Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Salum Mwinyi Rehani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nakushukuru kupata nafasi hii ya kuweza kuchangia hotuba hii ya Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa taarifa yake na hotuba yake ya bajeti hii ambapo angalau tunaona mwelekeo kidogo ukisimamiwa mambo yataweza kwenda vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile niwashukuru Mawaziri ambao wamo ndani ya Wizara hii Ofisi ya Waziri Mkuu, swahiba yangu pale dada Mheshimiwa Jenista, lakini vilevile na kaka Mheshimiwa Mavunde kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujielekeza kwenye mambo matatu makubwa ambayo nahisi kama nchi tunaweza tukaleta mabadiliko. La mwanzo niombe ofisi yako na tuiombe Wizara ya Kilimo na Serikali kwa ujumla ili nchi hii kuinusuru na janga kubwa la njaa ambalo linatokea katika maeneo mbalimbali ambalo hasa linasababishwa na tatizo la hali ya hewa lazima tuwe na kilimo cha umwagiliaji maji, hatuna njia ya mkato. Mataifa yote ya wenzetu wengine mkakati uliokuwepo ni kuwa na kilimo cha umwagiliaji maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi Novemba mwaka jana tulishiriki kwenye Agriculture Council ya SADC nchi zote zinazotuzunguka tamko lao limejielekeza kwenye umwagiliaji maji. Napenda kutoa rai tufanyaje katika hili ili tuweze kupata mlango wa kutokea. Niombe Serikali kwa ujumla iridhie kuufufua Mfuko wa Umwagiliaji Maji uwe unachangiwa kama inavyochangiwa mifuko mingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mfuko huu ni muhimu na ndiyo dawa ya kuweza kukomboka na kuwa na miundombinu ya umwagiliaji maji. Hesabu ya haraka haraka kama tutakuwa na wachangiaji wa shilingi 50 tu, tukiwa na wapiga simu au wamiliki wa simu milioni 20 ambao kwa Tanzania tunafika idadi hiyo, pesa ile kwa mitandao mitano iliyokuweko ndani ya nchi tunaweza kuwa na zaidi ya shilingi bilioni 144. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi tunaweza kuwa na maeneo maalum ya kimkakati na mazao ya kimkakati, kila eneo tukaweza kuchimba visima vinane, tukaweza kuwa na zaidi ya hekta 1200, tayari tuna uhakika wa reserve ya tani 300,000 za chakula kwa mwaka. Hivyo, tishio la NFRA na mazao yale mchanganyiko ya kusema tutanunua wapi chakula, wale watanunua kwa hawa ambao wamewekeza kwenye umwagiliaji maji hivyo Taifa litakuwa na uhakika wa akiba ya chakula na tatizo kubwa la njaa litakuwa halipo katika maeneo yetu, hiyo ni rai yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, nataka kumuomba Waziri Mkuu, kazi nzuri aliyoifanya kwenye Bodi ya Korosho ahamishie kazi ile kwenye bodi nyingine za Wizara ya Kilimo. Kuna matatizo na hakuendi vizuri kwenye Bodi ya Pamba, kuna matatizo na hakuendi vizuri kwenye Bodi ya Kahawa, kuna matatizo kwenye Bodi ya Chai, chai kama kaachiwa limekuwa shamba la bibi tu hamna anayemuuliza mtu. Tulikuwa na Bodi ya Pareto, leo hii tumeanzisha vilevile Bodi
ya Maziwa, bodi hizi zinatakiwa zipitiwe, zifuatiliwe, utendaji wao wa kazi ujulikane lakini vilevile yale makato wanayowakata lazima yajulikane yanatumika vipi. Hali ilivyo sasa hivi kama hakuna anayesimamia bodi hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe sana Waziri Mkuu mkakati zaidi ulioufanya kwenye Bodi ya Korosho ambapo umewakomboa wakulima na wamerudisha imani wakulima wa korosho tuhamishie kwenye bodi nyingine hizi ili kurejesha imani ya wakulima wa kahawa ambao wengi
wao wameacha kulima kahawa kutokana na makato na mazingira mabaya yaliyokuweko kwenye kahawa. Hali kadhalika, tuangalie pamba inakuwaje, chai inakuwaje lakini tusisahau na pareto vilevile. Tulikuwa ba Bodi ya Pareto ambayo sasa hivi hata haizungumzwi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala kubwa linalotukabili kwenye kilimo ni kutokutilia maanani suala zima la upatikanaji wa pembejeo. Kilimo bila pembejeo hatuna kilimo, ardhi yetu tumeshaitumia imechoka. Serikali kadri tunavyoishauri kuhusiana na pembejeo linaonekana suala lile kwamba ni jepesi na halina uzito wowote.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka juzi nchi ilitenga zaidi ya shilingi bilioni 250 kwa ajili ya pembejeo, zikapatikana zaidi ya shilingi bilioni 120, mwaka jana tumekwenda na shilingi bilioni 20, hali imekuwa tete. Tumetoka kwenye wakulima waliopewa ruzuku ya pembejeo 99,000 sasa hivi tumekuja kwenye wakulima karibu 350, hali ni ngumu. Niiombe Serikali hili suala iliangalie kwa jicho la maana, bila pembejeo utazalishaje? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe wito wangu kwamba, Kamati ya Bajeti na Wizara ya Fedha hili jambo iliangalie kwa jicho la huruma. Wakulima hawa wana nia ya kuzalisha, pamoja na ukata na hali ngumu ya hali ya hewa lakini ukosefu wa pembejeo nao vilevile unachangia kudumaza
maendeleo yao. Hili tulitilie maanani na tuweze kuwasaidia wakulima katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nataka kuzungumza ni la mifugo. Nikushukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu umeshughulikia vizuri suala zima la mifugo hasa maeneo ya Loliondo. Wafugaji wale wa Loliondo bila Kamati ile wangefikia pabaya, sasa hivi wangekuwa wameshafukuzwa na hawaelewi pa kwenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, wale wafugaji kule wako zaidi ya 64,000 ukiwaondoa pale wana ng’ombe zaidi ya 500,000 wale wanakwenda maeneo ya Morogoro na wanakwenda maeneo ya Kusini kitu ambacho kinakwenda kuchochea machafuko baina ya wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, wito wangu, suala hili tuweze kuli-handle vizuri kwa sababu bado Wamasai wale wana uwezo wa kufuga ng’ombe na wakatunza zile rasilimali zilizokuwapo pale za hifadhi bila kuathiri na maisha yakaweza kuendelea baina ya wanyama wa porini na wanyama wa kufugwa. Wito wangu, Kamati iendelee na uchunguzi na mkakati wake, lakini ifike mahali uwekwe utaratibu mzuri wa kufuga pasiwe na wazo la kuwafukuza watu wale. Kwa sababu kuondoka kwao sio kama watachinja wale ng’ombe wao, watahama maeneo na
hivyo tutaongeza tatizo la ugomvi baina ya wakulima na wafugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuzungumzia Bodi ya Maziwa. Bodi hii ina malengo mazuri, imesema mwaka huu inataka kuimarisha ng’ombe wa maziwa angalau wafike milioni moja na laki tano. Ushauri wangu tuanzishe cowshed au vijiji vya ufugaji ili kuweza kuwapelekea huduma hawa wafugaji ambao watapewa hawa ng’ombe wa maziwa. Tutakapoanzisha cowshed hizi itakuwa rahisi kuweza kuwapelekea elimu ya ugani kwa wale wafugaji ambao
wataanzisha mabanda haya kwa pamoja lakini vilevile tutaweza kuweka zile collection centre. Bado Tanzania inaathirika na maziwa ambayo yanatoka nje, ni aibu jamani! Tanzania hatuna kiwanda cha maziwa ya unga tunashindwa na Zimbabwe walau wana kiwanda cha maziwa ya unga. Tatizo letu ni kwamba maziwa yetu hayana viwango na ng’ombe tulionao hawana uwezo wa kutoa maziwa ya kutosha tukaweza kuanzisha hivyo viwanda tulivyokusudia. Kwa hiyo, kama hatukujipanga kuweza kusambaza ng’ombe wa kutosha katika nchi hii… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.