Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Hassan Elias Masala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nachingwea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafsi hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu pamoja na Serikali yake kwa utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Mafanikio makubwa yameonekana ndani ya mwaka mmoja ambao tunakwenda kujadili bajeti ya Awamu ya Pili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze kutoa mchango wangu katika maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la kwanza ni kilimo, kama ambavyo limezungumziwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nataka nijielekeze katika kilimo cha zao la korosho.
Mheshimiwa Naibu Spika, yako baadhi ya mapendekezo ambayo nilitaka niyatoe ili kuweza kuboresha Mfumo wa Stakabadhi Ghalani. Kwanza tunaipongeza Serikali, mwaka 2016 tulileta hoja hapa za kuondoa tozo ambazo zilikuwa ni kikwazo kwa wakulima wetu. Takriban
tozo tano ziliondolewa na hii ilipelekea kuweza kupata bei kubwa mpaka kufikia 3,800 kwa zao la korosho. Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Nachingwea na wananchi wa Kusini kwa ujumla, tunaomba tuseme ahsante kwa Serikali yetu sikivu kwa kufuatiliwa kilio chao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, mambo ambayo nilitaka niboreshe kwanza ni eneo la ucheleweshaji wa malipo. Minada imekuwa inafanyika na kwa mujibu wa catalogue za ufanyikaji wa minada, minada ile ilikuwa inatakiwa malipo yafanyike ndani ya siku zisizopungua sita, lakini kwa bahati mbaya makampuni mengi ambayo yalikuwa yanashinda zabuni ya kuchukua korosho za wakulima walikuwa wanachelewesha malipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka leo ninapozungumza, toka mwezi wa Kumi na Moja kuna baadhi ya wakulima ndani ya eneo langu na maeneo ya Kusini baadhi, bado hawajapata malipo yao. Kwa hiyo, hii ni sehemu ya kero ambayo nafikiri Wizara pamoja na wadau wote wa zao la korosho lazima tujitahidi kurekebisha kasoro hizi ili mfumo uweze kuwa mzuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo napenda kushauri ni suala zima la usajili wa vyama, hasa Vyama Vikuu wa Ushirika. Kwa Jimbo langu la Nachingwea tunatumia Chama Kikuu cha Lunali. Chama hiki kinajumuisha Ruangwa, Nachingwea pamoja na Liwale. Naomba tayari wameshaanza kuonesha utashi wa kwenda kusajili mara baada ya kukamilisha taratibu za kufilisi Chama Kikuu cha IIulu ambacho kilikuwa kinahudumia wakulima wa Mkoa wa Lindi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba kupitia bajeti tunayoenda kuijadili, jambo hili litiliwe mkazo, sisi tunaotumia chama ambapo sasa hivi ni Kamati ya muda, tuweze kupata chama kikuu ambacho kitaenda kusimamia maslahi ya wakulima wa zao la korosho kabla hatujaingia
katika msimu wa korosho ndani ya mwezi wa Kumi kuanzia mwaka huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili, ambalo nataka nishauri pia katika kilimo ni eneo la ajira kwa Watendaji. Kwa kipindi cha nyuma, kabla ya mfumo haujaboreshwa, Watendaji wengi ambao walikuwa wamechukuliwa katika Vyama vya Ushirika ni wale ambao hawakuwa na uwezo
lakini pia hawakuwa na elimu ya utunzaji wa fedha.
