Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Dr. Raphael Masunga Chegeni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Nami napenda niungane na wachangiaji wenzangu, kwanza kuwapongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, Waziri wa Fedha na Mipango kwa kuwasilisha Mpango mzuri, Mpango ambao unaonekana una mwelekeo, Mpango ambao unatia bashasha Watanzania kutoka hapa tulipo kufikia malengo ambayo Mheshimiwa Rais ameyaweka Mheshimiwa Spika, ni vigumu sana kuzungumzia Mpango huu kwanza bila kutambua na kufahamu kwamba Mheshimiwa Rais ana nia ya dhati ya kuwapenda Watanzania ya kuwatoa Watanzania kwenye hali waliyonayo waende kwenye hali nzuri zaidi. Itakuwa ni kitu cha ajabu sana kuzungumzia mshahara wa Rais. What is mshahara wa Rais? Ni mtu ameajiriwa na Watanzania, anapata mshahara na ni Rais wa kwanza katika historia hapa nchini aliyetangaza mshahara wake hadharani. Napenda tumpongeze Mheshimiwa Rais kwa hilo kwanza! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, napenda nilipongeze Bunge lako pamoja na Waziri wa Habari, Michezo na Utamaduni, kwa sababu suala la kuonekana kwenye TV, Watanzania lengo lao siyo kuona kwenye TV, wanataka kuona nini Wabunge tunafanya ili kuwatumikia wao. Hii inaonekana kwa vitendo, haionekani kwa maneno ya kuja hapa na kupiga porojo. Naomba Watanzania wote watuelewe kwa hilo na wameshaanza kuelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa hivi nikwambie, hapa Bungeni hata vijembe vimepungua kwa sababu hakuna anayewaona kule. Mbwembwe zote sasa hivi hakuna anayewaona kule! Ndiyo maana wamekuwa wapole. Nami nasema hivi, watulie tuwanyoe taratibu. Maana ukitaka kunyolewa, tega kichwa chako unyolewe taratibu. Tujengane hapa kwa hoja, tupingane kwa hoja na siyo kwa mbwembwe ambazo haziwasaidii Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, watu wanaona majipu yanatumbuliwa! Mimi nasema hivi na bado, yazidi kutumbuliwa zaidi. Kwa sababu, Watanzania wanasema hivi, moja ya sekta ambayo imekuwa ikisumbua ni Sekta ya Utumishi wa Umma. Kuna baadhi ya watu walishajigeuza kuwa miungu watu, hawaguswi! Sasa majipu yameanza kutumbuliwa, wengine wanasema aah, msitumbue watu, msifanye hivi, mnakiuka haki, haki gani? Haki ya kuwanyima Watanzania haki yao? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nasema acha watumbuliwe majipu na vipele na matambazi na wao kama wanataka, waendelee kutumbuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika Mpango huu, napenda nimsifu Mheshimiwa Rais. Mpango wa Kwanza uliokwisha, ulikuwa wa Shilingi trilioni 44.5. Huu ni wa Shilingi trilioni 107. Uone jinsi ambavyo Mheshimiwa Rais na Serikali yake amejipanga kuwatumikia Watanzania. Hivi mnataka nini zaidi hapa jamani? Mnataka tutoke hapa twende wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni mtu ambaye atakuwa na matatizo au upungufu wa akili kidogo, kama ataona Mpango huu unakuwa na kichefuchefu kwake.
MHE. MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, Taarifa! Kanuni ya 68(8).
SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Chegeni, kuna taarifa....
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Spika, wala siipokei kwa sababu ameeleza tu, amezungumza hapa, lakini tutaendelea kuyatumbua yawe yako wapi, yako kwenye shavu, yako wapi yatatumbuliwa tu. Hata wanaosema hawa na wenyewe wengine ni sehemu ya majipu!
