Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru pia kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kidogo kwenye hotuba ya Waziri Mkuu ambayo iko mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaenda kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba nizungumze kwa uchache sana upotoshwaji ambao unafanya ndani ya Bunge na kwa Watanzania kuhusiana na suala la mgogoro wa CUF. Nashangaa sana kwa Wabunge wanaotumia muda wa Bunge kupotosha umma kumshambulia Msajili wa Vyama kwamba anaingilia migogoro ndani ya vyama wakati wao wenyewe wameshindwa kuijua, kuisimamia na kuiheshimu Katiba ya chama chao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wapo waliodiriki kusema kwamba Msajili wa Vyama ni karani tu anayekusanya na kutunza mafaili ya vyama vya siasa, hii ni aibu kubwa kwamba Mbunge hajui hata Sheria ya Vyama vya Siasa inasemaje juu ya majukumu ya Msajili wa Vyama. Msajili wa
Vyama anafanaya kazi ya kulea na kusimamia vyama vya siasa, kazi yake siyo karani, waende wakasome Sheria ya Vyama vya Siasa, majukumu na kazi za Msajili wa Vyama vya Siasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Msajili wa Vyama vya Siasa hakuingilia mgogoro wa CUF peke yake, alipelekewa malalamiko na viongozi ndani ya Chama cha Wananchi CUF, chombo cha mwisho cha maamuzi ni Mkutano Mkuu wa Taifa, Wajumbe 324 walipeleka malalamiko kwa Msajili wa
Vyama juu ya uhuni uliofanyika ndani ya Mkutano Mkuu wa Chama uliofanyika tarehe 21 Agosti, hakuingilia alipelekewa malalamiko.
Mheshimiwa Naibu Spika, Msajili wa Vyama hajamteua Mheshimiwa Sakaya kuwa Kaimu Katibu Mkuu, Katiba ya Chama cha CUF, kipengele 93, Sura ya Tatu kinampa Naibu Katibu Mkuu wa upande wa Bara mamlaka ya kufanya kazi za Katibu Mkuu pale Katibu Mkuu anaposhindwa kutekeleza wajibu wake kama Katiba inavyomwongoza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wabunge wasipotoshe Umma, wasipotoshe Bunge, wasitumie muda wa Bunge kwa ajili ya kudanganya Watanzania, wafanye kazi kwa ajili ya maslahi ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naungana na Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Tabora kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri aliyofanya kuweza kurekebisha Chama cha Ushirika cha Mkoa wa Tabora na ku-overhaul system nzima ya ushirika ya Mkoa wa Tabora, ni matumaini yangu kama watendaji wa Serikali watazingatia maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu na kuyafanya vizuri nina imani kabisa kwamba kilimo cha
tumbaku cha Mkoa wa Tabora kitanufaisha wakulima kama tunavyotarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu hasa suala linalozungumzia suala la uchumi…
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la uchumi. Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu inasema kwamba uchumi unapanda na umekua kwa asilimia saba lakini pia kwamba mfumuko wa bei
umepungua. Naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati wa ku-wind up atuambie, uchumi unapanda wakati hali ya maisha ya Tanzania inazidi kuwa mbaya, hali ya uchumi inazidi kuwa mbaya, pia wafanyabiashara wengi mitaji inazidi kuzama, wanafunga maduka yao, hali ya upatikanaji wa fedha kwa ajili ya maisha ya kawaida unazidi kuwa mbaya unazidi kuwa mdogo. Sasa huu uchumi unapanda, mimi sio mchumi, uchumi unaopanda wakati fedha mifukoni inazidi kupotea ni uchumi wa aina gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya kupanda kwa bei ya gharama za vyakula, wakati tunaambiwa kwamba mfumuko wa bei unapungua lakini ukienda sokoni, leo nimekwenda sokoni na jana nimekwenda sokoni, kilo ya mchele shilingi 2,400, kilo ya unga shilingi 2,200, maharage
nimenunua leo shilingi 2,400 bei zinazidi kupanda. Kwa hali ya kawaida, Watanzania wengi kwa hali ilivyo sasa hivi hawana uwezo wa kuweza kula milo miwili ya uhakika kwa siku. Kwa hiyo, tunaomba Serikali lazima iangalie namna, kama vyakula vimefichwa vitoke vije ndani ya masoko ili bei zishuke. Kuambiwa kwamba bei zinashuka mfumuko wa bei unapungua wakati hali inazidi kubana, haiendani na hali halisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la uwezeshaji wa vijana. Hotuba ya Waziri Mkuu inatuambia kwamba Serikali imetoa almost 1.5 billion kwa ajili ya kusaidia mfuko wa vijana na akina mama pia halmashauri zetu zimetenga fedha karibu shilingi bilioni 4.6 kwa ajili ya kuwezesha vijana na akina mama, kwa Mikoa yote ya Tanzania na Wilaya zetu karibu 140 bado ni fedha kidogo sana. Kwanza