jinsi hiyo tutaonekana tumefanya kazi kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na hapo tunarudi kwenye dawa ni pale pale sasa TAMISEMI kuna dawa nyingine wananunua wenyewe Waziri wa Afya hajui kwahiyo yeye atakapo report ata-report hali ya dawa ambayo yeye ni custodian wake lakini kule TAMISEMI wanaweza wakanunua bila kumwambia Waziri wa Afya, kwa hiyo, cha msingi hii mifumo tuiunganishe ili tuweze kujua hali halisi ya dawa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vifaa tiba na niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge, najua hili Serikali linakigugumizi nalo sana, lakini niwaombe sana Serikali dunia ya leo hatuwezi kununua vifaa vyote kwenye hospitali zote, hatuwezi. Ziko taasisi kubwa duniani watakuja hapa, wataleta vifaa tiba, watafunga kwenye hospitali zote, wataviendesha lakini sisi tusimamie wasitoze bei kubwa. Teknolojia ikibadilika watabadilisha wao. Lakini sisi tukisema lazima tununue safari yetu ya kwenda kila Mkoa tutatumia miaka mingi sana kwa sababu vifaa hivi ni bei ghali sana. Niwaombe Serikali imefika wakati twende kwenye PPP kwa ajili ya kupata hizi mashine kubwa na ambazo advantage zake ni tatu; moja ni unahakika utapata the latest technology; pili, teknolojia ikipitwa na wakati watabadilisha na tatu, watu wetu watapata huduma bora zaidi kwa sababu watu hawa watakuja na watu wa kuviendesha vyombo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani hili ni suala la Serikali naomba muende mkalisimamie ili tuone namna ambavyo tunaweza tukafanikiwa katika mambo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo tumelitolea kama Kamati ni suala la Bima ya Afya. Bima ya Afya ni jambo jema sana lakini inaumiza sisi Wabunge una kadi ya Bima ya Afya eti hapa Tanzania tu kuna hospitali hawapokei Bima ya Afya, haiwezekani.
Mimi ni matarajio yangu Serikali sasa muende mkaliangalie angalau tunapokwenda kwenye universal coverage, lakini hata hii iliyopo ya kwanza iwe na maana kwa maana kwamba popote nitakapoenda hawataniambia kadi hii siipokei. Kama suala ni fedha muongeze ili wanaochangia wachangie fedha nyingi, lakini waweze kupata huduma bora zaidi na muanze kufikiria suala la kwenda mpaka huko kwa Afrika ya Mashariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo Waheshimiwa Wabunge mmelichangia kwa nguvu zote ni suala la mikopo wa elimu ya juu. Waheshimiwa Wabunge sisi Kama Kamati tumesema kuhusu namna bora ya kuangalia kuhusu suala la mikopo ya elimu ya juu. Moja ya jambo ambalo tumesema lakini hakuna Mbunge ambaye alili-pick up, lakini mimi naona kwetu ni muhimu sana; suala la kuanzisha scholarship program.
Waheshimiwa Wabunge, nchi zote wanaotuzunguka kuna scholarship program, ikiwezekana tuiite Magufuli Scholarship Program ili wale watoto ambao wamefaulu sana form six awe mtoto wa tajiri, awe mtoto wa maskini lakini ni mtoto ambaye ana kipaji, amefaulu sana kwenye yale maeneo ya vipaumbele watoto hawa wapewe scholarship.