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Spika, nao ni sehemu ya majipu! Kwa hiyo, wasione haya! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sasa nijielekeze kwenye mpango wa miaka mitano huu ujao kwa sababu haya ni mambo ya msingi. Nchi hii ili tuweze kutoka hapa tulipo, ni lazima kwanza tuangalie mfumo mzima wa kukusanya kodi yetu ili kila Mtanzania alipe kodi na ashiriki kwenye uchumi wa nchi hii. Huwezi kujenga uchumi wa nchi bila kuwa na mfumo mzuri wa kukusanya kodi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana hii; kwa kweli, ukiangalia sasa hivi licha ya Wahisani na baadhi ya watu mbalimbali wameshindwa kuanza kutupa pesa zao, lakini mapato yetu yameweza kupanda kutoka Shilingi bilioni 850 kwa mwezi mpaka Shilingi trilioni 1.3 kwa mwezi; hii ni achievement moja kubwa sana kwa nchi, lakini imepatikana siyo kwa sababu ya mambo ya rojorojo, ni kwa sababu moja tu ya kutumbua majipu. Haya majipu nayo yalikuwa ni tatizo! Ndiyo maana ukusanyaji wa kodi umeweza kuongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, uchumi huu wetu, naomba Mheshimiwa Waziri alielewe hili; tunahitaji tukusanye kodi kutoka vyanzo vingine mbadala. Tusiwe na msingi wa kudhani kwamba ni kupandisha tu kodi kwenye vitu vilevile, hapana! Tubuni vyanzo vingine mbadala vingi vya kuweza kutupatia kodi. Kwa mfano, haya wa Makampuni ya Simu. Makampuni ya Simu, watu wa TCRA walishawaonesha watu wa TRA kwamba kodi yenu kwa mwezi ni kiasi fulani, sasa kwa sababu mpaka Finance Bill ije, ndiyo kodi iweze kubadilishwa; naomba tuanze kutafuta namna ya kufanya adjustments! Haiwezekani hawa watu wanafanya biashara hawalipi kodi stahiki na hili ni pato moja kubwa sana kwa nchi hii na hawa watu wanakwepa sana kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba sana kupitia Bunge lako hili, mfumo mzima wa ukusanyaji wa kodi kwa Makampuni ya Simu ni lazima sasa ubadilike, lakini hauishii pale. Hawa watu wamejenga minara kila kona nchi hii. Kuna Halmashauri hazipati Service Levy kutoka kwenye minara hii! Unakuta minara imetapakaa, lakini Halmashauri haipati chochote! Hivi hii inakwenda wapi? Ni lazima Halmashauri zetu ziweze kupata kodi kutokana na hii shughuli ya biashara ya minara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nchi hii ili tuweze kupanua uchumi wetu, ni lazima tuweke miundombinu iliyo sahihi. Huwezi ukazungumzia uchumi wa nchi hii bila kuzungumzia reli. Lazima reli ifufuliwe na kutengenezwa kwa kiwango kinachostahili cha standard gauge ili sasa mizigo iweze kusafirishwa kutoka bandari zetu, kutoka mikoa yetu, ukianzia Mtwara kwenda Mchuchuma, ukitoka Dar es Salam kwenda Kigoma, ukitoka Dar es Salaam kwenda Tanga, Mwanza na yote ile inaleta connectivity ya mawasiliano katika nchi na ili tuweze kupunguza gharama katika utengenezaji wa barabara zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, repair ya barabara ni gharama kubwa sana. Leo hii barabara ya Chalinze imekuwa kama chapati, kwa sababu magari mengi yanapita pale pale. Kila kukicha unakuta barabara inaharibika! Vile vile na magari ya mizigo mikubwa yanapita pale. Kwa hiyo, naomba sana hili suala la miundombinu na hasa reli tuweze kuipa kipaumbele katika mkakati wetu wa kufufua uchumi wetu.
Mheshimiwa Spika, kuna baadhi ya maeneo, kwa mfano Kanda ya Ziwa. Wenzetu wa Mbeya wana Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe. Historia yake ukiingalia, ilikuwa ni hela za kujenga uwanja wa Mwanza, ikaonekana hazitoshi zikahamishwa kupelekwa uwanja wa Songwe Mbeya. Mwanza ile ni hub, Uwanja wa Ndege wa Mwanza naomba upewe kipaumbele.
Mheshimiwa Spika, kutoka Mwanza kwenda Serengeti ni kilometa 140, umefika kwenye geti la Serengeti ambapo hata ndugu yangu Mheshimiwa Heche pale na watu wanaokwenda huko akina Mheshimiwa Esther Matiko, ndiyo barabara yao wanapokwenda kule. Unakuta unatumia kilometa 380 kufika kwenye geti la Serengeti kutokea Kilimanjaro, wakati Mwanza ni karibu. Kwa hiyo, naomba sana Mwanza Airport iweze kukamilika ili iweze kufufua uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, naamini kwa kuwa na uwanja wa ndege wa Mwanza itasaidia sana kuleta biashara, itasaidia sana kusukuma uchumi wa Kanda ya Ziwa. Leo hii kwenda Nairobi inabidi pengine upitie Dar es Salaam ndiyo uende Nairobi kwa sababu, ndege hakuna. Kwenda Kampala, inabidi uje Dar es Salaam ndiyo uende Kampala na kadha wa kadha. Naomba sana, uwanja wa ndege wa Mwanza uweze kuimarishwa.
