Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Abdallah Ally Mtolea

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Temeke

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi nami niweze kuishauri Serikali mambo mawili, matatu. Awali ya yote kwanza niwape pole wananchi wangu wa Temeke kwa changamoto wanazozipata kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha Jijini Dar es Salaam. Niwaombe tu tuendelee kuomba kwamba ziendelee kunyesha mvua zenye neema na wala zisiwe zile zenye balaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu katika maeneo machache hasa katika ukurasa wake wa 15 mpaka ukurasa wa 18 ambapo anazungumzia masula mazima ya uwezeshaji, ajira na mahusiano kazini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni kwamba bado ratio ya Watanzania wasiokuwa na ajira imezidi kuongezeka na mpaka sasa takwimu bado zinatuonesha kwamba zaidi ya watu laki nane wanaingia kwenye soko la ajira kila mwaka na takribani watu 50,000 pekee ndio hubahatika
kupata nafasi za kazi na hapa haijalishi zile ajira bora au ajira ilimradi ajira. Ukweli bado upo pale pale kwamba hata hao wachache ambao wanapata nafasi za ajira mazingira yao ya kufanya kazi bado ni magumu sana. Wafanyakazi ambao wanafanya kazi kwenye magodauni, viwandani bado wanafanya kazi katika mazingira magumu sana, wanafanya kazi katika mazingira ya unyanyasaji mkubwa, wanafanya kazi bila kuwa na protective gears, kuwa na vifaa vya kuwazuia na hatari zozote ambazo zinaweza kujitokeza katika mazingira yao ya kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapo hapo bado pia hakuna vyama vya wafanyakazi katika sehemu za kazi ambazo zinaweza kutetea maslahi ya wafanyakazi. Naitaka Serikali ihakikishe kwamba kila sehemu ambayo watu wanafanya kazi kuwe na chama cha wafanyakazi. Jambo hili wanapoachiwa wafanyakazi wenyewe wajiundie vyama vyao wanapata changamoto kubwa, wanapata upinzani mkubwa kutoka kwa waajiri kwa sababu waajiri hawataki kuona kuna vyama vya wafanyakazi kwa sababu vitadai maslahi ya wafanyakazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kazi ni vizuri akaunda taskforce ambayo itasimamia uanzishwaji wa vyama vya wafanyakazi kila eneo ambapo kuna wafanyakazi wanafanya kazi katika eneo hilo, kwa sababu hakuna mtu mwingine wa kuweza kutetea maslahi ya wafanyakazi kama hakuna chama cha wafanyakazi katika hilo eneo husika. Hao ndio watakaoweza kuhakikisha kwamba wafanyakazi maslahi yao yanaboreshwa, lakini pia mazingira yenyewe yanakuwa rafiki na wezeshi kwa wafanyakazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo tatizo kubwa sana la fao la kujitoa kwenye mifuko ya hifadhi za jamii. Kumekuwa na kero kubwa na kelele nyingi sana kwa wafanyakazi huko mtaani. Katika Bunge la Kumi ilipitisha sheria hapa ya kuondoa fao la kujitoa kwenye mifuko ya hifadhi ya kijamii. Hili limekuwa ni pigo kubwa sana kwa wafanyakazi. Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi sisi ambao tumefanya kazi katika private sectors hatukuwa hata siku moja tuna malengo ya kufanya kazi mpaka uzeeke. Unafanya kazi kwa malengo, kwamba ufanye kazi labda miaka mitano au sita uache kazi uende ukajiajiri mwenyewe. Unategemea baada ya kuacha kazi uende ukalitumie fao lako la kujitoa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii upate fedha uende ukafanye uwekezaji mwingine, uendeshe maisha yako kwa kujiajiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii wafanyakazi hawezi kwenda ku-access fao la kujitoa eti mpaka wafikishe miaka 55, nani ana uhakika wa kesho? Kwa hiyo yapo mambo mazuri ambayo yamefanywa na Bunge la Kumi lakini yapo pia mambo mabaya ambayo yamefanywa na Bunge la kumi. Ni wajibu sasa wa awamu hii kuyarekebisha yale mabaya kwa maslahi ya wananchi wetu. kwa hiyo, nilikuwa nategemea katika bajeti ya mwaka huu Mheshimiwa Waziri aje hapa na mpango wa kutaka kuileta sheria hiyo Bungeni, ili tuifanyie mabadiliko turudishe fao la kujitoa kwa wafanyakazi katika mifuko ya kijamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ni kweli Serikali inaamini kwenye yale ambayo inayahubiri, tunahubiri hapa kuijenga Tanzania ya viwanda. Hatuhitaji hivyo viwanda vijengwe na wageni, tunahitaji Watanzania wenyewe ndio waweze kuvijenga viwanda hivyo, ili viwanufaishe Watanzania. Kwa maelezo ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Mheshimiwa Mwijage, anakwambia kwamba, ukiwa na milioni 15, milioni 20, milioni 30 una uwezo wa kuanzisha kiwanda chako.