Mzunguko wa fedha katika msimu wa mwaka huu, umefikia siyo chini ya shilingi bilioni 40 katika Mkoa wa Lindi. Ukiangalia Watendaji ambao wanatoa fedha kwa wakulima, uwezo wao ni mdogo sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa sababu mapato yamekua na fedha imeongezeka, naomba niishauri Wizara ya Kilimo itoe maelekezo kwa Vyama vyote Vikuu vya Ushirika na Vyama vya Msingi vitoe ajira kwa watu ambao wana elimu ya utunzaji wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii nina vyama vitatu ndani ya Jimbo langu, wahasibu wake wana kesi, wamepelekwa Mahakamani kwa sababu ya kupoteza fedha za wakulima na hii yote ni kwa sababu walishindwa kutoa fedha kwa taratibu za kifedha jinsi inavyotaka. Kwa hiyo, ili
tuweze kuwasaidia vizuri, ni lazima ajira sasa za wale Wahasibu wa hivi vyama zitolewe kwa watu ambao angalau wana elimu ambayo itaweza kuwasaidia kuweza kutunza fedha za wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nilitaka nishauri katika kilimo ni suala la usimamizi wa tozo ambazo zimeondolewa. Ziko tozo katika zile tozo tano, bado mwaka huu, katika msimu huu zimeendelea kufanya kazi. Kwa mfano, iko tozo ya usafiri iliondolewa na hii tozo iliondolewa kwa sababu tulishauri maghala yatakayotumika, yatumike yale ambayo yako katika ngazi ya Vijiji pamoja na Kata. Bahati mbaya kutokana na kuchelewa kuanza kwa msimu, maghala yaliyotumika ni maghala makuu tu. Kwa hiyo, tozo ya usafiri ikalazimika kurudi tena na hivyo kuwakata wakulima kinyume na makubaliano na sheria ambayo tayari tulishaipitisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo naomba hili tulichukue, safari hii tungependa kuona maghala yote katika ngazi ya Kata, Vijiji yanakarabatiwa mapema iwezekavyo ili tozo hii ambayo ilijirudia, isijirudie tena katika msimu huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la mwisho katika kilimo ni suala zima la pembejeo za ruzuku. Mwaka 2016 kwa maana ya msimu huu wa kilimo, Mkoa wa Lindi peke yake tumepokea tani 80. Themanini ukigawanya katika wilaya sita maana yake ni takriban kila wilaya ilikuwa inaenda kupata tani zisizopungua 20 mpaka 18, kitu ambacho ilikuwa ni utani mkubwa sana. Sasa hili naomba watu wa Wizara waliangalie; tunataka kilimo, tunataka tuimarishe viwanda; unapoleta mbegu tani 80 kwa mkoa mzima, ukagawanywe kwa wilaya sita, kwa kweli hii imetushangaza sana, hatujajua tatizo ni nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba watakapokwenda kujumuisha, watuambie kwa nini Mkoa wa Lindi safari hii tani za mbolea na mbegu za ruzuku ambazo mpaka sasa hivi ninavyozungumza zimeshindwa kwenda kwa wakulima, hazijaletwa kwa wingi kama ilivyo mikoa mingine
ukilinganisha na Iringa na Mbeya ambako wamepeleka ziadi ya tani 1,000 wakati Mkoa wa Lindi na Mtwara, jumla yake tani hata 200 hazifiki? Hili tunaomba tupate ufafanuzi ili tujue kama Mkoa wa Lindi na Mtwara kwa sasa hivi hatushiriki kilimo au kuna jambo gani ambalo linaenda kujitokeza?
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo napenda kuchangia katika hotuba ya Waziri Mkuu ni eneo la maji. Naipongeza Wizara ya Maji, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Maji na Naibu wake; walikuja Jimboni kwetu Nachingwea wameona hali halisi. Tunao mradi
mkubwa wa maji ya Mbwinji pale Nachingwea sasa hivi, unafanya kazi nzuri. Moja ya ahadi ambayo ilitolewa ni kuhakikisha maji yanasambazwa umbali wa kilomita tano katika vijiji vinavyozunguka yale maeneo ya chanzo kikuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti hii tunayoenda kuimalizia, jumla ya shilingi bilioni moja ilitengwa. Shilingi bilioni moja hii ilitakiwa itumike kwa watu wa Masasi, Nachingwea pamoja na Ruangwa. Ndani na Wilaya ya Nachingwea tumepata vijiji sita; tuna kijiji cha Naipanga,
Mtepeche, Mkotokuyana, Mandai pamoja na Chemchem. Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nipate ufafanuzi wakati unapokwenda kujumuisha kiasi hiki cha fedha ambacho tayari mchakato wa kumpata mkandarasi umeshafanyika, ni lini sasa mradi huu unaenda kutekelezwa ili wananchi wa haya maeneo niliyoyataja waweze kupata maji safi na maji salama ili tuweze kuwasaidia wananchi
wetu ambao kwa kweli wanateseka kwa adha ya kupata maji umbali mrefu?
