Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Ignas Aloyce Malocha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuwa miongoni mwa wachangiaji katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na wachangaiaji waliotangulia kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, Waheshimiwa Mawaziri, Manaibu Waziri na Makatibu Wakuu kwa speed tunayokwenda nayo sasa hivi. Niwatie moyo kwamba endeleeni kukaza uzi mambo yanakwenda barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuchangia upande wa kilimo. Sisi wote tunatambua kwamba asilimia kubwa ya Watanzania wanategemea kilimo kwa zaidi ya asilimia 85. Hata hivyo, ukiangalia hali halisi ya Serikali kutilia maanani suala hili sijaona. Serikali haijazama kwa undani zaidi kuona kwamba kilimo ndiyo kinachoweza kuwasadia Watanzania hawa wengi na mtiririko wa vijana wengi wanaomaliza vyuo vikuu hatutaweza kuwaajiri wote wangeweza kukimbilia kwenye kilimo kama tungeweka mipango yetu vizuri. Kilimo kinalipa kwa mtu ambaye atakuwa amejipanga vizuri na Serikali imeweka mazingira mazuri. Kwa hiyo, naiomba Serikali itilie maanani sana upande wa kilimo ambacho ndiyo kinaweza kuokoa Watanzania walio wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu mbolea na pembejeo. Toka nimeingia katika Bunge hili sijawahi kuona mwaka ambao pembejeo kwa maana ya mbolea na mbegu imewahi msimu wa kilimo hata siku moja. Ni miaka yote imekuwa ikichelewa na sijajua ni kwa sababu gani. Kama tuna dhamira thabiti ya kuwasaidia wananchi tupeleke pembejeo kabla ya msimu kuanza. Ningefurahi mwaka huu jambo hili iwe ni mara ya kwanza Serikali kuwahisha pembejeo kwa wakulima kabla ya msimu kuanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo tatizo lingine la kupeleka mbegu fake na dawa fake za palizi. Yapo maeneo ambayo yanatengeneza mbegu fake na dawa fake za palizi wakulima wetu wananunua na kwenda kuyatumia yanatia hasara kubwa sana. Naomba vyombo vinavyohusika vijaribu kufuatilia makampuni haya ambayo yanapeleka mbegu fake na dawa fake za palizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bado lipo tatizo kubwa la upungufu wa ardhi katika maeneo mbalimbali. Vijana wengi wanapenda kulima, lakini lazima tukubali baadhi ya maeneo ardhi haitoshi. Hii ni kutokana na watu wachache kukumbatia ardhi. Vilevile Serikali ijaribu kuangalia yale maeneo ambayo tulitenga kwa kazi nyingine iyatoe kwa vijana hawa waweze kujiendeleza kwa kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni umwagiliaji. Sisi wote lazima tukubali kwamba kilimo ni sahihi kisicho na risk ni kilimo cha umwagiliaji. Huwezi ukalinganisha kilimo cha umwagiliaji na kilimo cha mvua. Kilimo cha mvua kina risk nyingi sana, unaweza ukapata mafuriko, upepo
mvua au kukosekana kwa mvua. Ndiyo maana hata benki ukienda kuomba mradi wa kilimo kwa kutegemea kilimo cha mvua hupati mkopo. Ukienda na kilimo cha umwagiliaji utapata mkopo kwa sababu wanajua kwamba ni kilimo cha uhakika. Naomba Serikali izame kwa undani zaidi kuhakikisha inainua kilimo cha umwagiliaji. Tunayo mito mingi, mabonde mengi, maziwa mengi, kuna tatizo gani la Serikali kutozama katika kilimo cha umwagiliaji ambacho tunajua kwamba ni kilimo cha uhakika? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, halmashauri yangu iliweza kuomba miradi ya umwagiliaji katika vijiji kadhaa vya Uzia, Ilemba, Msia, Milepa hatujawahi kupewa hata mwaka mmoja. Naomba safari hii tuweze kupewa angalau hata kwa mradi mmoja hasa ule mradi wa Mareza ambao una hekta 7,000 ambazo zinaweza kutumika kwa kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunao upungufu wa maghala kwa baadhi ya mikoa inayozalisha sana kwa mfano Mkoa wa Rukwa. Ukienda pale kwenye maghala ya Serikali utakuta mahindi yamepangwa nje jambo ambalo ni risk mvua zitakapokuwa nyingi. Tungeomba Serikali iweze
