Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwanza nianze na jambo ambalo nisingelianza, lakini kwa sababu kuna mtu amegusa inabidi niseme. Kuna mchangiaji mmoja alizungumzia Msemaji wa Kambi ya Upinzani kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu ambaye ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, kuzungumza ni kwa namna gani bajeti za Serikali hii zimekuwa hewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa bahati mbaya akatolea mifano ya hela ndogo wakati sisi tulikuwa tunaongelea mambo mazito, tulikuwa hatuongelei mambo peanut. Sasa nimuoneshe tu ni kwa nini Kiongozi wa Upinzani Bungeni amesema ni hewa, nitanukuu hotuba yetu. Mosi,
Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ilipewa shilingi bilioni 2.2 kwenye Wizara ya Kilimo ambayo ni sawa na asilimia 2.2 ya bilioni 101 ilizotakiwa ipewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kitengo cha Mifugo na Uvuvi ilitengewa shilingi bilioni 1.2 sawa na asilimia 7.9 kati ya shilingi bilioni 15.8. Amekiri mwenyewe muongeaji kwamba kilimo kwa mwaka huu kimekuwa kwa asilimia 2.9 badala ya asilimia sita iliyokuwa ikitarajiwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani akaenda mbele zaidi, akasema tunashangaa kwamba asilimia 70 ambayo inaajiri Watanzania wengi wamepewa asilimia 2.2 wakati eti tumenunua ndege ama kupeleka advance payment ya bilioni 128 ambayo inahudumia watu 10,000 tu. Sasa naona kuna Wabunge wanakaa wanalalamika hapa halafu wanashindwa kuiambia Serikali ukweli. (Makofi)
Wizara ya Viwanda na Biashara tunaambiwa huu ni mwaka wa viwanda, hii ni Serikali ya viwanda, hii Wizara inatakiwa iratibu wawekezaji waweze kuja, hivi viwanda viweze kupatikana, wawekezaji waweze kuwekeza nchini, imepewa shilingi bilioni 7.2 sawa na asilimia nane ya shilingi bilioni 40 zilizoidhinishwa na Bunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Miundombinu ilipewa shilingi trilioni 1.7 sawa na asilimia 58.7 ya shilingi trilioni 2.1 ambayo Bunge hili lilipitisha; Wizara ya Uchukuzi asilimia 30; Wizara ya Nishati na Madini asilimia 36 na Wizara ya Afya asilimia 25. Hivi mkiambiwa hewa ndugu zangu siyo kweli kwa bajeti nzima ya maendeleo kwa wastani kwa mwaka huu unaoisha ni asilimia kati ya 26 na 34 ambazo zimetolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ndugu zangu kama kweli zaidi ya asilimia 70 ya fedha za maendeleo hazijapatikana, mkiambiwa bajeti yenu ni hewa mnakasirika nini? Kupanga ni kuchagua, tujue uwezo wetu ni upi, tujipange kutokana na uwezo wetu ili tujue tunaendaje
mbele kama Taifa. Ndugu zangu niwaombe wanaopitapita huko mbele wanaambiwa nenda katetee ni hivi, hapa hakuna cha kutetea, hatetei mtu hapa, yaani huu mwaka mmoja wa Mheshimiwa Magufuli na Serikali yake kwenye bajeti ya maendeleo mmechemka, tukubali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Halmashauri zetu, tukiacha kuwa wanafiki hapa ni vilio, mwaka jana Serikali ilikuja kwa mbwembwe hapa tunachukua property tax, tumejipanga vizuri wakijua kwenye Halmashauri nyingi za miji hicho ndio moja ya vyanzo wanavyovitegemea, kwa
mbwembwe nyingi huu mwaka umeisha. Mimi nimetoka juzi kwenye Baraza letu la Madiwani, tunapoenda bajeti nyingine ya mwaka huu hakuna hata shilingi moja iliyotoka Serikali Kuu kwa property tax. Wakati wenyewe tulikuwa tuna uwezo wa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 10, tulikusanya mwaka mmoja ule uliopita, tumepanga kukusanya mwaka huu Serikali imechukua pato hamjaturudishia pato, shughuli za maendeleo zinakwama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sisi ni wa Mjini ambao japo tuna vyanzo vingine, sasa wenzangu na mimi wa vijijini mkikaa hapa mnapiga makelele, mnapiga makofi, oyaoya hatutawanyoosha hawa Mawaziri ili waweze kuwajibika vizuri kwa Bunge. Kwa hiyo, mimi niombe kati ya kipindi ambacho Wabunge tunatakiwa tuwe wamoja kuisaidia nchi yetu na siyo