Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Lucy Simon Magereli

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa na mimi leo nichangie katika hotuba hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nianze kwa kuunga mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na mimi nitajielekeza eneo moja mahsusi kabisa la ukuaji wa uchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ukurasa wa 10, kuna quotation pale alitoa iko kwa lugha ya Kiingereza lakini ilitolewa pia tafsiri isiyo rasmi ambayo na mimi ningependa pia niirejee, nayo inasema hivi; “Ukuaji wa uchumi unakuwa shirikishi unapotokea kwenye sekta ambazo watu maskini wanafanya kazi kama vile kilimo. Unatokea katika maeneo ambayo watu maskini wanaishi, kwa mfano, maeneo ambayo hayajaendelea na yasiyo na rasilimali. Unatumia nyenzo za uzalishaji ambazo watu maskini wanazo, kwa mfano, nguvu kazi isiyo ya kitaalamu na unapunguza bei za bidhaa ambazo watu maskini wanatumia kwa mfano chakula, mafuta na nguo.” Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu yeye kati ya maeneo aliyoyazungumzia kwamba yamefanya vizuri sana ni eneo hili la ukuaji wa uchumi. Maoni yangu mimi binafsi ni kwamba ukuaji wa uchumi hauwezi kuja kama katika uchumi wa leo hatuwezi kuishirikisha sekta binafsi. Sekta binafsi imetengwa kabisa na kwa bahati mbaya kuna baadhi ya kauli ambazo
zimekuwa zikitolewa na Kiongozi Mkuu wa nchi ambazo kwa kweli ukizitafakari kwa undani unaona kabisa kwamba kuna a missing link somewhere ambayo inatupelekea sisi kwenda kudumaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimuombe Mheshimiwa Rais, lakini na Serikali kwa ujumla kwamba ile kampeni yake aliyoianzisha ya malaika waishi kama mashetani, sasa umefika wakati muafaka kwamba kauli hiyo ifutwe kwa sababu ugomvi huo wa kuwataka wale malaika
sasa warudi kuishi kama mashetani umegeuka kiama kwa wale wenyewe mnaowaita mashetani kwa maana ya Watanzania wa hali ya chini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, inaposhindikana sekta binafsi au wawekezaji walioko ndani ya nchi hii kuendesha na kukuza mitaji yao lakini kutoa michango yao katika uchumi wa nchi, mwisho wa siku anayeathirika siyo yule ambaye ni mwenye kipato hicho cha juu ambaye kwa reference ya Mheshimiwa Rais ni malaika lakini anayeathirika ni yule ambaye anaitwa shetani. Sasa na mimi kwa sababu niko kwenye kundi hilo la mashetani, naomba nilete ujumbe wangu maalum nikisema tunaomba waacheni malaika waendelee kuwa malaika, waacheni waendelee kufanya zile karamu zao kwa sababu zile karamu, yale makombo yanayodondoka kwenye zile meza za malaika kwetu sisi ndiyo riziki, ndiyo neema. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapotaka malaika wageuke mashetani, shida kubwa iko kwa Watanzania wa chini. Sasa nastaajabu tunapoona hotuba zinazosema kwamba kuna ukuaji wa uchumi. Tuwaache malaika wanaoshughulika na sekta ya ujenzi waendelee lakini tuwasaidie waweze kuendelea kwa ustawi kwa sababu wanapofanya kazi zao za ujenzi sisi mashetani tunaokotaokota makombo kwa kupata kazi za ajira za ujenzi lakini wakiagiza bidhaa in bulk kwa maana ya bidhaa nyingi basi na sisi tunapata ahueni kwa sababu zinapokuwa nyingi sokoni na sisi tunapata kuzipata katika bei ya ambayo ni ya ahueni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitolee mfano wa mzalishaji na mwekezaji mmoja Bakhressa ambaye katika kibano ambacho amekipata kwa muda mfupi wa Serikali ya Awamu ya Tano, amebadilisha kabisa mkakati wake wa uwekezaji na kwa kiasi kikubwa mtaji wake sasa anauhamishia maeneo mengine ya Afrika kwa maana ya nchi nyingine za Afrika. Hatua hiyo tu inaleta ujumbe straight kwamba kuna ajira ambazo zimeathirika. Kuna hao mashetani sasa ambao kwa yule malaika Bakhressa kuadhibiwa na kupangiwa kodi ambazo haziko realistic na masharti mengine ambayo hayatekelezeki kibiashara, amepunguza wafanyakazi lakini zingatieni ndiye anayezalisha mpaka maziwa na maji ya shilingi 500 na sisi mashetani tunapata ahueni ya kunywa maji ya chupa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo kama la Breweries, tuache malaika hawa wa Breweries wazalishe kwa sababu wakizalisha sisi mashetani wa kule mashambani, mazao yetu ya ngano na shairi yanapata soko la uhakika. Pia wale wanaojishughulisha na shughuli za usafirishaji na sisi vijana wetu wako kwenye kuwa madereva wa hayo magari lakini wako katika kuwa utingo wa hayo magari na kutoka hapo na sisi tunapa riziki na vijana wetu wanakwenda shule.