Mheshimiwa Mwenyekiti, itasaidia kuonyesha kwamba hatujawabagua. Kwa hiyo wale watoto ambao wamepata point tatu, mtoto amepata point nne kwenye PCM hata kama ni mtoto wa nani ni muhimu sana Serikali iangalie uwezo wa kuanzisha scholarship program. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa suala la vigezo; naomba sana watu wa Wizara ya Elimu, vigezo vya mikopo visibadilishwe badilishwe. Maneno mengine yanaletwa kwa sababu kila mwaka kuna vigezo vyake. Ni vizuri vigezo viwe vinajulikana, vikishajulikana ni rahisi lakini ukishaanzisha na scholarship program itasaidia sana kwa wale watoto ambao wamefanya vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu madai ya walimu; tumesema hapa ndani, tunaomba sana Wizara ya Elimu, Wizara ya TAMISEMI na hili naomba Waziri Mkuu wewe upo hapa ikiwezekana Waziri Mkuu watu hawa wawili wakae, vyombo hivi viwili ama vitatu; Chama cha Walimu, TAMISEMI pamoja na Wizara ya Elimu tukae tulijadili suala la madai ya walimu ili tujue madai ya walimu kiukweli ni kiasi gani, yahakikiwe, tusiwe na figure mbili mbili na baadaye sasa Serikali kadri itakavyokuwa na uwezo iweze kuwalipa hao walimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ndiyo mambo mengi ambayo Waheshimiwa Wabunge kwa suala la Wizara ya Afya na Elimu wameyasema sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mengine ni suala la ugonjwa wa saratani ambalo kwa kweli wengi wamelisema, ndugu zangu tukubaliane ugonjwa huu unakuja kwa kasi sana. Tumeweka kwenye pendekezo letu, tuombe sasa Serikali ianze kuwekeza fedha nyingi kwa ajili ya kutatua tatizo hili. Ni ugonjwa mkubwa, ugonjwa unaotumia fedha nyingi lakini hatuna choice lazima tuhangaike kuwasaidia Watanzania hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TBC; Waheshimiwa Wabunge wamesema kwa kweli chombo chetu cha TBC ndugu zangu Wabunge naomba mniunge mkono kwenye bajeti ijayo tuhakikishe wanapata fedha za kutosha ili angalau TBC waweze kusikika kwenye Wilaya zote Tanzania, redio yetu ya Taifa iweze kusikika kwenye Wilaya zote za Tanzania maana kupata habari ni jambo muhimu sana kama Taifa. Naombeni tuungane mkono ili tuweze kupata bajeti ili waweze kufanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo Waheshimiwa Wabunge wamelisemea ambalo ni kupongeza kuhusu Muswada wa Habari lakini kikubwa zaidi, Mheshimiwa Devotha Minja anasema suala la diploma katika uandishi wa habari kwamba sasa kuweka kigezo cha uandishi wa habari lazima awe na elimu kwanza ya diploma Mheshimiwa Devotha anasema ni jambo kubwa hili na ni jambo jema anaamini safari yetu ya kuleta weledi kwenye uandishi wa habari Tanzania tunaanza kuelekea huko. Tunaipongeza Serikali, tunaomba tutekeleze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni suala la michezo; Mheshimiwa Kadutu anasema, ili tuweze na sisi kushangilia kwenye Michezo hatuna shortcut lazima tuwekeze. Tuwekeze kuanzia kindergarten mpaka watoto wanapopanda huku juu; na ili tuweze kupata mafanikio hayo ambayo tunayataka lazima tuwekeze na kwa kweli ndugu zangu michezo ni ajira. Tukifanikiwa kama nchi na sisi tukafika wakati ambapo tutakuwa tunatoa Watanzania wasiopungua hata wanne, watano kwenda kucheza Kimataifa maana yake tutakuwa tumesaidia sana kwa vijana wetu na fedha zile zitakuja kwenye uchumi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni suala la mfumo wa Elimu. Waheshimiwa Wabunge wamelisema sana na sisi kwenye pendekezo letu tumesema tunaomba sasa Serikali iende ikakae, ikaungalie mfumo wetu wa elimu ili wautatue tutakapokuja kukutana baadaye watuambie wamefanya nini, kwa sababau matatizo haya tusipoyaangalia kwa upana, hatuwezi kuyatatua vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo Waheshimiwa Wabunge naomba sasa niweze kutoa hoja ili Bunge lako tukufu liweze kupitisha mapendekezo yetu yote ya Kamati, naomba kutoa hoja Waheshimiwa Wabunge.