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ambalo napenda kuchangia katika hotuba hii ni suala la barabara. Mheshimiwa Rais alipofika Nachingwea, alitoa ahadi ya kusimamia, kuhakikisha ujenzi wa barabara ya Nachingwea - Masasi, Nachingwea - Nanganga inakwenda kujengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2016 niliposimama hapa kuuliza swali, niliomba kupata ufafanuzi kwa sababu feasibility study ilishakamilika, ni lini barabara hii itajengwa? Bahati mbaya tulipata shilingi bilioni moja; naomba kupitia bajeti hii ambayo tunaijadili, nijue kupitia utaratibu wa watu wa Wizara ya Ujenzi, wana mkakati gani sasa wa kwenda kuhakikisha barabara hii ambayo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, lakini tayari imeshakidhi vigezo ni lini itaaanza kujengwa kwa kiwango cha lami ili tuweze kuunganisha kati ya Wilaya za Nachingwea, Ruangwa, Liwale pamoja na Masasi ambao ni Mkoa wa Mtwara?
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri Mheshimiwa Waziri Mkuu anajua namna gani ambavyo tunahangaika kupata adha kubwa ya usafiri katika maeneo haya yote. Kwa hiyo, watu wa Wizara ya Ujenzi, tunaomba sana watu wa mikoa hii na maeneo haya waweze kuangalia kilio chetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni la nishati. Mkoa wa Lindi na Mtwara kwa sasa tuko gizani. Hali ya upatikanaji wa umeme siyo ya uhakika. Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru
Mheshimiwa Waziri, amekuwa akitolea majibu mazuri pale tulipomwuliza, lakini naomba pamoja na kujenga kituo kile ambacho kiko pale maeneo ya Mnazi Mmoja, bado naomba nijue ni jitihada gani ambazo Wizara inakwenda kufanya, kwa sababu sasa hivi mashine zinazofanya kazi kwa umeme ambao unasambazwa mikoa yote miwili, hazizidi mashine nne. Je, tukishajenga kituo tunachojenga, bado inaweza kwenda kuwa ni suluhu ya kudumu ukiondoa jitihada nyingine za kuongeza mashine?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kupitia Wizara, naomba Mheshimiwa Muhongo Profesa wangu, tusaidie watu wa Mikoa hii ya Lindi na Mtwara. Kuna utaratibu gani kupitia Wizara za kuongeza hizi mashine ambazo zitakwenda kututoa gizani sasa hivi kama ambavyo hali imekuwa? Pia naomba na nitafurahi sana nikimwona anakuja katika maeneo haya ambayo sisi kwa muda mrefu wananchi wetu wametutupia lawama kwamba hatusemi na hatujawasilisha kero hii ambayo kwa kweli imekuwa ni changamoto kwa maendeleo ya Wilaya kubwa kama ya Nachingwea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri tukishamaliza kikao hiki atutembelee katika haya maeneo ili kuona hali halisi ya namna tunavyopata athari.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la mwisho ambalo nataka nilizungumzie ni suala la ajira kwa vijana. Nampongeza Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana pamoja na Naibu Waziri, rafiki yangu, Ndugu yangu, Mheshimiwa Anthony Mavunde, wamekuwa wanafanya kazi, ni wabunifu
wa project mbalimbali ambazo zinaenda kuwainua vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie katika eneo moja, sisi Lindi na Mtwara tuna vyuo hivyo ambavyo tumevitja. Tuna VETA Lindi na Mtwara. Programu ambazo zimepitishwa… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana.