Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Josephine Johnson Genzabuke

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa rehema kwa kunijalia kusimama kwa mara nyingine ndani ya Bunge hili Tukufu. Haikuwa kazi rahisi lakini Mungu ni muweza wa mambo yote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru wana CCM wenzangu, lakini nikimshukuru Mwenyekiti wa chama changu na viongozi wakubwa wa chama kwa kuniombea. Mimi naomba niseme nitaendelea kuwa mwana CCM mwaminifu, muadilifu kwa kukipigania na kukitetea chama changu mpaka tone la mwisho la damu yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee kuhusu kilimo. Asilimia kubwa ya Watanzania na hasa wanawake, wengi ni wakulima. Ukifanya sensa utawakuta wanawake wa Tanzania wanaongoza katika shughuli za kilimo. Kwa hiyo, ninachotaka kusema ni kwamba mvua za kwanza ni za kupandia. Ukichelewa kupeleka mbegu wakati mvua zinaanza kunyesha wananchi hawawezi kupata mazao mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo mengi wananchi walipanda bila pembejeo kwa sababu zilichelewa kwa maana ya mbegu, dawa na mbolea kwa ujumla. Hata wakati mwingine waliweza kupanda kwa kutumia mbegu ambazo ni tofauti na mbegu walizotegemea kupata, kwa hiyo, sehemu nyingine mazao yao hayakuweza kuwa mazuri. Naomba basi Serikali ijitahidi kuwahisha kupeleka pembejeo. Vilevile kutokana na ufinyu wa bajeti ya Wizara ya Kilimo, mwaka huu wananchi wengi hawakuweza kupata mbolea, walipata mbolea kiasi kidogo sana ambayo haikuweza kuwatosheleza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hekima yake. Namshukuru sana kwa sababu leo hii ameweza kukutana na mawakala wa Tanzania walioweza kuwawakilisha wenzao akakaa na kuzungumza nao. Nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa usikivu wako. Kutokana na kazi ulizonazo isingeweza kuwa rahisi kuweza kuwakubalia kukaa nao, lakini umetumia nafasi yako kuweza kuwasikiliza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kutokana na jinsi ulivyowaahidi, naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, watakapokuwa wamefanya utafiti, najua wako mawakala wengine sio waaminifu, tunafahamu wapo wengine ni waaminifu na wengine sio waaminifu. Kwa hiyo, wale ambao ni waaminifu watendewe haki na wale ambao sio waaminifu, wachakachuaji wasiwaponze wenzao, wale ambao watakutwa wamefanya vizuri, hawakuweza kuliibia taifa hili waweze kulipwa mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nitumie nafasi hii Mheshimiwa Waziri Mkuu kueleza kwamba wananchi wengi walikopa wakati wanafanya kazi ya uwakala. Naomba muwasaidie kuwaombea kule kwenye mabenki wakati wanasubiri kulipwa haki zao mabenki yale yaweze kusitisha kuuza mali zao ili watakapopata pesa zao waweze kwenda kulipa mikopo yao. Mheshimiwa Waziri Mkuu, chonde chonde kupitia Waziri wa Fedha, tunaomba aongee na mameneja wa mabenki mbalimbali ambako wananchi walikopa mikopo, waweze kusubiri. Wananchi watakapokuwa wamelipwa madeni yao waweze kwenda kulipa madeni yale kwenye mabenki, watu wengi wanapoteza maisha kwa sababu mtu akiuziwa nyumba yake na hana njia nyingine, hana nyumba nyingine anapoteza maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie kuhusu vituo vya afya na zahanati. Tuliahidi kujenga zahanati na vituo vya afya katika kila kijiji na kila kata. Kwa bahati mbaya yapo majengo ambayo tayari yalishajengwa hayajaweza kukamilika na ili yakamilike Halmashauri ndizo zinazotakiwa kujenga yale majengo na Halmashauri hazina pesa. Naomba Serikali isaidie Wizara ya Afya ili Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Halmashauri waweze kupeleka pesa kumalizia vituo vile vya afya na zahanati zilizoko kule kwenye vijiji na kata zetu ilia kina mama na watoto waendelee kupata huduma bora kutokana na vituo vitakapokuwa vimefunguliwa katika Wilaya zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kuwapongeza wanawake wa Tanzania. Wanawake wa Tanzania wameweza kuungana pamoja wakaanzisha vikundi mbalimbali, wakaanzisha vikundi vya SACCOS na SACAS. Naomba niseme vikundi vilivyo vingi havina elimu, vinaishia kukopeshana vyenyewe kwa vyenyewe kwa sababu havijaungana pamoja na hakuna sheria ambayo imeshaundwa kwa ajili ya kuvilinda vikundi hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba basi Serikali iweze kutunga sheria mahsusi ili vikundi hivyo viweze kuendeshwa kitaalam na viungane pamoja kusudi viweze kutambulika katika mabenki hatimaye viweze kukopesheka kwa sababu mabenki siyo rafiki wa maskini. Wale wenye vikundi
hawajaweza kwenda kufungua akaunti kwenye benki, wanakopeshana wao wenyewe huko mitaani kila baada ya mwaka wanafanya sherehe, wananunua nguo mpya, wanapika wali, wanavunja vikundi wanagawana na benki kama hawana sehemu ambayo wataenda kuangalia vikundi vinafanyaje hawawezi kukopesha wanawake hao na vikundi mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuzungumzia kuhusu maliasili na utalii pamoja na Wizara ya Ardhi. Waliahidi kuunda Tume, Tume iliundwa kwenda kutembelea maeneo yenye migogoro, lakini kabla ya matokeo ya ile Tume iliyoundwa baadhi ya watu wamefukuzwa. Tunaomba basi
Serikali iweze kufanya haraka kutoa matokeo ili kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji na kuweza kusogeza mipaka baadhi ya maeneo ili wananchi waweze kupata maeneo ya kulima kwa sababu watu wanaongezeka, ardhi haiongezeki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuzungumzia maji kwa sababu mimi ni mama nafahamu adha wanayokutana nayo akina mama vijijini na hata mijini. Mwaka jana Mkoa wa Kigoma tulitengewa fedha za kutosha, lakini mpaka sasa hivi bado tuna tatizo la maji hasa Wilaya ya Kasulu ninayoishi mimi yako maeneo ambayo maji hayajaweza kufika. Katika eneo la Kibondo maji bado ni tatizo pamoja na Kakonko. Kwa hiyo, naomba zile pesa zilizotengwa, zisiondoshwe mahali pale ziweze kurudishwa Kigoma zikafanye kazi kuwaondolea adha wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la mwisho nataka kuzungumzia kuhusu barabara. Mara nyingi pesa za kutengeneza barabara zimekuwa zikipangwa lakini wakati mwingine hazipelekwi jinsi zilivyopangwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba basi pesa zinazopangwa kwa ajili ya barabara za Kigoma ziende jinsi zilivyo ili tuweze kukamilisha barabara ambazo zimeshaanza kujengwa na hasa kipande cha kutoka Uvinza kwenda Malagarasi, Malagarasi kwenda mpaka Kaliua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru sana na naunga mkono hoja.