Mheshimiwa Spika, kuna baadhi ya vipaumbele ambavyo tunavyo, lakini suala la kilimo; unaposema tufufue uchumi wa viwanda, ni lazima iwe based na agromechanics na agroeconomy. Sasa hii yote itasaidia sana kufanya wakulima ambao ni wengi zaidi wa Tanzania waweze kuzalisha mazao yatakayochakatwa na kuongezewa thamani, itaondoa na tatizo la ajira kwa vijana, itaondoa na tatizo la kupata kipato kwa watu. Naomba sana suala hili lizingatiwe.
Mheshimiwa Spika, lingine ni suala la uvuvi na mifugo. Mimi najiuliza, tunachoma nyavu moto, lakini nani analeta nyavu hizo na zinapitia wapi? Kwa sababu huyu mvuvi yeye hana kosa! Amekwenda dukani, amekuta nyavu zinauzwa, ananunua. Sipendi kusema kwamba, tuwaambie watu wafanye uvuvi haramu, lakini hizi nyavu zinaingia hapa nchini na mnajua zinaingiaje. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nasema hivi, wanaoingiza nyavu ambazo hazistahili, basi zipigwe marufuku ili kuondokana na tatizo la kuanza kuwatia hasara wavuvi. Mtu amewekeza kwa shilingi kadhaa kwenye mtaji wake pale, halafu mnakuja mnashika nyavu mnachoma! Hii siyo sahihi.
Mheshimiwa Spika, naomba sana Serikali yetu tuliangalie hilo na hasa nikizingatia kwamba Mheshimiwa Rais amekuja na nia thabiti sana kuwatumikia Watanzania na naomba Waheshimiwa Wabunge wote tumuunge mkono. Kwa kupitia bajeti hii naomba kwa kweli, tujipambanue nayo kwamba ni bajeti ya kumsaidia kila Mtanzania. Kipindi hiki ni kipindi ambacho siyo kizuri sana kwetu, lakini lazima tukubali kwamba mabadiliko yoyote yanahitaji kidogo watu kuumia. Tuumie, lakini kwa nia njema ya kujenga nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya watu wanaweza wakawa wanasema kwa kubeza eti kwamba Mheshimiwa Magufuli ni nguvu ya soda, nawashangaa sana! Mheshimiwa Magufuli ana nia ya dhati! Rais wetu tumemchagua kwa kura nyingi sana, Watanzania wamemwamini na niwahakikishie kwamba amekuwa siku zote anaonesha dhamira yake ya kuwatumikia Watanzania. Kama kuna watu wana mkakati wa kutaka kubadilisha au ku-undermine anachokifanya, tunasema washindwe na walegee! Mshindwe na mlegee kabisa! Mlegee kabisaa! Mjilegeze, mlegee, iwe sawasawa!
Mheshimiwa Spika, nasema hivi, lazima tumuunge mkono! Hataweza kupigana vita hii akiwa peke yake. Waheshimiwa Mawaziri mmeanza vizuri, endeleeni! Sitaweza kuwataja mmoja mmoja, lakini nikianzia kwa Mheshimiwa Lukuvi, kwa Mheshimiwa Jenista Mhagama, kwa Mheshimiwa Mwijage mnamwona kila siku anaweka mambo yake hapa, mnaona! Ukija kwa mzee wa TAMISEMI, ukija kwa Mheshimiwa Mwigulu na wengine wote mnawaona hapa. Timu hii ni nzuri! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ila kuna tatizo moja la kimuundo. Tatizo hili Waheshimiwa Wabunge mlielewe. Leo hii Waziri wa Elimu kwa mfano, anazungumzia mambo ya Sera katika Wizara yake, shughuli zote ziko TAMISEMI. Msingi na Sekondari ziko TAMISEMI, yeye ni wa Elimu ya Juu na Sera. Ukija kwa Waziri wa Afya, yeye anazungumzia Sera. Ukienda kwenye Zahanati, Kituo cha Afya, Hospitali ya Wilaya mpaka ya Mkoa ziko chini ya TAMISEMI! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kuna haja kupitia Mpango huu. Unajua siku zote mnapoona kuna tatizo, mnatafuta namna ya kuweza kulitatua tatizo hilo. Mimi naona kama kuna tatizo hapa! Kwa hiyo, kuna haja ya kujaribu kuoanisha vizuri na kuhuisha vizuri mfumo wa utendaji kazi ndani ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, naomba wale wote waliokuwa na nia mbaya, walegee na washindwe. Ahsante sana.