Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Neema William Mgaya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi nami kuweza kuchangia Hotuba hii ya Waziri Mkuu. Kwanza nianze kwa kutoa pole kwa kifo cha mpendwa wetu Mheshimiwa Dkt. Elly Macha, Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema peponi. Amina.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuanza mchango wangu kwa kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Naipongeza kwa kuweza kujenga na kukarabati barabara urefu wa kilometa 430 ambayo ni 62% ya lengo alilojiwekea
katika kujenga barabara urefu wa kilometa 692 kuanzia Julai, 2016 hadi Februari, 2017. Naipongeza sana Serikali yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwa masikitiko makubwa, pamoja na pongezi hizo, Mkoa wangu wa Njombe hauna barabara ya lami hata moja. Naishukuru Serikali imeweza kutenga bajeti katika barabara zote za Mkoa wa Njombe, lakini hakuna barabara hata moja iliyoanza kutengenezwa. Mfano, Barabara ya Itonyi – Ludewa – Manda; kuna Barabara ya Kibena – Lupembe – Madeke; kuna Barabara ya Njombe – Makete; Barabara ya Njombe – Mdandu – Iyai; zote hizo zimetengewa bajeti, lakini bado hazijaanza kutengenezwa. Naiomba Serikali yangu sikivu, ianze sasa mchakato wa kuweza kutengeneza barabara hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye suala la afya. Siku zote nimekuwa nikisimama ndani ya Bunge hili na kuiomba Serikali; Wilaya ya Wanging’ombe ni wilaya mpya, hatuna hospitali. Wananchi wa Wilaya ya Wanging’ombe wanakwenda kutibiwa Hospitali ya Ilembula
ambayo gharama zake ni kubwa. Wananchi wanashindwa kukidhi mahitaji ya afya kwa sababu gharama ni kubwa sana. Naiomba Serikali iangalie umuhimu wa kuweza kujenga Hopitali ya Wilaya ndani ya Wilaya ya Wanging’ombe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna pesa ambazo zilielekezwa zipelekwe kwenye Zahanati na Vituo vya Afya vilivyomo ndani ya Wilaya ya Wanging’ombe, lakini mpaka sasa hivi pesa zile hazijapelekwa ili kuweza kujenga Zahanati na Vituo vya Afya. Matokeo yake sasa wananchi
wamekusanya nguvu kubwa kuweza kujenga maboma kwa ajili ya Zahanati hizo na Vituo vya Afya, lakini pesa kwa ajili ya kuendeleza ujenzi hazijapelekwa. Hii inawavunja nguvu wananchi kwa sababu wanatumia nguvu kubwa kujenga maboma kwa ajili ya hizo Zahanati na hivyo Vituo vya Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naweza nikataja tu Vituo vya Afya na Zahanati chache ambazo ziko ndani ya Wilaya ya Wanging’ombe hazijapelekewa pesa ilhali pesa zilipangwa. Kuna Zahanati ya Itambo, Katenge, Igima, Mmerenge, Ivigo na kuna Vituo vya Afya, Mdandu, Igagala na Ilembula. Tunaomba sasa pesa zipelekwe ili Zahanati na Vituo vya Afya hivyo viweze kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tuna Hospitali ya Mkoa ya Kibena. Ile Hospitali ya Kibena ndiyo ambayo tunaitegemea sisi pale kwenye Mkoa wa Njombe, lakini hospitali ile majengo ni machakavu, vilevile wodi za wagonjwa ni chache. Kwa mfano, kuna wodi moja tu ya wanaume, wagonjwa wa Kifua Kikuu wanalala humo humo, wagonjwa wa ajali za bodaboda wanalala humo humo. Mtu anakwenda na ugonjwa mwingine, anakuja kupata ugonjwa mwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali iweze kuongeza wodi za wagonjwa katika Hospitali ya Kibena, vilevile na kukarabati yale majengo kwani yamekuwa machakavu sana. Tunaomba Serikali iweze kutatua tatizo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Jimbo la Lupembe, wananchi wamejitolea ekari 52 kwa ajili ya kuweza kujengewa hospitali katika Halmashauri ile ya Mji wa Njombe. Naiomba Serikali ifikirie sasa kwa kina na kuona umuhimu kwamba wananchi wa Jimbo la Lupembe nao wanahitaji hospitali ukizingatia