kujenga maghala ya kutosha katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende Wizara ya Afya, katika ukurasa wa 40, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameelezea vizuri sana kwamba kumekuwa na ongezeko la fedha za kununua dawa kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015/2016 kwenda shilingi bilioni 251 mwaka 2016/2017. Tunapongeza kitendo hicho na tunaomba Serikali iendelee kuongeza fedha mwaka hadi mwaka kwa suala la ununuzi wa dawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lazima tukubali, sera yetu ya Serikali kupitia Chama cha Mapinduzi iliji-commit kwamba lazima kuwe na zahanati kila kijiji, kituo cha afya kila kijiji na Wilaya kuwa na Hospitali ya Wilaya. Sera hiyo ilieleweka vizuri sana kwa wananchi na ndiyo maana wamejitoa kujenga maboma mengi sana katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu kwa sababu wanajua ingeweza kuwasaidia. Cha ajabu maboma hayo hayajamalizika kutokana na Serikali kutopeleka fedha kwenye halmashauri. Ni nguvu za wananchi na wakati mwingine unakuta Mbunge anajitolea kupitia Mfuko wake wa Jimbo lakini Serikali kama Serikali tungeomba ipeleke fedha ili miradi hiyo iweze kumalizika mapema iwezekanavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kwenye Jimbo langu kuna maboma karibu 13 ambayo wananchi wamejenga, mengine yamefikia hatua nzuri mengine bado katika vijiji vya Ilambo, Maleza, Kirando, Kiryamatundu, Mtapenda, Kasekela, Lyapoo, Nakazi, Mumba, Jangwani,
Kizumbi, Kawila na kasekela. Wananchi wamejitoa kujenga majengo haya, naomba Serikali iweze kupeleka pesa kwenye halmashauri zetu ili iweze kukamilisha majengo haya. Kadhalika, vituo vya afya wananchi wamejitoa michango yao, nguvu zao, wamejenga majengo kwenye Kata za Mfinga, Muza, Ilemba, Kaoze, Kipeta na kalambazite. Tunaomba Serikali ipeleke fedha ili iweze kumalizia majengo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni ukosefu wa magari ya kubeba wagonjwa katika vituo vya afya. Ninavyo vituo vya afya vinne ambavyo havina magari vya Milepa, Lahela, Mpui na Msandamugano lakini sanasana nizungumzie Kituo cha Afya Milepa ambacho kimejengwa
kwenye mazingira magumu kulingana na jiografia ilivyo. Kile kituo kimepoteza akina mama wengi na watoto. Mheshimiwa Waziri Ummy nimekueleza mara kadhaa hata Naibu Waziri nimewaeleza athari kubwa inayotokea ya vifo vya akina mama kutokana na kituo hiki kukosa usafiri. Nina imani kwa maelezo ya leo kwa huruma yako tungeomba uwapatie gari la wagonjwa katika kituo hiki cha afya cha Milepa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunao upungufu mkubwa sana wa watumishi kwenye zahanati zetu hasa mikoa ya pembezoni. Unakuta zahanati inaongozwa na Mhudumu Muuguzi sasa unategemea nini katika mazingira ya namna hiyo? Tunaomba Serikali iweze kuliangalia hilo na ikiwezekana kutoa ajira kwa watumishi wenye sifa wa kuweza kuongoza hizo zahanati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba vilevile nikumbushie maombi ya Halmashauri ya kuomba
halmashauri, wilaya na jimbo. Jambo hili wengine wamekuwa wakiona kwamba labda tunafanya mzaha. Mimi nataka nieleze ukweli, kama Watanzania tuna huduma, Mheshimiwa
Waziri Mkuu umefika katika maeneo yale, tena nikushukuru sana, hukupangiwa kwenda, mimi ndiye niliyekuomba na ukafika. Hata hivyo, nakuambia, sehemu uliyofika ni moja ya nane ya eneo langu. Ulijionea hali halisi ilivyo, jiografia ilivyo na ukubwa wa jimbo ulivyo. Pamoja na Serikali kuweka msimamo wa kutoongeza maeneo, myaangalie maeneo nyeti kama haya. Mimi nazungumza kwa niaba ya wananchi. Wananchi ndiyo wamenituma nizungumze jambo hili
isionekane mimi ndiye ninayezungumza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wananchi wapiga kura zaidi ya 200,000 na idadi ya wananchi karibu 400,000…waaminifu kwa Chama cha Mapinduzi inakuwaje hawa watu msiwaangalie? Kama tulifanya makosa ya kutoa halmashauri kwenye maeneo ambayo hayana sifa basi yavunjeni hayo mtoe haki kwa wale ambao wanastahili kupewa haki kuliko kuweka kizuizi watu
wengine wasiweze kuomba. Mimi nadhani hili ni tatizo kubwa sana katika eneo langu. Nakuomba Mheshimiwa Waziri Mkuu uweze kulibeba kama ulivyokuwa umelibeba toka siku ile
wala siyo jambo la kupuuza. Wananchi ndiyo kilio chao kikubwa kutokana na mazingira na huduma mbovu wanayoipata kutokana na mazingira yaliyopo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nililotaka kuzungumzia ni upande wa elimu. Tuna upungufu mkubwa sana wa walimu wa sayansi kwa shule zetu za sekondari hata shule za msingi. Vilevile umaliziaji wa maabara ambazo wananchi wameshajenga, tungeomba Serikali iweze kumalizia hizo maabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni uanzishwaji wa shule mpya... (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.