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mtu ambaye anadai fedha zake NSSF au PPF ambazo zinaweza kuwa milioni 30 au milioni 40 anaweza kumbe na yeye kuanzisha kiwanda chake. Leo unapomzuwia kuweza kuchukua fedha yake eti mpaka atimize miaka 55 maana yake ni kwamba hamtaki vijana wa nchi hii sasa wamiliki viwanda wakiwa na umri mdogo, sasa, kwa nini Serikali iwazuie vijana kutajirika wakiwa na umri mdogo?. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watu ambao wako makazini leo ni kati ya miaka 25 mpaka miaka 35. Kumbe huyu anaweza kupata fedha yake na akaamua kuachana na ajira akaenda kuwekeza kwenye viwanda. Leo Serikali inamzuia mtu huyu asimiliki kiwanda kwa sababu tu eti hajafikisha miaka 55. Hii haiwezi kuwa sahihi. Kwa hiyo, nizidi kuishauri Serikali ilete hapa hiyo sheria ili tubadilishe turudishe fao la kujitoa katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni utumiaji wa dawa za kulevya. Nashukuru sana kwa jitihada ambazo zimeanza za kuanzisha vituo vile vya kutoa dawa za methadone, kwa kuwasaidia wale ambao wameathirika na matumizi ya dawa za kulevya ili waweze kuacha matumizi hayo taratibu. Ukweli ni kwamba, inaonekana kama hivyo vituo vilikuwa tu vya majaribio, dawa hizo zinatolewa kwa ubaguzi mkubwa. Waathirika wanapokwenda wanatengwa, wanaambiwa kwamba wale ambao wanatumia dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga ndio wanapewa hizo dawa za methadone, lakini wale ambao bado wanatumia ile njia inayoitwa cocktail, wao hawapewi dawa hizo za methadone. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kinachotokea ni nini; wale wanaotumia cocktail ambao na wenyewe wana nia ya kujitoa kwenye dawa za kulevya, wanalazimika sasa na wao kuanza kutumia ile njia ya kujidunga, ili waweze kupata hizo dawa. Hiyo njia ya kujidunga ni njia hatari sana, sasa kama kweli lengo ni kuwasaidia vijana wetu kwa nini tuwabague? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuongeze tuongeze uwezeshaji, tuongeze hizo dawa ziwe za kutosha, ili kila aliyekuwa tayari kuachana na dawa za kulevya aweze kupata hizo dawa na aache, tuache kuwatenga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia, ni vizuri hivi vituo vikasogezwa karibu na maeneo ya watu. Kwa mfano katika Jimbo la Temeke, sehemu pekee ambazo hizo dawa zinatolewa ni kwenye Hospitali ya Temeke. Sasa kwa nini huduma hii isisogezwe kwenye kila kata? Sisogezwe kwenye kila zahanati kuwe pia na huduma hii ya kutoa hizo dawa za methadone? Kwa sababu, hawa waathirika wanapotembea umbali mrefu kuzipata hizi dawa, wakati mwingine wanashindwa kwenda kwa hivyo, wanakatiza zile dozi. Kwa hiyo, kama lengo la Serikali ni kuwasaidia hawa vijana, basi wahakikishe tunakuwa na dawa za kutosha, lakini pia hivi vituo vinasogea kwenye maeneo ambayo wananchi ndiko wanakotokea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho nililokuwa nataka kuchangia hapa ni kuhusu utendaji wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Kwa masikitiko makubwa sana Ofisi hii ya Msajili wa Vyama vya Siasa katika hizi siku za karibuni imekuwa ni ofisi yenye vituko na kufanya mambo ya ajabu, tofauti na majukumu ya Ofisi hii yanavyotakiwa kufanywa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia ofisi hii ikiviamulia vyama nani awe kiongozi wa chama hicho kwa vile tu Msajili labda pengine ana maslahi yake binafsi. Sitaki kuzungumzia namna ambavyo amemrudisha Profesa Lipumba, eti awe Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi –
CUF kwa sababu kesi iko Mahakamani. Pia juzi tu hapa amemrudisha mtu kumfanya awe ndiye makamu mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi wakati hakuwa na sifa wala hakustahili kuwa hivyo. Sasa tunataka kuuliza haya mabadiliko ya majukumu na nguvu ya Msajili wa Vyama vya Siasa yametoka wapi na yameanza lini na kwa maslahi ya nani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunavyotambua sisi, Msajili wa Vyama vya Siasa ni Karani tu wa kutunza kumbukumbu za vyama vya siasa. Lakini leo anajipa nguvu kubwa na kuvipangia vyama nani aweze kuviongoza. Lakini amekwenda mbali zaidi, juzi hapa kati ameshirikiana na wahuni wachache kutoa ruzuku ya Chama cha Wananchi – CUF kuipeleka iende huko mtaani iende ikaliwe. Sasa tunajiuliza, hivi fedha za Serikali ambazo ni fedha za walipa kodi wa nchi hii, zinawezaje kutolewa bila utaratibu na zikaingia mtaani?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.