kulinda Serikali yetu, kuisaidia nchi yetu ni kipindi cha bajeti hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya pili, suala la mauaji na utekaji unaoendelea. Asubuhi ilitolewa hoja hapa na Mheshimiwa Hussein Bashe, ukaikatiza hoja, mimi ninaamini kwamba Spika wetu huko anasikiliza. Ninaamini mtu mwingine akija akitoa hoja hiyo hiyo Spika wetu akija ataweza kulitendea haki hili jambo. Nadhani umeona ni jambo zito sana ukasema ngoja kwanza nimsikilizie bosi wangu akija atasema nini, inawezekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kauli zinapotolewa na watu wazito na ninashukuru hili suala halina chama, linatoka upande wa CCM na linatoka kwa upande wa Kambi ya Upinzani. Kwa sababu CCM wanaamini miongoni mwa watu wa Serikali hii kuna watu wana nia njema na Taifa hili, vilevile wanajua kuna watu miongoni mwa Serikali hii hii wanafikiria wao wako juu ya sheria, kwa sababu fulani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana tunasema haya mambo lazima tuyajadili, kama Bunge lisipojadili, kama Bunge linaogopa kujadili leo, nani ajadili. Nilimsikiliza Mheshimiwa Nape akiongea Mtama, alikuwa ni Waziri Mheshimiwa Nape alitoa kauli nzito, kauli ambayo inaonesha kwamba kuna watu ndani ya Serikali wanatumia genge la Usalama wa Taifa kuteka watu, kufanya mauaji. Huyu ni former Minister, siyo mtu mdogo, wiki mbili zilizopita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo Mheshimiwa Bashe amezungumza, mimi kwangu Mbunge wa CCM akizungumza ni kama Serikali inazungumza, that is my opinion kwa sababu ninaamini hakuna Mbunge yeyote makini wa kutoka Chama Tawala akasema kitu ambacho hana uhakika nacho.
Mheshimiwa Bashe amerudia amesema kuna genge ndani ya Usalama wa Taifa linashirikiana na bahati mbaya anatajwa dogo sijui Bashite yule, wamekuwa wakimtajataja kwamba Bashite ndiyo anaongoza hili genge. Sasa tunajiuliza sasa kama Bashite anaongoza genge, kama Bashite anasemwa hachukuliwi hatua, juzi ambaye alimtolea Mheshimiwa Nape silaha lile gari lililombeba limeonesha limesajiliwa kwa namba ya Ikulu, halafu watu wanakauka tafsiri yake ni nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Rais anajua? Sisi hatutaki ionekane Rais anajua, ndiyo maana tunasema hili Bunge likaondoe mzizi wa fitina, kwa sababu inaoneka Mheshimiwa Mwigulu ngoma imeshamshinda na ndiyo jukumu letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunaambiwa kuna Wabunge 11 ni wanted, hivi kweli viongozi wetu mnaambiwa kuna Wabunge 11 wanted na imetoka kwenye proper authority, hakuna mtu yeyote aliyesimama hapa akamwambia thibitisha, futa kauli yako sisi tunajuana, yaani huku ndani tunajuana, sindano ikigusa pale pahali pake inabidi kila mtu anakaa chini anatulia, hakuna mtu aliyepinga kile kilichosemwa. Kwa hiyo, je, tusubiri aanze kufa Mbunge mmoja mmoja ndiyo tuunde hii timu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Ben Saanane kijana wetu amepotea, zikaanza kupigwa propaganda eti CHADEMA tunajua alipo. Sasa kama mnajua sisi wauaji kwa nini msitukamate mtuweke ndani? Kwa nini maisha ya watu tunachukulia simple?
Mheshimiwa Naibu Spika, Ben Saanane aliandika waraka tarehe 8 Septemba, 2016 naomba ninukuu, kaandikiwa na namba ifuatayo; “Ben Saanane unachokitafuta ndani ya Serikali hii utakipata kwa elimu na uwezo wako hatukutarajia ungefikia hatua ya ajabu kwa namna uliyofikia hujiulizi kwa nini upo huru hadi muda huu, your too young to die. Tunajua utaandika na hii, andika lakini the next force hutaandika ukiwa na uhuru wa kutosha. Andika but your days are numbered, unajua kuna rafiki yako alipuuza na hatutaki kuandika kuhusu yeye labda kwa kuwa alitangulia, andika Ben, andika sana, ongea sana lakini utajikuta mwenyewe.”
Mheshimiwa Naibu Spika, namba iliyomwandikia ni 0768 79982 hii namba polisi wanaijua, Serikali mnaijua, mkitaka ku-trace watu...(Makofi)
NAIBU SPIKA: Haya ahsante Mheshimiwa Halima Mdee.