Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Maryam Salum Msabaha

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kunijalia uhai na uzima na mimi kusimama mbele yako kwenye Bunge lako Tukufu na kuchangia Wizara ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, naipongeza hotuba ya Kambi ya Upinzani iliyowasilishwa na kiongozi wetu wa Kambi ya Upinzani. Naishauri Serikali, yale yote mazuri yaliyozungumzwa kwenye hotuba ya Kambi ya Upinzani myachukue na myafanyie kazi kwa mustakabali wa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika Hotuba ya Waziri Mkuu nitachangia ukurasa wa 11 kuhusu mambo ya Muungano. Kweli kuna mambo mengi ya Muungano, kero zimetatuliwa na nyingine mpaka leo hazijapata ufumbuzi na sio vibaya pia kuuliza ni zipi zilizopata ufumbuzi na zipi ambazo
hazijapata ufumbuzi. Nakumbuka kuna Tume ya Pamoja ilianzishwa miaka mitano ya nyuma kwa ajili ya masuala ya kifedha na Akaunti ya Pamoja kwa pande zote mbili, kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara lakini mpaka sasa hivi hii Tume sijui imeingiziwa kiasi gani cha fedha. Ukitazama hata fedha wanazozipata ni za kulipana tu mishahara, ukiangalia majengo wanayoyatumia ni ya kukodi. Nataka niulize Serikali ni kiasi gani cha fedha kimeingizwa katika Akaunti hii ya Pamoja ya masuala ya Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Akaunti hii ya Pamoja inashughulikia mambo mengi lakini sasa kuna kizungumkuti, hatujui kinachoingizwa. Nadhani ni vizuri wananchi kwa pande zote mbili tujue pande hii ya Zanzibar wanachangia kiasi gani na Tanzania Bara wanachangia kiasi gani ili wananchi wajue faida za Muungano na hasara za Muungano.
Mheshimiwa Spika, naomba Serikali zile kero za Muungano ambazo zimekuwa ni kero sugu na kama zimepatiwa ufumbuzi wa kudumu ziwe zinatolewa kwenye magazeti ya Zanzibar Leo au magazeti ya Serikali ili wananchi na vyombo vya habari mbalimbali wapate kufuatilia kero hizi
za Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikiondoka kwenye masuala ya Muungano bado nimo kwenye kitabu cha Waziri Mkuu kwenye ukurasa wa 10 kuhusu masuala ya siasa. Siasa ni maendeleo, tukiwa na siasa safi lazima tutakuwa na maendeleo. Tukiwa na utawala bora lazima tutakuwa na
maendeleo. Tukiwa na utawala ambao unaheshimu haki za binadamu, haki za sheria na kufuata misingi ya demokrasia ni lazima maendeleo na uchumi wa Taifa utakua kwa kasi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo vyama vya siasa vimezuiliwa kufanya mikutano, vyama vya siasa mtaji wao uko kwa wananchi na chama cha siasa bila kufanya mikutano, bila kutangaza sera za chama chao hamwezi kuingiza wanachama na hawawezi kujua sera za chama ni nini. Nashauri Ofisi ya Rais iangalie suala hili, Waziri Mkuu aangalie suala hili kwa mustakabali wa Taifa hili tusiingize migogoro isiyokuwa ya lazima, vyama vya siasa viruhusiwe kufanya mikutano. Vyama vya siasa vyote vyenye usajili wa kudumu vina haki ya kufanya mikutano.
Mheshimiwa Spika, tuangalie pia katika Marais wote waliopita, Zanzibar lazima kulikuwa na changamoto zake. Pia niwapongeze kwa dhati ya moyo wangu Marais waliothubutu kukaa na upande wa Zanzibar kuangalia zile changamoto na matatizo ya kisiasa na hata wakakaa wakapata muafaka.
Mheshimiwa Spika, niombe haya yaliyotokea sio mambo mazuri kwa Tanzania hii tuliyokuwa nayo. Turudi tukae mezani tuzungumze kwa kina tuangalie mustakabali wa nchi kwanza na maslahi ya wananchi kwa pande zote za Muungano ili tupate maendeleo, tupate muafaka wa
kisiasa. Tusifanye siasa za kuburuzana, chuki na ubabe. Ndiyo maana nimetangulia kusema tukiwa na siasa safi lazima tutapata maendeleo.
Mheshimiwa Spika, nimwombe Mheshimiwa Rais aangalie kisiwa cha Zanzibar na Pemba kama ambavyo Marais waliotangulia wa Muungano walikaa meza moja wakaangalia mustakabali wa Zanzibar, wakaangalia mustakabali wa Pemba na Muungano ili tupate muafaka tusonge mbele tujenge Tanzania yetu, utaifa kwanza. (Makafi)
Mheshimiwa Spika, hakuna kitu kizuri kama masikilizano, hakuna kitu kizuri kama kufahamiana na mkifahamiana na mkisikilizana Mwenyezi Mungu huleta baraka, neema na kila lenye heri kwa wanaosikilizana lakini kukiwa na mfarakano mkawa hamsikilizani baraka pia inaondoka. Namshauri Mheshimiwa Rais asiogope arudi meza moja wakae na Maalim Seif, wakae na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar waangalie mustakabali wa Zanzibar na Muungano unakokwenda tupate kujenga nchi kwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nasema hayo kwa nini? Kuna wengi wanaogopa kumshauri Rais, lakini mimi namshauri Rais wangu namwambia rudi Zanzibar tunakupenda, wakae meza moja watafute mustakabali wa Taifa hili. Hatuwezi kwenda na siasa za chuki, hatuwezi kwenda na utawala usiokuwa na mantiki na Tanzania hii.
Mheshimiwa Spika, nirudi kwenye masuala ya vyombo vya ulinzi na usalama. Suala hili ni mtambuka, nimeshangaa sana na namshauri Mheshimiwa Rais kama wengine mnaogopa kumshauri, tangu enzi ya Mwalimu Nyerere vikosi vya jeshi havijawahi kulipa umeme wala
havijawahi kuwekewa LUKU. Majeshi ni kitu muhimu katika nchi yetu, vyombo vya ulinzi ni kitu muhimu katika nchi yetu, maslahi ya vyombo vya ulinzi na usalama yatazamwe kwa jicho pana, yatazamwe kwa uangalifu, yatazamwe kwa maslahi ya nchi. Leo tusiingize migogoro isiyokuwa na sababu katika vikosi vya ulinzi na usalama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hii nchi ni yetu sote, hakuna nchi ya CHADEMA, CCM, CUF, ACT wala ya NCCR-Mageuzi, tukae tusikilizane, tusibaguane. Leo mimi huwezi kuniambia nisiende kwa mtoto wa Ali Hassan Mwinyi kumsalimia, utakuwa umenikwaza au nisiende sijui kwa ndugu yangu Mheshimiwa Nahodha pale kumsalimia utakuwa umenikwaza, tukae tusikilizane. Tushauriane tuangalie nchi inakwenda wapi na wao watanishauri wataniambia Bi. Maryam unavyokwenda sivyo nitapokea ushauri wao kama kaka zangu, tuondoshe chuki za kisiasa, tujenge Tanzania yetu.
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Mungu ibariki Tanzania.