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna eneo kwa mfano la bandari. Wakati bandari ina-operate katika kiwango chake ilitusaidia sana sisi tunaoitwa mashetani kupata kiasi kikubwa cha ajira na vijana wetu kutumika katika eneo la bandari ambapo kwa sasa kutokana na kiwango cha uingizaji na utoaji wa mizigo kushuka, vijana wengi sana wamepoteza ajira bandarini. Vilevile yale magari yaliyokuwa yanaondoa mizigo bandarini na kupeleka mikoani na nchi za jirani napo palikuwa kuna kundi kubwa la Watanzania ambao walikuwa wanahudumia kama madereva, utingo lakini mama ntilie katika maeneo tofauti walikuwa wanapata riziki zao kutokana na eneo hilo. Naamini sasa nimeeleweka ninapojaribu kusema ya kwamba tuwaache malaika waendelee kuwa malaika kwa sababu sisi mashetani tunapotea kwenye karamu za meza zao, wanapodondosha
na sisi ndiyo tunaishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilipata taarifa juzi kupitia vyombo vya habari kwamba Private Sector Foundation wanakuja Dodoma kwa ajili ya kuonana na Serikali, naamini taarifa hiyo mnayo. Nimuombe Mheshimiwa Waziri Mkuu, hao ndiyo watu ambao unatakiwa kuwapokea na mimi sijui niombe kama Mheshimiwa mwingine aliyesema, muache Waziri Mkuu atusikilize. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba hawa watu wa private sector wanapokuja Dodoma kuja kuonana na Serikali wapewe fursa, wapewe usikivu…
Mheshimiwa Naibu Spika, nilimaanisha kumueleza Waziri Mkuu nilisikia kupitia vyombo vya habari kwamba The Private Sector Foundation wanakuja Dodoma kuja kuonana na Serikali. Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba uwapokee hao watu na uwasikilize kwa sababu kama nilivyosema awali makombo ya kwenye meza za karamu zao kwetu sisi ni neema. Hebu acheni private sector sasa ishamiri, itoe ajira kwa Watanzania, izalishe bidhaa nyingi ili bidhaa zishuke bei lakini muwape na access ya ku-import ili bidhaa ziwe nyingi kwenye masoko na kwenye mzunguko ili na sisi tunaokuwa referred kama mashetani, naupenda sana huo msemo sana kwa sababu ni fahari kweli kuitwa na Rais wako kwamba wale wote ambao tuna kipato cha chini basi sisi ni mashetani na sisi tupate kuneemeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nataka niende kwenye suala moja la msingi ambalo nimeliona na niombe attention. Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, kuna suala limejitokeza ambalo naendelea kulistaajabiwa. Jambo hili ni kwamba, Mheshimiwa Rais ametoa kibali kwa mwekezaji mmoja wa hapa Tanzania, Dangote, achukue mgodi wetu wa makaa ya mawe, achimbe mwenyewe, asafirishe mwenyewe, atumie mwenyewe, huu ni utaratibu gani? Huu ni wizi wa namna gani wa wazi na hadharani? Sasa leo tunahangaika na mchanga wa ACACIA bandarini nimeona mpaka leo Tume imeundwa wakati kuna mahali tumemfungia fisi buchani halafu tutamuuliza umekula kilo ngapi? Hivi uwezekano huo kweli upo? Mheshmiwa Naibu Spika, kati ya mambo sasa ambayo Bunge hili linatakiwa liisimamie Serikali na kulitazama upya ni hili suala la Mgodi wa Makaa ya Mawe. Haya ni kati ya makosa makubwa kabisa ambayo tumeyafanya hata kama lengo ni kumbembeleza mwekezaji basi hapa tumekwenda kinyume kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna eneo lingine la wawekezaji na mitaji yao. Kauli za Mheshimiwa Rais zimeendelea kuwa tata kila mara na kusababisha wawekezaji wengi kupata mashaka kuhusu mitaji yao wanayoiwekeza ndani ya nchi hii lakini na wanaotaka kuja sasa na wao wanaongeza mashaka ya kwamba wawekeze ama la.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru ingawa naona muda umekuwa mfupi, ahsante.