kwamba Mkoa wetu wa Njombe ndiyo kwanza unaanza kukua na hivyo huduma nyingi za afya tunakuwa bado hatujapata vile inavyostahiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la maji. Nimekuwa nikizungumzia suala la maji mara nyingi sana ndani ya Bunge hili na kuiomba Serikali iweze kutatua tatizo la maji katika Tarafa ya Wanging’ombe. Tatizo la maji Tarafa ya Wanging’ombe katika Jimbo la Wanging’ombe limekuwa ni tatizo sugu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikwenda mwaka 2015 kuomba kura kwa ajili ya kumwombea Mbunge ambaye ni Waziri wa Maji, Mheshimiwa Lwenge, kwa kweli akinamama na akinababa tatizo lao kubwa sana kule ambalo walikuwa wakilitaja mara kwa mara ni tatizo la maji. Ukienda Kata ya Kijombe, Saja, Ilembula, Wanging’ombe yenyewe tatizo la maji ni kubwa sana. Tunaomba tatizo hilo liweze kutatuliwa mara moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mji wa Makambako wanapata maji kwa msimu. Kipindi cha kiangazi maji hakuna kabisa. Maji yanapatikana kipindi cha masika tu. Tunaomba Serikali iweze kuangalia tatizo hilo la maji katika Mji wa Makambako ili akina mama wa Makambako waweze
kujikwamua katika tatizo hilo la maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Njombe Mjini hali ni hiyo hiyo, tatizo la maji bado lipo na inapunguza ufanisi mkubwa sana kwa akinamama kufanya kazi kwa sababu, muda mwingi wanakuwa wanatumia kwenda kutafuta maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Lupembe katika vijiji 45, vijiji 31 vyote havina huduma ya maji. Hali ni mbaya. Tunaomba Serikali iweze kutatua tatizo hilo la maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye elimu. Shule zetu zilizopo ndani ya Mkoa wa Njombe, kwa maana ya Shule za Msingi na za Sekondari majengo yetu ni machakavu, lakini vilevile tuna uhaba wa madarasa na uhaba wa Walimu wa Sayansi katika Shule za Sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, unaweza ukakuta Shule ya Sekondari haina Mwalimu hata mmoja wa sayansi na shule nyingine zina Mwalimu mmoja au wawili. Kwa kweli, naiomba Serikali sasa itambue umuhimu wa kuongeza Walimu wa sayansi katika shule zetu za sekondari ndani ya Mkoa wa Njombe na kuweza kukarabati madarasa hayo pamoja na kujenga madarasa mapya kwa ajili ya wanafunzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kilimo. Kule kwetu Njombe tuna zao kubwa la chai, lakini hivi sasa bei ya chai imeshuka sana. Kilo moja wanauza 250/= wakati gharama za uzalishaji zinazidi kilo moja ya chai. Gharama za uzalishaji katika kilo moja ya chai ni shilingi 450/=, unaona kuna tofauti hapo ya karibu sh. 200/=. Tunaomba Serikali iangalie soko la chai katika kilimo chetu cha chai ndani ya Mkoa wetu wa Njombe ili wale wakulima ambao wanalima chai waweze kupata faida na wasiwe wanazalisha kwa hasara.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pembejeo. Mbegu zinachelewa kufika kwa wakati, lakini mbolea ya kukuzia inachelewa kufika. Hazifiki kwa wakati, lakini cha kusikitisha zaidi muda wa kupanda umeshapita, muda wa kuweka ile mbolea ya kukuzia umeshapita; wananchi wanalazimishwa wanunue zile mbolea, wanunue na zile mbegu, wakati huo muda unakuwa umeshakwisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli, hiyo siyo sawa na siyo jambo jema kwa wananchi wetu kuwafanyia hivyo. Tunaomba mbegu na mbolea za kupandia zifike kwa wakati ili zisije zikachelewa halafu tena bado mnawalazimisha wanunue hizo mbolea na hizo mbegu, inakuwa ni hasara
kwao.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, nimalizie tu katika suala la umeme. Lupembe bado kuna changamoto kubwa sana ya umeme. Katika vijiji 45, vijiji 30 vizima havina umeme. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.