fedha inayotolewa na Serikali, shilingi bilioni 1.5 ni ndogo kwa sababu vikundi ni vingi na vingi havipati hiyo hela ya kukopeshwa. Halmashauri zetu ile asilimia tano haitengwi, wanatenga kidogo sana kwa sababu hali ya Halmashauri pia makusanyo siyo mazuri na wengine fedha zao ni kidogo, hawana uwezo wa kutenga asilimia tano kwa ukamilifu, matokeo yake vikundi vimeundwa vingi vya akina mama, vya vijana, hawapati mikopo wanafuatilia mwaka baada ya mwaka hawapati mikopo ya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kwanza Serikali ihakikishe inaongeza fedha za mikopo ya vijana na akina mama za kutosha kwenda kwenye Halmashauri zetu. Pili, kuwepo ufuatiliaji wa kutosha, Halmashauri zitenge fedha za kutosha na kulipa, vikundi vinakopa zile fedha hazirejeshwi, matokeo yake inashindwa kuwa revolving fund ambayo kama ingekuwa inarejeshwa kwa wakati wengine wangepewa, matokeo yake Halmashauri hazirejeshi, vijana
wengine wanasubiri miaka miwili hawajapata mikopo. Kwa hiyo, suala la uwezeshaji wa vijana bado ni tatizo kubwa, fedha inayotolewa ni kidogo, haitoshelezi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la ajira, bado tatizo ajira ni kubwa ndani ya nchi yetu na vijana wengi bado wanazurura, wapo kwenye vijiwe, wapo mitaani. Ni kweli kwamba asilimia karibu 57 ya Watanzania wameajiriwa kwenye sekta binafsi, lakini mazingira wanayofanyia kazi
kwenye sekta binafsi ni magumu mno. Mishahara yao ni midogo, kwanza hawaingizwi kwenye mifuko ya jamii lakini wengine hawana likizo, hawana chochote, wanashindwa wafanye nini kwenye mashirika binafsi. Wengine wananyimwa mpaka haki zao za uzazi, mwanamke akipata
mimba akiwa kwenye mashirika binafsi au viwanda anaachishwa kazi kwa sababu tu kapata mimba, hata ile haki ya kuzaa ananyimwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Serikali ifuatilie, ni kweli kwamba sekta binafsi zinasaidia sana kwenye ajira ya Watanzania lazima tuwapongeze, lakini lazima sheria za kazi zifuatwe. Kama Serikali imesema kima cha chini cha mshahara kwa nini kule wakatoe shilingi 100,000, 120,000 kwa mwezi. Kwa maisha ya sasa hivi kumpa mtu 120,000 kwa mwezi anaishije? Anafanya kazi zaidi hata muda wa saa za kazi wengine mpaka usiku. Pia wengine hawapewi mikataba ya kazi wanafanya kazi kama vibarua, miaka saba mpaka kumi wanaajiriwa kwa miezi mitatu, mitatu wanakosa haki zao za msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, wametuambia kwamba wanatengeneza Mabaraza ya Kazi, maeneo mengine hawaruhusiwi kutengeneza mabaraza ya kazi. Mimi nimeshuhudia kabisa makampuni yetu haya ya Kichina, hawawaruhusu kutengeneza Mabaraza ya Kazi, hata
sehemu ya kupeleka malalamiko yao hakuna. Kwa hiyo, ninaomba Serikali ihakikishe kwamba pamoja na kwamba wanatusaidia ni lazima pia wahakikishe kwamba wanaweza kutoa haki zinazostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ni suala la uzalishaji. Hatuwezi kuwa na uchumi wa viwanda kama hatusimamii vizuri suala la kilimo. Kilimo tusimamie kuanzia uzalishaji, utunzaji, usafirishaji mpaka kwenye masoko. Njia pekee ya kuweza kuwa na uhakika wa masoko ni kuwa na viwanda vidogo vidogo na viwanda vikubwa. Kila Mkoa Mungu ameubariki una zao la biashara, hebu Serikali iweke mkakati, nashukuru kwamba mashirika ya kijamii yameanza kuingia kwenye kutengeneza viwanda, wahakikishe kila Mkoa, tukianza na Mkoa wa Tabora, kiwanda cha tumbaku kijengwe mkoani Tabora, vijana wa Tabora wapate kazi ndani ya kiwanda cha tumbaku.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa Dodoma tuna zao la zabibu, tumeweka kiwanda kilichopo hapa kinachukua concentrate kutoka nje, tuhakikishe kila kiwanda kinachowekwa ndani ya Mkoa wowote kinatumia materials kutoka ndani ya mkoa wenyewe. Tukihakikisha kila Mkoa
tumekuwa na kiwanda, kutumia material ya kilimo yanayopatikana ndani ya mkoa ule, kwanza tutazalisha ajira kwa wingi pia tutaweza kuwainua wakulima kwa sababu watalima kwa tija wana uhakika na masoko yao. Vinginevyo ni tatizo kubwa tutaimba mpaka tuchoke wakulima
hatuwezi kuwainua na ukizingatia asilimia 80 ya Watanzania ni wakulima na wengi wako vijijini wanategemea kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, tuboreshe kilimo, pembejeo ziwepo kwa wakati, tujenge maghala ya kutosha. Tukihakikisha kilimo kimekuwa na tija nina imani kabisa Watanzania walio wengi watanufaika na tutaweza kuondoa umaskini kwa kiasi kikubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Ahsante.